Tafuta

Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika warsha hii ya pili kufanyika Barani Afrika. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika warsha hii ya pili kufanyika Barani Afrika.  

Hotuba ya Dr. Dorothy Gwajima kwa Warsha ya Wanawake Wakatoliki Barani Afrika

Hii ni warsha ambayo imeandaliwa na Kikundi cha Utafiti wa Masuala ya Wanawake Duniani, (WWO: World Women Observatory) kilichopewa jina la “Mtandao wa Kiafrika Dhidi ya Ukatili na Ubguzi wa Wanawake. Hatua za Kwanza.” Katika hotuba yake Dr. Dorothy Onessphoro Gwajima, MB, amegusia kuhusu: WAWATA kama chombo cha uinjilishaji, Wito wa Serikali kwa WAWATA na WUCWO, pamoja na Sera na mikakati ya kuendelea kushughulikia changamoto za ukatili.

Na Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima, - Dar Es Salaam

Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum ndiye aliyepewa heshima ya kuwa ni mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha ya siku nne kuanzia tarehe 3 Julai- 6 Julai 2023 inayofanyika Jijini Dar es Salaam, ili kuwawezesha wanawake wa kiafrika kuwa na mustakabali usi ona ubaguzi, dhuluma, unyanyasaji wala ubaguzi. Hii ni warsha ambayo imeandaliwa na Kikundi cha Utafiti wa Masuala ya Wanawake Duniani, (WWO: World Women Observatory) kilichopewa jina la “Mtandao wa Kiafrika Dhidi ya Ukatili na Ubaguzi wa Wanawake. Hatua za Kwanza.” Katika hotuba yake amegusia kuhusu: WAWATA kama chombo cha uinjilishaji, Wito wa Serikali kwa WAWATA na WUCWO, pamoja na Sera na mikakati ya kuendelea kushughulikia changamoto za ukatili. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii ya kuwepo hapa leo na kwa mwaliko wenu wa kunishirikisha kama Mgeni Rasmi katika Warsha hii ya Kimataifa. Ni heshima kubwa kwa nchi yetu kuwa wenyeji wa Warsha hii, hivyo kwa niaba ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Wananchi kwa ujumla napenda kuwakaribisha kwa moyo mkunjufu wageni wetu wote kutoka nje ya Tanzania wanaohudhuria Warsha hii KARIBUNI SANA! Pamoja na kuhudhuria Warsha hii na nawasihi wajumbe kutumia fursa ya kuwepo Tanzania kutembelea vivutio mbali mbali vinavyopatikana ndani ya Tanzania Bara na Visiwani pia kuonja ukarimu wa Watanzania.

Wanawake wakatoliki wajenzi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu
Wanawake wakatoliki wajenzi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu

Ninatambua kwamba WAWATA ni chombo cha kuwaunganisha Wanawake Wote Wakatoliki Tanzania na mwaka 2022 mliadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya umoja wenu, hongera sana WAWATA. Kazi kubwa ya WAWATA ni pamoja na kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili ili waweze kutoa mchango wao kikamilifu katika Kanisa; waweze kujenga familia bora kiroho, kimwili, kiuchumi na kijamii ili kuongeza pato la familia na kuchangia uchumi wa Taifa. Yote haya yanafanyika kwa upendo na uwajibikaji. Nimefurahi kujulishwa kuwa huu Umoja wenu pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization) iliyoanzishwa mwaka 1910 yenye makao yake makuu huko Ufaransa. Kumbe kupitia WAWATA mnashiriki katika kutunga sera na mikakati ya kuwakomboa Wanawake kiuchumi katika ngazi za Kimataifa. Nimefarijika sana kusikia Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika kwa kipindi cha 2023 – 2027 anatoka hapa Tanzania, kumbe mchango wenu ni mkubwa sana ndani na nje ya Tanzania, hongera sana Mama Evaline Ntenga.

Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika
Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika

Katika Risala iliyosomwa na WAWATA, imedhihirisha wazi dhamira yenu njema ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na kazi hii inafayonywa bila kujali itikadi za dini ama siasa. Warsha inayoanza leo inawapa nafasi kubwa ya kujifunza na kushirikishana mbinu za kukabiliana na changamoto hizi kwa kuwa na sauti ya pamoja. Hili ni jambo jema kwani siku zote tunatambua umoja unaleta matunda chanya na ya haraka zaidi. Wito wa Serikali kwa WAWATA na WUCWO: Kwa kuzingatia karama na wito wa maisha katika Jumuiya yenu pamoja na Wanawake Wakatoliki Duniani chini ya Mwavuli wa WUCWO na Kanisa Katoliki Mahalia na ulimwenguni, mnaweza kuisaidia Serikali kupitia Wizara yangu katika kupata taarifa (moja ya malengo ya WWO ni Kuwa kitovu cha taarifa zinazohusu ukweli wa Maisha ya wanawake ulimwenguni ndani na nje ya kanisa pamoja na ustahimilivu wao na uwezekano wa kujikomboa wakiwezeshwa). Nafarijika kwamba WAWATA pia ina lengo la kumfanya mwanamke ajitambue kuwa yeye ni muhimu katika maendeleo ya kiroho na kimwili katika jamii. Huu ni mpango mathubuti utakaoisaidia serikali kupitia Wizara kuweka mikakati stahiki ya kuendelea kushughulikia changamoto za ukatili ili kuiwezesha jamii ya watanzania kujikita katika kazi za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni; na kwa kufanya hivyo kutawezesha serikali kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26), Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2030); na Agenda ya Afrika Tuitakayo (2063).

Wanawake wakiwezeshwa wanaweza kufanya mageuzi makubwa kijamii
Wanawake wakiwezeshwa wanaweza kufanya mageuzi makubwa kijamii

Kutokana na Dira na Malengo hayo ya ya kitaifa na kimataifa hayo natoa Mwito kwa Jumuiya yenu ikishirikiana na WUCWO kusaidia kufanya utafiti wenye mlengo wa kijinsia ili utume wenu utambulike katika jamii kwamba ni utume mwafaka kwa jamii, na unachangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya kweli ya kibinadamu kwa raia wote wa Tanzania, Afrika na Dunia bila kujali itikadi za dini. Kama taasisi ya kijamii pia, Serikali inatarajia kuwa WAWATA itatoa ushirikiano mwafaka kama ambavyo imejitahidi kufanya katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Hiyo ina maanisha kwamba, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa katika historia ya nchi yetu, WAWATA mtatoa ushirikiano unaoongeza thamani katika uongozi wa nchi, uchumi wake na ustawi wake ambao ni mwafaka kwa hadhi na utu wa mwanadamu. Serikali ingependa WAWATA itumie karama zake kama wanawake na wazazi katika masuala ya kifamilia, ulinzi wa mtoto, malezi kamilifu na himilivu ya vijana, masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanaume na wanawake, na pia kwa wahitaji hasa wazee, wafungwa na watoto yatima. Serikali iko tayari kusikiliza na kutoa msaada kwenu katika jitihada za masuala haya katika mipango na utekelezaji wenu. TAMATI: Napenda kumalizia kwa kuwatakia WUCWO Warsha njema. Naamini baada ya Warsha hii mtatuletea maazimio mliyofikia ili Wizara yangu iendelee kushirikiana nanyi katika utekelezaji wa malengo hayo hapa Tanzania. Kama Wanawake Wakatoliki Duniani mna nafasi kubwa ya kutokomeza kabisa masuala ya unyanyasaji katika jamii zenu kwa ushirikiano na Kanisa na Serikali. KWA UPENDO WA KRISTO, TUTUMIKIE NA KUWAJIBIKA!!

Dr Gwajima

 

03 July 2023, 18:41