Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema Siku ya 60 ya Kuombea Miito: Kutangaza & Wongofu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika ya nne ya Pasaka ni dominika inayofahamika pia kama dominika ya Mchungaji mwema. Injili ya dominika hii huchukuliwa daima kutoka Injili ya Yohana sura ya 10, sura ambayo Yesu mwenyewe anajitambulisha kuwa ndiye Mchungaji Mwema. Katika dominika hii Kanisa huadhimisha siku ya kuombea Miito hasa miito ya Upadre na Utawa. Ni kama Kanisa linapenda kuielekeza sala yake ya miito kuomba ili hawa wanaoipokea miito hii waakisi daima mfano wa Yesu Mchungaji mwema katika kulihudumia kundi la Bwana wanalokabidhiwa kulichunga. Maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Wito: Neema na Utume.” Huu ni mwaliko wa kutafakari kwamba, watu wameumbwa, kwa upendo, kwa ajili ya upendo na kwa upendo. Mimi ni utume katika dunia hii, hiyo ndiyo sababu ya kuwepo kwangu mimi katika ulimwengu, kuwa pamoja na wengine na kwa ajili ya wengine. Tunaitwa kuwa wamoja ili kuunda jumuiya ya wamisionari mitume kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia upendo kwa ajili ya wengine kwa kutambua kwamba, neema na utume ni zawadi na dhamana. Kabla ya kuingia katika tafakari ya Injili ya dominika hii, nawaalika tuyapitie kwanza masomo mawili yanayotangulia yaani somo la kwanza kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:14a, 36-41) na somo la pili kutoka Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote (1Pet 2:20b-25).
Ufafanuzi wa Masomo: Somo la kwanza linaelezea mwitikio wa watu kwa hotuba au mahubiri ambayo Petro aliyatoa siku ya Pentekoste. Itakumbukwa kwamba ni katika siku hii ambapo Petro alijitokeza nje kwa mara ya kwanza akiwa na mitume wanzake na kuanza kuhubiri kuwa Kristo aliyeteswa, akasulubiwa na kufa sasa amefufuka kama alivyosema. Mahubiri haya ya Petro yaliwachoma watu mioyo kwa maana yaliwaonesha kuwa Kristo alikuja kwa ajili ya wokovu wao lakini wao hawakumpokea na badala yake walimuua kwa kumtundika msalabani. Petro aliwaonesha kuwa mlango wa kumpokea Kristo haujafungwa kwa kifo chake, badala yake uko wazi na wote wanaalikwa kuuingia kwa kuupokea ubatizo kwa jina lake kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Umati mkubwa ulilipokea Neno na wakabatizwa siku hiyo watu wapatao elfu tatu. Katika nafasi ya kwanza, somo hili linaonesha ule uliokuwa muundo na ukuaji wa Kanisa la mwanzo baada ya ufufuko wa Kristo. Kama tunavyoona katika mahubiri ya Petro, kiini cha utendaji wa kanisa la mwanzo kilikuwa ni kutangaza Habari Njema na kuwaalika watu kumuongokea Kristo na kubatizwa. Mitume walizunguka huku na kule kutangaza kuwa Kristo aliyeteswa na kufa sasa yu mzima na kwa njia yake wote wanaompokea kwa imani watapata wokovu. Kwetu sisi tunaolisikia Neno hili likitangazwa kwetu tunapokea mwaliko wa kuliruhusu Neno la Mungu tunalolisikia liyachokoze maisha yetu. Ni kwa kuyachokoza maisha yetu ndipo nguvu yake ya kuokoa inadhihirik ndani yetu. Bila kuliruhusu Neno la Mungu kuyachokoza na kuyachokonoa maisha yetu tutakuwa tunalisoma na kulisikiliza kama tunavyosikiliza “michapo” na kuiachia hapo hapo. Ni somo linalotualika tuikubali changamoto ya wongovu ambayo Neno la Mungu linaweka daima mbele yetu.
Tukiingia katika somo la pili, tunamsikia Mtume Petro anaelekeza mafundisho kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesukwa watu wa tabaka la chini katika mazingira ya wakati wake. Kwa kiasi kikubwa kundi hili la tabaka la chini lilikuwa ni kundi la watumwa na watumishi wa ndani ambao licha ya kuwa na kazi ngumu, walipokea pia manyanyaso mengi kutoka kwa waajiri na bwana zao. Tofauti kabisa na ambavyo huenda tungetegemea kwamba Petro awahamasishe kupindua hali mara moja au na wao kuonesha ukaidi, yeye anawafundisha kudumu katika kutenda mema na kujifunza kutoka katika kielelezo cha Kristo. Anawaonesha kuwa Kristo aliteseka bila kuwa na hatia yoyote, alipotukanwa hakujibu kwa tukano bali aliyaweka maisha yake yote mikononi mwa Mungu, hakimu mwenye haki. Mtume Petro anapotoa mafundisho ya mateso ya Kristo kwa kundi la watu ambao kwa wakati huo wanateseka, anawafanya watu hao kupata picha halisi juu ya kile ambacho Kristo mwenyewe alikipitia katika mateso yake. Kutoka katika msingi huu wa kibiblia, Kanisa halibariki utumwa, ukoloni wala unyanyasaji wa watu kwa namna yoyote ile. Linachosisitiza ni kutafuta haki, usawa na kukuza tunu za kiutu kwa njia za amani na wala si njia za mapambano au vita ambazo huishia kuongeza matatizo, chuki na uhasama kuliko hata ambao ulikuwapo awali. Amani haipatikani kwa ncha ya upanga. Amani hupatikana kwa mageuzi ya moyo.
Tafakari ya somo la Injili: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunapenda kuichota tafakari ya dominika hii kutoka katika somo la Injili, injili ambayo kama tulivyoisikia, ni ile ya Mchungaji Mwema. Yesu anaanza kwanza kuzungumzia mlango wa zizi la kondoo. Mchungaji huingia kupitia mlangoni kwa sababu anayo mamlaka hayo bali mwizi haingii kupitia mlangoni bali hukwea kwingineko. Mamlaka ya kuchunga kondoo wa Bwana, mtu hajitwalii mwenyewe, bali huitwa na kupewa na Mungu mwenyewe kupitia Kanisa lake. Mchungaji aliyeitwa na kupewa mamlaka hayo huitekeleza kazi yake si kwa jina lake yeye aliyemtuma. Mtakatifu Agostino anasema, yule anayeingia zizini kwa kuruka ukuta hatafuti kumpa Mungu utukufu kwa kazi ya uchungaji bali anajitafutia utukufu wake mwenyewe. Yesu Mchungaji mwema anaeleza pia vitu viwili vinavyomtambulisha kama mchungji na kumtofautisha na wale waliomtangulia ambao anawaita ni wevi na wanyang’anyi. Jambo la kwanza ni kwamba kondoo wake huitambua sauti yake, huwaita kwa majina nao humsikia na kumfuata. Jambo la pili ni kuwa anapowapeleka machungani, hawatangulizi kondoo yeye akibaki nyuma bali hutangulia mbele yeye na kondoo wake humfuata. Mambo haya mawili yanatuambia nini sisi leo? Jambo la kwanza linatuambia kuwa Yesu hujenga uhusiano wa pekee na kila mmoja wetu.
Katika imani, katika Kanisa, na katika ufuasi wetu wote, Yesu hatuangalii kama kundi wala hahusiani na sisi kama kundi bali huhusiana na kila mmoja wetu kwa jinsi alivyo, kwa hali aliyonayo na kwa hatua aliyofikia katika makuzi ya imani. Ndiyo maana anaita kondoo wake kwa jina, akilenga daima kujenga na kukuza mahusiano hayo binafsi na kila mmoja wetu. Jambo la pili ni kwamba yeye kama mchungaji wetu hututangulia mbele kututayarishia njia ya kupita. Na huu ndio msingi wa wito. Anayekuita hakuiti akiwa hajatayarisha njia utakayopitia ili umfikie. Tunakumbua wito wa nabii Yeremia, Mungu alimwambia “kabla hujaumba nalikujua, ungali tumboni mwa mama nalikutakasa...” Maana yake ni kuwa Mungu alikuwa mblele yake daima na njia yake alikuwa tayari amekwishaiandaa. Yesu mchungji mwema anapotuita tumfuate katika ukristo, anapotuita tumfuate katika utumishi, ni yeye anayetangulia mbele akitutayarishia njia ya kupita ili tuukeleze utume anaotuitia. Hii pia ni mialiko miwili ambayo Kanisa linatupatika wachungaji katika dominika hii ya miito. Yeye anayeitikia wito wa kuwa mchungaji ajenge ukaribu na kundi analokabidhiwa. Yeye anayeitikia wito wa uchugaji awe msari wa mbele kuliongoza kundi. Ni wazi hataliongoza kwa sababu ya ukamilifu wake bali ataliongoza akiwa mfano wa kuutafuta ukamilifu huo kama kielelezo cha bidii ya kitume na juhudi ya kuamka pale uzito wa binafsi na ule wa utume vinapomwelemea. Kristo Mchungaji mwema wa roho zetu atupe neema na nguvu za kumfuata ili atufikishe kwenye uzima.