Sherehe ya Pentekoste: Mwanzo wa Kanisa Na Siku ya Waamini Walei
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Pentekoste, siku ya hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ya kuadhimisha tukio la kipekee na la msingi sana kwa Kanisa - kuzaliwa kwake kwa njia ya Roho Mtakatifu yaani kuumbwa upya kwa Taifa jipya la Mungu. Siku ya Pentekoste ni kilele cha sikukuu ya Pasaka, kwa sababu utajiri wote aliotufunulia Yesu mfufuka unaanza kuonekana katika mioyo na maisha ya Mitume. Kumbe tunasherehekea utimilifu wa fumbo la ukombozi wetu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliye ishara ya umoja wetu na Mungu kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti” (Hek.1:7). Na “pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi, Aleluya” (Rum.5:5). Kwa minajili hii, Pentekoste ni sherehe ya waamini walei wote. Basi baada ya huo utangulizi tuyapitie japo kwa kifupi masomo tunayoyasoma katika sherehe hii ili tupate nafasi ya kuweke mkazo zaidi katika katekesi ya Sherehe hii na nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya Kanisa na ya waamini. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:1-11). Somo hili linasimulia jinsi “upepo wa nguvu” na “ndimi za moto” vilivyotokea siku ya Pentekoste ya kwanza zikiwa ni alama ya uwepo wa Roho Mtakatifu aliyewajaza mitume nguvu na ujasiri wa kuhubiri habari za Kristo Mfufuka na wongofu wa watu. Pia umoja na uelewano uliopotea sababu ya dhambi ulivyoletwa tena kwa watu wa mataifa mbalimbali kuwasikia mitume wakiwahubiria kwa lugha yao ya kuzaliwa. Ndiyo maana sala ya mwanzo inatilia mkazo ikisema; “Ee Mungu, wewe unalitakasa Kanisa lako lote lililo kati ya makabila na mataifa yote kwa fumbo la sikukuu ya leo. Eneza mapaji ya Roho Mtakatifu popote duniani; na zile karama ulizozitoa tangu mwanzo wa kuhubiri Injili, hata sasa uzieneze kwa juhudi ya waamini wako.”
Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 12:3b-7, 12-13). Somo hili linatueleza kuwa Roho Mtakatifu ni msingi wa karama na hudumu mbalimbali katika Kanisa. Yeye ndiye anayefanya karama hizo zilete umoja katika kuihudumia jumuiya nzima ya waamini kama viungo mbalimbali vya mwili vinavyosaidiana kwa faida ya mwili mmoja. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:19-23). Sehemu hii ya Injili inaeleza jinsi Roho Mtakatifu alivyofanya kazi ya kuwaunganisha mitume na Yesu mfufuka na sasa anawaunganisha watu na Mungu kwa kuwaondolea dhambi zao. Pato la kazi hii ya Roho Mtakatifu ni upatanisho na amani kati ya Mungu na watu. Ndivyo inavyosisitiza sala ya kuombea dhabihu; “Ee Bwana, tunakuomba Roho Mtakatifu atufumbulie zaidi siri ya sadaka hii, kama alivyotuahidia Mwanao. Atujulishe pia ukweli wote kwa rehema yake”. Na katika utangulizi tunasali; “Wewe umetimiza fumbo la Paska na kuwajalia Roho Mtakatifu wale uliowafanya kuwa wanao, kwa sababu ni ndugu zake Mwanao wa pekee. Hapo mwanzo wa Kanisa huyo Roho Mtakatifu aliyafundisha mataifa yote kumjua Mungu, akawaunganisha watu wa lugha mbalimbali katika kuungama imani moja. Kwa hiyo watu wote wanaishangilia Paska kwa furaha kubwa sana po pote duniani”. Kumbe, tunaona kuwa Pentekoste na Pasaka ni sherehe mbili zenye uhusiano wa karibu sana. Kwa asili Pentekoste ilikuwa ni Sherehe ya pili kwa ukuu kwa Wayahudi baada ya sherehe ya Pasaka. Sherehe hii ilisherehekewa katika juma saba baada ya Pasaka. Ndiyo maana halisi ya neno Pentekoste, ikimaanisha “siku ya hamsini” baada ya Pasaka ya Wayahudi. Kwetu wakristo ni siku ya hamsini baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Wayahudi waliadhimisha mambo matatu katika sherehe yao ya pentekoste; Kufanyika kwa agano kati ya Mungu na wao mlimani Sinai, kupewa amri kumi za Mungu na kutoa shukrani ya mavuno ya kwanza ndiyo maana iliitwa pia Sikukuu ya mavuno ya kwanza. Sisi katika sikukuu hii ya Pentekoste tunaadhimisha kuwekwa kwa Agano Jipya na la milele kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya Yesu Kristo na kuthibitishwa kwa ujio wa Roho Mtakatifu. Nasi kwa njia ya Kristo tumepewa Amri kuu mpya ya mapendo, kiini cha Agano jipya na la milele. Pentekoste kwetu pia ni “sikukuu ya mavuno” ya waamini waliobatizwa siku hiyo yapata watu elfu tatu, mavuno yanayoendelea kuongezeka kila inapoadhimishwa Sakramenti ya ubatizo.
Nyakati zetu wapo wanaomfukarisha Roho Mtakatifu kwa kumuwekea mipaka katika karama zake wakimfanya kuwa ni Roho wa miujiza na kunena kwa lugha tu. Mafundisho haya ni potofu kweli. Shida ni kutokufahamu Maandiko Matakatifu yanayotufunulia utajiri mkubwa wa karama za Roho Mtakatifu na kupuuzia mafundisho ya Mama Kanisa yatokanayo na mapokea na mamlaka funzi ya Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na Mitume. Nabii Yoeli kwa kugusia tu anasimulia maajabu ya nyakati za mwisho, kumiminwa kwa roho, ishara na miujiza, wokovu kwa wale wanaoliita jina la Bwana akisema: “Hata itakuwa baada ya hayo ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili, na wana wenu waume kwa wake watatabiri, wazee wenu wataota ndoto na vijana wenu wataona maono. Tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake katika siku zile, nitamimina roho yangu” (Yoeli 2:28-29). Mtume Paulo katika barua na nyaraka zake anatupa mafundisho na katekesi ya kina sana kuhusu nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Roho Mtakatifu kweli ni “nguvu ya kutenda miujiza” (Mdo 1:8). Zaidi sana Roho Mtakatifu “ni chanzo na nguvu ya uzima mpya” ndani mwetu (1The 4:8). Roho Mtakatifu atuwezesha kumjua Mungu sawasawa (1Kor 2:10-16). Ndiye anatuwezesha kumtambua Mungu kama Baba; “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu, aliaye, Abba, yaani Baba” (Gal 4:6). “Roho huyo amiminwa mioyoni mwetu” (Rum 5:5) nasi twampewa kwa imani na ubatizo (Gal 3:2,14). Roho Mtakatifu anakaa ndani ya Mkristo sio kwa watenda miujiza na wanena kwa lugha tu (1Kor 6:11). Katika roho na mwili wake Roho Mtakatifu, “mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Rum. 8:9,16). Roho Mtakatifu aliye Roho wa Kristo anatufanya kuwa watoto wa Mungu (Rum 8:14-16). Yeye ni chanzo cha ufufuko wa Mkristo (1Kor 6:19). Mtume Paulo anasisitiza; Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa kwa Roho wake anayekaa ndani yenu (Rum 8:11).
Kama ilivyo matendo ya hali ya kimwili katika mtu anaweza kuwa chanzo cha dhambi (Rum 7:5) vivi hivi Roho Mtakatifu ni chanzo cha imani, uhai na utakatifu (1Kor 12:30. Zaidi sana Roho Mtakatifu ni chanzo cha utakaso wetu (Rum 15:16; 2The 2:13). Mtume Paulo anaendelea kusisitiza kuwa; “Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu na kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo, ili kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana na urefu, na kimo na kina, na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Efe 3:14-19). Roho Mtakatifu ni nguvu ya maisha adili. “Basi nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili…lakini mkiongozwa na Roho, hampo tena chini ya sheria … basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawaurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi, juu ya mambo kama hayo hakuna sheria …. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana (Gal 5:16-25; Rum 8:4-9). Roho Mtakatifu aleta nguvu na imara ya kitume (Fil. 1:19; 2Tim 1:7-8), aleta mapendo kwa sala (Rum 8:26) na atuunganisha na Kristo kuwa mwili mmoja (1Kor 12:13; Efe 2:16-18). Ndiyo maana Paulo anatuonya tusimzimishe Roho (1The 5:19) wala kumhuzunisha (Efe 4:30).
Katekisimu ya Kanisa Katoliki nayo inatufundisha vizuri sana kuhusu Pentekoste na ujio wa Roho Mtakatifu. Siku ya Pentekoste, mwisho wa juma saba za Pasaka, Pasaka ya Kristo inatimilika kwa kumimina Roho Mtakatifu, ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama nafsi ya Mungu: kutoka utimilifu wake Kristo, Bwana, anamimina Roho kwa wingi (KKK 731). Ni siku ambayo Utatu Mtakatifu umefunuliwa katika ukamilifu wake. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na Kristo ukawa wazi kwa ajili yao wanaomsadiki: katika unyenyekevu wa mwili na katika imani na kushirikishwa katika ushirika wa Utatu Mtakatifu. Kwa ujio wake ambao hauna mwisho, Roho Mtakatifu anauingiza ulimwengu katika nyakati za mwisho, nyakati za Kanisa, ufalme uliorithiwa tayari, lakini bado haujakamilika. Kwa njia yake tunaiona Nuru ya kweli, tunampokea Roho wa mbingu, tunapata imani ya kweli na tunauabudu Utatu usiogawanyika, kwa sababu umetukomboa (KKK 732). “Baada ya kutimiliza kazi ambayo Baba alikuwa amemkabidhi Mwana duniani, Roho Mtakatifu alipelekwa siku ya Pentekoste ili kulitakasa daima Kanisa” (LG 4). Hapo Kanisa lilidhihirishwa hadharani kwa umati wa watu na lilianza kuenea kwa njia ya mahubiri ya Injili (AG 4). Kwa kuwa Kanisa ni kusanyiko la watu wote kwa ajili ya wokovu, kwa tabia yake ni la kimisionari lililotumwa na Kristo kwa mataifa yote ili kuwafanya wafuasi (KKK 767). Kusudi Kanisa litekeleze utume wake, Roho Mtakatifu analipa na kuliongoza kwa njia ya vipawa vya namna mbalimbali vya kihierakia na karama. Kwa hiyo Kanisa lilijazwa vipawa vya mwanzilishi wake na kuhifadhi kiaminifu amri zake za upendo na unyenyekevu. Hivyo likawa kama mbegu na mwanzo wa ufalme wa Mungu duniani (KKK 768).
Siku ya Pentekoste, kwa mmimino wa Roho Mtakatifu, Kanisa limedhihirishwa kwa ulimwengu. Kristo anaishi na kutenda kazi katika Kanisa lake, na pamoja nalo, kwa namna iliyo mpya inayofaa katika nyakati hizi mpya. Naye anatenda kwa njia ya Sakramenti. Mpango huu umo katika ushirikishaji au ugawaji wa mafumbo ya Pasaka ya Kristo katika adhimisho la liturujia ya sakramenti za Kanisa (KKK1076). Siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu anamiminwa juu ya wafuasi waliokusanyika mahali pamoja, wakimngoja kwa moyo mmoja katika kusali. Roho huyu analikumbusha Kanisa yote aliyosema Yesu na analilea katika maisha ya sala (KKK 2623). Hizi ndizo hazina za Roho Mtakatifu katika Kanisa na maisha ya kila mkristo. Kabla ya kuhitimishe tafakari yetu tukumbuke kuwa kwa sherehe ya Pentekoste tunahitimisha kipindi cha Pasaka. Hivyo kuna mambo muhimu ya kiliturujia ya kuzingatia: Kwanza kabisa Mshumaa wa Pasaka unatolewa mahali pa patakatifu karibu na Altare uliposimikwa usiku ule wa vijilia vya Pasaka na kuweka karibu na kisima cha ubatizo kama kipo au sehemu nyingine. Mshumaa huo utakuwa unawashwa wakati wa ubatizo ili mishumaa ya wabatizwa iwashwe kutokea katika mshumaa huu ishara ya kufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo na wakati wa mazishi unawekwa kando ya jeneza ishara ya ufufuko kwa mkristo aliyekufa akiwa na muunganiko na Kristo mfufuka. Pili, kuanzia Jumatatu baada ya Jumapili ya Pentekoste, tunaacha kusali sala ya Malkia wa mbingu na tunaanza kusali sala ya Malaika wa Bwana na tunaendelea na liturujia ya kipindi cha kawaida cha mwaka A. Itakumbukwa kuwa kabla ya kuanza kipindi cha Kwaresima siku ya jumatano ya majivu – mwaka huu 2023A wa kiliturujia tuliishia wiki ya saba katika kipindi cha kawaida. Hivyo tutaendelea na wiki ya juma la nane. Basi tumruhusu Roho Mtakatifu atuwezeshe kuishi vyema maisha ya hapa duniani kadiri ya karama anazotujalia, tukitumaini kuyapata na yale ya mbinguni kama sala baada ya komunyo inavyohitimisha maadhimisho ya sherehe hii ikisema; “Ee Mungu, umelijalia Kanisa lako mapaji yako ya mbinguni. Uilinde neema hiyo uliyotujalia, ili mapaji ya Roho Mtakatifu tuliyoyapokea yasitawi daima, nacho chakula cha roho kituongezee ukombozi wa milele.”