Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Kitovu na Chemchemi ya Maisha ya Kanisa
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu mwaka A wa Kiliturujia. Sherehe hii kimsingi inapaswa kuadhimishwa siku ya Alhamisi Kuu, siku ambayo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu akiwaagiza wanafunzi wake akisema; “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Lk. 22:19). Kwa kuamuru hivyo Yesu alitaka fumbo la mwili na Damu yake liadhimishwe nyakati zote. Katika sikukuu hii tunaadhimisha tena ukumbusho wa Karamu ya Mwisho. Tulipoadhimisha karamu ya Yesu siku ya Alhamisi Kuu jioni, hatukuweza kufanya hivyo kwa shangwe kwa sababu tulikuwa katika Juma Kuu tumeukaza uso wetu na kuelekeza mioyo yetu katika tafakari ya mateso, kifo na ufufuka wake. Hivyo Mama Kanisa anatupa nafasi ya kurudia kuadhimisha sherehe hii Alhamisi baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu au dominika baada ya Utatu Mtakatifu ili kuwapa nafasi waamini wengi zaidi washiriki katika kumshangilia na kumshukuru Kristo kwa ajili ya zawadi kubwa ya kubaki na kukaa nasi nyakati zote katika Ekaristi Takatifu - Mwili na damu yake mwenyewe inayotukumbusha kufa na kufufuka kwake kama sala ya mwanzo inavyotilia mkazo; “Ee Mungu, umetuachia ukumbusho wa mateso yako katika sakramenti ya ajabu. Tunakuomba utujalie kuyaheshimu mafumbo matakatifu ya mwili na damu yako, tupate daima neema ya ukombozi wako ndani yetu”. Ekaristi Takatifu ni chakula chetu cha kiroho ndiyo maana wimbo wa mwanzo unaisistiza kuhusu kula; “Nimewalisha kwa unono wa ngano na kuwashibisha kwa asali itokayo mwambani” (Zab. 80:17). Kutokana na umuhimu wa Ekaristi Takatifu katika maisha ya Kanisa, basi tutafakari japo kwa kifupi sana masomo tunayoyasoma katika sherehe hii ili tupate nafasi ya kujikita zaidi katika tafakuri ya kina mafundisho kuhusu Ekaristi Takatifu.
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kum.8:2-3; 14-16a). Somo hili linatueleza jinsi Waisraeli walipokuwa jangwani walivyolazimika kujifunza kumtegemea Mungu katika mahitaji yao ya maisha yaki la siku. Maana huko jangwani hawakuweza kujipatia chakula isipokuwa manna aliyowashushia Mungu mwenyewe kutoka mbinguni. Chakula hicho ni mfano wa Ekaristi Takatifu katika Agano Jipya ambayo ndicho chakula chetu cha kiroho. Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 10:16-17). Somo hili linatueleza kuwa wanaopokea Ekaristi Takatifu humpokea Yesu mzima na huunganika Kristo na kwa kuunganika naye huunda umoja kati yao akisema: “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja”. Na Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 6:51-58) inatusihi na kutuasa kuwa tusadiki kuwa Yesu Kristo ni chakula cha kweli na cha uzima, sababu Kristo ametoa uhai wake ili kutupa sisi uzima wa Kimungu. Hivyo tukitaka kweli kupata uzima wa milele na kushiriki furaha za mbingu inatupasa kumpokea Yesu katika Ekaristi Takatifu. Sasa tujikite kwenye mafundisho msingi ya Kanisa kuhusu Ekaristi Takatifu. Neno Ekaristi asili yake ni neno la Kigiriki Eucharistein likimaanisha shukrani. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya shukrani kwa kukombolewa kwa Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Sadaka hii pia huitwa Misa Takatifu, Sadaka Takatifu ya Misa, Karamu ya Bwana, Kumega mkate, Kusanyiko la Kiekaristi, Ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana, Liturujia Takatifu, Sakramenti Takatifu sana ya Altare na Komunyo Takatifu. Kiujumla Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo waamini humpokea Kristo na roho hujazwa neema na kupewa amana ya uzima wa milele (KKK 1322 – 1323, 1409). Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo anaungana na Kanisa lake na waamini wake wote kwa sadaka ya sifa na shukrani iliyotolewa mara moja msalabani kwa Mungu Baba. Kwa sadaka hii anamimina neema za wokovu kwa mwili wake ambao ni Kanisa (KKK 1407).
Papa Leo XIII anasema; Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa (Denz.3364). Kimsingi, Ekaristi Takatifu ni kiini kamili cha Kanisa, na Kanisa haliwezi kitu pasipo Ekaristi Takatifu, kwasababu ni Kristo mwenyewe anayejitoa kweli kama sadaka kwa ajili ya Kanisa katika Ekaristi Takatifu na ni katika hiyo Kanisa hufikia uhalisia wake wa juu wa asili yake, yaani, kuwa linaonekana, la daima, na alama wazi ya neema ya wokovu ya Mungu iliyopo duniani kupitia Kristo. Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Katika Ekaristi Takatifu tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo na kilele cha tendo la watu kumwabudu Mungu katika Kristo hufanyika. Katika Ekaristi Takatifu mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu. Ekaristi Takatifu ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule wa Taifa la Mungu ambao unalifanya Kanisa liwepo. Kwa njia ya adhimisho la Ekaristi Takatifu tunaungana tayari sisi wenyewe na liturujia ya mbinguni na tunaanza kushiriki uzima wa milele (KKK 1324 – 1327). Katika sadaka ya Ekaristi Takatifu, Kanisa hutolea maisha, masifu, mateso, sala na kazi za waamini na kuyaunganisha na yale ya Kristo kwa Mungu Baba. Kwa vile ni sadaka, Ekaristi Takatifu hutolewa kwa waamini wote, wazima na wafu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na kupata rehema ya Mungu. Kanisa la Mbinguni pia linaungana na matoleo ya Kristo. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti mojawapo kati ya sakramenti saba za Kanisa - alama wazi zilizowekwa na Yesu Kristo mwenyewe ili kutuletea neema ya wokovu. Ekaristi Takatifu ni sakramenti inayokamilisha tendo zima la kumwingiza Mkatukumeni katika ukristo. Tofauti na sakramenti zingine Ekaristi Takatifu ni Kristo mwenyewe katika maumbo ya mkate na divai. Ni Sakramenti ya Sakramenti (KKK. 1211). Mtakatifu Tomaso wa Akwino anasema; Sakramenti zingine zote zimeimarishwa kwake kama ndio mwisho wa Sakramenti hizo. Uwepo wa Kristo katika Ekaristi Takatifu unaiinua sakramenti hii juu zaidi kuliko sakramenti zingine ukiwa ndio utimilifu wa maisha ya kiroho na ndio mwisho ambao sakramenti zote hulenga kwani ndani yake kuna mwili na damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, kweli, halisi na uwamo kamili pamoja na roho na umungu wake na hivi ni Kristo mzima kabisa (KKK 1374).
Mababa wa Mtaguso wa Trento walitoa tamko kuwa: “Kwa sababu Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba ulikuwa ni mwili wake kweli ambao alikuwa anautoa sadaka kwa namna ya mkate na damu yake halisi kwa namna ya divai, imekuwa tayari imethibitishwa kwa Kanisa la Mungu, kwamba kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate na divai kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na ya kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake (1376). Uwepo huu huanza dakika ya mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwepo. Hivyo Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao, kwa jinsi hii kwamba kuimega Ekaristi Takatifu hakumgawanyi Kristo hata kidogo” (KKK 1377), uwepo wake unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika na hata katika kila tone la damu yake uwepo wake umo kamili kabisa kama katika Ekaristi Takatifu nzima. Huu ni ukweli wa kiimani aliotufunulia Kristo mwenyewe, na imani tu yaelewa. Chanzo na asili ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Yesu Kristo mwenyewe alipoiweka siku ile ya Alhamisi kuu, alipokula karamu ya mwisho pamoja na wanafunzi wake kwenye chumba cha juu-Cenaculum, usiku ule alipojitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yetu siku zote mpaka atakaporudi kwa utukufu (1Kor. 11:23 -26, KKK. 1337). Uwezo wa kuugeuza mkate kuwa mwili wake na divai kuwa damu yake, Yesu Kristo mwenyewe aliwapa Maaskofu na Mapadre wote wa Agano Jipya kwa njia ya mitume (Lk 2:19; 1Kor 11:23-25).
Mtaguso wa Pili wa Vatikano unathibitisha kwamba, Ekaristi Takatifu ni “Chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo” (Lumen gentium11), na “chemchemi na kilele cha uinjilishaji wote” (Presbyterorum Ordinis 5). Kumbe Ekaristi Takatifu inaunda Kanisa na Kanisa linaitengeneza Ekaristi Takatifu, na ndimo linamochota nguvu ya kiroho. Hivyo hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza kujengwa na kusimama imara bila adhimisho la Sakramanti Kuu ya Ekaristi Takatifu (Presbyterorum Ordinis 6). Katika Ekaristi Takatifu fumbo la Ukombozi wetu linawekwa hai na kufikia kilele chake wakati yanapotamkwa maneno ya konsekrasio: “Huu ndio Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na Hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu”, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Luka 22:19-20). Sisi sote tunaalikwa kwenye karamu hii ili tuweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo maana yeye mwenyewe anasema; “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yn 6:56-57). Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, hivyo inatuunganisha na watu wote kwa muda wote bila kujali tofauti zetu za aina yoyote ile. Kwa maana Kristo anasema; “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu nami ndani yake.” Kwa kuwa tunakuwa kile tunachokula, tukila mwili na kunywa damu yake tunakuwa na ukristo ndani mwetu tunakuwa kitu kimoja, ndiyo maana tunaitwa wakristo. Mbele ya Ekaristi Takatifu, tofauti zetu za kisiasa, kikabila, kivyama, kitaifa au kirangi, hazipaswi kuwa na nafasi kwa kuwa kila mmoja ana Ukristo ndani yake na Ekaristi Takatifu inatupatia msamaha wadhambi nasi tunapaswa kusameheana na kuwa wamoja kwani adhimisho la Ekaristi Takatifu ni tendo la toba linalotutakasa kabisa kutokana na dhambi ndogondogo, linatupa nguvu katika vita dhidi ya uovu na hutuepusha na kuanguka tena dhambini. Mtakatifu Ambrosi anasema; “Ekaristi Takatifu ni mkate wetu wa kila siku kwa ajili ya dhambi zetu za kila siku, inatupatia silaha bora dhidi ya vishawishi.”
Lakini kwa habari ya dhambi za mauti, Sakramenti ya Kitubio ni ya lazima na haiepukiki. Ndiyo maana Didache yaani mafundisho ya mitume inasema; “Pasiwepo mtu wa kunywa wala kupokea Ekaristi Takatifu pamoja nanyi isipokuwa wale tu waliobatizwa kwa jina la Bwana, kwa maana ilikuwa ni kwa marejesho ya jambo hili kwamba Bwana alisema; “Msiwape mbwa vitu vitakatifu” (Mt. 7: 6). Ifikapo siku ya Bwana baada ya kukusanyika na kuwa pamoja, mtamega na kutoa Ekaristi Takatifu, baada ya kuungama makosa yenu, kusudi sadaka yenu iweze kuwa safi. Lakini asiruhusiwe mtu yeyote aliye na ugomvi na jirani yake ajiunge nanyi mpaka awe amefanya usuluhisho, la sivyo sadaka yenu ni batili” (Didache 9,14,1-2). Hivyo, kwa mkristo kuinua upanga dhidi ya mwingine ni kwamba anajiinulia upanga mwenyewe na anamuinulia Kristo upanga. Hivi ndivyo alivyomwambia Paulo alipokuwa anawatesa Wakristo; “Saulo, Saulo, kwanini wanitesa … Ni mimi Kristo unayenitesa” na ndiyo maana anasema; “chochote ulichowatenda hawa wadogo umenitendea mimi.” Ekaristi Takatifu yatufanya tujitoe mhanga kwa maskini (KKK 1391 – 1397, 1416). Kumbe, ni hasara kubwa sana kutopokea Ekaristi Takatifu kwa kuwa umejiwekea vizuizi, umejifungia. Wale wasiopokea Ekaristi Takatifu nawasihi fanyeni bidii kubomoa kuta za vizuizi mpokee Ekaristi Takatifu, ili muungane na jamii ya waamini katika Ekaristi Takatifu na kuwa kweli wakristo. Tukiwa na tofauti katika familia, katika nafasi za kazi, katika vyama vyetu vya siasa, tuiangalie Ekaristi Takatifu ili iwe sababu yetu ya kusameheana, kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana kwa kuwa Ekaristi Takatifu inatuunganisha inatufanya tuwe wamoja. Ndiyo maana maneno ya wimbo wa komunyo unaopendekezwa yanasema; “Bwana asema: Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake (Yn. 6:51). Nayo sala ya kuombea dhabihu inakazia kusema; “Ee Bwana, tunakuomba kwa wema wako ulijalie Kanisa lako neema ya umoja na amani; kwa maana umoja na amani huonyeshwa kwa fumbo katika dhabihu hizi tunazokutolea”. Kwa namna hii tunaanza kuonja furaha za mbinguni tungali bado tuko duniani kama sala baada ya komunyo inavyohitimisha maadhimishoya sherehe hii ikisema; “Ee Bwana, tunakuomba utujaze na furaha isiyo na mwisho ya kuutazama umungu wako. Tunaona ishara ya furaha hiyo hapa duniani katika kupokea Mwili na Damu yako takatifu.” Tumsifu Yesu Kristo.