Tafuta

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 44 wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, Kitaifa uliofanyika mjini Bagamoyo, mkoani Pwani kuanzia tarehe 9 -11 Juni 2023: Mpango kazi wa WAWATA kwa Mwaka 2023-2026 Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 44 wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, Kitaifa uliofanyika mjini Bagamoyo, mkoani Pwani kuanzia tarehe 9 -11 Juni 2023: Mpango kazi wa WAWATA kwa Mwaka 2023-2026 

Mkutano Mkuu wa 44 Mpango Kazi wa WAWATA Kuanzia Mwaka 2023 -2026: Utu wa Binadamu!

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA Taifa katika makala hii, anatoa muhtasari wa semina iliyofanyika wakati wa maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 44 wa Kitaifa uliofanyika mjini Bagamoyo, Vipaumbele vya miaka mitatu pamoja na mpangokazi wa WAWATA kwa mwaka 2023-2024 unaopaswa kuanza kutekelezwa mara moja. Unazingatia mikakati ya mpango endelevu wa muda mrefu na vipaumbele vya Mkutano mkuu wa 44 wa WAWATA Kitaifa.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Bagamoyo, Pwani, Tanzania.

Mkutano Mkuu wa 44 wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA Taifa, hulifunguliwa rasmi tarehe 9 Juni na kuhitimishwa tarehe 11 Juni 2023. Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA Taifa katika makala hii, anatoa muhtasari wa semina iliyofanyika wakati wa maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 44 wa Kitaifa uliofanyika mjini Bagamoyo, Vipaumbele vya miaka mitatu pamoja na mpangokazi wa WAWATA kwa mwaka 2023-2024 unaopaswa kuanza kutekelezwa mara moja. Mpangokazi wa mwaka 2023/24 unatokana mapendekezo ya vipaumbele vya mpango kazi wa miaka mitatu 2023-2026 kama ulivyowasilishwa katika Mkutano mkuu wa 44 ukizingatia mpango kazi wa miaka minne 2023-2027 uliopitishwa kwa ajili ya utekelezaji   katika ngazi zote za WAWATA kama sehemu ya Jumuiya za Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO (World Union of Catholic Women Organisations). Pia umezingatia vipaumbele vya Mkutano Mkuu wa 44, semina zilizotolewa wakati wa Mkutano mkuu wa 44, Malengo ya Sinodi na kwa namna ya pekee, kuendelea kuwafikia wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii bila kujali imani zao, umri au jinsia! Ushuhuda wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji yam tu mzima: kiroho na kimwili. KAULI MBIU: Wanawake Wakatoliki Wajenzi Stadi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu kwa Dunia ya Amani – (women of wucwo artisans of human fratenity for world peace). Lengo kuu: Wanawake Wakatoliki Duniani tunaitwa kuwa kweli wajenzi wa amani kwa kuishi maisha ya kuweka mbele maridhiano, utu wema, ubinadamu; udugu na mshikamano.”

Wakurugenzi wa utume wa walei kutoka majimbo mbalimbali ya Tanzania
Wakurugenzi wa utume wa walei kutoka majimbo mbalimbali ya Tanzania

UTEKELEZAJI UTAZINGATIA YAFUATAYO: MIKAKATI YA MPANGO endelevu wa Muda Mrefu: WAWATA itajikita katika malezi ya familia kwa kuitia wito wa Baba Mtakatifu wa kuanza kwa ari mpya safari ya maisha ya upendo ndani ya familia; (rej: Kauli mbiu ya mkutano wa kumi wa familia duniani Juni 2022, ‘Upendo wa Familia wito na njia ya Maisha ya Utakatifu’; pamoja na Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia,” “The Joy of Love.” Nguvu zaidi ziwekezwe kwa mtoto wa kiume ambaye kwa kiasi amesahaulika kwa muda mrefu. WAWATA itaendela na juhudi zilizoanza kwenye mpango kazi wa 2019 za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kutetea uhai kwa kutoa elimu zaidi kwa watoto na vijana. Utunzaji wa Uumbaji/mazingira – kwani dunia yenye afya inatutegemea sote ‘A healthy planet depends on all of us’ (rej. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.”). WAWATA itaendeleza na kuimarisha kazi ya utafiti kuhusu nyanyaso kwa wanawake na watoto na wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii kupitia mradi wa World Women Observatory (WWO) wakishirikiana na nchi nyingine za Afrika kwa kuwa na mpango mathubuti wa kuwatambua na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili. WAWATA Itatetea uhuru wa kuabudu kama msingi wa njia ya kujenga udugu wa kibinadamu na kuleta amani, sawa na Waraka wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” kwa kushirikiana na dini na madhehebu mengine kutafuta suluhu ya changamoto mtambuka katika jamii zinazosababishwa na migogoro ya kidini na kiimani.

Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika
Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika

WAWATA itawekeza katika malezi ya wanawake na vijana ili kupitia uongofu wa kiroho, kiakili na kichungaji, kusikiliza, mang’amuzi, mazungumzo na vitendo waweze kutembea pamoja na wanaume na Wakleri katika kujenga Kanisa mahalia. Tunaamini kuwa tutajitahidi kumwezesha kila mmoja kushiriki majukumu ya Kanisa ni jukumu muhimu la kikanisa; rej: Papa Francisko Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.  Kundelea kutoa elimu kuhusu Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ili kuwasaidia waamini wengi kujiandaa kupokea Ekaristi vizuri zaidi kadiri ya maelekezo ya Baba Mtakatifu Francisko tukirejea Waraka wake wa Kitume wa “Desiderio desideravi” of the Holy Father Francis On the Liturgical Formation of The People of God.” Yaani “Kuhusu Majiundo ya Kiliturujia ya Watu wa Mungu.” WAWATA itashirikiana na vyama vingine vya kitume hasa UWAKA kutoa elimu ya uraia na siasa ili kushiriki kikamilifu uchaguzi serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025. Kuendeleza mpango wa kutafuta kitega uchumi cha kudumu kitakachokidhi mahitaji ya kiutawala na kiuchumi cha WAWATA kwa kutumia jengo na kiwanja cha Ilala kama mtaji. Kuitikia wito wa Baba Mtakatifu Francisko, anayetualika kushiriki kujenga mustakabali wa wahamiaji na wakimbizi. WAWATA watashirikiana na mashirika ya kijamii na WUCWO kupitia na kupendekeza marekebisho katika sheria za Kimataifa zinazohusu wakimbizi na wahamiaji.

Wajumbe wa Mkutano mkuu
Wajumbe wa Mkutano mkuu

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu: “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Kwa kutambua kiu ya wanawake wengi kutembelea Madhabahu ya Mama Bikira Maria na kwa kuzingatia kipaumbele cha Kanisa la Ulimwengu kuutangaza Mwaka Mtakatifu 2025, WAWATA wataandaa hija za ndani katika kituo cha Hija cha Bagamayo kwenye Groto la Bikira Maria lenye hadhi sawa na Fatima, Nyakijoga yenye hadhi sawa na Lourdes, Kawekamo, Ifucha, Loleza, Kilema, Sukamahela, Kiabakari na pia hija za nje kwenda Kibeho, Rwanda, Italia, Ureno na Ufaransa. 

Mama Evaline Malisa Ntenga. MWENYEKITI WAWATA TAIFA.

WAWATA Vipaumbele
13 June 2023, 14:42