Tafuta

Tafakatri Dominika 12 ya Mwaka A wa Kanisa: Mwanadamu anakabiliwa pia na hofu za kiroho ambazo chimbuko lake ni dhambi, yaani kukokuwa na mahusiano mazuri na Mungu. Tafakatri Dominika 12 ya Mwaka A wa Kanisa: Mwanadamu anakabiliwa pia na hofu za kiroho ambazo chimbuko lake ni dhambi, yaani kukokuwa na mahusiano mazuri na Mungu.  

Tafakari Neno la Mungu Dominika 12 Mwaka A Kanisa: Dhambi Ni Chanzo Cha Hofu na Ukosefu wa ...

Leo tunayapokea maneno ya Kristo mwenyewe anayetuambia “msiwaogope wauuao mwili wasiweze kuiua na roho”. Maisha ya mwanadamu ni maisha yanayoambatana na hofu mbalimbali katika kila hatua. Neno la Mungu katika dominika hii linakuja kutuimarisha na kutuangaza ili tuweze kuzikabili hofu hizo tuishi katika amani ya wana wapendwa wa Mungu. Dhambi ni chanzo cha hofu na ukosefu wa amani na utulivu wa ndani; Sakramenti ya Upatanisho inatuondolea hofu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Dominika ya 12 ya mwaka A wa Kanisa tunayapokea maneno ya Kristo mwenyewe anayetuambia “msiwaogope wauuao mwili wasiweze kuiua na roho”. Maisha ya mwanadamu ni maisha yanayoambatana na hofu mbalimbali katika kila hatua. Neno la Mungu katika dominika hii linakuja kutuimarisha na kutuangaza ili tuweze kuzikabili hofu hizo tuishi katika amani ya wana wapendwa wa Mungu: Ufafanuzi wa Masomo ya Misa: Katika somo la kwanza tunakutana na mtu ambaye hofu yake kubwa ilikuwa ni tishio la maisha kutoka kwa maadui zake. Tunasoma kutoka kitabu cha nabii Yeremia (Yer 20:10-13) masimulizi ya Yeremia mwenyewe. Kazi yake ya kuwa mjumbe wa Mungu kwa watu wake, uadilifu wake wa kutopindisha utume wake wa unabii ili kulinda na kutetea maslahi ya mwanadamu vinamletea maadui katika maisha yake. Katika somo la leo yeye mwenyewe anasema amesikia watu wanamshutumu na wanapanga mipango wamuangamize. Mbele ya tishio hili kubwa, Yeremia anafanya nini? Yeremia anaweka matumaini yake kwa Mungu. Kadiri hofu inavyozidi kuwa kubwa, imani na matumaini kwa Mungu vinapaswa kuongezeka. Yeremia hakati tamaa, harudi nyuma wala hasemi “sifanyi tena kazi ya kuwa nabii”. Anachosema ni kuwa “Bwana yu pamoja nami”. Neno hili analolisema Yeremia kuwa “Bwana yu pamoja nami” ni sala. Nabii Yeremia anamwomba Mungu asimuache peke yake katika hofu inayomkabili na katika hatari inayomkabili. Ni sala ambayo inakuwa ni kana kwamba imekwisha sikilizwa kwa maana anayeisali ana uhakika kuwa itasikilizwa. Ni kwa sababu hii Yeremia anaongeza katika sala hiyo mategemeo ya kibinadamu katika lugha ambayo ni ya kibinadamu.

Upatanisho ni zawadi ya Mungu kwa binadamu
Upatanisho ni zawadi ya Mungu kwa binadamu

Nabii Yeremia anasema wanaonionea wivu watajikwaa, hawatashinda, wataaibika na aibu yao itakuwa ni ya milele. Ni maneno ya kibinadamu yanayoonesha uhakika alionao mtu anayeukimbilia ulinzi wa Mungu katika hofu zake. Si maneno yanayochora picha ya namna ya moja kwa moja ambayo Mungu huonesha msaada wake wa kila anayemkimbilia. Somo la pili kutoka Waraka kwa Warumi (Rum 5:12-15)  linapanua wigo wa tafakari yetu juu ya hofu katika maisha ya mwanadamu. Ni somo linalokuja kutuonesha kuwa mwanadamu hakabiliwi na hofu za kimwili tu au hofu za nje zinazogusa maisha yake ya kawaida, maisha ya kila siku. Mwanadamu anakabiliwa pia na hofu za kiroho ambazo chimbuko lake ni dhambi, yaani kukokuwa na mahusiano mazuri na Mungu. Mtume Paulo analionesha hilo kwa kueleza madhara ya dhambi ya Adamu na matokeo yake kwa binadamu wote na hapo hapo anaonesha karama ya upatanisho aliouleta Kristo na matokeo ya upatanisho huo kwa binadamu wote. Ni somo linalokuja kutuonesha kuwa dhambi ni chanzo kikubwa cha hofu na kutokuwa na amani ya roho maishani. Upatanisho na Mwenyezi Mungu ni njia ya kuondokana na hofu hizo na ni njia ya kukaribisha amani ya roho maishani. Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake kuhusu sakramenti ya upatanisho husisitiza kuonesha kuwa kupokea Sakramenti ya upatanisho ni hatua muhimu sana kwa anayetaka kuanza maisha mapya au kupiga hatua katika maisha yake.

Upatanisho wa kweli ni chanzo cha amani na utulivu wa ndani.
Upatanisho wa kweli ni chanzo cha amani na utulivu wa ndani.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika mwanga wa somo la Nabii Yeremia na la waraka kwa Warumi tunaingia katika tafakari ya somo la Injili (Mt 10:26-33). Yesu anasema “msiogope wauuao mwili wasiweze kuiua na roho”.  Maneno haya si tu kwamba yanatualika kuzishinda hofu maishani kama alivyofanya nabii Yeremia, ni maneno ambayo kwa namna fulani yanatuonesha pia kuwa katika maisha kuna hiarakia ya tunu, kuna madaraja au ngazi katika kushughulikia vitu vilivyo muhimu maishani. Zipo hofu ambazo inabidi tuzikubali, yapo mahangaiko ambayo inabidi tuyapitie na hatuwezi kuyaepa ili tusipoteze zile tunu zilizo na thamani zaidi katika maisha yetu. Mwili na roho humkamilisha mwanadamu na vyote ni muhimu. Pamoja na hayo, mwili huwakilisha vile vitu vinavyopita na roho huwakilisha vile vitu vinavyodumu. Hofu ya mambo yanayopita isitufanye tukayakosa yale yanayodumu, yale yaliyo bora zaidi na yale yaliyo matakatifu. Waswahili husema “usiache mbachao kwa msala upitao”. Kutokuzikubali hofu au kutokubali mahangaiko katika yale yapitayo kumewafanya wengi wasiishi maisha halisi. Kumewafanya waishi maisha ya juu juu tu na yale yanayowapendeza watu hata kama ndani yake hayana uzito wa tunu za kiutu na za kiimani. Kutokukubali hofu za yale yapitayo kumewafanya watu kukosa ujasiri wa kusimamia misingi ya kitu na ya kiimani kwa hofu ya kupoteza kile ambacho kwa asili yake tu hakidumu.

Waamini katika maisha na utume wao wajitahidi kujiaminisha kwa Mungu.
Waamini katika maisha na utume wao wajitahidi kujiaminisha kwa Mungu.

Kristo anaonya akisema anayeishi namna hii, anayenikana mbele ya watu ili kulinda nafsi yake nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. Zipo hofu ambazo tunapaswa kuzikubali na kutokuzionea aibu kwamba tunazo, yapo mahangaiko ambao katika wakati fulani inabidi tuyapokee na kuyakubali ili tu kulinda yale yaliyo na thamani zaidi katika maisha yetu, ili kulinda imani yetu kwa Kristo na ili kulinda utakatifu Mungu aliouweka ndani yetu. Injili hii ya leo inatuongezea nguvu pale ambapo inatualika tujiaminishe kwa Mungu. Yapo mambo ambapo pale yanapotokea hatujui kuchagua. Hatujui kuyapa thamani hili iwe ni ile inayopita au iwe ni ile inayodumu. Anayechagua akiwa amejiaminisha kwa Mungu huchagua akiongozwa na mwanga wake. Zaidi ya hapo tunapaswa kukubali kuwa si kazi rahisi kuchukua uamuzi huo kwa sababu daima ni uamuzi unaoambatana na sadaka kubwa. Katika yote hayo injili ya leo inatualika tujiaminishe kwa Mungu. Yesu anasema “mashomoro wawili, yaani aina duni kabisa ya ndege, hawauzwi kwa senti moja? Lakini hata hao ndege duni kabisa hakuna mmoja anayeanguka na Baba wa mbinguni asijue. Sembuse nyinyi mlio wanae aliyewaumba kwa sura na mfano wake?  Kwa maneno hayo Yesu analenga kutuonesha kuwa Mungu baba yetu hajatuacha tutangetange ulimwenguni bila kutuhakikishia msaada wake. Yupo. Na wote wanajiaminisha kwake, wote wanaomkimbilia, wote wanaomtegemea na wote ambao kwa ujasiri wanaamua kuzitii dhamiri zao katika kufanya maamuzi sahihi maishani wana uhakika wa kupata ulinzi na uangalizi wake. Neno la Mungu katika dominika hii litupe nguvu, litusaidie kuzishinda hofu zinazotukabili maishani na litupe mwanga wa kuchagua kubaki na Mungu na yeye tu kumpa sifa na utukufu katika maisha yetu.

Liturujia D12 ya Mwaka
24 June 2023, 08:34