Tafakari Dominika ya Sita Kipindi cha Pasaka Mwaka A: Roho wa Kweli
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii Kanisa linaadhimisha dominika ya 6 ya Pasaka. Tunaendelea kukutana na Kristo Mfufuka katika maadhimisho ya siku 50 za Pasaka, na Kristo huyo huyo anaendelea kujidhihirisha kwetu kila tunaposoma na kutafakari Neno lake. Maandiko Matakatifu tunayokwenda kuyatafakari katika kipindi cha leo ni masomo ya dominika ya 6 ya Pasaka, nayo yanazungumza nasi kuhusu Roho Mtakatifu. Tunasikia katika somo la Injili Yesu anawaambia wanafunzi wake “nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele”. Msaidizi anayemzungumzia Yesu ni Roho Mtakatifu. Na yeye anamwita Roho wa kweli. Kabla ya kuliingia kwa undani somo hilo la Injili, tuyapitie kwanza kwa kifupi masomo yanayolitangulia: somo la kwanza kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 8:5-8, 14-17) na somo la pili kutoka Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote (1Pet 3:15-18). Ufafanuzi wa Masomo: Katika somo la kwanza tunasikia habari ya Filipo. Huyu alikuwa ni mmojawapo wa mashemasi saba ambao mitume waliwachagua ili wawasaidie kutoa huduma katika jumuiya ya wakristo ambayo ilikuwa inazidi kukua kwa idadi ya waamini. Shemasi huyu anatoka katika mji walipokuwa wamekusanyika mitume wote, mji wa Yerusalemu, anakwenda katika mji mwingine, mji wa Samaria, kumhubiri Kristo. Somo letu halielezi kwa nini Filipo alienda Samaria ila tukirudi kusoma katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunaona kuwa kipindi hicho katika mji wa Yerusalemu Mitume na waamini walikuwa wanatafutwa ili wauwawe. Na mateso haya ya wakristo yalianza baada ya kifodini cha Stefano.
Huko Samaria, Filipo anamhubiri Kristo, watu wakalipokea Neno la Mungu na wakabatizwa. Habari hizi njema zilipowafikia mitume, wakawatuma Petro na Yohane kwenda huko Samaria wakawaimarisha wakristo wapya kwa kwa kuwawekea mikono nao wakampokea Roho Mtakatifu. Somo hili linatuonesha kuwa Roho Mtakatifu ambaye ni Roho wa Mungu mwenyewe ni kipawa cha Mungu. Naye humjalia yoyote na wote anaopenda kuwashushia kipawa chake. Pamoja na hayo, kipawa hiki cha Mungu wamekabidhiwa Mitume na Kanisa kwa ujumla kama amana. Si wao wamiliki wa Roho Mtakatifu na si wao wanaomtawala Roho Mtakatifu ila wao ni chombo ambacho Roho huyo huyo amekichagua ili kupitia chombo hicho aweze kuwafikia wote anaopenda kuwajalia kipawa chake. Wakristo wa Samaria kabla ya kumpokea Roho Mtakatifu waliiandaa mioyo yao kwa kulipokea kwanza Neno la Mungu. Neno linapopokelewa katika moyo wa mtu hufanya kazi ya kuuandaa moyo uwe makazi ya Roho wa Mungu. Bila imani, bila utayari wa kumpokea Kristo ni vigumu kufungua mlango wa moyo kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Somo la pili ni mafundisho au mausia ya Mtume Petro kwa wakristo wapya, wale ambao wamempokea Kristo kwa ubatizo na wamempokea Roho Mtakatifu. Mausia ya Petro kwa wakristo hawa ni mausia kwetu pia ambao kwa Ubatizo na Kipaimara tumempokea Kristo na kujazwa na mapaji ya Roho Mtakatifu. Kati ya anayofundisha Petro, anasema “muwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu.” Yaani, mkristo anapaswa kuwa na majibu kuhusu tumaini lililo ndani yake. Hii haimaanishi kwamba kila mkristo anapaswa kuwa mbobezi wa mafundisho ya imani na kila swali lazima awe na jibu lake. Petro anamaanisha ajijengee ndani yake uhakika wa kile anachokiamini katika Kristo na uhakika wa kile anachokitumaini kutoka wa Kristo, yaani kuungana naye milele mbinguni. Roho Mtakatifu tunayempokea ni Roho anayetusaidia kuyashinda mashaka tuliyonayo ndani yetu sisi wenyewe. Ni Roho anayetusaidia kujikita na kuzama katika imani. Kile mkristo anachokiamini katika Kristo, kiwe kikubwa au kiwe kidogo anapaswa kukishikilia.
Tafakari ya somo la Injili: Somo hili la Injili linaturudisha katika siku ile ya Karamu ya Mwisho, yaani siku moja kabla ya Yesu kukamatwa, kuteswa na kufa Msalabani. Yesu anajua kwamba bado muda kidogo arudi kwa Baba na hivyo anawapa maneno ya faraja na kuwaahidia ujio wa Roho Mtakatifu atakayekaa nao milele. Mambo mawili yanatusaidia kulielewa fundisho la Yesu katika injili ya dominika hii. Jambo la kwanza: Yesu anamwita Roho Mtakatifu kuwa ni Msaidizi mwingine. Neno hilo Msaidizi linaunganisha maneno mengi tunayoweza kutafsiri kutoka lugha ya asili ya Injili ya Yohane. Ni neno linalomaanisha mfariji, mtetezi, wakili, mwalimu, muwezeshaji n.k. Na hayo yote ndiyo anayofanya Roho Mtakatifu kwa waamini wake na kwa Kanisa lake. Yesu anaongeza kusema huyo ni Msaidizi mwingine kwa maana kwamba Yesu japokuwa anarudi kwa Baba, bado anabaki pamoja na wanafunzi wake. Roho Mtakatifu ni msaidizi mwingine katika Utatu Mtakatifu pamoja na Baba na Mwana.
Jambo la pili: Yesu anasema “sitawaacha yatima”. Yatima ni yule aliyebaki pake yake bila wazazi. Yesu anapowaambia wanafunzi wake “sitawaacha yatima” anawaambia kuwa kwa kipawa cha Roho Mtakatifu anawaunganisha katika familia moja ya kiimani. Zaidi ya hayo anawafanya washiriki muungano na Utatu Mtakatifu. Anasema “mtatambua kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.” Kama alivyokwisha kusema “aulaye mwili wangu na kuinjwa damu yangu hukaa ndani yangu nami hukaa ndani yake”. Jambo hili sio dogo. Linatupa wajibu sote tunaomwamini Kristo kujenga umoja wa Kanisa: kwa njia ya Kanisa na ndani ya Kanisa. Anayempokea Roho Mtakatifu hatafuti kuishi au kutenda peke yake kama yatima bali hutafuta kuishi katika muungano, muungano na waamini wenzake na muungano na Kanisa katika ngazi zake zote. Kristo Mfufuka aliyetuahidia ujio wa Roho Mtakatifu atujalie kwa wingi paji la Roho huyo atuimarishe katika imani, atuwezeshe kumpenda Mungu na atuunganishe katika Kanisa lake kama katika familia moja.