Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Ufunuo wa Upendo
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Dominika baada ya Pentecoste Kanisa huadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu, Sherehe ambayo kwa njia yake tunamkiri na kumtukuza Mungu mmoja aliyejifunua katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Nafsi tatu si miungu watatu, ni utatu wa nafsi katika Mungu mmoja. Utatu Mtakatifu ni fumbo la kimungu na kwa sababu linagusa moja kwa moja undani wa Mungu mwenyewe undani ambao mwanadamu kwa uwezo wake hawezi kuuingia kuupambanua. Kumbe licha ya kuwa sherehe ya kuadhimisha kiri ya imani yetu juu ya Mungu mmoja katika nafsi tatu, ni sherehe inayotualika kuielekeza akili, mioyo na utashi wetu kumuelekea Mungu ambaye hujifunua kwetu kila siku ya maisha yetu. Ufafanuzi wa Masomo: Masomo yote matatu ya dominika hii yanakazia kuonesha kuwa upendo ndio sifa inayomtambulisha Mungu katika asili yake, katika utendaji wake na katika namna anavyohusiana na mwanadamu. Katika somo la kwanza, somo linalotoka katika kitabu cha Kutoka (Kut. 34:4b-6, 8-9), Mungu anajitambulisha kwa Musa. Mwanzoni katika kitabu hiki hiki cha Kutoka, wakati ambapo Mungu alimwita Musa ili amtume kwa Farao, Musa alitaka kujua jina la Mungu huyu anayemtuma. Mungu akalifunua jina lake kuwa ni “Mimi Niko ambaye Niko” (Kut. 3:14). Leo anachokifunua si jina bali asili yake. Musa amepanda mlima Sinai ili Mungu aandike upya amri zake 10 baada ya Musa kuvunja mawe yaliyokuwa na amri 10 alipoona uasi wa Haruni na wa Waisraeli.
Kabla ya kuandika upya Amri 10, Mungu anajitambulisha kuwa Yeye ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli, mwenye msamaha na asiyetunza hesabu ya maovu. Sifa zote hizi tunaweza kuziunganisha katika neno moja tu – upendo. Upendo wa Mungu unabeba sifa zote hizo na unatambulisha sifa yake. Mtume Yohane katika waraka wake anaandika akisema Mungu ni upendo: “Yeye apendaye amezaliwa na Mungu naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa hamjui Mungu kwa maana Mungu ni upendo” (1Yoh 4:7-8). Somo la pili ambalo linatoka katika Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho linatupatia maneno ambayo tunayasikia daima mwanzoni mwa Misa: “neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote.” Paulo anatumia maneno hayo kuhitimisha mausia aliyowaandikia wakorintho. Haya ni maneno ambayo wachambuzi wa Maandiko Matakatifu wanatuonesha kuwa sio maneno ya Paulo bali ni maneno ambayo tayari wakristo wa mwanzo kabla ya Paulo walikuwa wakiyatumia katika mikutano yao ya sala. Ni maneno yanayoonesha kuwa tangu mwanzo wakristo waliukiri Utatu Mtakatifu. Kwa wakristo hao wa mwanzo, Utatu Mtakatifu ulikuwa ni mwaliko wa Mungu na kichocheo kwa mwanadamu kuuishi ubinadamu mtakatifu katika Neema, Upendo na Ushirika.
Tukiingia sasa katika Injili ambayo katika dominika ya Utatu Mtakatifu inatoka kwa mwinjili Yohane Injili (Yoh 3:16-18), tunalikuta tena lile wazo la somo la kwanza. Mungu aliyejifunua kwa Musa kama ni Mungu mwenye upendo, anaudhihirisha upendo wake kwa kumtuma mwanae ulimwenguni ili aukomboe ulimwengu. Katika kifungu hiki cha Injili ya Yohana, neno ulimwengu linamaanisha ubinadamu ambao kwa mwenendo wake umejitenga na Mungu. Ni ubinadamu ambao hautaki kujishughulisha na Mungu: haufungui mlango wa moyo ili kumruhusu Mungu aingie katika maisha yake na hivi tunaweza kusema pia ni ubinadamu uliomwasi Mungu. Jibu la Mungu kwa ubinadamu huu sio hukumu bali ni upendo. Injili inasema Mungu hakumtuma mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu unaotaka kujitenga naye bali yeye alimtuma mwanae ulimwenguni ili ulimwengu uokolewe kwa njia yake. Mungu ambaye ni upendo anashughulikia wokovu wa mwanadamu. Mungu huyo huyo anaikamilisha kazi ya ukombozi wa mwanadamu na Mungu huyo huyo anaiendeleza kazi yake ya ukombozi hadi mwisho wa nyakati. Huyu ndiye Mungu anyejifunua kama Baba kama Mwana wa Pekee Yesu Kristo na kama Roho Mtakatifu.
Tafakari:Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyafafanua masomo ya Misa, turudi katika kipengele kile tulichokiweka mwanzoni kama njia ya kutusaidia kuelewa mantiki ya sherehe hii tunayoadhimisha dominika hii, sherehe ya Utatu Mtakatifu. Katika kipengele hicho tulisema kuwa sherehe hii ya Utatu Mtakatifu licha ya kuwa ni sherehe ya kuadhimisha kiri ya imani yetu juu ya Mungu mmoja katika nafsi tatu, ni sherehe inayotualika kuielekeza akili, mioyo na utashi wetu kumuelekea Mungu ambaye hujifunua kwetu kila siku ya maisha yetu. Katika hili, binafsi ninaguswa kutafakari nawe ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, mambo makuu matatu. Jambo la kwanza ni kuwa Mungu tunayemwabudu sio Mungu wa nadharia bali ni Mungu anayejidhihirisha katika maisha yetu ya kila siku. Mungu yupo na ni Mungu anayetenda na anayeendelea kutenda. Sio Mungu wa kufikirika tu ambaye anabaki akilini au moyoni katika imani, bali ni Mungu mwenye uhalisia katika maisha ya mwanadamu. Zipo nyakati na yapo mazingira ambapo mtu anapoangalia namna mambo yanavyoenda katika maisha yake na hata katika ulimwengu unaomzunguka anaanza kupata mashaka kama Mungu kweli yupo. Ni nyakati ambazo mtu anajiuliza “kama kweli Mungu yupo mbona hili liko hivi na lile linaendelea kuwa vile nk. Sherrehe ya Utatu Mtakatifu inakuja pia kutukumbusha kuwa Mungu yupo na yuko kazini. Ni Mungu muumbaji anayeendelea kuumba, ni Mungu mkombozi katika Yesu Kristo anayeendelea kukomboa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na Mungu mtakasaji anayeendelea kutakasa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Jibu lake kwa ulimwengu, kama tulivyosikia katika Injili ya Yohane, ni jibu la Upendo ili aukomboe ulimwengu na si kuuhukumu katika uharibifu. Kila tunapopiga goti kumuabudu, kila tunapoinua mikono yetu kuomba na kila tunapoinama kushukuru tunakutana na upendo wake na tunakutana na nguvu yake inayotugusa na kutujibu.
Jambo la pili ni kwamba Mungu tunayemwabudu ni Mungu aliyejifunua katika ushirika: ni Baba na ni Mwana na ni Roho Mtakatifu. Ushirika huo wa nafsi unazivuta nafsi zetu kuuingia ili nasi tuwe kitu kimoja na Mungu wetu. Mungu wetu si Mungu anayekaa mbali na watu wake, ni Mungu anayetafuta daima kushuka ili awafikie watu wake na awe kitu kimoja nao. Biblia imejaa masimulizi yanayoonesha Mungu akishuka ili kukaa na watu wake. Ushirika huu, kama tulivyoona katika ufafanuzi wa masomo unatuvuta na sisi tuuishi ubinadamu mtakatifu mithili ya Utatu Mtakatifu. Kuishi katika ushirikiano na watu katika kujenga familia, jumuiya, kanisa na jamii inayounganishwa na upendo wa Mungu. Jambo la tatu na la mwisho ni kuwa Utatu Mtakatifu unaonesha ukuu na upekee wa Mungu wetu. Tunaishi katika mazingira yenye mchanganyiko na wingi wa imani. Umoja wetu wa kijamii na ushirikiano wa kindugu hutusukuma daima kuondoa tofauti zetu ili kujikita katika yale yanayotuunganisha. Katika hili tumejikuta tunarahisisha mno kiri yetu ya imani kwa Mungu mmoja katika nafsi tatu tukijiridhisha tu kusema tunamwabudu Mungu mmoja sawa na imani nyingine. Kama wakristo wakatoliki hatupaswi kuufifisha ufunuo wa Mungu wetu katika nafsi Tatu kama ni kitu kisicho na uzito katika imani yetu. Yeye anayeniambia kuwa tunamwabudu Mungu yule yule lakini hamkiri Kristo kuwa nafsi ya pili ya Mungu Baba na wala hamkiri Roho Mtakatifu kuwa nafsi ya tatu ya Mungu ananipa mashaka kukubali kuwa mimi na yeye tunamwabudu Mungu yule yule. Kutokuona tofauti hii ya msingi ni mwanzo wa kutokuona tofauti kati ya imani Katoliki na imani za madhehebu mengine ya kikristo na yasiyo ya kikristo. Matokeo yake ni kupoteza utambulisho wa kiimani na kuififisha imani yenyewe. Ufunuo wa Mungu mmoja katika Utatu Mtakatifu ni ufunuo wa ukuu na upekee wa Mungu tunayemwabudu. Nakutakia heri na baraka za Mwenyezi Mungu katika sherehe ya Utatu Mtakatifu.