Tafuta

Waamini wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Buhingo katika Jimbo Kuu Katoliki Mwanza wanayo shangwe kubwa kumshukuru Mungu kwa miaka 100 ya Parokia toka ilipojengwa Misioni ya Kashishi mwaka 1923 Waamini wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Buhingo katika Jimbo Kuu Katoliki Mwanza wanayo shangwe kubwa kumshukuru Mungu kwa miaka 100 ya Parokia toka ilipojengwa Misioni ya Kashishi mwaka 1923  

Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Buhingo Jimbo Kuu la Mwanza

Waamini wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Buhingo katika Jimbo Kuu Katoliki Mwanza wanayo shangwe kubwa kumshukuru Mungu kwa miaka 100 ya Parokia toka ilipojengwa Misioni ya Kashishi mwaka 1923 na baadaye kuhamishiwa Buhingo ilipo sasa. Ni maadhimisho ya miaka 100 ya Uenezaji Imani Katoliki katika Parokia ya Buhingo. Kilele cha Maadhimisho haya ni Jumamosi tarehe 22 Julai 2023 kwa Ibada ya Misa Takatifu. Waamini wamejiandaa barabara kwa Jubilei.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama- Idara ya Habari na Mahusiano ya Umma, Jimbo Kuu Mwanza

Jubilei maana yake shangwe. Ni katika maana halisi ya neno “Jubilei” ambapo waamini wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Buhingo katika Jimbo Kuu Katoliki Mwanza wanayo shangwe kubwa kumshukuru Mungu kwa miaka 100 ya Parokia toka ilipojengwa Misioni ya Kashishi mwaka 1923 na baadaye kuhamishiwa Buhingo ilipo sasa. Ni maadhimisho ya miaka 100 ya Uenezaji Imani Katoliki katika Parokia ya Buhingo. Kilele cha Jubilei ya Miaka 100 ni Jumamosi Julai 22, 2023 ambapo kutakuwa na adhimisho la Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu. Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Buhingo inapatikana katika wilaya ya Misungwi umbali wa kilometa 80 toka Mwanza mjini. Ni moja kati ya Parokia 61 zinazounda Jimbo Kuu la Mwanza na ndiyo Parokia kubwa kuliko zote katika Jimbo Kuu la Mwanza ikiwa na vigango 46, Parokia Teule 3 za Misasi, Ibinza na Kasololo na waamini Wakatoliki takribani 25,000. Kwa miaka 100 imehudumiwa na mapadre mbalimbali, wakiwemo Mapadre wa Mashirika hasa Wamisionari wa Afrika (White Fathers) pamoja na Mapadre Wazalendo wa kwanza Tanzania wakiwemo Wilbald Mupapi, Angelo Mwilabure na Celestine Kipanda “Kasisi”. Mupapi na Kipanda walihudumu Buhingo kwa takribani miaka 16 kwa nyakati tofauti. Buhingo imewahi kuhudumiwa pia na hayati Askofu Renatus Butibubage wa Mwanza! Buhingo kumenoga! Ikumbukwe kwamba Parokia ya Buhingo inachota historia yake toka Parokia ya Bukumbi, Parokia ya kwanza kabisa kuanzishwa katika Jimbo Kuu la Mwanza. Mapadre Wamisionari waliwasili eneo la Bukumbi mwaka 1883 wakitokea Uganda baada ya kupata upinzani mkubwa toka kwa Waprotestanti na kutoka kwa Kabaka mfalme wa Buganda. Walipowasili Bukumbi walipokelewa na Chifu Kiganga wa Kigongo na kupewa eneo la kuanzisha Misioni Bukumbi. Na hivyo Bukumbi ikawa parokia ya kwanza ya Jimbo Kuu la Mwanza na huduma mbalimbali za kiroho zikaanza mara moja. Baadaye wamisionari hao waliona uhitaji wa kupanua huduma za kiroho maeneo mbalimbali na hivyo mwaka 1902 Mapadre Wamisionari waliokuwa wakihudumia Parokia ya Bukumbi walifungua vigango mbalimbali katika eneo la kusini mwa Bukumbi, yaani Buhingo ya wakati huo. Vigango vilivyofunguliwa katika eneo la Buhingo ya nyakati hizo ni Igudija (Bugisha), Isesa (Gukuma), Igenge, Nyabuhele (Mbalika) na Sasi (Ng’wasagela).

Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kisima cha huruma ya Mungu
Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kisima cha huruma ya Mungu

Ombi la Helena Majenga wa kigango cha Isesa (Gukuma): Baada ya kufunguliwa kwa kigango cha Isesa (Gukuma), mwaka 1920 binti mdogo kutoka kigango hicho aitwaye Ng’wana Majenga alithubutu kwenda Bukumbi kuomba abatizwe. Alifundishwa mafundisho ya dini katoliki kwa miaka miwili. Huko Bukumbi Ng’wana Majenga alipata bahati ya kukutana na binti mwingine kutoka Kasololo aliyeitwa Bibiana Fundi akiwa na umri wa miaka 16. Ng’wana Majenga alibatizwa na kupewa jina la Helena. Helena Majenga aliporudi Gukuma (Isesa, sasa kigango cha Parokia ya Mbalika) akitokea Bukumbi aliwavuta wasichana wengine wawili katika imani. Wasichana hao wawili walibatizwa na kupewa majina ya Fransiska Shinaga na Margareth Izengo. Helena Majenga na wenzake walizoea kwenda kila mwezi Bukumbi kwa mtumbwi katika ziwa Victoria ili kupokea Ekaristi Takatifu. Katika safari yao kuelekea Bukumbi walikumbana mara kwa mara na hatari, hasa ziwani (Ziwa Victoria) maana walipaswa kupanda mtumbwi toka Gukuma (Mbalika) hadi Bukumbi: hatari ya mamba na mitumbwi kupinduka. Lakini hata baada ya kutoka ziwani iliwapasa kutembea kwa miguu na njiani kulikuwa na tishio la wanyama wakali. Hatari hizi ndizo zilizopelekea Helena Majenga na wenzake kumwandikia Padre Vekemans (maarufu kama Venge) aliyekuwa akihudumu Bukumbi ujumbe maalum: “Afadhali, njoni kwetu Bulima kwa Mtemi Nkondo Lunyalula; mwombeni ploti, mkajenge Misioni…” Padre Vekemans hakusita na mwaka 1921 alifika kwa Mtemi Nkondo kuomba eneo ambapo alipewa ploti katika eneo la Nyabuhele mwendo wa kilometa 3 toka Mbalika. Hata hivyo baadaye mahusiano kati ya mtemi Nkondo na Padre Vekemans yaliingia dosari baada ya mtemi Nkondo kufikiri kuwa Mapadre watabadili mawazo ya watoto wake na hivyo kuwa na misimamo tofauti ya kumpinga. Hali hii ilimfanya Padre Vekemans kwenda kumwonya mtemi na “kuiangusha kofia ya mtemi” kwa ukali. Kutokana na mgogoro huu padre Vekemans aliamua kuhamia Kashishi baada ya kupokelewa kwa furaha na mtemi Mpuya bin Kwangu wa Busongo. Wamisionari walifanikiwa kuanzisha “bush school” eneo la Kashishi.

Zaidi ya waamini 500 wamepokea Komunyo ya kwanza.
Zaidi ya waamini 500 wamepokea Komunyo ya kwanza.

Mwaka 1922 Mapadre wa Bukumbi waliitambua Kashishi kama Senta na kiunganishi kati ya Buhungukila (kusini), Nera (Mashariki) na Bulima (Kaskazini). Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri wa uenezaji wa Injili katika maeneo yaliyozunguka Buhingo. Kati ya mwaka 1922 hadi 1923 Padre Michel Gass raia wa ufaransa aliyekuwa akihudumu Parokia ya Bukumbi alijaribu kuanza ujenzi wa kanisa la kwanza la udongo pamoja na nyumba ya muda ya mapadre katika eneo la Kashishi. Nyuma ilikuwa na vyumba viwili tu: chumba cha chakula na chumba kidogo cha kulala watu watatu. Mapadre walilala kwa kujibanabana sana na wengine walilalia majani. Baadaye waliwasili kwa baiskeli kutokea Bukumbi Mapadre wawili wahaya Padre Wilbald Mupapi (alikuwa Paroko) na Trifoni Rwechungura. Hawa waliendeleza kazi ya ujenzi hapo Kashishi. Hata hivyo kazi ya ujenzi haikuwa rahisi maana vibarua walikuwa haba, baadhi ya wenyeji walikataa kazi ya kuleta mawe, miti na majani na hata mafundi hawakupatikana kirahisi. Hata hivyo penye nia pana njia kwani Oktoba 21, 1923 alifika Padre Vekemans (Venge) kubariki kanisa lililojengwa. Ilikuwa siku ya furaha kubwa maana sherehe ilidumu kwa siku mbili mfululizo ambapo watu walikula, kunywa na kusaza huku miili ikiburudishwa kwa ngoma za asili. Tarehe 19 Aprili 1924 walibatizwa waamini wa kwanza katika Parokia ya Kashishi. Mnamo 27 Desemba 1924 Askofu Joseph Sweens kutoka Bukoba alifika kukagua misheni ya Kashishi na hata kuazima gari kwa ajili ya kusomba mawe kufanikisha kazi za ujenzi zilizokuwa zinaendelea hapo Kashishi. Askofu Sweens alikuwa akitumia usafiri wa punda. Majanga ya mara kwa mara yalazimu Parokia kuhamishiwa Buhingo ilipo sasa: Mnamo mwaka 1928 kulitokea mafuriko makubwa sana ya mvua eneo la Kashishi na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika misheni ya Kashishi: nyumba za mapadre ziliharibika, mikaratusi ilianguka, paa la kanisa likang’olewa na kupeperushwa na vitu vitakatifu vikadhurika sana. Hali hii iliwafanya mapadre kuhamia shuleni hapo Kashishi kwa huzuni kubwa. Majanga ya mara kwa mara yaliyosababishwa na mvua yaliendelea kuwa changamoto kubwa maana eneo la Kashishi lilikuwa mbugani. Hali hii ilimfanya Askofu Sweens awahurumie sana mapadre na kuamua Parokia ya Kashishi ihamie juu ya kilima kidogo cha BUHINGO ambapo palikuwa pakavu zaidi. Neno “Buhingo” siyo neno la Kisukuma kwa asili bali ni neno la kabila la Balongo maana katika eneo hilo walikaribishwa watu wa kabila la Kilongo ambao walijishughulisha na uhunzi wa majembe “magembe” na pia walikuwa mafundi wa kuyeyusha mawe ili watengeneze namna ya vidonge vya chuma vilivyokuwa na umbo kama mpira wa tenesi. Kidonge kiliitwa “kihingo.” Kwa kuwa kidonge cha chuma kiliitwa kihingo, wasukuma wakaanza kuwaita watengenezaji wa kidonge hicho Bahingo. Baada ya muda sehemu walipofanyia kazi “Bahingo” pakaanza kuitwa Buhingo.

Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Buhingo, Jimbo kuu la Mwanza
Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Buhingo, Jimbo kuu la Mwanza

Baada ya maamuzi ya Askofu ya kuhamisha Parokia kutoka Kashishi kwenda Buhingo (ilipo sasa parokia), mnamo tarehe 06/06/1933 Askofu Sweens alifika Buhingo akiwa na Brother Beatus aliyekuwa mtaalamu wa ujenzi (alijenga pia Nyegezi Seminari) na kuanza upimaji wa nyumba ya Misioni Buhingo na kusaidiana na waamini kufyeka eneo na kufukuza wanyama wakali. Waliamua kujenga Kanisa la msonge kwa kufuata muundo wa nyumba za kisukuma za wakati huo. Ndivyo ilivyozaliwa misioni ya Buhingo. Na baadaye ikajengwa shule. Kwa sasa Parokia ya Buhingo ina vigango 46 na Parokia Teule 3 za Misasi, Ibinza na Kasololo. Kwa takribani miaka 100 Parokia ya Buhingo imepiga hatua kubwa za kimaendeleo zikiwemo ujenzi wa makanisa imara na ya kudumu katika vigango, ujenzi wa nyumba za mapadre katika Parokia teule, maboresho ya nyumba kubwa ya mapadre iliyojengwa na wamisionari pamoja na ujenzi wa nyumba mpya ya Mapadre Buhingo na Misasi. Kwa miaka 100 Parokia ya Buhingo imetoa Mapadre wazawa watatu: Padre Alex Kitwala, Padre Moses Mapela na Padre William Ndhone. Parokia ya Buhingo inayo pia waseminari wakubwa waliopo katika majiundo ya wito wa upadre na inayo pia waseminari wadogo katika seminari za Nyegezi, Makoko, Shanwa na Sengerema. Hata hivyo licha ya mafanikio haya bado katika maeneo ya Buhingo kuna mila, mawazo na desturi potofu kama vile kuamini kuwa watoto wanaozaliwa mapacha huleta laana katika jamii, wakazi kuchangishana pesa ili kumleta mtu wa kuleta mvua (abagemi ba mbula) nyakati za ukame, mauaji ya wanawake kwa imani ya kupata utajiri. Pamoja na changamoto hizi pia ukubwa wa parokia na wingi wa vigango vimekuwa vikwazo vya ufanisi wa kichungaji. Katika maandalizi ya kilele cha Jubilei zaidi ya waamini 900 wamebatizwa, zaidi ya waamini 500 wamepokea Komunyo ya kwanza na jozi 10 zimefunga ndoa na katika siku ya kilele cha Jubilei zaidi ya waamini 300 wataimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, kubariki nyumba mpya ya mapadre inayoendelea kujengwa na kusimika Msalaba wa Jubilei. Ijumaa Julai 21, 2023 waamini na maaskofu watakaohudhuria watafanya maandamano toka eneo la Kashishi ilipoanza Misioni ya kwanza hadi Parokiani Buhingo, maandamano yatakayoenzi safari ya Mapadre toka Kashishi hadi Buhingo.

20 July 2023, 15:10