Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa: Kukutana na kumtambua Kristo Yesu katika kuumega Mkate – Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho ni furaha kumbwa isiyo na kifani Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa: Kukutana na kumtambua Kristo Yesu katika kuumega Mkate – Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho ni furaha kumbwa isiyo na kifani   (Vatican Media)

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya III ya Pasaka: Liturujia ya Neno na Ekaristi Takatifu

Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika kumfahamu Bwana Mfufuka katika kulisikiliza Neno la Mungu kuanzia Agano la Kale hasa Torati ya Musa na utabiri wa Manabii kama msingi wa kumtambua katika kuumega mkate. Kukutana na kumtambua Kristo katika kuumega Mkate – Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho ni furaha kumbwa isiyo na kifani ndio maana wimbo wa mwanzo unaimba ukisema: Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote, imbeni!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 3 ya Pasaka mwaka A. Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika kumfahamu Bwana Mfufuka katika kulisikiliza Neno la Mungu kuanzia Agano la Kale hasa Torati ya Musa na utabiri wa Manabii kama msingi wa kumtambua katika kuumega mkate. Kukutana na kumtambua Kristo katika kuumega Mkate – Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho ni furaha kumbwa isiyo na kifani ndio maana wimbo wa mwanzo unaimba ukisema; “Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote, imbeni utukufu wa jina lake. Tukuzeni sifa zake, aleluya (Zab. 66:1-2). Na katika sala ya Koleta Padre kwa niaba ya waamini anasali; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha siku zote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafurahi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wa Mungu, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi”. Na katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana tunakuomba dhabihu za Kanisa lako linalofanya shangwe. Na kama ulivyolifanya lifurahi sana sasa, ulijalie pia furaha ya milele”. Ni furaha kwa sababu Kristo amefufuka, kweli yu mzima, Aleluya. Somo la kwanza ni la Matendo ya Mitume (Mdo. 2:14, 22-28). Katika somo hili tunaona kuwa kiini cha mafundisho ya mtume Petro ni kutoa ushahidi juu ya kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Yesu aliyeteswa, akafa msalabani na akazikwa, amefufuka kama ilivyotabiriwa katika Maandiko Matakatifu. Yeye pekee ni matumaini ya ufufuko wetu katika heri ya mbinguni. Petro anaeleza kuwa kifo cha Yesu hakikuja kwa bahati mbaya bali ulikuwa ni mpango wa Mungu kuwakomboa wanadamu (Mdo 2:23). Ndiyo maana baada ya kifo chake Mungu alimfufua siku ya tatu kutoka wafu ishara ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti (Mdo 2:23-24).

Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate
Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate

Zaidi sana Petro anasisitiza juu ya ubinadamu na Umungu wa Yesu. Yeye alikuwa binadamu, mtu wa Nazareti, mseremala, aliyefanana nasi isipokuwa hakutenda dhambi na ubinadamu wake ulijidhihirisha katika mateso na kifo chake. Yesu ni mwana wa Mungu na ni Mungu; alifanya miujiza, ishara na maajabu mengi yaliyoshuhudia kuwa alikuwa na nguvu za kimungu. Hata hivyo, viongozi wa wayahudi walimkataa yeye na ujumbe wake na wakamtoa kwa Warumi asulibiwe. Ilikuwa Pilato aliyetoa hukumu ya mwisho. Petro anawaambia wayahudi wazi kuwa; “Ninyi ndiyo mliyemwua” kwa kusema asulubiwe (Mdo 2:23). Yesu mwenyewe alisema kwa Pilato; “Yule aliyenitoa kwako ana dhambi kubwa zaidi” (Yn 19:11). Lengo la Petro sio kuwalaani Wayahudi bali ni kujaribu kuwafanya wamwamini Kristo. Kazi ya kumwua Yesu ilikuwa kazi ya mwanadamu, kazi ya kumfufua Yesu ilikuwa kazi ya Mungu. Cha kujivunia zaidi ni kwamba historia yake haiishii na kifo kwani Kristo amefufuka na mitume ni mashahidi wa ukweli huo. Nasi kwa ubatizo tumeshirikisha unabii, ukuhani na ufalme wake. Hivyo tunapaswa kuwa kweli mashahidi wake mpaka ukamilifu wa dahari. Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 1:17-21). Katika somo hili Mtume Petro anashuhudia kuwa Mungu ni Baba yetu mwema na mwenye haki. Ndiyo maana alimtuma Mwana wake wa pekee kuja kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kwa kuwa tumekombolewa kwa damu ya thamani, damu ya Kristo, yatupasa kujitahidi kuishi kitakatifu tukiyatazama yaliyo juu Kristo aliko ili nasi tuweze kufika aliko yeye Mkombozi wetu.

Akawafafanulia Neno la Mungu kumhusu Yeye mwenyewe!
Akawafafanulia Neno la Mungu kumhusu Yeye mwenyewe!

Hii ina maana ya kuzingatia haki na kutenda mema yanayojidhihirisha katika matunda ya Roho ambayo Mtume Paulo anayataja kuwa ni upendo, furaha, amani, mshikamamo, uvumilivu, unyenyekevu, utii na uchaji kwa Mungu (Wagalatia 5:22-23). Na yale yaliyochini ambayo kwa kuwa tumefufuka hatupaswi kuyagn’ang’ania kwa nguvu ni matendo ya mwili ambayo mtume Paulo anayataja kuwa ni; chuki, fitina, ufisadi, ibada ya sanamu, uadui, ugomvi, kijicho, hasira, ubinafsi, utengano, mafarakano, wivu, ulevi, ulafi, uzinzi na uasherati (Wagalatia 5:19-20). Kumbe, Mtume Petro anasisitiza kuwa sisi sote tulikuwa watumwa. Shetani alikuwa Bwana wetu na dhambi zetu zilikuwa kama minyonyoro iliyotufanya tuwe wafungwa. Lakini tumewekwa huru kwa fidia ya damu azizi ya Yesu. Itakumbukwa kuwa kulingana na sheria ya Kirumi mtumwa aliweza kupata uhuru kwa yeye mwenyewe kujilipia au kulipiwa na mtu mwingine fedha au vitu vya thamani vinavyotosha kumuweka huyu. Kiasi hiki cha fedha au vitu vya thamani kiliitwa fidia. Hakuna kiasi cha fedha au vitu vya dhamani kama fadia kilichoweza kumfanya mtu aachiwe huru kutoka katika utumwa wa dhambi. Gharama ambayo Yesu aliilipa kutuweka huru haikuwa fedha au dhahabu, bali ni damu yake azizi iliyotufanya tuwe wana wa Mungu (1Pet1:19). Petro anaendelea kusema kama sisi ni watoto wa Mungu tunapaswa kuenenda kama watoto wake, tunapaswa kufanana na Yesu, kaka yetu zaidi na zaidi. Hatupaswi kurudi tena katika utumwa wa shetani. Lakini inachukua muda kwa mtumwa kujifunza namna ya kuenenda kama mtu huru. Tunapaswa kuingia katika maisha tukijifunza namna ya kufikiri, kuongea na kutenda kama Yesu alivyofanya tukiongozwa na Roho Mtakatifu.

Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate
Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate

Injili tunayosoma katika dominika hii ya tatu ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 24:13-35). Sehemu hii ya Injili ni simulizi la Yesu kuwatokea wafuasi wawili wa Emau. Mmoja wao anatajwa kwa jina la Kleopa na mwingine hatajwi. Huyu anatuwakilisha sisi sote. Itakumbukwa kuwa Injili zote nne zinaeleza jinsi Yesu mfufuka alivyowatokea mitume na wafuasi wake akiwaimarisha katika imani yao. Naye aliwatokea mpaka mara nane: 1/. Maria Magdalena (Mk 16:9-10; Yn 20:11-18); 2/. Wanawake wawili kwenye kaburi (Mt 28:9-10); 3/. Wanafunzi wa Emau (Lk 24:13-35); 4/. Mitume bila Tomaso (Yn 20:19-24); 5/. Mitume pamoja na Tomaso (Yn 20:26-29); 6/. Wafuasi kwenye ziwa Tiberia (Yn 21:1-14); 7/. Wafuasi katika mlima wa mizeituni (Mt 28:16-20; Lk24:36-49; Mk 16:14-18); 8/. Alimtokea Petro (Lk 24:34). Naye Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho analeta habari za kutokea kwake na Kristo (1Kor 15:3-8). Tendo hili la Yesu kuwatokea wafuasi wake mara nyingi hivi baada ya ufufuko wake ni kutaka kuwadhihirishia kuwa mafundisho yake juu ya Ufufuko wake, ni ukweli kabisa usiopingika na ni msingi wa imani yetu. Imani tunayoisadiki na kuiishi kama msingi wa jumuiya ya kwanza ya Kikristo. Ufufuko wa Yesu ni ishara ya matumaini, nguvu katika safari yetu ya maisha ya kiroho. Ufufuko wa Yesu Kristo ni uthibitisho mkubwa kabisa wa Umungu wake. Ufufuko wa Yesu sio tu ni muujiza mkubwa kupita yote aliyofanya kuthibitisha kuwa yeye ni Mungu, lakini pia ni fumbo la wokovu wetu. Ufufuko wa Yesu ni sehemu ya wokovu wetu. Tumekombelewa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Kifo na ufufuko wake havitenganishwi.

Kristo Yesu Mfufuka yuko pamoja na waja wake daima
Kristo Yesu Mfufuka yuko pamoja na waja wake daima

Tukirudi katika tukio la Yesu kuwatokea wafuasi wa Emau, tunaona kuwa wale wafuasi wawili walikuwa na huzuni na kukata tamaa. Hii ilitokea kwamba baada ya kifo cha Kristo, baadhi ya wafuasi wake walitawanyika toka Yerusalemu na kurudi vijijini mwao. Kifo chake kiliwafanya wapoteze imani juu yake maana hawakutegemea afe kifo cha aibu kama hicho. Wakiwa katika safari yao, Yesu anawatokea na kuambatana nao, kisha akawauliza juu ya kile walichojadiliana. Nao wanamweleza kinaganaga habari za Yesu Mnazareti aliyefundisha na kutenda miujiza mingi na mwisho akatiwa mikononi mwa Mayahudi na kuuawa msalabani, na walimshangaa kuona kuwa alikuwa hafahamu kilichokuwa kinaendelea Yerusalemu. Nao hakumtambua kuwa ndiye Bwana Mfufuka. Yesu mwenyewe anawakumbusha yaliyoandikwa katika Maandiko hasa Torati ya Musa na yaliyonenwa Manabii ya kuwa imempasa Kristo kupata mateso na kuingia katika Utukufu wake. Na walipofika mwisho wa safari yao wakamsihi akae pamoja nao kwa kuwa kumekuchwa. Jioni ile walimkaribisha chakula bila kujua yeye ndiye Kristo mfufuka. Walikuja kumtambua alipotwaa mkate, akaubariki, akaumega akawapa. Hapo macho yao yalifumbuliwa naye akatoweka mara. Basi nao wakaanza safari ya kurudi Yerusalemu kwenda kuwapasha habari mitume wake.

Kuna haja ya kutoka ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka
Kuna haja ya kutoka ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka

Maisha yetu yote ni safari, na katika safari hii tunakutana na vitisho, hofu au wasiwasi pamoja na kukata tamaa kwa sababu mbalimbali. Mara nyingine kama wafuasi wa Emau kunapotokea shida au matatizo katika familia, ndani ya kanisa, jumuiya, kigango, parokia, jimbo, shirika au taasisi yoyote ile, wapo wanaojitenga na kuanza kuwanyooshea wengine vidole. Hatupaswi kujitenga na wengine wakati wa matatizo na majaribu bali kuungana pamoja na kutafuta suluhu kwa pamoja. Bali tunapaswa kushirikishana na wengine magumu yanayotukabili ili kumruhusu Yesu kuwa pamoja nasi atusaidie kufanya mang’amuzi sahihi na kupata suluhisho linalotujenga. Kwani yeye anasema “wakutanapo wawili au watatu kwa jina langu mimi nipo katikati yao”. Zaidi sana tukio hili la Emau lina kila chembe za maadhimisho ya Ekaristi Takatifu. Lilianza kwa liturujia ya Neno na kisha Kuumega mkate (Ekaristi Takatifu) tukio linalowafanya wafuasi hawa wawili waweze kumtambua Kristo Mfufuka. Hivyo, liturujia ya Ekaristi Takatifu ni lazima itanguliwe na liturujia ya Neno ambayo ni maandalizi kwa ajili ya Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Hivyo, tukitaka kushiriki vyema na kikamilifu maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni lazima tushiriki sehemu zote mbili – Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Kumbe tutaweza kumtambua Yesu na uwepo wake katika maisha yetu ikiwa tutasoma Maandiko Matakatifu na kushiriki vema sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Lakini pia wafuasi wa Emau baada ya kumtambua Yesu walirudi Yerusalemu kwa wenzao kutoa ushuhuda na kuwatangazia kuwa Kristo afufuko kweli yu mzima. Nasi hatuna budi kutoa ushuhuda na kutangaza ukweli wa jambo hili kwa kuishi maisha ya kipasaka. Hivyo nasi tutakuwa ishara ya ufufuko wake kwa kuishi maisha mapya ya kipasaka. Na hivyo sala baada ya Komunyo inayosema; “Ee Bwana, tunakuomba utuangalie kwa wema sisi taifa lako. Utujalie tufufuke na miili mitukufu, sisi ambao umependa kutufanya wapya kwa mafumbo haya ya milele” itakuwa na maana katika maisha yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika ya III ya Pasaka
20 April 2023, 17:39