Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni kielelezo makini cha upendo unaomwilishwa katika imani na matumaini. Huu ni muhtasari wa imani ya Kanisa inayotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni kielelezo makini cha upendo unaomwilishwa katika imani na matumaini. Huu ni muhtasari wa imani ya Kanisa inayotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa  (Vatican Media)

Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Ufufuko Ni Kiini cha Imani na Ushuhuda wa Kanisa

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Mama wa Kanisa katika ungamo ya imani ya Kikristo “Credo” wanafundisha na kuungama katika Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; na katika tendo lake la uumbaji, la wokovu na lenye kutakasa, hitimishwa na tangazo la ufufuko wa wafu siku ya mwisho na katika uzima wa milele. Kama vile Kristo Yesu alivyofufuka kutoka wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki, baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Mfufuka, naye atawafufua siku ya mwisho. Rej. KKK 988. Kristo amefufuka ni hakika na kweli. Mdo 10:34, 37-43; II. Kol 3:1-4, III. Yn 20:1-9. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Pasaka, siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, siku ya tatu baada ya kifo chake kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Nimefufuka na ningali pamoja nawe; umeniwekea mkono wako, maarifa hayo ni ya ajabu, alaluya” (Zab. 139:18, 5-6). Bwana amefufuka kweli kweli, aleluya. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele (Lk. 24:34; Ufu. 1:6). Sherehe ya ufufuko wa Yesu Kristo ni chimbuko la maadhimisho yote katika mwaka wa liturujia. Tunaalikwa na mama Kanisa kufurahi na kushangilia ushindi dhidi ya dhambi na mauti kama anavyoimba mzaburi; “Hii ndiyo siku hii, aliyoifanya Bwana, tuishangilie na tuimbe aleluya” (Zab 118:24). Ndiyo maana katika sala ya mwanzo Padre kwa niaba ya waamini anasali; “Ee Mungu, umetufungulia mlango wa milele kwa njia ya Mwanao wa pekee aliyeshinda mauti. Tunakuomba utujalie sisi tunaodhimisha kufufuka kwake Bwana wetu, tufufuke katika nuru yako kwa kufanywa wapya na Roho wako."

Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini
Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini

Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 10:34; 37-43). Somo hili ni hotuba ya Mtume Petro kwa wapagani/wakatekumeni waliokuwa wakijiandaa kupokea ubatizo. Hotuba hii ni ufupisho wa mafundisho msingi ya Kikristo. Petro ameyagawa mafundisho haya katika sehemu kuu nne akitaja matukio makuu katika maisha ya Yesu Kristo ya kwamba. 1/ Yesu alikuwa Mtu kweli kama sisi isipokuwa hakuwa na dhambi. 2/ Yesu alienda huku na huko akifundisha habari za Ufalme wa Mungu, akiponya wagonjwa na kutenda mema mengine. 3/ Yesu ni mjumbe wa Mungu ambaye watu wake hawakumkubalika, hivyo walimtesa, wakamtundika msalabani, wakamuua. 4/ Mungu alimfufua Yesu siku ya tatu ili kuthibitisha na kuthihirisha utabiri wa Manabii juu yake. Mitume na wafuasi wa Kristo ndio mashahidi wake wa kweli kwa kuwa waliishi naye, walikula na kunywa naye, waliyasikia mafundisho yake na aliwatuma wakafundishe kile walichojifunza, walichoona kwa miujiza aliyoifanya kwa kuwaponya na kuwafufua watu. Kwa Sakramenti ya Ubatizo sisi nasi tumefunuliwa kwa njia ya Roho Mtakatifu maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Hivyo tunapaswa kuwa kweli mashahidi wake. Ikiwa katika Ubatizo maisha yetu yalibadilika kwa kuuvua utu wa kale, utu wa dhambi – tukauvaa utu mpya wa Kristo mfufuka basi tunapaswa kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu na kuyakemea maovu yote yanayojitokeza katika maisha yetu kwa ujasiri bila hofu wala woga wowote.

Pasaka ya Bwana Ni Sherehe ya Upendo na mwanzo wa maisha mapya.
Pasaka ya Bwana Ni Sherehe ya Upendo na mwanzo wa maisha mapya.

Katika dominika ya ufufuko wa Bwana Misa ya mchana, Mama Kanisa ameweka masomo mawili ya kuchagua kwa somo la pili. Linaweza kusomwa somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4) au somo la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1 Kor. 5:6-8). Somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4); linatufundisha kuwa; Katika Ubatizo tulikufa na kufufuka na Kristo; tukaahidi kumfuata daima katika maisha ya taabu na raha, hivyo yatupasa kuishi kadiri ya ahadi hiyo tukiacha mabaya na kutenda mema. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu...Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu”. Somo la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa wakorinto (1 Kor. 5:6-8); linatufundisha kuwa; Kabla ya kula mwana kondoo wa Pasaka Waisraeli walitoa chachu yote ya zamani nyumbani mwao – yaani kujipatanisha wao kwa wao, na kujipatanisha wao na Mungu. Tendo hili ni alama ya kuacha maisha mabaya ya zamani na kuanza maisha mapya, maisha mema, maisha ya baada ya kifo na ufufuko wa Bwana. Mwaliko ni huu; “Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli”.

Pasaka ni fumbo letu la wokovu.
Pasaka ni fumbo letu la wokovu.

Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:1-9). Sehemu hii ya injili inaweka wazi ukweli mkuu wa imani yetu kwamba Kristo amefufuka kweli. Ushahidi ni wazi: Kaburi liko tupu, vitambaa alivyolalia, na baadaye akajionyesha kwa wafuasi wake. Kumbe ufufuko wake ni utimilifu wa ukombozi wetu. Ilikuwa asubuhi na mapema siku ya kwanza ya Juma, Maria Magdalena alipofika kaburini.” Maneno haya ya ufunguzi wa Injii yanaashiria ushindi wa Kristo dhidi ya kifo na mauti. Kulikuwa na ukimya mkubwa duniani na utulivu wa hali ya juu, kungali bado giza lakini Maria Magdalena hakuona shida kwenda kaburini ili aweze kuupaka mwili wa Yesu manukato kama ilivyokuwa desturi ya kuzika kwao ili kukamilisha ibada za maziko. Naye alipofika aliona kaburi li-wazi. Kisha kuona vile alirudi kwa haraka kuwapa habari mitume. Itakumbukwa kuwa ushuhuda wa wanawake nyakati hizo haukudhaminiwa. Tena Wanawake katika familia za Kiyahudi ambao walihesabiwa kati ya watumwa au vitu alivyomiliki mwanaume, mwanamke ambaye hakuaminika, hakuruhusiwa kutoa maoni yake mbele ya wanaume, hakuruhusiwa kutoa ushahidi ndiye ambaye Mungu anamfanya kuwa shahidi wa kwanza wa ufufuko na ukombozi wa mwanadamu. Mwanamke anashirikishwa katika kazi ya ufufuko na kwenda kuwa shuhuda wa ufufuko kwa mitume. Hawa ndiyo waliokuwa watangazaji wa habari njema. Wakiisha kuwatangazia mitume habari hii njema, ndipo Petro na mitume nao wakapata ujasiri wa kutoka kwenda kaburini kushuhudia habari hizi. Naye Yohane alipoingia kaburini na kuona aliamini.

Fumbo la Pasaka limetangazwa na kushuhudiwa pia.
Fumbo la Pasaka limetangazwa na kushuhudiwa pia.

Yesu Kristo alifufuka siku ya kwanza ya juma - kwa Wayahudi ni siku ya Jumatatu. Wakristo walianza kuiita “Siku ya Bwana” – dies Domini, Dominika ndiyo Jumapili (Mdo 20:7, Ufu 1:10). Siku hii ikawa muhimu sana na kuchukua nafasi ya sabato ya Kiyahudi. Ilikuwa siku hii ya kwanza ya juma Mungu alipo umba mwanga: Mungu akasema; “Iwe Nuru” ikawa Nuru. Mungu akaona ya kuwa Nuru ni njema, Mungu akatenga Nuru na Giza, Mungu akaiita Nuru Mchana na giza Usiku, ikawa asubuhi ikawa jioni, siku moja (Mwa 1:3-5). Kristo ni mwanga mpya na jua la haki. Katika siku hii ya kwanza ya Juma, maisha yanaanza upya. Mungu anaanzisha historia mpya ya maisha ya mwanadamu. Kristo amefufuka. Kifo hakitutawali tena. Kwa sasa tunao mwanga wa Pasaka. Kwa mwanga huu giza halipaswi kututawala tena. Ndiyo maana wakati wa maadhimisho ya vijilia vya pasaka tulipoingia kanisani katika hali ya giza, mwanga utokanao na Mshumaa wa Pasaka ishara ya Yesu Mfufuks ulituzukia. Uzima unatawala dhidi ya mauti, wema unatawala dhidi ya uovu. Ufufuko wa Yesu unaleta uhai mpya, mwanga mpya na uumbaji mpya katika maisha ya kiroho tuliyopata kwa njia ya ubatizo. Kristo mfufuka ndiye mwanga mpya wa maisha yetu ya kiroho. Ufufuko wa Yesu unatuwezesha kuelewa maana ya mateso na kifo chake katika mpango wa Mungu wa kutukomboa sisi kutoka utumwa wa dhambi na mauti na kutufanya kuwa watoto wake. Hii inatusaidia nasi kuyapokea mateso, kifo na magumu ya maisha tukiamini kwamba ikiwa Mungu ameruhusu yatupate ni kwa sababu jambo jema litatiririka katika hayo. Maisha yetu ni kama mbegu, ili iote lazima kwanza ife – “Punje ya ngano isipoanguka katika nchi ikafa, hubaki hali hiyo hiyo, bali ikifa huzaa mazao mengi”. Kwa hiyo kifo chetu kinapata maana kwa ufufuko wa Yesu.

Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu
Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu

Akifufuka kutoka wafu, Bwana wetu Yesu Kristo ameondoa giza la kifo na dhambi na kutuongoza kwa Mungu Baba. Kwa kuwa Kristo alifufuka kutoka wafu, maisha mapya, maisha katika Roho yanapatikana kwa wote walio tayari kuyapokea. Yeyote anayekufa kuhusu dhambi na kumkataa shetani anapokea hali mpya ya maisha ya kiroho, ni sawa na kuumbwa upya. Tunapomwamini Kristo, maisha halisi ya Kristo yanakuwa maisha yetu pia. Upendo wake unatuleta katika imani kwa Mungu na upendo kwa Jirani zetu. Upendo kwa Jirani ni kama cheche inayoamsha imani ndani ya mioyo yetu. Upendo kwa jirani ni hitaji msingi kama tunataka imani yetu kwa Mungu ikue na kuzaa matunda nasi tutaimba kwa furaha; “Mkono wa Bwana umeniinua, sitakufa bali nitaishi, na kuyatangaza aliyonitendea Bwana” (Zab 118:16-17). Tumsifu Yesu Kristo.

Pasaka ya Nwana 2023

 

08 April 2023, 14:54