Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Wito: Neema na Utume.” Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Wito: Neema na Utume.”   (AFP or licensors)

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Wito: Neema na Utume.” Liturujia ya Neno la Mungu inakazia hasa toba na wongofu wa ndani. Mateso ambayo Wakristo wanakumbana nayo yana faida kwa ajili ya wokovu wa roho zao na kwamba, Kristo Yesu ndiye Mchungaji mwema na mlango wa kuwawezesha waamini kuingia mbinguni; anawatambua kondoo wake kwa majina!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli), Italia

Maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Wito: Neema na Utume.” Huu ni mwaliko wa kutafakari kwamba, watu wameumbwa, wa upendo, kwa ajili ya upendo na kwa upendo. Mimi ni utume katika dunia hii, hiyo ndiyo sababu ya kuwepo kwangu mimi katika ulimwengu, kuwa pamoja na wengine na kwa ajili ya wengine. Tunaitwa kuwa wamoja ili kuunda jumuiya ya wamisionari mitume kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia upendo kwa ajili ya wengine kwa kutambua kwamba, neema na utume ni zawadi na dhamana. Habari Njema ya Kristo tunayohubiriwa inatudai “kutubu” yaani kufanya mabadiliko ya dhati katika mwenendo wetu wa maisha, ndiyo “metanoia.” Mabadiliko haya yatawezekana ikiwa tutakuwa tayari kumfuata Kristo Mchungaji Mwema na kuitikia sauti yake ili tuweze kuongozwa katika uzima wa milele. Kristo Mchungaji Mwema ndiye mlango ambao sisi kondoo tunaweza kupita kuingia mbinguni. Hakuna mlango mwingine! Karibu mpenzi msomaji na msikilizaji wa Vatican News katika Tafakari ya Masomo ya Dominika ya Nne ya Pasaka, ambayo Mama Kanisa Mtakatifu sana anadhimisha Dominika ya Kristo Mchungaji Mwema.

Kristo Yesu Ni Mlango wa Kondoo wake
Kristo Yesu Ni Mlango wa Kondoo wake

Tuanze kwa kulitazama SOMO LA KWANZA linalotoka kitabu cha Matendo ya Mitume 2:14a, 36-41. Somo hili la kwanza ni sehemu ya hotuba ya Petro siku ya Pentekoste mara baada ya Mitume kushukiwa na Roho Mtakatifu na hivyo kuimarishwa katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Leo Petro anahuburi kwa ujasiri juu ya Yesu aliyesulibishwa: anatangaza wazi wazi kuwa Yesu ni Kristo na Bwana. Habari hii njema inawafanya watu wanaomsikiliza Petro “kuchomwa mioyo” yaani mahubiri ya Petro yanapenya ndani ya mioyo yao na wanaamua kuongoka na hivyo wanamuuliza Petro na mitume wengine, “Tutendeje, ndugu zetu?” – yaani wanauliza “Tufanye nini sasa?” Petro akawajibu, “Tubuni mkabatizwe…” Kwa Kigiriki neno “toba” linalotokana na kitendo “tubu” lililozaa neno “metanoia” - lenye maana ya mabadiliko ya uelekeo, mabadiliko ya moyo au mabadiliko katika mtazamo. Hivyo Petro anawaalika wasikilizaji wake kufanya mabadiliko ya uelekeo/njia- yaani kutoka njia ya dhambi kwenda njia ya mema. Lengo la Injili ni kutufanya tubadili uelekeo wa maisha yetu kutoka mwenendo mbaya wa maisha na kugeukia mwenendo mwema wa maisha kwa ajili ya kupata wokovu. Je, mimi na wewe “tumetubu” (tumefanya metanoia)? Kwa bahati mbaya wengi wetu tunahubiriwa Injili kila uchao lakini hatutaki kubadilika: ukristo wetu kwa sehemu kubwa ni wa kanisani tu na wala siyo wa kwenye maisha yetu ya kila siku. Tumebaki vile vile kama jiwe ambalo lipo katikati ya maji ziwani lakini ukilipasua ndani ni kavu kabisa, halina hata tone la maji. Tufanye “metanoia” - mabadiliko ya mwenendo wa maisha. Kadhalika katika hotuba yake, Petro ameeleza teolojia ya ubatizo (umuhimu wa ubatizo): ni kwa njia ya ubatizo tunapata ondoleo la dhambi na ni kwa njia ya ubatizo tunampokea Roho Mtakatifu. Hivyo mwamini anampokea Roho Mtakatifu kwa mara ya kwanza wakati wa ubatizo.

Toba na Wongofu wa ndani ni chanzo cha maisha mapya
Toba na Wongofu wa ndani ni chanzo cha maisha mapya

SOMO LA PILI: 1 Pet. 2:20b-25: Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote kwa asili uliwalenga Wakristo ambao hapo awali walikuwa watu wa Mataifa (yaani hawakuwa Wayahudi kwa asili). Nia kubwa ya waraka huu ulikuwa ni kuimarisha imani ya Wakristo hao ambao kwa wakati huo walikuwa wakiteswa na hata kuuawa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo. Katika somo la pili leo, Petro anawahimiza Wakristo waamini kuwa wastahimilivu (wawe mavumilivu) wanapokabiliana na mateso kwa ajili ya imani. Hoja ya Mtume Petro ni hii: Kwa kuwa Kristo alivumilia mateso makali bila kukwepa au kukata tamaa, kadhalika Wakristo nao wanapaswa kuvumilia mateso maana Kristo amewapa kielelezo. Na kwa kuwa mateso ya Kristo hayakuwa kazi bure, kadhalika mateso wanayokumbana nayo yana faida kwa wokovu wa roho zao. Kutoka kwenye somo la pili tunajifunza kuwa: (1) Mateso tunayopitia yana faida na hivyo tuyavumilie kama Kristo alivyovumilia. Bwana wetu Yesu Kristo hakuwepa mateso wala hakupambana na watesi wake bali alivumilia mateso ili mwanadamu apate kuponywa na kurudishwa katika njia ya wokovu. Hata sisi Wakristo wa zama hizi tunakabiliwa na changamoto mbalimbali: magonjwa, kuna Wakristo wenzetu wanauawa kwa sababu ya kuwa Wakristo, kuna wengine wananyimwa haki zao kama Wakristo, kuna wengine wanatengwa na ndugu zao kwa sababu ya ukristo, tunasononeshwa na misiba ya wapendwa wetu, tunateseka kwa ugumu wa maisha, hatuna amani katika ndoa zetu, tunafanya utume katika mazingira magumu na mengineyo.

Ni Siku ya 60 ya Kuombea Miito Mbalimbali ndani ya Kanisa
Ni Siku ya 60 ya Kuombea Miito Mbalimbali ndani ya Kanisa

Haya yote hayapaswi kutukatisha tamaa na hata kufikia hatua ya kumkufuru Mungu au kufikiri kuwa Mungu ametuacha. Tunapaswa kuwa wastahimilivu (wavumilivu) maana sisi siyo wa kwanza kuteseka- Kristo ambaye ni Mungu-Mtu naye aliteseka lakini alivumilia mpaka mwisho: Kristo alitukanwa, kuteswa msalabani na hatimaye kuuawa. Daima tusiyatazame mateso kwa mtazamo hasi bali tuyatazame mateso kwa mtazamo chanya. Mungu anaruhusu tuteseke ili kutuimarisha kiimani, kuturudisha katika njia sahihi, kutakasa roho zetu na kutukumbusha uwepo wake. Mungu pia anaruhusu tuteseke akifahamu kuwa mateso yetu yaweza kuwa njia ya wokovu kwa mtu mwingine. Somo hili linatufundisha kuwa (2) Tunapaswa kujikabidhi kwa Mungu nyakati za mateso. Kipindi chote cha mateso Bwana Wetu Yesu Kristo alijiaminisha kwa Mungu. Somo linatuambia kuwa, “Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki [yaani kwa Mungu].” Kujikabidhi kwa Mungu maana yake ni kujisalimisha, kujiweka na kujiaminisha kwa Mungu. Kwa maneno mengine ni kujiweka chini ya maongozi na mapenzi ya Mungu. Je, mimi na wewe tunajikabidhi kwa Mungu nyakati tunapokabiliwa na mateso, taabu, adha na changamoto za maisha na imani? Wengi wetu tunaposongwa na mateso na adha mbalimbali tunaacha kujikabidhi kwa Mungu na badala yake tunajikabidhi kwa waganga, kwa wachungaji wa uwongo (ambao ni wevi na wanyang’anyi), kwa vitulizo vya muda tu (ulevi wa pombe ili kusahau matatizo, michepuko) na mengineyo. Hilo silo suluhisho. Suluhisho ni kujikabidhi kwa Mungu ambaye ni Muweza na Suluhisho la yote. Tuwapo katika mateso sala yetu kwa Mungu iwe fupi tu: FIAT (neno la kilatini lenye maana ya “Mapenzi yako yatimizwe”) - Let it be done.

Kristo Yesu ni Mchungaji mwema walio wake wanaisikia sauti yake.
Kristo Yesu ni Mchungaji mwema walio wake wanaisikia sauti yake.

SOMO LA INJILI linatoka Yn. 10:1-10: Katika somo letu la Injili tunafunuliwa kuwa “Kristo Mchungaji Mwema ni mlango wa kutuwezesha kuingia mbinguni.” Kwa kawaida Yesu alipenda kutumia mifano mbalimbali ambayo iliakisi mazingira na tamaduni za kiyahudi. Kwa sehemu kubwa Wayahudi walikuwa ni wakulima na wafugaji, ndio maana mifano mingi ya Yesu inahusu wakulima na wafugaji. Leo Yesu anatumia mfano kutoka nyanja ya ufugaji kwa kujibainisha kuwa “Yeye ni mchungaji na pia ni mlango wa kondoo.” Ili kuelewa mfano wa Yesu ni vizuri tuangalie shughuli nzima ya ufugaji na wafugaji wenyewe kwa mazingira ya Wayahudi: (i) Kwa kawaida mifugo ya kijiji kizima ilikaa kwenye zizi moja (ii) kulikuwa na desturi ya wachungaji kuipa majina mifugo yao, desturi ambayo hata kwa mazingira yetu bado ipo, (iii) mchungaji wa Kiyahudi alitangulia mbele ya kundi lake ili ikitokea hatari (mfano mnyama mkali) kwa mbele awe tayari kupambana nayo kabla haijawadhuru kondoo wake. Kwa hiyo ilipofika wakati wa kwenda kuwachunga kondoo (ama asubuhi au jioni), wachungaji wote wa kijiji kizima walifika kwenye zizi ambalo mifugo yote ya kijiji inawekwa na kila mmoja alianza kuchambua kondoo wake kwa kuwaita kwa majina, nao wanamfuata. Kitendo cha mchungaji kuwaita na kuwatambua kondoo wake kwa majina kinaonesha kuwa mchungaji anawajua kondoo wake kwa namna ya upekee kabisa, ana ukaribu na urafiki nao (familiarity and intimacy). Ni kwa sababu ya ukaribu huo kati ya mchungaji na kondoo, kondoo nao wanaijua sauti ya mchungaji wao. Kuna msemo usemao kuwa “daima mchungaji hunukia harufu ya kondoo wake.” Ni katika picha hii ya wafugaji wa Kiyahudi Yesu anaeleza sifa za mchungaji mzuri na sifa za kondoo wazuri: mchungaji mwema (i) anawajua kondoo wake kwa majina (ana ukaribu nao wa kipekee), (ii) anawatangulia kondoo kwa mbele kuwaongoza njia na kuwalinda na hatari (hakai nyuma ya kondoo kama wachungaji wa zama zetu), (iii) ni mchungaji halali (anafuata utaratibu- hapitii njia za panya kuingia kwenye zizi); Kwa upande wa sifa za kondoo wazuri: (i) husikia sauti ya mchungaji wao (ii) humfuata mchungaji wao (iii) humkimbia mchungaji wasiyemjua, yaani mchungaji asiye na sifa za mchungaji mwema.

Kristo Yesu ni Mchungaji mwema
Kristo Yesu ni Mchungaji mwema

Kwa kutumia mfano wa mchungaji, Yesu anajibainisha kama “Mchungaji Mwema.” (1) Yesu Kristo anatujua kwa namna ya pekee (kwa majina) sisi ambao ni kondoo wake. Kila mmoja wetu asingependa kuitwa “wewe” ilihali huyo anayemuita anafahamu jina lake. Mtu anapokuita kwa jina lako anaonesha kukuheshimu na kukuthamini, anaonesha kuthamini utu wako, anaonesha upekee wako, anaonesha kukujua, anaonesha ukaribu nawe. Hivyo, Kristo Mchungaji Mwema anatujua kwa namna ya pekee sisi kondoo wake: anajua hulka na tabia zetu, anajua mahangaiko yetu, anajua madhaifu na mazuri yetu. Katika hali hili zote bado Kristo yupo tayari kutuita kila mmoja kwa jina lake ili kutupandisha hadhi ya kuwa wana wa Mungu ikiwa tutatambua kuwa daima Mungu yu karibu nasi- Mungu anatupenda sana licha ya hulka yetu ya dhambi. Kristo yu tayari kutuongoza kwenye malisho ya uzima wa milele ikiwa tutaisikia sauti yake ya kuifuata. (2) Kadhalika Kristo Mchungaji Mwema anaongoza maisha yetu. Yesu ametuambia kuwa mchungaji mwema huwatangulia kondoo wake: kutangulia kundi na kuwa mbele yake ni ishara ya kuwaongoza njia. Sisi ambao ni kondoo wa Kristo tunapaswa kuongozwa na Kristo. Sisi tuwe nyuma na Kristo awe mbele yetu. Je, mimi na wewe tunaongozwa na nani? Wengi wetu tunaongozwa na kutanguliwa na mitandao ya kijamii, mali, biashara zetu, wake/waume zetu, wazazi wetu kiasi kwamba nafasi ya Kristo katika maisha yetu inafifishwa. Kristo Mchungaji Mwema yupo tayari kutuongoza katika safari hii ya wokovu, hivyo nasi tunapaswa kuwa tayari kuongozwa naye. Mawazo yetu, mipango, harakati na maisha yetu kwa ujumla vinapaswa kuongozwa na Kristo. (3) Kristo Mchungaji Mwema ni njia ya kuingia mbinguni (njia ya wokovu).

Kristo Yesu ni Mlango wa Kondoo wake.
Kristo Yesu ni Mlango wa Kondoo wake.

Yesu pia amejifunua kwetu kama “mlango wa kondoo.” Tunafahamu kazi ya mlango. Kazi ya mlango ni kuwawezesha watu (na hata wanyama) kuingia ndani ya jengo au zizi. Yesu anajifunua kuwa Yeye ni mlango wa kondoo- “kondoo wataweza tu kuingia kwenye zizi kupitia mlango”. Sisi ni kondoo na mlango wetu ni Kristo. Yesu anamaanisha kuwa hatuwezi kuingia mbinguni bila kupitia Yeye ambaye ni njia ya kupata uzima wa milele. Kristo ndiyo mlango wetu wa kuingia mbinguni. Kwa bahati mbaya wengi wetu tumemkataa Kristo kama njia ya wokovu. Wengi tumechagua njia tofauti: wengine tumemchagua Ibilisi na fahari zake kama njia yetu ya maisha, wengine tumechagua waganga, wengine tumechagua mila na desturi zinazopingana na ukristo, wengine tumechagua kuwafuata manabii wa uongo ambao ni “wevi na wanyang’anyi.” (4) Kristo Mchungaji Mwema anatualika kuisikia sauti yake na kuifuata. Kondoo wazuri ni wale wanaoisikia na kuifuata sauti ya mchungaji wao. Sisi ni kondoo na mchungaji wetu ni Kristo. Sisi tulio kondoo tunapaswa kuisikia sauti ya mchungaji wetu. Sauti ya Kristo i wapi? Sauti ya Kristo i katika Neno la Mungu, sauti ya Kristo i katika amri na maagizo yake, sauti ya Kristo i katika sakramenti zake, sauti ya Kristo i katika sala na ibada mbalimbali, sauti ya Kristo i katika kujibu mahitaji ya wanyonge, maskini na wahitaji, sauti ya Kristo i katika kufuata dhamiri njema na iliyo hai. Je, mimi na wewe tunaisikia sauti ya Kristo? Kwa bahati mbaya wetu hatupendi kusikia sauti ya Kristo na badala yake tunasikia sauti na kelele za malimwengu ambazo mara nyingi hututenga na Kristo mchungaji wetu. Tumuombe Mungu atujalie neema ya kumtambua Kristo Mchungaji Mwema na kumfuata, huku tukisali na kuombea Miito Mitakatifu katika Kanisa: Ndoa Takatifu, Upadre na Utawa. Dominika Njema.

27 April 2023, 11:24