Tafuta

Dominika ya tano ya Pasaka inatulelea maneno ya Yesu anayesema “mimi ndimi njia, ukweli na uzima: Dominika ya tano ya Pasaka inatulelea maneno ya Yesu anayesema “mimi ndimi njia, ukweli na uzima:   (ANSA)

Tafakari Dominika ya 5 ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A: Wosia Kwa Mitume: Njia, Ukweli na Uzima

Dominika ya tano ya Pasaka inatulelea maneno ya Yesu anayesema “mimi ndimi njia, ukweli na uzima: mtu haji kwa Baba ila kwa njia yangu.” Ni maneno ambayo tunaweza kusema yanatoa muhtasari wa utambulisho mzima wa Yesu katika Injili ya Yohana: Yesu ndiye kila kitu tunachohitaji ili kujenga mahusiano yetu na Mungu, ili kumfikia Mungu na ili tuwe na uzima wa kimungu ndani yetu. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi usaidie kukabiliana na changamoto za kichungaji!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News,  dominika ya tano ya Pasaka inatulelea maneno ya Yesu anayesema “mimi ndimi njia, ukweli na uzima: mtu haji kwa Baba ila kwa njia yangu.” Ni maneno ambayo tunaweza kusema yanatoa muhtasari wa utambulisho mzima wa Yesu katika Injili ya Yohana: Yesu ndiye kila kitu tunachohitaji ili kujenga mahusiano yetu na Mungu, ili kumfikia Mungu na ili tuwe na uzima wa kimungu ndani yetu. Kama kawaida ya kipindi hiki, kabla hatujaingia kutafakari ujumbe huo ambao Injili ya dominika hii inatupatia, tunapenda kwanza kuyapitia masomo mawili yanayotangulia, yaani somo la kwanza kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 6:1-7) na somo la pili kutoka waraka wa Mtume Petro kwa watu wote (1Pet 2:4-9). Ufafanuzi wa Masomo: Tumekwisha ona kuwa katika kipindi hiki cha Pasaka, kila dominika tumesoma somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Hiki ni kitabu kutuchotupatia mafundisho kwa njia ya masimulizi yanayohusu hatua mbalimbali ya ukuaji wa kanisa la mwanzo baada tu ya ufufuko wa Yesu. Ni kitabu hiki kinachoonesha  kwa namna iliyo wazi zaidi kuwa ufufuko wa Kristo ndio ulioashiria mwanzo wa kanisa. Katika dominika zilizopita, masimulizi ya kitabu hiki yamekuwa yanatoa zaidi picha chanya ya ukuaji wa kanisa: mahubiri ya Petro, ujasiri wa mitume, wongofu na ubatizo wa watu wengi hadi hatua ya uundwaji wa Jumuiya ya kwanza ya wakristo. Somo la leo linaonesha kuwa pamoja na mambo yake yote mazuri, kanisa hilo la mwanzo halikukosa changamoto. Kundi moja katika jumuiya lilianza kunung’unika kuwa linabaguliwa katika kupata huduma na mahitaji ya kila siku. Tatizo hili lilikuwa kubwa na lilihatarisha umoja wa jumuiya nzima.

Mitume wakabaki kusali na kuhubiri, Mashemasi huduma mezani
Mitume wakabaki kusali na kuhubiri, Mashemasi huduma mezani

Mitume waliguswa na tatizo hili. Walilikusanya kundi zima na kuzungumza pamoja. Wakaona si vema wao kuendelea kushugulika na mambo yote mawili yaani huduma ya Neno na huduma ya kijamii. Hivyo wakachagua mashemasi saba, wakawakabidhi huduma ya jamii na wao wakabaki na huduma ya Neno. Huduma zote hizi mbili zinawakilisha kazi nzima ya uchungaji ambayo kanisa inalitekeleza kama wajibu wake wa msingi. Si huduma zinazopingana bali zina mlengo mmoja wa kumkomboa mwanadamu katika ukamilifu wa ubinadamu wake yaani roho na mwili. Ni katika mtazamo huu pia somo linatoa chimbuko la huduma ya ushemasi ambayo imeunganishwa katika sakramenti moja ya daraja takatifu na huduma ya kikuhani. Somo hili linatupatia tafakari kuhusu utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jumuiya zetu. Hakuna jumuiya wala familia isiyokutana na changamoto. Na changamoto hizi, ziwe ndogo au kubwa, kama zisiposhughulikiwa vizuri na kwa wakati, zinaweza kuhatarisha uhai wa jumuiya yenyewe. Jumuiya kamili siyo ile isiyo na changamoto bali ni ile inayojitahidi katika hatua zake mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa changamoto zake ili kulinda uhai wake. Katika somo la pili, Mtume Petro anazungumzia hali na hadhi mpya ya wakristo baada ya ubatizo. Anaeleza kuwa kwa ubatizo mkristo anafanywa kuwa jiwe hai linalojenga mwili wa kiroho wa Kristo, yaani kanisa. Tunafahamu kanisa kama jengo linalojengwa kwa mawe au matofali. Petro analiona jengo hilo la kanisa kama alama ya mwili wa kiroho wa Kristo na hivyo yale mawe au matofali ambayo kwayo kanisa zima linasimama, ndio sisi wakristo wenyewe. Mtume Petro anaongeza kuwa kwa ubatizo, mkristo anafanywa kuwa kuhani, yaani Padre. Ukuhani huu wa mbatizwa ndio ule ukuhani ambao Kanisa linauita ukuhani wa jumla ukitofautishwa na ule ukuhani wa daraja. Kwa ukuhani huu wa jumla, kila mbatizwa anashirikishwa kazi zile zile za Kristo: kuhani, nabii na mfalme. Mkristo hushiriki ukuhani wa Kristo  kwa kujitakatifuza na kuutakatifuza ulimwengu kwa sala;  hushiriki unabii wa Kristo kwa kufundisha, kutetea na kushuhudia ukweli kama ulivyofunuliwa na Mungu na kuendelezwa na mafundisho ya Kanisa;  na hushiriki ufalme wa Kristo kwa kujibidiisha kuujenga ufalme wa Mungu katika mazingira ya jamii anayoishi na kufanya kazi.

Baada ya Ubatizo, Mkristo anapata hadhi mpya.
Baada ya Ubatizo, Mkristo anapata hadhi mpya.

Tafakari ya somo la Injili: Injili tunayokwenda kuitafakari dominika hii inatoka sura ya 14 ya Injili ya Yohana. Mazingira ya somo hili ni katika Karamu ya Mwisho yaani ile siku ya Alhamisi Kuu Yesu alipoketi na wanafunzi wake kula pasaka ya wayahudi na ni hapo alipowaachia wanafunzi wake Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja na amri kuu ya Upendo. Mazingira haya ya karamu ya mwisho, yaani siku moja kabla ya Yesu kukamatwa na kusulubishwa msalabani, yanatusaidia kuelewa kwa nini Yesu anawaambia “msifadhaike mioyoni mwenu, mwaminini Mungu na niaminini mimi pia.” Yesu anasema hivyo kwa sababu anatambua yale yatakayowakabili wanafunzi wake baada ya Yeye kuondoka. Anatambua kuwa watakuwa wanaanza awamu mpya ya maisha ambayo hawakuwahi kuyaishi. Utume anaokwenda kuwaachia sio mdogo; una madai mengi na utawahitaji vingi, na hayo yote yanaweza kuwa sababu ya kuwahangaisha na hata kuwakatisha tamaa. Ni kwa sababu hii anawaambia maneno hayo ili kuwatia moyo. Na maneno hayo yanaposemwa na Yesu hayabaki maneno tu ya faraja bali kweli yanaileta faraja na matumaini kwa wale wanaoyashika. Ni maneno yanayokuwa uhakika wa uwepo wake mwenyewe kati yao. Maneno yanayofuata, ambayo tumeyanukuu pia mwanzoni wa kipindi hiki, Yesu akisema mimi ndimi Njia, ukweli na uzima, ni maneno ambayo tumeyasoma na kuyasikia mara nyingi sana.  Tunafahamu njia aliyoitia Yesu kuwa ni njia ya Msalaba na hiyo ndiyo anayotualika sote na kila mmoja wetu kuipokea na kuipitia hadi mwisho. Tunafahamu kwamba yeye ndiye Ukweli: ndiye ufunuo wa kweli za kimungu na msingi wa kweli zote za kumhusu mwanadamu. Na Yeye ndiye uzima. Ndiye kitulizo cha waamini wake tuwapo duniani na tuzo letu mbinguni. Yeye ndio uzima tunaoupokea katika Neno na Sakramenti alizotuachia. Neno la Mungu huwezi kulisoma au kulisikia kama habari ambayo tayari unaifahamu.

Neno la Mungu kila wakati linaleta upya katika maisha ya mwamini
Neno la Mungu kila wakati linaleta upya katika maisha ya mwamini

Neno la Mungu ni jipya. Kila unapolipa nafasi linakuletea mwanga mpya wa ufunuo wa kimungu katika wakati na mazingira uliyopo. Ndiyo maana mara nyingi tunasema Biblia sio andiko ambalo mtu anakwenda kulisoma ili kudadisi kilichomo, bali Biblia ni andiko linaloyafunua maisha ya yule anayelisoma. Binafsi ninapoyasoma na kuyasikia maneno haya na hata sasa ninapoyatafakari pamoja nawe ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, ninavutwa kumpokea Yesu kama kila kitu katika maisha yangu. Yeye ni kila kitu kwa sababu ni katika yeye jinsi nilivyo, vile nivionavyo, vile nisivyonavyo, yaliyopita, yaliyopo na yajayo katika maisha yangu yanapata umaana wake. Bila yeye vyote hivyo havina uzito. Na ni Yesu mwenyew anayejitambulisha hivyo kwangu. Hili sio wazo ninalolijenga mwenyewe. Njia, ukweli na uzima ni vitu vitatu vinavyobeba matamanio na mahitaji ya kila binadamu. Njia ndiyo mahitaji ya kimwili, ukweli ndio mahitaji ya kiakili, uzima ndio mahitaji ya kiroho na ndiyo ile amani ya roho ambayo sote tunaitafuta. Kati ya vitu hivi vitatu kikikosekana kimoja vile viwili vinavyobaki huwezi kuvifurahia. Na katika ulimwengu huu hakuna anayeweza kukupatia vyote hivi vitatu ila Yesu tu. Leo Yesu huyu anagonga tena mlango wa maisha yako akisubiri umwambie “karibu” ili aingie ndani. Anagonga akisema mimi ndimi njia unayoitafuta, mimi ndimi ukweli utakaoangaza giza la ufahamu wako na mimi ndimi uzima utakaokufanya uendelee kupata ladha ya maisha baada ya kuwa umeipoteza katika hayo yaliyokutokea. Tuitikie mwaliko huu tukiyafanya kuwa yetu maneno ya Zaburi ya wimbo wa katikati katika dominika hii “upendo wako Bwana uwe pamoja nasi, ndiwe tumaini letu."

Liturujia D5 ya Pasaka
05 May 2023, 16:27