Rais wa Mfuko wa WYD wa Lisbon alitembelea vijana Nchi Takatifu

Askofu Americo Aguiar, Msaidizi wa Jimbo la Lisbon na Rais wa Mfuko wa WYD na ambaye ni kardinali mteule tarehe 30 Septemba ijayo alikweda Nchi Takatifu katika ziara kwa ajili ya vijana ambao hawataweza kwenda huko Lisbon.Ujumbe wake umesindikizwa kwenye Video kupitia jukwaa la YouTube.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Siku chache kabla ya Siku ya Vijana Duniani ambayo mwaka huu itafanyika nchini Ureno kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosti 2023 , Sekretarieti Kuu ya Vijana Wakristo huko Palestina iliandaa misa  Takatifu tarehe 22 Julai 2023 huko Beit Jala, Bethlehem, iliyoongozwa na Patriaki wa Yerusalemu wa Kilatini, Pierbattista Pizzaballa, na Askofu  Americo Aguiar, Askofu Msaidizi wa Lisbon na Rais wa Mfuko wa Siku ya Vijana duniani  WYD – Lisbon ambaye ni Kardinali mteule kati ya waliyotangazwa mnamo tarehe 9 Julai 2023. Katika mahubiri yake Patriaki Pizzaballa, alirejea ushiriki mkubwa wa vijana wa Nchi Takatifu mwaka huu katika Siku ya Vijana Duniani: tisini kutoka Yordani, hamsini kutoka Galilaya, mia mbili kutoka Palestina na ishirini kwa mara ya kwanza kutoka Kupro. Kwa hiyo Patriaki  aliwaalika vijana hawa kuwekeza muda wao katika kutenda mema licha ya dhuluma nyingi wanazozishuhudia katika maisha yao.

Na akielezea zaidi, Askofu wa Lisbon kinyume chake alielezea kuwa kuna  sababu mbili za ziara yake: "ya kwanza ni kutimiza ahadi iliyotolewa kwa vijana ambao wametoka Nchi Takatifu kwenda Lisbon ili kujiandaa kwa hija hiyo. Niliwaambia kwamba kabla ya WYD ningepata muda wa kuwatembelea. Na mimi niko  hapa. Sababu nyingine inahusu kile ambacho Papa Francisko ameniambia kila mara: “Usiwasahau wale ambao hawawezi kuja Lisbon”. "Nilifanya juhudi hii! Tumejitolea kukutana na vijana ambao wana shida kwenda Lisbon: kama vile kutoka Ukraine na Nchi Takatifu. Vijana hawa ni mfano. Shukrani kwa ujasiri wao wanafanikiwa kushinda vikwazo vyote tunavyoona. Mazungumzo na mkutano, licha ya kila kitu, inawezekana. Siku ya Vijana Duniani ni mkusanyiko wa kimataifa. Ni muhimu sana na tunafanya kazi kuleta vijana kutoka duniani kote hadi Lisbon, ambao wanawakilisha undugu huo wa ulimwengu wote.  Kwa hakika Wapalestina vijana watakuwa, kwa namna ya pekee, uwepo unaopendwa sana, unaopendwa sana na vijana duniani kote."

Askofu Msaidizi wa Lisbon pia alitembelea baadhi ya maabara za ufundi ambazo zimetengeneza maelfu ya shanga za Rozari kuwagawia washiriki wa  Siku ya Vijana duniani (WYD.) Mradi huu unaotekelezwa na Caritas Jerusalem, umetoa kazi kwa familia nyingi katika mji wa Bethlehem. Inakumbukwa tayari wakati wa siku ya vijana duniani WYD  huko Panama tayari ilikuwa na itifaki ya ushirikiano na Caritas Jerusalem kwa ajili ya utengenezaji wa rozari hiyo . “Kwa hivyo tulianza kuzungumza nao ili kutoa ahadi mpya kwa  ajili ya siku ya vijana WYD huko Lisbon. Wakati huo huo tumeanza kutafuta msaada wa kifedha. Tuliomba kwa  "Msaada kwa Kanisa Linalohitaji" na sasa linasaidia mradi huo. Mradi unaoruhusu familia nyingi kuwa na mapato kutokana na uzalishaji wa rozari ambazo zitasambazwa katika Siku ya Dunia ya mwaka huu. Na WYD inampatia kila kijana mang’amuzi ya kukutana na Kristo, mazungumzo ya kibinafsi naye, ni vijana ambao, kama akumbukavyo Baba Mtakatifu Francisko, wanatoa mchango mkubwa katika utume wa Kanisa zima, hasa kwa vizazi vijavyo."

26 July 2023, 15:38