IJUMAA KUU: Wokovu wa Binadamu Umetundikwa Juu ya Msalaba
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Msalaba: Ishara na alama ya ushindi: I. Isa. 52:13-53:12; II. Ebr 4:14-16; 5: 7-9; III. Yn. 18:1-19, 42. Tafakari ya Neno la Mungu, siku ya Ijumaa Kuu. Ni siku ya kukaa kimya, kuzama ndani ya mtima wa mioyo yetu, tukitafakari mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo kilichotuletea wokovu kama inavyoashiria sala ya mwanzo anavyosali Padre kwa niaba ya waamini ikisema; “Ee Mungu, kwa mateso ya Kristo Mwanao Bwana wetu, umetuondolea mauti tuliyorithi sisi binadamu wote kwa dhambi ya kale. Utujalie sisi tuliozaliwa na hali ya kibinadamu kwa maumbile, vivyo hivyo tuzaliwe na hali ya kimungu kwa kutakaswa na neema yake.” Siku hii ya Ijumaa Kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu kwa sababu ni siku ambapo Yesu mwenyewe alijitoa Sadaka msalabani. Hali kadhalika, siku ya Jumamosi Kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu, liko kimya likiyawaza-waza mateso na kifo cha Yesu, Meza Takatifu, Altare ya Bwana ikiwa tupu, mpaka zitakapoanza sherehe za Pasaka baada ya Kesha Takatifu au Kesha la ufufuko. Hapo tena sherehe zitaendelea muda wa siku hamsini. Ibada tunayoiadhimishwa siku ya Ijumaa Kuu imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni Liturujia ya Neno kiini chake ni simulizi la mateso ya Yesu ambayo inamalizika kwa maombezi kwa watu wote. Sehemu ya pili ni Kuuabudu wokovu wa dunia uliotundikwa Msalabani, ndiye Yesu Kristo. Na sehemu ya tatu ni ibada ya Komunyo Takatifu.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:13-53:12). Sehemu ya somo hili ni tafakari ya wasifu wa mtumishi wa Mungu aliyetuokoa kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mateso; uso wake uliharibiwa sana, hakuwa na umbo wala uzuri wa kumtamani, alidharauliwa na kukataliwa na watu wake, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko, hakuhesabiwa kuwa kitu, lakini ndiye aliyeyachukua masikitiko yetu, akajitwika huzuni zetu, alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu, adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Bwana aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, hakufunua kinywa chake mbele ya watesi wake, kwa kuonewa na kuhukumiwa, akapigwa kwa sababu ya makosa yetu, akafanyiwa kaburi pamoja na wabaya. Ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake; Bwana aliridhia kumchukua amehuzunisha, akaifanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi zetu. Kwa haki yake akawafanya wengi kuwa wenye haki kwa kuyachukua maovu yetu kwa kumwaga nafsi yake hata kufa ili kutukomboa sisi wakosaji. Tumlipe nini kwa mateso hayo sababu ya dhambi zetu? Hatuna chochote cha kutoa na kutosha kama fidia isipokuwa kujinyenyekeza kwake kwa moyo wa toba na majuto kumuomba msamaha na kuzitupilia mbali dhambi zetu na kuanza maisha mapya ya kiroho, tukiishi kwa kupendana na kusaidia kidugu. Somo la pili la waraka kwa Waebrania (Ebr 4:14-16; 5: 7-9); linatuasa tumwamini Yesu Kristo kuhani wetu mkuu aliyeonja na kuvumilia taabu na mateso mengi kwa ajili yetu, maana yeye anafahamu taabu na matatizo yetu, daima yupo tayari kutuombea kwa Baba. Sharti ni hili; kuyashike maangano yetu tuliyofanya naye. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji yetu kwa njia yake yeye aliye Wokovu wetu.
Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 18:1-19, 42); inasimulia Yuda kumsaliti Yesu kwa busu na hivyo kukamatwa na maaskari wakiwa na taa mienge na silaha (Yn. 18:3) akiwa katika bustani ya mizeituni. Baada ya kukamatwa, Yesu alipelekwa kwa kuhani mkuu Kayafa, mkuu wa baraza la wayahudi, “Sanhedri”, chombo chenye mamlaka ya juu ya kidini (Yn. 18:12-14); baraza likaamuru apelekwe kwa gavana wa Kirumi - Pontio Pilato - naye akaamuru apelekwe kwa mkuu wa mkoa wa Galilaya - Herode Antipas - kwa vile Yesu alikuwa mwenyeji wa Nazareti katika Galilaya (Yn.18:28ff). Mahangaiko haya yote ni kwasababu kila mamlaka haikuona hatia yoyote juu yake. Lakini akamhukumiwa hukumu isiyo haki na kufanyiwa dhihaka nyingi na kuteswa sana: akapigwa mijeledi, akavikwa taji ya miiba, akapigwa kwa mwanzi, akatemewa mate, akabebeshwa Msalaba mzito, akavuliwa nguo, akasulubiwa msalabani, akafa, nchi ikatetemeka, jua likafifia, kukawa na giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, naye askari mmoja wapo akamtoboa ubavu kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji, chemchemi za Sakramenti za Kanisa. Kristo alishtakiwa kwa makosa matatu ya kidini ambayo adhabu yake ilikuwa ni kifo. Kwanza ni kulidhihaki hekalu la Yerusalemu, mahali patakatifu pa Mungu ambapo Wakuu wa Makuhani na kuhani mkuu pamoja na watu wa kabila la Yuda waliishi kwa kulitegemea kwa mahitaji yao kwa kupokea zaka na sadaka, akidai walivunje naye atalisimamisha kwa siku tatu (Yn. 2:19). Pili alijiita Masiha naye hakuwa na sifa za masiha waliyemngojea - mtu shupavu na shujaa wa kivita, mwenye uwezo wa kuwatoa mikononi mwa utawala wa Kirumi. Hivyo walimwona ni mzushi na adhabu yake ni kifo. Tatu alijiita mwana wa Mungu (Yn. 5:16), hivyo alikufuru. Adhabu ya kukufuru ni kifo kwani hakuna mtu anayeweza kujifananisha na Mungu. Mashtaka haya yote ni ya uongo, kwani kweli Yesu ni mwana wa Mungu hata akida aliyeshuhudia kifo chake anakiri wazi – “Hakika mtu huyu alikuwa mwana wa Mungu”, Yeye ni masiha na hekalu walilolivunja alilisimamisha kwa siku tatu ndilo mwili wake (Yn. 2:21).
Kwa makosa haya kadiri ya sheria ya Kiyahudi Yesu alistahili adhabu ya kifo. Lakini kwa kuwa wayahudi walikuwa chini ya utawala wa kirumi, hawakuruhusiwa kutoa adhabu ya kifo (Yn.18:31) na kwa sheria za kirumi makosa ya kidini hayakuwa makosa ya kutoa hukumu ya kifo. Hivyo walilazimika kutunga makosa mengine ya uongo matatu ambayo ni ya kisiasa/uhaini. Kosa la kwanza ni kujiita na kujifanya mfalme hivyo kumpinga Kaisari, na kuchezea mamlaka ya serikali, adhabu ni kifo. Kosa la pili ni kukataza watu kulipa kodi hivyo kupinga maendeleo ya kitaifa. Na kosa la tatu ni kuchochea migomo. Ili kumshitaki Yesu kwa kosa la kuchochea mgomo, watu waukatae utawala wa Kirumi walisema anatoka Nazareth, mji wa Galilaya ambao watu wake walijulikana kwa upinzani, fujo na wanamapinduzi. Katika mji huu waliishi watu mchanganyiko wapagani – watu kutoka mataifa mengine na Wayahudi. Yesu anaitwa Mnazareti sio kwa kuzaliwa bali kwasababu alikulia katika mji wa Nazareth. Yeye alizaliwa Bethlehemu katika mji wa Daudi ili kuthihirisha kuwa anatoka katika ukoo wa Daudi. Kwa makosa yote haya Yesu hakuwa na hatia, maana hata yeye alilipa kodi alipomwambia Petro aende ziwani, na samaki wa kwanza atakayemshika achukue humu shekeli akalipe kodi kwa ajili yake na yeye pia. Hata walipomuuliza swali kama ni halali kutoa kodi au la, jibu lake lilikuwa wazi – “Ya Kaisari mpeni Kaizari na ya Mungu mpeni Mungu”. Yuda anashuhudia; “Nimekosa nilipoisaliti damu isiyo na kosa.” Akarudisha vipande 30 vya pesa kwa wakuu wa Makuhani. Pilato naye anasema: “Mimi sioni kosa la mtu huyu”. Kwa uwoga anamtoa Yesu ateswe akisema; “Mimi sina hatia juu ya kifo cha mtu huyu” (Yn.18:38; 19:4). Kumbe ni dhambi zetu ndizo zilizomsulubisha na zinaendelea kumsulubisha Yesu. Hatuna budi kuutazama msalaba kwa moyo wa toba na majuto, kuomba msamaha na kuanza maisha mapya ya kumpendeza Mungu.
Sehemu ya pili ya Liturujia ya Ijumaa Kuu ni ibada ya “kuabudu Msalaba”, yaani kuuabudu wokovu wetu ndiye Yesu Kristo aliyetundikwa juu yake. Msalaba ulitumiwa na Warumi tangu zamani kabla ya Yesu kwa kutoa adhabu ili kukomesha uhalifu, wizi, ujangili, ujambazi, uhaini au uasi. Mtu aliyefanya makosa haya aliteswa sana na baadae kusulibiwa msalabani na kuachwa hapo mpaka afe. Kwa Wayahudi adhabu hii pia ilitumika kama tunavyosoma katika kitabu cha kumbukumbu la Torati; “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utauzika siku hiyohiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; asije akatia najisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako iwe urithi wako” (Kum.21:22-23). Kwetu sisi Msalaba si tena alama ya adhabu bali ya wokovu. Msalaba ni bendera na bango la ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Msalaba ni alama ya ukombozi (Yn.12:13-33), msalaba ni alama ya upendo wa Kristo kwetu sisi wadhambi (Yn.3:14-18). Msalaba ni alama ya maisha ya kikristo (Mk.8:34). Msalaba ni alama ya umoja na Kristo. Msalaba ni alama ya ufuasi wa kweli wa Yesu Kristo (Mk 8: 34). Msalaba ni sadaka ya Yesu, ni zao la upendo (Yn 13:1; 15: 13). Ni kwa njia ya msalaba tumekombolewa. Je, ni mara ngapi tumeukana na kuutupilia mbali msalaba? Jogoo amekwisha wika mara ya tatu tunaalikwa kujirudi na kujiweka chini ya msalaba kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, tuutazame basi msalaba kwa imani kuu na moyo wa toba.
Katika simulizi la mateso ya Yesu, Baraba anaachwa huru na Yesu kusulibiwa. Huku kuachwa huru kwa Baraba kuna maana kubwa sana. Baraba alikuwa mdhambi. Kuachwa kwake huru ili Yesu auawe ni kudhihirisha kuwa kifo cha Yesu kinawaweka huru wale wote walio katika vifungo vya dhambi watakaomwamini. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema; “Msalaba siyo ishara ya kifo, bali uzima; siyo jambo la kutuvunja moyo, bali matumaini; siyo ishara ya kushindwa, bali ya ushindi”. Nasi hatuna shaka yoyote kuinama, kupiga magoti na kuubusu msalaba ambao juu yake ametundikwa Wokovu wetu, Yesu Kristo, Nafsi ya Pili ya Utatu Mtakatifu, Mungu halisi anayestahili kuabudiwa ndiyo maana mwaliko wa ibada hii unasema: “Huu ndio mti wa Msalaba ambao Wokovu wa dunia umetundikwa juu yake, njoni, njoni, njoni tuuabudu”. Mwenye macho ya imani anaukaribia msalaba, kwa unyenyekevu, kwa utulivu, na kwa moyo wa majuto na toba, na kwa moyo wa ibada na shukurani kwa makuu aliyotufanyia Yesu Kristo, kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti.Katika ibada hii kimsingi tunachoabudu sio msalaba bali ni wokovu wetu uliotundukwa juu yake. Sio ibada ya kuabudu sanamu. Maana ili ibada iwe kweli ni ibada ya kuabudu sanamu ni lazima kuwepo na mambo mawili muhimu: Kwanza kabisa ni nia kamili ya kuabudu sanamu na makusudi ya ndani moyoni ya kwamba hiyo sanamu ichukue nafasi ya Mungu.
Pili ni lazima kuwe na ibada ya dhati ya kuabudu sanamu inayoambatana na matendo mbalimbali kama vile: kuzitolea sadaka za kuteketezwa (Hos. 4:13) au nafaka, vyakula na vinywaji (2Fal. 5:17); kuzifukizia ubani (1Fal. 11:8; Yer. 7:18); kuzimwagia matambiko (Isa. 57:6); kuzitolea sehemu ya kumi ya mapato ya mwaka (Hos. 2:8); kuziandikia meza mbele yao (Isa. 65:11); kuzibusu na kuzisujudia (1Fal. 19:18; Hos. 13:2); kuziinulia mikono katika kuzisujudia (Isa. 44:20); kuziangukia kifudifudi; na kuzichezea ngoma na wakati mwingine kujikatakata kwa visu kama tendo la ibada kwa sanamu (1Fal. 18:26, 28) pamoja na matendo mengine ya giza. Haya yote Kanisa halitualiki kuyafanya, bali linatuelekeza kumwabudu Mungu wa kweli kupitia kwa Yesu Kristo, wokovu wetu aliyetundikwa msalabani. Basi, kama mtume Paulo nasi tuone fahari kwa msalaba wa Yesu Kristo (Gal. 6:14). Kristo yupo anatuona hadi moyoni. Wakati wa kumwabudu, tujongee mbele zake tukimwomba atusamehe dhambi zetu na kumwahidi kwamba sasa tunaachana na dhambi na tupo tayari kumwamini yeye tu. Tumwombe atuondolee udhaifu wetu ili tuwe kweli wafuasi wake waaminifu. Tumsifu Yesu Kristo.