Tafakari Dominika ya 11 Ya Mwaka A Kanisa: Wito wa Utakatifu Na Kuombea Miito!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 11 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika ya kumi na moja ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni wito wa kila mwanadamu kuishi maisha ya kitakatifu. Wazo hili linajitokeza katika kuitwa na kuteuliwa kwa Taifa la Israeli kuwa taifa teule, kuitwa, kuchaguliwa na kutumwa kwa Mitume kumi na wawili na wito wa Jumuiya ya kikristo kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. Licha ya kuwa wito huu ni wa kila mtu mmoja mmoja, lakini unapaswa kijidhihirisha katika maisha ya kifamilia, kijumuiya na Kanisa kwa ujumla wake ili kumpa kila mmoja nafasi ya kuiishi amri ya mapendo kwa kutenda matendo ya huruma kwa wale anaoishi nao kwa msaaada wa neema za Mungu. Hii ni kwasababu binadamu ni kiumbe ambaye hajakamiika, ana mapungufu na bila Mungu hawezi chochote. Ndiyo maana sala ya koleta inatilia mkazo ikisema; “Ee Mungu, uliye nguvu yao wanaokutumaini, uwe radhi kusikiliza dua zetu. Na kwa kuwa pasipo wewe hatuwezi kitu sisi wanadamu dhaifu, utujalie daima msaada wa neema yako, tupate kukupendeza kwa moyo na matendo katika kutimiza amri zako”. Nasi tunaamini kuwa Mungu daima anasikiliza sala na maombi yetu tunapomuomba na kumlilia kwa moyo mnyoofu kama mzaburi anavyoimba katika wimbo wa mwanzo; “Ee Bwana, usikie, sauti yangu ninalia. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, wala usiniache, ee Mungu wa wokovu wangu” (Zab. 27:7, 9). Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kutoka (Kut. 19: 2-6). Somo hili limebeba mambo makuu matatu yanayotoa utangulizi wa maisha ya waisraeli chini ya mlima Sinai. Jambo la kwanza ni Mungu kuwakumbusha Waisraeli mambo makuu aliyowatendea katika historia ya ukombozi wao kutoka utumwani Misri.
Mungu anawaambia Waisraeli wakumbuke daima mambo aliyowatendea alipowatoa katika utumwa wa Wamisri akiwachukua juu ya mbawa za tai. Hapa ieleweke kuwa lugha inayotumika hapa ni lugha ya picha. Itakumbukwa kuwa Wamisri waliabudu mungu aliyeitwa horus. Ishara yake ilikuwa ni mwewe. Mungu anajifananaisha na tai kuwaonyesha nguvu zake zilivyo juu ya nguvu za mungu wa wamisri aliyewakilishwa kwa ishara ya mwewe. Hivyo kwa mkono wa nguvu zake aliwatoa Waisraeli kutoka utumwani Misri, nazo nguvu za mungu wa Misri na za Farao hazikuweza kulingana na nguvu za Mungu wa Israeli kwa namna alivyowaokoa wao. Hapa tunaona jinsi Mungu anavyojifunua katika historia ya mwanadamu. Jambo la pili linawahusu Waisraeli wenyewe kuchagua kuisikiliza au kutoisikiliza sauti ya Mungu, kulishika au kutokulishika Agano la Mungu na wao. Kama wataisikiliza ya sauti ya Mungu na kulishika Agano lake kwa uhuru kabisa bila kushurutishwa watakuwa watu wake Mungu. Kumbe jambo la tatu ni kuzaliwa kwa jumuiya mpya yenye muungano na Mungu wa kweli, jumuiya inayozaliwa inategemea utii na usikivu wao kwa sauti ya Mungu na uaminifu wao kwa Agano lake naye Mungu anachukua jukumu la kuwalinda na kuwakinga na kila baya litakalojitokeza mbele yao maana wao sasa watakuwa taifa teule la Mungu. Hivyo Mungu mwenyewe atawafanya kuwa watakatifu. Na zaidi sana watakuwa makuhani wake, watu waliowekwa wakfu kwa kazi ya kumtangaza Mungu wa kweli na kuwaongoza watu wote duniani kumwabudu Mungu wa kweli aliyeumba mbingu na dunia. Nayo mataifa yote watamsifu wakiona hekima, uwezo na upendo aliounyesha kwao. Ndiyo kusema kuwa watu wa Israeli waliitwa kuwaandaa watu wa mataifa mengine kumpokea Masiya, Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Nasi kwa ubatizo tumepokea neema juu ya neema kwa kushirikwa unabii, ukuhani na ufalme wa Yesu Kristo. Tumechaguliwa, tumetengwa na kuwekwa wakfu hivyo tunao wajibu wa kuwa manabii, makuhani na wafalme kwa watu wengine ambao bado hawamjui Mungu wa kweli aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo ili waweza kumjua, kumpenda na kumtumikia ili mwisho tuweza kufika kwake mbinguni kwa pamoja tukamsifu milele yote.
Somo la pili ni la Waraka Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 5:6-11). Katika somo hili Mtume Paulo anatufundisha kuwa utukufu na heri yetu ya milele ni hakika, kwa vile Mungu ametukomboa kwa damu ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo tulipokuwa bado wenye dhambi. Kama msaada wa Mungu wa kututakia ukombozi kutoka dhambi ni mkubwa hivyo, basi msaada huo utakuwa mkubwa zaidi siku ya hukumu ya mwisho kwa wale wanaoweka tumaini lao kwake. Kumbe somo hili linatonyesha tendo la upendo wa kiukombozi wa Yesu Kristo kwetu sisi wanadamu uliojidhihirisha kwa kifo chake msalabani. Huu ni ujumbe wa faraja na matumaini kwetu sisi wakristo kuwa tumepatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Hivyo tunapaswa kuwa mitume, manabii na wawakilishi waaminifu wa upendo wa Mungu kwa binadamu wote uliojifunua na kujidhihirisha kwa njia Yesu Kristo. Basi tukubali daima kuendelea kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo hasa katika Sakraenti ya kitubio kila tunapojitenga kwa dhambi zetu. Tuikimbilie daima Sakramenti hii ili tusuluhishwe na kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo anayefanya kazi hii katika nafsi za Mapadre. Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 9: 36-10:8). Sehemu hii ya Injili inatuonesha jinsi huruma ya Mungu ilivyo kuu kwa watu wake aliyoidhihirisha kwa njia ya Yesu Kristo mwanae wa pekee. Yesu anawahurumia watu kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyikwa kama kondoo wasio na mchungaji. Kisha anawaagiza wanafunzi wake – mitume kumi na wawili, wasali na kumwomba Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Kisha kuwapa amri juu ya pepo wachafu na mamlaka ya kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Anawaagiza wakaihubiri habari njema ya wokovu kuwa Ufalme wa mbinguni uko karibu na watu wake nao unajidhihirisha kwa kuponywa kwa wagonjwa, kufufuliwa kwa wafu, kutakaswa kwa wenye ukoma na watu kutolewa pepo wachafu tena bure bila malipo yoyote.
Itakumbukwa kuwa katika kuwatuma Mitume wake kabla ya kuteswa, kufa na kufufuka kwake, Yesu aliwaambia wawahubirie Wayahudi tu na wasiende kwa Wasamaria wala kwa watu wasio wayahudi akisisitiza; “Nendeni kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” (Mt. 10:5). “Nimetumwa tu kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” (Mt. 15:24). Tukirejea katika somo la kwanza tunaona kuwa hii ni kwa sababu ilikuwa mpango wa Mungu kwamba watu wa Israeli wahubiriwe habari za wokovu kwanza kabla ya watu wengine. Watakapokwisha kumpokea Kristo, na wao wawahubirie watu wa mataifa mengine. Ndiyo maana Mungu aliwaita kuwa ufalme wa makuhani. Lakini walipomkataa Masiha na kumsulibisha, mambo yakabadilika. Hawakuwa tena taifa teule la Mungu badala yake taifa jipya liliundwa kwa njia mitume, ambao baada ya kufufuka kwake na kabla ya kupaa mbinguni, Yesu aliwatuma upya akiwaambia: “Nendeni duniani kote mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la mwana na la roho mtakatifu” (Mt 28:19). Ndiyo maana katika safari zake za kitume, mtume Paulo alisisitiza jambo hili kuwa Habari Njema ilipaswa kuhubiriwa kwanza kwa Wayahudi. Lakini kwa kuwa waliikata basi aliwageukia wapagani – watu wa mataifa (Mdo 13:46). Mungu aliwachagua wana wa Israeli ili wamtangaze kwa watu wa mataifa mengine. Kazi hii ilianza katika agano la kale na ilipaswa kuendelea baada ya Israeli kumpokea Yesu kama mwokozi wa dunia. Wayahudi walipomkataa Yesu, Mungu alichagua watu wapya, wakristo, taifa jipya la Israeli ambalo viongozi wake ni Mitume 12 na sasa ni Maaskofu na Mapadre. Zaidi sana Mungu amewafanya wakristo taifa lake jipya na takatifu kwa kuwapa Roho wake Mtakatifu. Wakristo tumeitwa kuwaongoza watu wa mataifa yote waurithi ufalme wa Mungu. Wajibu na majukumu waliyokabidhiwa mitume, sisi watu wa mataifa, wakristo tumeyashirikishwa kwa njia ya ubatizo. Kama Mungu alivyoliteua taifa la Israeli pasipo mastahili kuwa taifa lake teule na kama Yesu alivyowateua mitume na kuwatuma kutangaza Injili bila mastahili yao, ndivyo nasi kwa njia ya ubatizo pasipo mastahili yetu sisi nasi tumeitwa kuwa watakatifu na kuwa makuhani. Tukumbuke kuwa maajabu Mungu aliyoyafanya kwa wana wa Israeli ameyafanya kwetu pia. Tumekombolewa kutoka utumwa wa shetani, mwonevu mkubwa kuliko Farao. Ubatizo umekuwa kwetu kile kilichokuwa kwa waisraeli walipovuka bahari ya shamu. Kwa ubatizo tumeshika njia kuelekea nchi mpya ya ahadi, mbinguni na Yesu Kristo ni Musa mpya anayetuongoza. Mungu amefanya agano nasi kwa damu ya Yesu Kristo mwanae wa pekee. Yeye ni Mungu wetu nasi tu watu wake.
Tunapaswa kuishika kiaminifu amri kuu ya mapendo. Roho Mtakatifu tuliyempokea siku ya ubatizo ametufanya watakatifu, anatusaidia kukua katika utakatifu siku kwa siku. Na sisi sote tumeitwa kuwa makuhani. “Ninyi pia ni makuhani, mlioitwa kuwa watakatifu, mlioitwa kutolea sadaka za kiroho ambazo Yesu Kristo alizifanya zipokelewe na Mungu” (1Pet 2:5). Mapadre na maaskofu wameitwa kwa namna ya pekee katika wito wa ukuhani. Kuitwa katika imani, kunatupa wajibu wa kueneza Injili. Kumbe hazina ya habari njema ipo sasa katika milki yetu. Tumeipokea na kuwa sehemu ya watu wake Mungu. Kama waisraeli, Mungu ametuita kuwa taifa lake teule, kumtangaza kwa wengine wasiomjua bado ili wamjue na kumpenda. Hata nyakati hizi zetu katika miji, vijiji na mitaa yetu wapo watu ambao wametawanyika, hawajui wanakoenda, wengine wamechoka, na wengine wamekata tamaa na maisha. Wapo wagonjwa wa kila aina, wapo watoto yatima, wapo vijana walioathirika na dawa za kulenya na pombe, wapo walemavu, wapo watu wasiojiweza kwa mahitaji ya kawaida yak ila siku. Kama mitume wa sasa tunao wajibu wa kutangaza habari njema ya wokovu kwa kuwahurumia na kuwahudumia ndugu zetu hawa kupata mahitaji ya muhimu katika maisa yao. Tukumbuke kuwa vyote tulivyo navyo tumepewa bure, tutoe bure. Huu ndio wito wetu tulioitiwa na Mungu tulipobatizwa. Lakini pia Kristo anatuambia kuwa; “Mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, mwombeni Bwana wa mavuno apeleke wafanya kazi katika shamba lake”. Ni wajibu wa kila mkristo kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Kazi ni nyingi na watenda kazi ni wachache. Viongozi wa Kanisa, Maaskofu, Mapadre, watawa na makatekista wanahitaji wasaidizi. Lakini kuomba tu, haitoshi. Tunao wajibu wa ziada. Pamoja na kusali tukiombea miito tunapaswa pia kuwasaidia kwa hali na mali wale walioitika ili waweza kukua na kukomaa hatua kwa hatua, waje kuwa watenda kazi bora katika shamba la Bwana na sio bora watenda kazi. Lakini zaidi sana tukumbuke kuwa maisha yetu yanapaswa kuwa mazuri ya kumpendeza Mungu ili yawe mfano bora na kuwavutia wengine watamani kuishi maisha ya kitakatifu kama sisi ili mwisho wa maisha ya hapa duniani tukafurahi sote milele yote mbinguni.