Tafuta

Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 12 ya Mwaka A wa Kanisa: Mungu ndiye anastahili kuogopwa kwa sababu ana uwezo wa kuua mwili na roho. Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 12 ya Mwaka A wa Kanisa: Mungu ndiye anastahili kuogopwa kwa sababu ana uwezo wa kuua mwili na roho.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 12 ya Mwaka A wa Kanisa: Msiogope Kumtangaza na Kumshuhudia Kristo Yesu

Mungu ndiye anastahili kuogopwa kwa sababu ana uwezo wa kuua mwili na roho. Binadamu anaweza kuua mwili tu, lakini hana mamlaka yoyote juu ya roho ya mtu. Ni Mungu peke yake mwenye uwezo wa kuiokoa roho na kuipa maisha ya raha milele yote mbinguni au kuitupwa katika moto wa milele. Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya matendo adili na matakatifu. Ushuhuda!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 12 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatutia moyo na kutuimarisha kuwa katika maisha yetu hatupaswi kuwa na hofu au mashaka ya kitu chochote au mtu yeyote yule isipokuwa kuwa na hofu kwa Mungu peke yake. Mungu ndiye anastahili kuogopwa kwa sababu ana uwezo wa kuua mwili na roho. Binadamu anaweza kuua mwili tu, lakini hana mamlaka yoyote juu ya roho ya mtu. Ni Mungu peke yake mwenye uwezo wa kuiokoa roho na kuipa maisha ya raha milele yote mbinguni au kuitupwa katika moto wa milele. Ndiyo maana katika wimbo wa mwanzo Mzaburi anasisitiza; “Bwana ni nguvu za watu wake, naye ni ngome ya wokovu kwa Kristo wake. Uwaokoe watu wako, uwabariki urithi wako, uwachunge, uwachukue milele (Zab. 28: 8-9). Lakini hofu yetu ya Mungu sio hofu itokanayo na ukatili wa Mungu, la hasha, bali ni hofu ya heshima inayosimikwa katika upendo wake kwetu sisi ndivyo inavyosisitiza sala ya mwanzo ikisema; “Ee Bwana, utujalie kuliheshimu na kulipenda daima jina lako takatifu; kwa maana huachi kamwe kuwaongoza wale uliowaimarisha katika upendo wako”.  Na sala ya kuombea dhabihu inakazia kusema; “Ee Bwana, pokea sadaka hii ya kutupatanisha nawe na kukusifu. Utujalie itutakase tupate kukutolea mapendo safi ya mioyo yetu”.      

Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka
Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Yeremia (Yer 20:10-13). Nabii Yeremia katika kitabu chake sura 10-20 ameeleza wazi ushuhuda wa maisha yake mwenyewe jinsi yaliyokuwa na mateso makali, lakini kwa kumtumaini Mungu daima alimpa nguvu ya kuyakabili na kuyashinda. Itakumbukwa kuwa manabii wote waliotumwa na Mungu walikumbana na mateso mengi kutoka kwa watu wao. Lakini Yeremia ndiye aliyepata upinzani mkubwa na mateso makali kuliko wote kwa sababu alitangaza waziwazi kubomolewa kwa mji wa Yerusalemu na watu wake kuchukuliwa mateka kama wasingalitubu na kumrudia Mungu. Viongozi wa Israeli walikataa ushauri wake na wakamshtaki kwa kosa la uhaini. Nabii alidhulumiwa kwa namna ya pekee na kuhani Pashhur, mtu aliyekuwa na ushawishi mkubwa kutoka katika mahakama ya mfalme. Ndivyo anavyoshuhudia Yeremia mwenyewe jinsi maadui zake walivyokuwa wanamshawishi huyu kuhani amshitaki Yeremia kama yeye mwenyewe anavyosimulia akisema: “Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake” (Yer.20:10). Katika matukio kadhaa Yeremia alinusurika kufa. Hivyo aliamua kutokuongelea habari hii mbaya ya kuangamizwa kwa mji wa Yerusalemu kama alivyoagizwa na Mungu. Yeremia alikata tamaa kwa sababu hakuna aliyesikiliza mahubiri yake na pia kwa sababu ya madhulumu yaliyoendelea kumpata. Alimlalamikia Mungu kwa uchungu kwa kumpa yeye kazi ngumu kiasi hiki hata kuilaani siku aliyozaliwa. Lakini uaminifu wake kwa Mungu ulikuwa mkubwa zaidi kuliko kusita kwake kuueleza uma ukweli (Yer 20:9). Hivyo akajisikia kuwa Mungu yupo pamoja naye kama shujaa mkuu kuliko adui zake ndiyo maana anasema; “Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala Kisha akajikabidhi mikononi mwa Mungu na kuomba akisema; “Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo yao, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu” (Yer. 20:12).

Ushuhuda unaobubujika katika kweli za Kiinjili, maadili na utu wema
Ushuhuda unaobubujika katika kweli za Kiinjili, maadili na utu wema

Ni kweli mji wa Yerusalemu ulivamiwa, kuta zake zikabomolea, hekalu likanajisiwa na watu wengi walichukuliwa mateka uhamishoni Babeli naye Yeremia akaachwa Yerusalemu. Mateso yake hayakuishia hapa baadaye alishurutishwa kwenda Misri ndipo alipokufa kwa kuuawa. Kumbe tunaona kuwa wajumbe wa Mungu wanapitia mateso mengi na makali. Kushuhudia neno la Mungu si rahisi. Mateso ndio malipo yake. Nasi tunapaswa kumshuhudia Kristo wakati wa amani na wakati wa mateso; hatupaswi kuacha kumshuhudia hata tukipatwa na mateso namna gani naye Mungu atakuwa nasi daima. Hili ni fundisho la wazi ambalo somo hili la kwanza linatupa. Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 5:12-15). Katika somo hili mtume Paulo anaeleza jinsi dhambi na adhabu zake zilivyoingia duniani na hivyo mateso na mahangaiko yote ya mwanadamu. Kwamba ni kwa njia ya Adamu wa kwanza dhambi iliingia duniani, pamoja na mateso yote, kifo au mauti ikawa adhabu yake. Lakini kwa njia ya Adamu wa pili, yaani Yesu Kristo, neema na baraka za Mungu zimeletwa duniani nazo ni nyingi kiasi cha kuishinda dhambi na adhabu yake. Paulo anatumia lugha ya biashara ya kununua na kulipa akisema kuwa Yesu alikuja duniani kulipa deni ambalo sisi binadamu hatukuwa na uwezo wa kulilipa. Ni kwa mateso na kifo chake, akaleta wokovu kwa dunia nzima, wokovu uliozidi uovu wa dhambi ya mwanadamu. Kwa hiyo wema wa Yesu ulizidi ubaya wa dhambi za watu wote duniani. Sasa tunapomshuhudia Kristo, tunaongeza wokovu wa ulimwengu kama tulivyoongeza mateso yake kwa kutenda dhambi. Hakuna kitu kilicho cha thamani kubwa kuliko wokovu unaoletwa kwa watu tunaoishi nao kwa kumshuhudia Kristo kwa maisha ya kweli ya kikristo.

Masharti ya kimisionari: kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu
Masharti ya kimisionari: kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 10:26-33). Katika sura yak umi ya Injili ya Mathayo ambapo Injili ya dominika hii inatoka, tunapata miongozo na masharti ya kimisionari waliyopewa Mitume na Yesu. Sharti la kwanza ni kumshuhudia Yesu, kuwa Bwana na Mwokozi kwa watu wote. Katika sehemu hii ya Injili Yesu anawaagiza Mitume kuyahubiri kwa watu wote yale aliyowaambia faraghani, wao wayaweke hadharani. Yesu anawatia moyo wasiogope watapokumbana na kupambana na matatizo katika kazi hiyo akisema; “Msiwaogoope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho.” Roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu. Licha ya kuwa siyo kila mmoja ameitwa kuacha yote na kumfuata Kristo na kwenda maeneo mbalimbali kuhubiri injili. Na siyo kila mmoja ameitwa kuongoza jumuiya ya kikristo kama Maaskofu, mapadre, watawa na makatekista. Kwa ubatizo kila mkristo ameshirikishwa unabii, ukuhani na ufalme wa Yesu na hivyo kuitwa kumshuhudia Kristo wakati wote na mahali popote alipo, kuanzia nyumbani kwake, katika jumuiya ya kikristo na mbele ya watu wa mataifa – yaani wale wasioamini Kristo. Hakuna wakati wowote katika maisha yetu ambapo hatupaswi kutimiza wajibu huu. Kwa kweli, tupende tusipende, maisha yetu yatakuwa kati ya vitu hivi viwili; aidha kumshuhudia Kristo au kutomshuhudia, aidha kumwungama Kristo au kumkana. Na katika kumshuhudia Kristo kunatudai mambo mawili. Kwanza kabisa ni kuziamini na kuzishika kweli alizofundisha na kuzifanya wakati wa uhai wake hapa duniani hasa kifo na ufufuko wake kutoka wafu kwa maondoleo ya dhambi na kutupatanisha na Mungu Baba naye baada ya hayo amepaa mbinguni na ameketi kuume kwa Mungu Baba akituombe. Yeye ni njia, ukweli na uhai. Na pili ni kutangaza kwamba Yesu Kristo ni Bwana na mkombozi wetu naye ni msingi na nguzo ya maisha yetu. Kumbe basi namna yetu ya kutoa ushuhuda kwa Kristo ni kuishi kulingana na kile alichotufundisha kadiri tulivyokipokea katika Maandiko Matakatifu hasa mashauri ya Injili yanayojikita katika Amri kuu ya mapendo.

Ushuhuda wa kweli unafumbatwa katika upendo kwa Mungu na jirani
Ushuhuda wa kweli unafumbatwa katika upendo kwa Mungu na jirani

Lakini tukumbuke kuwa tunapomshuhudia Kristo katika maisha yetu ya kila siku, madhulumu na mateso ni mambo ya kutegemewa kama ilivyokuwa kwa Manabii na Mitume. Na Yesu mwenyewe alisema; “Mtachukiwa na watu kwa ajili ya jina langu” (Mt. 10:1-22). Na Mtume Paulo alipomwandikia Timoteo alisema; “Mnafahamu vema kwamba mtu yeyote anayeishi kulingana na Injili ya Yesu hakika atadhulumiwa” (2Tim 3:12). Hili liko hivyo kwa sababu madhulumu ni matokeo ya mgongano kati ya mema na mabaya, kati ya upendo na chuki, kati ya Mungu na shetani. Na tena yanaweza kutoka kwa watu wa karibu kabisa; wanafamilia, wazazi, watoto, ndugu, jamaa na marafiki. Lakini tunapodhulumiwa badala ya kulia, kuogopa na kukata tamaa na kutafuta namna ya kulipiza kisasi, tunapaswa kufurahi kama anavyoseama Yesu; “Furahini na kushangilia kwa kuwa tuzo lenu ni kubwa mbinguni, hivi ndivyo walivyowadhulumu manabii kabla yenu” (Mt 5:12) tena anasisitiza akisema; “Mioyo yenu isisumbuke” (Yn 14:1-27). Tukiona kuwa tunapata madhulumu tujue kuwa tuko katika njia sahihi ya kutoa ushuhuda wa imani yetu na kinyume chake ni kweli. Zaidi sana tuwe na uhakika kuwa katika madhulumu na mateso Yesu yuko karibu nasi wakati wote maana Yeye ni “ndiyo kwa ahadi zote za Mungu” (2Kor 1:20) na “shahidi mwaminifu” (Uf 1,5;3,14) nasi tunaamini kuwa tutashinda Mungu akiwa upande wetu. Tukumbuke daima kuwa kumshuhudia Kristo siyo tunda la jitihada na juhudi za kibinadamu. Bali ni kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu atutiaye nguvu na neema za Mungu. Mwangaza huu na nguvu hii vinaletwa na roho aliye ndani yetu kulingana na ahadi ya Yesu; “Mtapokea Roho Mtakatifu na kuwa mashahidi wangu siyo tu Yerusalemu, bali katika nchi yote ya Uyahudi na Samaria na hata miisho ya dunia (Mdo 1:8). Na hivi ndivyo tunavyoweza kuupokea ukombozi wa roho zetu kama sala baada ya komunyo inavyohitisha ikisema; “Ee Bwana, sisi tuliolishwa Mwili na Damu takatifu ya Mwanao, tunaomba rehema yako ili ibada hii tunayofanya mara nyingi ituletee kweli ukombozi”. Na hili ndilo tumaini letu la milele.

Dominika 12 Mwaka A
22 June 2023, 08:36