Askofu Mkuu Ruwai’ch kwa UKWAKATA:msiwe na mpasuko na mitafaruku
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Askofu Mkuu Jude Thaddeus Ruwai’ch wa Jimbo Kuu Katoliki Dar Es Salaam, hivi karibuni, Jumatatu ya Pasaka, tarehe 10 Aprili 2023 aliongoza misa Takatifu kwa ajili ya Umoja wa Kwaya Katoliki Tanzania(UKWAKATA), katika Parokia ya Salasala, Jimbo Kuu katoliki la Dar Es Salaam, kwa kuongozwa na Injili ya siku iliyosoma na ambayo ilikuwa inaelezea ushuhuda wa wanawake walioacha kaburi kwa haraka wakiwa na hofu na furaha kubwa wakakimbia kuwatangazia wanafunzi wa Yesu Ufuko wake ili waende Galilaya ndipo wangemwona Yesu Mfufuka. Askofu Mkuu Ruwai’ch alisisitiza juu ya kutoa ushuhuda kama wanakwaya ambao walifika kumshuhudia Kristo kwa sababu ni jambo jema. Tendo hilo ni kuonesha wazi kwamba wao ni Wakristo wengine, na ambao wanapaswa kufanana na Kristo zaidi.
“Tunapojiruhusu tusakamwe na dhambi tunaharibu ule wasifu wa kuwa kama Kristo, tunavuruga maana ya ubatizo tuliopewa, ambao ulitufanya tuzaliwe upya, tuwe watoto wa Mungu, tuwe ndugu zake Kristo na ambaye alitufanya tuwe hekalu au makao ya Roho Mtakatifu”, Alisisitiza Askofu Mkuu. Askofu Mkuu Taddeus, kwa njia hiyo aliwaomba wajifunze kutoka katika udhaifu wa Petro, lakini udhaifu huo uwasaidie kushinda udhaifu wao na kwa kila mmoja. Kwa upande mwingine aliwaomba wajifunze kuwa na uthubutu na ufuasi amini wa kama wale wanawake waliomfuata Yesu mpaka wakaona anakufa msalabani. Lakini pia hawakuishia hapo, bali walihangaika pia na kutaka kuutunza mwili wake baada ya kuzikwa. Askofu Mkuu Ruwai’ch pamoja na kuwatia moyo, na kuwasifu, alipenda pia kutoa angalisho ambalo ni muhimu katika utume wao kwa sababu wamepewa kipaji cha kutangaza Injili kwa njia ya kwaya.
Kwa kufanya hivyo aliomba wakumbuke maneno ya Mtakatifu Agostino, ambaye alikuwa Askofu wa Hippo, Barani la Afrika (alizaliwa tarehe 13 Novemba 354 mjini Thagaste katika mkoa wa Numidia, leo hii mji huo unaitwa Souk Ahras nchini Algeria) ambaye alifundisha kwamba: “anayeimba vizuri anasali mara mbili”. Askofu Mkuu awali ya yote aliwaomba watafiti moyo na kuwaliza maswali kwamba kuimba kwao kunahusisha sauti zao au kuhusisha mioyo, dhamiri na nafsi zao? Aliwashauri kwa hiyo wapende kuimba vizuri na waimbe vizuri kutoka katika kina cha mioyo yao na roho zao. Wanapoimba waimbe, wakitangaza kile wanachoamini, waimbe na wakishi kile wanacho kiamini, waimbe wakishuhudia kile wanachoamini, wakiimbe wakishangilia kile wanachokiamini.
Kwa kuongezea Askofu Mkuu Ruwai’ch alisema na ili hilo liweze kufanyika, lazima kazi ifanyike ya kutafiti moyo. Kwa udadisi zaidi, Askofu Mkuu Taddeus aliuliza maswali wanakwaya waliokuwa hapo na wakiwa wa kweli kunyosha mikono: “Ni wangapi wangeweza kupata komunia siku hiyo? Baada ya kunyosha mikono aliendelea tena kuuliza: “Je ni wangapi ambao wasingeweza kukomunika siku hiyo? Na wakati huo huo akiwaomba wasiogope kunyosha kwa sababu hasingewauliza maswali maana wao wanajua wenyewe sababu gani zinawafanya hivyo. Lakini kwa kujibu alisema hicho “ndicho kinachowafanya pia washindwe kuimba na kusali mara mbili; kushinda kuimba kutoka katika kina ya moyo, nafsi zao, na kushindwa kumtukuza na kumtukia Mungu kwa uwepo wao wote”.
Askofu Mkuu Jimbo katoliki la Dar Es Salaam vile vile aliuliza swali la pili kwa sababu hapo walikuwapo wanawaka kutoka parokia mbali mbali kwamba: “Ni kwaya ngapi ambazo zimekwisha gubikwa na mgogoro? Je huo mgogoro umesababishwa na nini? Je huo mgogoro unamtumika Mungu? Kwa kuongezea alisema: “kwa sababu zipo kwaya ambazo zimeingia mgororo na paroko, mgogoro na wanakwaya wenzao, zipo kwaya ambazo zimeingia mgogoro na kamati tendaji, zipo kwaya ambazo zimeingia migogoro mingine mengi”. Kwa hiyo alibainisha kuwa wanapoingia kwenye migororo wao “ni watu wa mipasuko, sio watu wa amani, sio wacha Mungu, sio wajumbe wa habari njema tena ni wajumbe wa mitafaruku”. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar Es Salaam aliwaomba wanakwaya wajitafiti, wajitathimini na daima wahakikishe kwamba chembe chembe za migogoro, chembe chembe za mitafaruku zisiingie kati yao. Aliwasihi wakatae hiyo mipasuko na mitafaruku, na wakatae chochote kile kinacholeta mivutano kati yao na waamini wenzao, kati yao na wachungaji wao, kati yao na kazi zao tendaji. Kama wajumbe wa Injili, basi wao wawe wajumbe wa amani.
Askofu Mkuu na Mfansiskani Mkapuchini na mkuu wa Kanisa la Dar Es Salaam, vile vile hakukosa pia kutoa angalisho jingine kwa UKWAKATA kwamba wao kama wanakwaya kazi yao msingi sio kutumbuiza. Kwa sababu kuna kuishawishi cha kutumbuiza. Kutokana na hilo aliomba wawasaidia wanapokuwa kwenye ibada, ili wasali nao na pamoja nao lakini sio kutumbuiza. “Msitutumbuize, tuhamasisheni tusali, tuhamasisheni tumsifu Mungu, tuhamasisheni tumtukuze Mungu na tujenge Ufalme wa Mungu kati yetu”, alisistiza Askofu Mkuu Ruaich. Pamoja na hayo, alisema kuwa wasikubali kuwa watumbuizaji na hivyo pia akawaomba wakwepe mtego wa kugeuza kwaya kuwa ni chombo cha kibiashara.
Kwa kutoa mfano, Askofu Mkuu Taddeus alisema: “siku hizi tunapata soko za kanda na vyombo mbali mbali vinavyobeba muziki, ni vizuri na, mkitengeneza album mbali mbali mtaziuza na zitatufurahisha, lakini lengo la kwanza lisiwe la kufanya biashara. Lengo lenu la kwanza kwa hiyo ni kutangaza Injili”, alisisitiza Askofu Mkuu. Kwa kuhitimisha alipenda kuwarudisha tena kwenye neno la Mtume Petro lisemalo: “Nasi tu mashahidi wake”, na aliomba umati mzima kanisani urudie kifungu hicho na kuwatakia heri za Pasaka.