Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Maana, Ukuu na Umuhimu wa Ekaristi Takatifu Katika Maisha ya Kanisa
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli) Italia.
Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake “Ecclesia De Eucharistia” yaani “Kanisa la Kiekaristi” ya Aprili 17, 2003 anasema kuwa “Kanisa linaishi kutokana na Ekaristi” (rejea namba 1). Kwa maneno mengine, Ekaristi ndio uhai wa Kanisa. Kwa kuwa Kanisa kwa maana halisi siyo jengo bali “jumuiya ya waamini katika Kristo,” basi tunapaswa kujua kuwa Ekaristi ndio uhai wa kili mwamini. Ni katika Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa anatufunulia maana, uzuri na umuhimu wa Ekaristi Takatifu. Somo letu la kwanza (Kum. 8:2-3, 14-16) ni sehemu ya wosia wa Musa kwa wana wa Israeli. Anawakumbusha wema wote aliotendewa na Mungu wakiwa jangwani na kwa namna ya pekee jinsi Mungu alivyowalisha kwa mana - chakula cha ajabu kilichoshuka toka mbinguni. Chakula hiki cha upendeleo wa pekee (yaani mana) ambacho hata baba zao hawakukijua wala kukionja ni kiashiria cha Ekaristi Takatifu, yaani mwili wa Kristo ulioshuka toka mbinguni. Kama vile mana ilivyokuwa kielelezo cha upendo na wema wa Mungu kwa watu wake waliosafiri jangwani, ndivyo na Ekaristi Takatifu (Mwili na Damu ya Kristo) ilivyo chakula cha uzima wa milele ambacho kwa wema na upendo wake Mungu anatujalia sisi tulio safarini hapa duniani: Ndiyo chakula cha wasafiri wenye raha ya milele, sio mkate wa kafiri. Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya somo la kwanza na somo la Injili kwa maana mana waliyokula Waisraeli jangwani ilikuwa ni kiashiria cha Ekaristi Takatifu, yaani mwili wa Kristo unaotolewa kwa ajili ya taifa jipya la Israeli (Wakristo). Hivyo Mwinjili Yohane anafungua akili na mioyo yote kutambua kuwa mana halisi ni Mwili na Damu ya Kristo (Ekaristi Takatifu).
Hivyo tulitazame kwa undani somo letu la Injili (Yn. 6:51-58). Katika somo letu la Injili tunafunuliwa kuwa “Ekaristi Takatifu ni Mwili kweli na Damu kweli ya Bwana Wetu Yesu Kristo- ndiyo mwili wake utupatiao uzima wa milele.’’ Injili yetu ya leo inatoka kwenye Injili ya Yohane. Moja ya tabia ya Injili ya Yohane ni kwamba anachozungumza Yesu kinaeleweka tofauti kwa wasikilizaji wake. Hebu tuone mifano michache: Yesu anapomwambia Nikodemo kuwa mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuingia mbinguni, Nikodemo anaelewa kuwa ni lazima mtu arudi tena tumboni mwa mamaye na kisha azaliwe tena kwa mara ya pili, ilihali Yesu alikuwa anamaanisha kubatizwa (kubatizwa ni kuzaliwa kwa mara ya pili); Yesu alipomwambia mwanamke Msamaria kuwa Yeye ni maji ya uzima, mwanamke alifikiri Yesu anaongelea maji yanayotiririka tofauti na maji yaliyotuama, ilihali Yesu alikuwa anaongelea kuwa Yeye ni chechemi ya neema ambazo humpatia mtu uzima. Hata katika Injili ya leo tabia ni ileile: mzungumzaji (Yesu) anamaanisha kitu fulani, lakini wasikilizaji [wa Yesu] wanaelewa tofafauti. Yesu anaposema “aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele” wasikilizaji wanaelewa tofauti: wasikilizaji wake wanafikiri kuwa Yesu anasema wachukue nyama ya mwili wake, waipike na kisha kuila. Mawazo haya ndiyo yaliyowafanya warudi nyuma (waondoke mmoja mmoja) na waache kufuatana naye. Bila shaka kama binadamu walisema, “huyu jamaa vipi? Hivi watu wengine wakisikia kuwa tumeanza kula nyama za binadamu watatuelewaje?” Hata hivyo Yesu alimaanisha kuwa Ekaristi Takatifu ni Yeye mwenyewe: mwili wake, damu yake, roho yake na umungu wake.
Maneno ya Yesu, “Mwili wangu ni chakula cha kweli… damu yangu ni kinywaji cha kweli” (Yn. 6:55) yanahitaji tafsiri sisisi, na wala si vinginevyo. Tafsiri sisisi ni tafsiri inayotokana na maneno kadiri yalivyotumika katika kifungu husika. Yesu anaposema “mwili wangu ni chakula cha kweli” anamaanisha kweli mwili wake ni chakula, na wala siyo mfano wa chakula au kiashiria cha chakula- bali ni chakula kweli, ni chakula halisi. Hiyo ndiyo tafsiri sisisi- haihitaji kukamilishwa, kupunguzwa wala kuboreshwa. Inajitosheleza kabisa. Baada ya Yesu kusema, “Mwili wangu ni chakula cha kweli… damu yangu ni kinywaji cha kweli,” yalifuata mabishano/mashindano yaliyowafanya wengi miongoni mwa wanafunzi wake kuacha kuandamana naye (rejea Yn. 6:66-69) maana fundisho la Yesu kuwa mwili wake ni chakula cha kweli na damu yake ni kinywaji cha kweli lilikuwa gumu sana “kwa wasikilizaji na wafuasi wake” kama lilivyo gumu hadi leo kwetu sisi wafuasi na hata wasio wafuasi. Baada ya wanafunzi kuanza kuondoka Yesu hakuwakimbilia kuwarudisha akisema “rudini, hamkunielewa, sikumaanisha kuwa mwili wangu ni chakula bali nilimaanisha ni mfano tu wa chakula, ni ishara tu ya chakula.” Yesu hakusema hivyo na wala hakuwaambia warudi. Katika masuala ya imani Yesu hakubembeleza mtu. Yesu alikuwa tayari kupoteza wanafunzi hata wote ikibidi kuliko kupindisha ukweli kuwa mwili wake ni chakula cha kweli na damu yake ni kinywaji cha kweli. Kitendo cha Yesu kutosahihisha mafundisho yake na kutowarudisha wale waliokuwa wanaondoka kinamaanisha kuwa yale aliyosema ndiyo aliyomaanisha.
Hata hivyo, kuna watu wanajenga hoja ambazo hazina mashiko kupinga fumbo la Ekaristi. Moja ya hoja zao zipo hivi: Yesu alisema, “Mimi ndimi mzabibu wa kweli” (rejea Yn. 15:1), sasa mbona Wakatoliki hamfundishi kuwa Yesu yumo kweli katika mti wa mzabibu kwa umungu wake, kwa roho yake, kwa mwili wake na kwa damu yake? Mbona mnafundisha uwepo wa Yesu katika maumbo ya mkate na divai ati kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate wa uhai” (rejea Yn. 6:35)? Jibu la hoja hii ni rahisi sana. Mjibizo (reaction) wa wasikilizaji wa Yesu ulitofautiana pale aliposema “Mimi ndimi mzabibu wa kweli” na pale aliposema “Mwili wangu ni chakula cha kweli… damu yangu ni kinywaji cha kweli.” Aliposema, “Mimi ndimi mzabibu wa kweli” hakuna mfuasi aliyeacha kuandamana na Yesu; lakini aliposema “Mwili wangu ni chakula cha kweli… damu yangu ni kinywaji cha kweli” wafuasi wake walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine, wakaacha kuandamana naye maana fundisho hilo lilikuwa gumu kwao kulielewa. Kwa nini kuna utofauti wa mjibizo (reaction)? Yesu aliposema, “Mimi ndimi mzabibu wa kweli” wanafunzi/wafuasi wake walijua wazi kuwa alikuwa anatumia lugha ya kistiari/ lugha ya picha (figurative language), na ndiyo sababu hawakuacha kuandamana naye. Lakini Yesu aliposema, “Mwili wangu ni chakula cha kweli… damu yangu ni kinywaji cha kweli,” wanafunzi/wafuasi wake walijua wazi kuwa Yesu alimaanisha alichosema, na wala haikuwa lugha ya kistiari/lugha ya picha (figurative language) na ndiyo maana walishtushwa na maneno ya Yesu na kuanza kuondoka. Hivyo, Yesu alimaanisha kwa dhati kuwa mwili wake ni chakula cha kweli na damu yake ni kinywaji cha kweli.
Kadhalika, huwa kuna swali naulizwa mara nyingi: sasa kama Yesu alizungumzia kuwa mwili wake ndio chakula cha kweli na damu yake ndio kinywaji cha kweli, mbona ninyi Wakatoliki mnazungumzia habari ya mkate na divai wakati wa Misa? Huwa nawapatia jibu kwa kuwarejesha kwenye Karama ya Mwisho (rejea Lk. 22: 14-20) na kuwauliza, “Je, Yesu aliposema huu ni mwili wangu na hii ni damu yangu alikuwa ameshika nini katika mikono yake? Jibu ni kwamba alikuwa ameshika mkate na kikombe cha divai. Hivyo, Yesu aligeuza mkate kuwa mwili wake na divai kuwa damu yake. Mara baada ya Padre kurudia maneno aliyotamka Yesu mwenyewe wakati wa Karamu ya Mwisho, mkate hugeuka kuwa mwili wa Yesu na divai hugeuka kuwa damu ya Yesu (Ekaristi Takatifu). Hivyo Ekaristi Takatifu ni Mwili kweli na Damu kweli ya Bwana Wetu Yesu Kristo. Mwisho, katika somo letu la pili (1Kor. 10:16-17), Mtume Paulo anajikita kutoa katekesi juu ya Ekaristi Takatifu ambayo tumeelezwa katika Injili na ambayo iliashiriwa katika somo la kwanza. Mtume Paulo anatukumbusha kuwa tunaposhiriki Ekaristi Takatifu tunakuwa na ushirika na Kristo na ya kwamba Ekaristi Takatifu ni kielelezo na kifungo cha umoja maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja, hivyo tunakuwa wamoja katika Kristo. Lakini tunapaswa kujua kuwa suala si kushiriki tu Ekaristi Takatifu, tena kushiriki kwa mazoea bali kushiriki Ekaristi Takatifu tukiwa na moyo safi na kwa uchaji. Hivyo inatupasa mara kwa mara kujitafiti ndani ya mioyo yetu kama kweli tunastahili kushiriki Ekaristi Takatifu, vinginevyo tutakuwa tunapokea hukumu yetu sisi wenyewe kama anavyotuonya Mtume Paulo (rejea 1Kor. 11:27-29). Sherehe njema ya Ekaristi Takatifu.