Askofu Masondole: Radio Maria Shuhudieni Kweli za Kiinjili na Utu Wema
Na Agatha Kisimba na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.
Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaosimikwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu na hiki ni kishawishi cha Shetani, Ibilisi hata katika karne ya ishirini na moja. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani, aliwaombea wafuasi wake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwatakasa kwa ile kweli kwani Neno la Mungu ndiyo ile kweli. Wametumwa ulimwenguni lakini wao si wa ulimwengu huu. (Rej. Yoh. 17: 12-19). Wadau wa tasnia ya mawasiliano wasishikwe na kishawishi cha kutaka kujifungia katika upweke wao, kwa kutaka kuendelea kubaki katika udogo wao Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu ni chanzo na kilele cha mawasiliano, kwani anataka kuwasiliana na waja wake jinsi alivyo, kutoka katika undani wake. Kumbe, wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwasiliana kwa kutumia akili, moyo na mikono yao; kwa maneno mengine, haya ni mawasiliano yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha mawasiliano ni upendo wa Mungu ambao umemwilishwa kati ya waja wake. Mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa si matangazo ya biashara wala wongofu wa shuruti. Kanisa linakuwa na kupeta kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, wanahabari ni chumvi na chachu ya kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuondokana na utamaduni wa watu kukata tamaa na kulalama kila wakati. Hata katika udogo na uchache wao, bado wanaweza kutenda makubwa kwa njia ya ushuhuda.
Huu ni ushuhuda unaotangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya tunu msingi za maisha ya Kikristo. Waandishi wa habari wanapaswa kutangaza kweli za Kiinjili bila kuweka chumvi au kuwabeza wengine. Ndani ya Kanisa, watu wote wajisikie kuwa ni ndugu wamoja na watangaze uzuri, ukweli na utakatifu wa maisha. Hii ndiyo lugha ya mashuhuda wa imani na wafiadini, waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waandishi wa habari wawe mashuhuda wa Kristo Yesu kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, kama inavyoshuhudiwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Waandishi wa habari, wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili, changamoto changamani katika ulimwengu mamboleo. Familia ya Mungu nchini Tanzania itaendelea kuiwezesha Radio Maria Tanzania kutekeleza malengo yake ya kuwainjilisha watanzania wote bila kujali dini, kabila wala rangi ya mtu kwani wote ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Radio Maria imekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina nchini Tanzania kwa kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni Radio ambao katika kipindi cha takribani miaka 25 iliyopita imejipambanua kwa kusoma alama za nyakati na hivyo kujibu maswali msingi yanayowatatiza watu wa Mungu katika medani mbalimbali za maisha. Imekuwa ni chombo cha faraja kwa wagonjwa na wazee. Ni Radio ambayo imeibukia kupendwa na watu wengi kutokana na mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania.
Ni katika muktadha huu, Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda, Tanzania, hivi karibuni amezindua Kampeni ya Mbio za Mama Bikira Maria kwa mwaka 2023 Kitaifa maarufu kama “MARIATHON” katika Parokia ya Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu, Nansio, Ukerewe, Jimbo Katoliki Bunda, yenye lengo la kuutegemeza utume wa Radio MARIA TANZANIA. Ameihimiza Radio Maria Tanzania kuwa ni chombo cha mawasiliano mazuri, kinachojipambanua kwa kufundisha, kuhabarisha na kuwaburudisha watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania, kwani chombo hiki kinapaswa kuwa ni sauti ya Mungu kwa waja wake. Radio Maria inapaswa kutangaza na kushuhudia ukweli pamoja na kukemea maovu yanayojitokeza ndani ya jamii dhidi ya kazi ya uumbaji, kama ilivyo kampeni ya ushoga inavyoendelea kushamiri katika jamii ya watanzania. Kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha kanuni maadili na utu wema, ili kujenga Tanzania inayosimikwa katika maadili, uchaji na hofu ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 3 Mei 2023 amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupyaisha Ibada ya Rozari Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria. Wajitahidi kupenya katika undani wa mafumbo ya maisha ya Bikira Maria, ili hatimaye, waweze kumpokea kama Mama yao wa Maisha ya kiroho, kielelezo na mfano wa uaminifu kwa Kristo Yesu. Waamini wamkimbilie kumwomba, ili aweze kuwaombea udumifu katika imani, umoja, ushirikiano na amani na hatimaye, aweze kuwakinga na hatari zote za roho na za mwili, tayari kushiriki katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu na heshima kwa kazi ya uumbaji.
Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya ufunuo wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu na ukombozi kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Mwezi Mei ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Akitoa salamu kwa niaba ya RADIO MARIA TANZANIA, Padri Dominic Mavula, C.PP.S., Mkurugenzi wa Matangazo Radio Maria amesema, waamini wanapotafakari mafumbo ya Bikira Maria ndani ya Mwezi Mei wakumbuke kuwa, wanatumwa kuinjilisha na kuwashirikisha watu wote ulimwenguni Habari Njema aya Wokovu hivyo kila mmoja apende kusali Rozari kutoka moyoni bila kubabaisha na asikimbie wala kusali kinafiki. Padri Mavula ameongeza kuwa ni afadhali kusali fungu moja kwa uchaji na heshima kuliko kusali mafungu yote bila heshima, uchaji na unyenyekevu kutoka moyoni, jambo aliloliita unafiki na kutoheshimu mafumbo ya Rozari Takatifu. Kampeni ya mbio za Mama Bikira Maria zinazoendeshwa na RADIO MARIA TANZANIA maarufu kama “MARIATHON” hufanyika ndani ya Mwezi Mei wote ambao ni Mwezi wa Rozari Takatifu na kuendelea mpaka Mwezi Juni, lengo likiwa ni kuutegemeza Utume wa Radio Maria Tanzania, ambayo sasa ina Vituo vya kurushia matangazo takribani 40 huku dhumuni kuu likiwa ni Uinjilishaji wa kina. Na kauli mbiu ya kampeni hiyo kwa mwaka huu ni "Mariathon 2023, Injilisha kwa furaha."