Tafuta

Hali ya Yesu aliyekufa ni Fumbo la Kaburi na kushuka kuzimu. Hili ndilo Fumbo la Jumamosi kuu au kama inavyojulikana na wengine, Jumamosi kuu, kipindi cha matumaini ya ufufuko kwa wafu. Hali ya Yesu aliyekufa ni Fumbo la Kaburi na kushuka kuzimu. Hili ndilo Fumbo la Jumamosi kuu au kama inavyojulikana na wengine, Jumamosi kuu, kipindi cha matumaini ya ufufuko kwa wafu.  (Vatican Media)

Mkesha wa Jumamosi Kuu: Historia ya Fumbo la Wokovu: Ufufuko na Uzima wa Milele

Mwenyezi Mungu katika mpango wake wa wokovu, alipanga kwamba, Mwanawe afe si tu kwa ajili ya dhambi zetu bali pia aonje mauti, ili apate mang’amuzi ya hali ya kifo, mtengano wa roho yake kutoka mwili wake kati ya muda ule alipokufa Msalabani na muda ule alipofufuka. Hali ya Yesu aliyekufa ni Fumbo la Kaburi na kushuka kuzimu. Hili ndilo Fumbo la Jumamosi kuu pale Kristo Yesu akilala kaburini anafunua pumziko kuu la Mungu la Sabato kutimiliza wokovu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu na Fumbo la Wokovu wetu katika kesha la Pasaka, Mama ya mikesha yote. Mwenyezi Mungu katika mpango wake wa wokovu, alipanga kwamba, Mwanawe asife tu kwa ajili ya dhambi zetu bali pia aonje mauti, ili apate mang’amuzi ya hali ya kifo, mtengano wa roho yake kutoka mwili wake kati ya muda ule alipokufa Msalabani na muda ule alipofufuka. Hali ya Yesu aliyekufa ni Fumbo la Kaburi na kushuka kuzimu. Hili ndilo Fumbo la Jumamosi kuu au kama inavyojulikana na wengine, Jumamosi kuu, pale Kristo Yesu akilala kaburini anafunua pumziko kuu la Mungu la Sabato kutimiliza wokovu wa watu, ambao unauletea ulimwengu wote amani. Rej. KKK 624-730. Liturujia ya kesha la Pasaka imepambwa na maneno ya matumaini yenye kiitikio cha neno “Aleluya” tunaloanza kulitumia katika wimbo wa katikati baada ya somo la nane, yaani somo la kwanza katika masomo ya Agano Jipya (Rum 6:3-11). Neno Aleluya ni muunganiko wa maneno mawili “Hallelu” – msifuni na “Yah” – kifupisho cha Yahweh –yaani Bwana/Mungu, maana yake ni “msifuni Bwana”/ “msifuni Mungu”, kama wimbo wa katikati unavyoanza na maneno “Aleluya mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema” (Zab. 118:1-2, 16-17, 22-23). Ndiyo kusema “Msifuni Bwana, mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema! Itakumbukwa kuwa neno “Aleluya” hatukulitamka kabisa kipindi chote cha kwaresima! Kristo amefufuka kweli kutoka wafu na tushangilie, Aleluya! Ameshinda dhambi na mauti, Aleluya! Ametustahilia uzima mpya wa milele rohoni mwetu, Aleluya! Tufurahi na kushangilia kwa sababu tumekombolewa kwa damu ya Yesu Kristo Msalabani Aleluya! Ni kweli, na ni jambo la hakika kabisa kwamba Yesu Kristo ameshinda dhambi na mauti. Wokovu na ukombozi wa mwanadamu umetimia kwa hakika.

Kesha la Pasaka ni Mama wa mikesha yote.
Kesha la Pasaka ni Mama wa mikesha yote.

Ni kweli, Yesu amefufuka kutoka wafu, Yesu sasa ni mzima kabisa na hili ndilo tukio tunalosherekea usiku wa Pasaka tukiimba Aleluya tushangilie, aleluya tushangilie. Ambaye hafurahi, haimbi wala hashangilii katika sikukuu hii ya Pasaka ni mwana wa Ibilisi kwani wana wa Mungu wote wanashangilia na kuimba Aleluya! Maanake wanaimba, “Msifuni Bwana”. Kesha hili la usiku wa Pasaka limegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ya ni Liturujia ya Mwanga. Katika Liturujia hii, Kanisa linatafakari maajabu ya Mungu aliyolifanyia taifa lake tangu mwanzo kwa kubariki moto na kuutayarisha mshumaa wa Pasaka, tukimwomba Mungu atutie moto wa upendo wake kwa njia ya Mwanae, atujalie tuwake tamaa ya mbinguni kwa sikukuu ya Pasaka, ili tuweze kuzifikia raha za heri yake ya milele kwa mioyo iliyotakata. Katika matayarisho ya mshumaa, Padre anauchora ishara ya msalaba kwa kalamu ya chuma. Kisha anauchora herufi za Kigiriki: Alfa juu ya Msalaba, Omega chini yake, kati ya mikono ya Msalaba anachora tarakimu nne za mwaka husika akisema: “Kristo jana na leo, Mwanzo na Mwisho, Alfa na Omega, nyakati ni zake na karne pia, utukufu ni wake na enzi pia, daima na milele”. Baada ya kuuchora mshumaa ishara ya Msalaba na ishara nyingine, Padre anachomeka katika mshumaa chembe tano za ubani kwa kuzipanga mfano wa msalaba, akisema: “Kwa majeraha yake matakatifu, na matukufu, Kristo Bwana wetu atulinde na atuweke salama”. Hii ni kuonesha na kukiri ukuu na utakatifu wa msalaba ambao kwao wokovu wetu, Yesu Kristo alitundikwa juu yake, akafa, akazikwa na sasa amefufuka yu mzima ameshinda dhambi na mauti, ametuweka huru kutoka utumwa wa shetani, utumwa wa dhambi na mauti tunda lake. Ishara ya ushindi wetu, ni mshumaa wa Pasaka, mwanga wa Kristo, uondoao giza la usiku huu, lililo ishara ya dhambi na mauti. Kwa hiyo katika adhimisho hili, Kanisa linausalimu na kuuheshimu mwanga wa Kristo katika alama na ishara ya mshumaa ndiye Kristo mfufuka, mleta uzima. Kwa furaha kubwa tunausimamisha mwanga huu katikati yetu.

Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka
Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka

Sehemu ya pili ni Liturujia ya Neno. Katika Vijilia hii, ambayo ni mama ya Vijilia zote, Mama Kanisa ametuwekea masomo kenda/tisa yakutuhabarisha habari za fumbo la ukombozi wetu; saba ya Agano la Kale na mawili ya Agano Jipya (Waraka na Injili). Baada ya kupigwa mbiu takatifu, Padre anawaalika waamini kulisikiliza Neno la Mungu kwa makini ili kulijua vyema fumbo la ukombozi wetu tangu matayarisho yake katika Agano la kale na utimilifu wake katika Agano jipya na la milele akisema; “Tumeingia katika vijilia vya Pasaka, sasa tusikilize neno la Mungu kwa moyo mtulivu. Tuwaze jinsi Mungu alivyolikomboa taifa lake wakati ulipowadia, na mwishowe akamtuma kwetu Mwanawe awe Mkombozi. Tumwombe Mungu wetu aifanikishe hii kazi ya wokovu wakati huu wa Pasaka, ili nasi tupate ukombozi kamili”. Masomo haya ni ya kusikiliza kwa makini sana, ili kulitambua na kuliishi vyema fumbo la ukombozi wetu, yaani Pasaka. Sehemu ya tatu ni Liturujia ya Ubatizo ambapo wakatekumeni walioandaliwa vyema wakati wa kwaresima wanapokea Sakramenti ya Ubatizo, wanazaliwa upya kwa maji na Roho Makatifu, wanakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo ndiyo maana kabla ya adhimisho la sakramenti hii Padre anawaalika waamini akisema; “Ndugu zangu, tuwasaidie kwa sala zetu hawa ndugu zetu wawe na matumaini ya wokovu. Na hapo watakapoijongea chemchem ya uzima mpya, Baba Mwenyezi azidi kuwasaidia kwa huruma yake.” Kumbe ufufuko wetu huonekana na kudhihirishwa katika sherehe ya ubatizo. Wanaobatizwa huzaliwa upya katika Kristo, lakini hata tuliokwisha batizwa, tunashirikishwa huko kuzaliwa kupya, kwa kuweka tena ahadi zetu za ubatizo. Kwa tendo hilo, umoja wetu na Kristo mfufuka huimarishwa.

Liturujia ya Ubatizo na Kurudia tena ahadi za Ubatizo
Liturujia ya Ubatizo na Kurudia tena ahadi za Ubatizo

Sehemu ya nne ni Liturujia ya Ekaristi Takatifu ndiyo kilele na kiini cha adhimisho la fumbo la ukombozi wetu ndiyo maana Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali akisema; “Ee Bwana, tunakuomba uzipokee sala na dhabihu za taifa lako, ili hayo tuliyoanza kutenda katika mafumbo yatusaidie tuupate uzima wa milele”. Sala ya utangulizi inatupa mhutasari kamili wa fumbo hili kuwa; “Kristo ametolewa Pasaka yetu. Yeye ndiye Mwana kondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za dunia, alishinda mauti yetu kwa kufa kwake, akaturudishia uzima wetu kwa kufufuka kwake. Na kwa sababu hiyo, watu wote wanaitukuza sikukuu ya Pasaka kwa furaha kubwa popote duniani. Nao Malaika wote wa mbinguni wanaimba wimbo wa kukutukuza, wakisema bila mwisho”. Ni furaha kweli kweli kwani “Kristo Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka”, yaani Kristo amefufuka; “basi na tuifanye karamu kwa yasiyo chachika, ndio weupe wa moyo na kweli”. Turudi sasa katika sehemu ya pili ya ibada ya vijilia vya Pasaka ambayo ni Liturujia ya Neno. Masomo kenda/tisa yanayosomwa katika liturujia ya neno katika vijilia vya mkesha wa Pasaka, yote kwa pamoja yanatupa simulizi kamili la historia ya wokovu wa mwanadamu tangu alipoanguka katika dhambi baada ya kuubwa. Somo la kwanza la kitabu cha mwanzo (Mw.1:1-2:2) ni simulizi la uumbaji. Somo hili linatufundisha kuwa asili na chanzo cha mwanadamu ni Mungu katika Utatu Mtakatifu. Katika viumbe vyote vilivyoumbwa (Mw.1-2), ni binadamu tu peke yake ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mw.1:26-27). Lengo ni ili amjue, ampende, amtumikie na mwisho afike kwake mbinguni. Mungu kabla ya kumuumba mwanadamu aliviumba vitu vingine vyote (Mw1:1-25). Haya yalikuwa maandalizi ya mazingira ya kuishi mwanadamu. Baada ya kumwumba mwanadamu alimkabidhi vyote ili avitiishe na kuvitawala (Mw. 1:28). Kisha akampa na ruhusa ya kuvitumia vyote (Mw.1:29-30) na kula matunda ya miti yote (Mw. 2:16). Lakini akampa sharti moja tu, asile matunda ya mti wa katikati (Mw. 2:17).

Liturujia ya Neno la Mungu: Historia ya Wokovu
Liturujia ya Neno la Mungu: Historia ya Wokovu

Maana yake jukumu la lipi ni jema na lipi ni baya sio jukumu lake mwanadamu bali la Mungu. Lakini ikawa ni kinyume chake, kwani mwanadamu akakaidi maagizo ya Mungu, akataka kuwa sawa na Mungu, akaamua lipi liwe jema na lipi liwe baya. Kwa lugha ya kibiblia akala alichokatazwa yaani akakosa utii kwa Mungu (Mw.3:6-7). Kwa kosa la kutotii amri na maagizo ya Mungu dhambi iliingia duniani. Mungu akawaadhibu kwa kosa lao la kutotii maagizo yake (Mw. 3:14-19). Dhambi hii ya kutaka kujiamulia lipi i baya na lipi ni jema, imeshika kasi zaidi katika nyakati zetu ambapo mwanadamu anataka uhuru wa kuhalalisha kila lililochukizo machoni pa Mungu. Baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva la kukaidi maagizo na amri za Mungu, walipoteza neema ya utakaso, sura na mfano wa Mungu ndani mwao na mahusiano mazuri na Mungu yakatoweka. Kwasababu ya kiburi na ukaidi, taabu, mahangaiko na mateso yakamwandama mwanadamu kwa kujitenga kwake na Muumba wake. Hata hivyo Mungu kwa upendo wake na kwa huruma yake hakumwacha mwanadamu apotee na kuangamia kabisa. “Kwa nyakati mbalimbali na tofauti, mara nyingi na kwa namna nyingi na njia mbalimbali, Mungu nyakati zote amefanya juhudi kubwa kumrudisha kwake mwanadamu aliyejitenga kwa ukaidi wake (Ebr.1:1-4). Kwanza aliwaadhibu kwa gharika kuu wakati wa Nuhu (Mw. 6:1-9:29), akamteua na kumwita Ibrahimu kuwa Baba wa Imani na kufanya naye Agano. Katika somo la pili la mkesha wa Pasaka Mungu anaijaribu imani ya Ibrahimu kwa kumtaka amtoe kafara mwanae Isaka (Mwa.22:1-18). Mungu akaliteua taifa la Israeli, si kwasababu ya ubora wake bali kwa mpango na makusudi yake akalifanya kuwa taifa teule litakalo mpokea Mwokozi. Kila walipokosea, Mungu aliwaadhibu kwa kuwapeleka utumwani na walipotubu makosa yao, aliwasamehe na kuwarudisha katika nchi yao. Kwanza ni utumwa wa Misri, akawatoa kwa mkono wa Musa akawavusha bahari ya shamu (Kut. 14:15 –15:1). Ndilo somo la tatu la mkesha wa Pasaka. Akafanya nao Agano na kuwapa Amri kumi ziwe mwongozo wa maisha yao (Kut. 19:3-24:8).

Mkesha wa Pasaka Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Neno: Historia ya Wokovu
Mkesha wa Pasaka Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Neno: Historia ya Wokovu

Ukaidi wa mwanadamu uliendelea. Mungu akawatuma waamuzi, wakaja pia wafalme na manabii wakati wa utumwa wa Babeli – Isaya 54:5-14 (somo 4), Isaya 55:1-11 (somo 5), Baruku 3:9-15, 32-4:4 (somo 6), Ezekieli 36:16-17a, 18-28 (somo la 7). Nao walipotambua makosa yao, wakatubu, wakamlilia Mungu, Mungu aliwasamehe na kuwarudisha katika nchi yao ya ahadi kwa mkono wa mfalme Koreshi wa uajemi. Lakini hata hivyo, Taifa la Israeli liliendelea kuwa na moyo mgumu kama binadamu wengine, kwa ukaidi wao, waliwatenda jeuri waliotumwa na Mungu na wengine kuwaua kabisa. Nabii Isaya akatabiri ujio wa masiha, mtumishi wa Mungu, mwana pekee wa Mungu, mpatanishi wetu na Mungu Baba. Aliyezaliwa na Bikira Maria muda ulipotimia. Mungu akamtambulisha siku ya ubatizo wake mtoni Yordani (Mk.1:9-10) na alipogeuka sura mlimani Tabor kuwa ndiye mwanaye mpendwa tumsikilize yeye (Mk.9:2-10). Huyu ndiye Kristo tuliyemtesa mateso mengi kama Injili zinavyoshuhudia; tukampiga mijeledi (Yn. 19:1), tukamvika taji ya miiba kichwani (Yn.19:2,5), tukampiga makofi usoni (Yn. 19:3), tukamtemea mate, akiwa amechoka kabisa yuko hoi tukambebesha msalaba mzito kwenda kumsulibisha (Yn19:17), alipoanguka kwa udhaifu wa kimwili tulimpiga bila huruma, hatimaye tukamtundika juu ya msalaba kwa kumpigilia misumari kama mhalifu katikati ya wahalifu (Yn. 19:18), alipoona kiu tukampa siki badala ya maji (Yn. 19: 28-30), alipokufa hatukuamini, tukaona haitoshi tukamtoboa ubavu wake kwa mkuki ikatoka damu na maji (Yn.19:34), ndizo chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. Kwa jina lake tumebatizwa (Rm.6:3-11 - somo 8). Watu wema wakazimka (Yn 19:38-40), siku ya tatu akafufuka ili arudishe tena uhusiano wetu na Mungu Baba na kuwatokea wengi katika wanafunzi wake (Yn. 20) akianza na wanawake (Lk 24:1-12 – Injili ya mkesha wa Pasaka).

Imani: Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele
Imani: Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele

Usiku mtakatifu wa Pasaka tunaimba na kushangilia kuwa Kristo amefufuka kweli kweli Aleluya/Tumsifu Mungu. Tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Ni usiku Mtakatifu, ni usiku wa wokovu. Ni usiku wa kuutangazia ulimwengu kuwa Kristo amefufuka yu hai. Ni usiku wa kuepuka nafasi za dhambi. Ni usiku wa amani, ni usiku wa kwenda mbio kuutangazia ulimwengu habari za ufufuko wa Bwana. Ni usiku wa kutanga habari za kaburi kuwa wazi, Kristo amefufuka, yu mzima nasi tunamtambua katika kuumega mkate. Kristo amefufuka kweli kweli, Aleluya. Herini kwa Sherehe ya Pasaka. Tumsifu Yesu Kristo.

Kesha la Pasaka 2023
07 April 2023, 17:02