Donimika ya Huruma ya Mungu: Huruma hii ni moja ya kazi tendaji ya Roho Mtakatifu anayehuisha imani ya waamini. Donimika ya Huruma ya Mungu: Huruma hii ni moja ya kazi tendaji ya Roho Mtakatifu anayehuisha imani ya waamini.   (Vatican Media)

Dominika ya Huruma ya Mungu: Mapadre ni Wahudumu wa Huruma ya Mungu

Mwenyezi Mungu ni Huruma yenyewe inayojifunua kwa wote waliotayari kuongozwa na imani na wala siyo vionjo vya milango ya fahamu. Huruma ya Mungu ni moja ya kazi tendaji ya Roho Mtakatifu anayehuisha imani ya waamini. Katika kazi tendaji zake Roho Mtakatifu anatuwezesha kuonja Huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho ambapo mitume wa Kristo wa zama zetu (Mapadre na Maaskofu) wanapewa mamlaka ya kufungua na kufungia dhambi.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli) Italia.

Mwenyezi Mungu ni Huruma yenyewe inayojifunua kwa wote waliotayari kuongozwa na imani na wala siyo vionjo vya milango ya fahamu. Huruma hii ya Mungu ni moja ya kazi tendaji ya Roho Mtakatifu anayehuisha imani ya waamini. Katika kazi tendaji zake Roho Mtakatifu anatuwezesha kuonja Huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho ambapo mitume wa Kristo wa zama zetu (Mapadre na Maaskofu) wanapewa mamlaka ya kufungua na kufungia dhambi: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.”  Huruma hii ya Mungu inaadhimishwa kwa namna ya pekee leo katika Dominika ya Huruma ya Mungu! TAFAKARI YA INJILI: Yn. 20:19-31: Injili yetu ya Dominika ya Huruma ya Mungu, Mwaka A wa Kanisa inatupatia masimulizi mawili ya Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kwake: kwanza, anawatokea mitume wengine pasipo uwepo wa Tomaso (Yn. 20:19-22) na pili, anawatokea wanafunzi wake, Tomaso akiwa pamoja nao (Yn. 20:24-29). Injili inatueleza kuwa Tomaso hakuwapo pamoja na wenzake mara ya kwanza Yesu alipowatokea wanafunzi wake. Wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wamejaribu kutafiti ni kwa nini Tomaso hakuwa na wenzake mara ya kwanza Yesu alipowatokea wanafunzi wake. Wengine wanasema: pengine alikuwa amekata tamaa baada ya kuona Yesu ameuawa na hivyo kuamua kujitoa kwenye kundi la wafuasi na kuendelea na shughuli zake au pengine alikuwa amejificha peke yake baada ya mazingira kushindwa kumruhusu kujumuika na wenzake au pengine alikuwa jasiri aliyeamua kuendelea kushuhudia imani yake kwa Kristo huko nje badala ya kuogopa na kujifungia chumbani. Haya yote ni sehemu ya utafiti tu, hakuna majibu ya moja kwa moja.

Mapadre ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu
Mapadre ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu

Katika sehemu ya kwanza ya Injili yetu (Yn. 20:19-22) tunaambiwa kuwa Mitume wamejifungia ndani ya chumba kwa hofu ya Wayahudi. Mpaka muda huu mitume wameishapata habari ya kufufuka kwa Yesu lakini wana hofu ya kutoka nje kuhofia kukamatwa na hata kuuawa na Wayahudi: wana hofu, mashaka, mahangaiko na mawazo mengi juu ya hatima ya maisha yao na ya imani yao kwa ujumla. Na mpaka sasa wamesikia habari ya ufufuko wa Yesu lakini bado hawana uhakika na habari hizo. Ni katika mazingira hayo Yesu anawatokea ghafla ndani ya chumba ilihali milango imefungwa. Yesu anawaonyesha mikono yake na ubavu wake ili kuwadhihirishia kuwa wanachoona siyo zimwi au mzuka bali ni Yeye kweli akiwa na mwili wa kibinadamu lakini uliotukuzwa (glorified body) ambao haufungwi tena na vizuizi vya kimaumbile kama kushindwa kupita mlangoni ilihali mlango umefungwa.  Maneno ya kwanza ya Yesu anapowatokea wanafunzi wake ni “Amani iwe kwenu”: anawapatia amani kwa kuwa anajua wazi hawana amani mioyoni mwao kutokana na magumu wanayopitia, hasa vitisho vya kukamatwa na kuuawa ambavyo wanapata kutoka kwa mamlaka ya kiyahudi. Hata sasa hatuna amani kwa sababu ya hofu za maisha, hivyo amani ya kweli lazima itoke kwa Kristo/Mungu: tunahitaji kumwomba Mungu atutulize kwa amani yake, amani ambayo ulimwengu hauwezi kutupatia, hasa katika mahangaiko yenu ya maisha.

Mitume wa huruma ya Mungu
Mitume wa huruma ya Mungu

Kutoka kwenye Injili ya Dominika ya Huruma ya Mungu, Mwaka A wa Kanisa tunafunuliwa yafuatayo: (1) Yesu ni Bwana na Mungu wetu. Fundisho la imani kwamba Yesu ni Mungu limepokea upinzani mkubwa hasa kutoka kwa watu wa itikadi na imani mbalimbali. Leo katika Injili yetu Tomaso pasipo shaka yoyote na kwa uwazi mbele ya Yesu anakiri kuwa Yesu ni Bwana na Mungu: “Bwana wangu na Mungu wangu.” Na kwa kuwa ndio ukweli Yesu hamkemei wala kumkosoa Tomaso kwa kumkiri kuwa Yeye ni Bwana na Mungu. Tomaso anapokiri kuwa Yesu ni Bwana na Mungu wake analenga kujiaminisha mazima mazima kwa Yesu kama Bwana na Mungu wake. Tomaso anakuwa mtume wa kwanza kukiri waziwazi kuwa Yesu ni Mungu. Tamko hili la imani siyo matokeo ya yeye kumgusa Yesu kama alivyoapa. Ni nguvu ya Mungu inayomfanya Tomaso atoke katika hali ya kutoamini na kufikia hatua ya kuamini. Tomaso anapofikia hatua ya kuamini, haamini kwa kubahatisha au kutetereka bali kwa imani thabiti. Ni kwa imani thabiti Tomaso anakiri kuwa Yesu ni Bwana na Mungu wake. Je, mimi na wewe Yesu ni nani katika maisha yetu? Je, Yesu ni Mungu wetu au tunaye mungu mwingine? Kwa bahati mbaya wengi wetu tunajiaminisha kwa miungu wengine: mali, waganga, anasa, viwango vyetu vya elimu, mipira kwenye runinga, teknolojia na mengineyo. (2) Kipimo cha imani siyo milango ya fahamu (kuona na kugusa). Siyo Tomaso peke yake aliyehitaji kuona na kugusa ili aamini. Hata wale mitume waliotokewa na Yesu wakati Tomaso hayupo nao waliamini kuwa Yesu amefufuka baada ya kuwa wamewona kwa macho yao: “…wakafurahi walipomwona Bwana.”

Sr. Maria Faustina Kowalska ni Mtume Hodari wa Huruma ya Mungu
Sr. Maria Faustina Kowalska ni Mtume Hodari wa Huruma ya Mungu

Pengine na wao wasingeamini kama wasingemwona. Kama wao wameamini baada ya kumwona mubashara, basi na yeye Tomaso alitaka amwone na kumgusa ili na yeye aamini: “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole change katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.” Imani ya Tomaso (na kwa kweli hata wale wengine) imejikita katika kuona na kusuga- ni imani ya milango ya fahamu. Tomaso anahitaji ushuhuda wa “kuona na kugusa” ili aweze kuamini. Hapa Tomaso alikumbwa na dalili ya ugonjwa uitwao “hakuna kuamini chochote mpaka nione na kugusa” maana bila kuona na kugusa hawezi kuamini. Imani ambayo haiwezi kuamini mafumbo ya imani mpaka ione na kugusa ni imani isiyo na mizizi, ni imani ambayo haijakomaa, ni imani ya ki-Tomaso. Katika ulimwengu wa leo watu wengi tunaongozwa na imani ya kuona na kugusa: tunataka tuone kwanza miujiza ndiyo tuamini uwepo na utendaji wa Mungu- bila miujiza hatuwezi kuamini. Hii ndiyo maana Wakristo wengi wanakimbilia miujiza: ati kumwamini Mungu/Kristo ni mpaka waone vipofi wanaona, viwete wanatembea, wafu wanafufuliwa, maskini wanapata pesa na mali wasizozisotea na mengineyo. Na kwa kutambua kuwa watu wanapenda imani ya kuona na kugusa ndiyo maana manabii wa uongo wanavutia watu kwa maneno matamu matamu ya kufufua watu, kufumbua macho ya vipofu na kulegeza miguu ya viwete. Hii siyo imani. Imani ni kusadiki/kuamini hata kile ambacho bado hatujakiona (rejea Ebr. 11:1).

Waamini wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu
Waamini wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu

Hii ndiyo imani ambayo Mungu anaihitaji kutoka kwetu. (3) Roho Mtakatifu ndiye anayetuhuisha na kutupa nguvu ya kuendeleza utume wake ndani yetu na kati yetu. Katika Injili ya leo tunasikia Yesu akiwavuvia Roho Mtakatifu wanafunzi wake. Kitendo cha kuwavuvia Roho Mtakatifu kina maana gani? Tukitaka kujua maana ya tendo hili ni lazima turudi katika simulizi la uumbaji ambapo Mungu aliumba mtu kwa mavumbi ya ardhi na kisha “akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” (rejea Mwa. 2:7). Neno “kuvuvia” lina maana pia ya “kupulizia.” Kama ambavyo mwanadamu alipata uhai baada ya kupuliziwa pumzi ya Mungu, ndivyo pia “Roho Mtakatifu analeta uhai (anawahuisha) kwa wanafunzi wa Yesu ambao kimsingi ni kama wamekufa kwa sababu ya hofu na woga wa kukamatwa na kuuawa na Wayahudi. Kwa maneno mengine tunapaswa kutambua kuwa ni Roho Mtakatifu anayetuhuisha kwa kutuletea uzima mpya- ni Roho Mtakatifu ambaye anatuumba mara ya pili, yaani anatuumba upya kwa kutupatia uzima wa milele. Bila nguvu ya Roho Mtakatifu tutabaki tumejifungia katika chumba cha dhambi. (4) Tukimbilie Huruma ya Mungu kwa kujongea Sakramenti ya Kitubio ambayo kwayo tunasamehewa dhambi. Katika Injili ya leo Bwana Wetu Yesu Kristo anaweka pia sakramenti ya kitubio kwa kuwapa mitume wake uwezo wa kuondoa dhambi: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Uwezo wa kuondoa dhambi waliopewa mitume ndiyo ambapo umerithishwa kwa Maaskofu na waandamizi wao, yaani Mapadre.

Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma ya Mungu.
Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma ya Mungu.

Bwana Wetu Yesu Kristo alifahamu fika kuwa mwanadamu ni dhaifu na hivyo kuna nyakati ataanguka dhambini. Hata hivyo, kuanguka dhambini siyo mwisho wa juhudi za kutafuta wokovu. Ndiyo maana Yesu anaweka Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho ambayo kwayo Huruma ya Mungu inafunguliwa kwa wadhambi wanaotubu. Leo pia ni Jumapili ya Huruma ya Mungu ambapo tunaalikwa kuikimbilia Huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Kitubio ambapo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu tunapatanishwa na Mungu. Sakramenti ya Kitubio ni Sakramenti ya Huruma. Tukiikataa kwa makusudi kabisa dhambi zetu zitaendelewa kufungiwa badala ya kuondolewa. Pia tusikubali mtu atupotoshe kuhusu Sakramenti ya Kitubio kwani Yeye Kristo Mwenyewe aliyeiweka hakuwa mjinga na pia hakuwa mjinga kuwapa watu wachache (mitume tu na sisi Mapadre ambao ni washiriki wa utume wa mitume) uwezo huo wa kuondolea watu dhambi. (5) Biblia siyo chanzo pekee cha mafundisho ya imani. Leo hii kuna watu wanataka kila fundisho la Kanisa lithibitishwe moja kwa moja kutoka kwenye Biblia. Wanasahau kuwa siyo kila jambo la kiimani limeandikwa moja kwa moja kwenye Biblia. Leo Injili inatuambia kuwa “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki.” Kwa hiyo siyo kila jambo au kila kitu kuhusu imani lazima kiwe kimeandikwa kwenye Biblia. Kwa hiyo ile kanuni ya wenzetu Waprotestanti ya “Biblia tu (Sola Scriptura)” (yaani Biblia pekee ndiyo chanzo cha mafundisho ya imani) haina mashiko. Dominika njema.

13 April 2023, 11:10