Tafakari Neno la Mungu Dominika 14 ya Mwaka A: Njooni Kwangu Nami Nitawapumzisha!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 14 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yamejikita katika kumuonesha Yesu Kristo kuwa ndiye Masiha aliyetabiriwa na manabii. Hivyo tumfuate yeye kwa kuishi maisha mema ya kiroho ili tupate uzima wa milele. Kumbe msisitizo ni juu ya kumkubali Yesu kama Masiha na mkombozi wetu aliyeshuka toka mbinguni akaja duniani kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti kama alivyoaguliwa na manabii nyakati zote. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Zekaria (Zek. 9:9-10). Katika somo hili Nabii Zekaria anatabiri juu ya ujio wa mfalme wa Kimasiya ambaye ni mnyenyekevu, hapandi farasi wa vita, bali anatumia punda. Hii ni baada ya nabii Zekaria kung’amua na kutambua mpango wa Mungu na kuachana na mawazo ya Masiha wa kisiasa, mwenye nguvu za kijeshi. Ndipo sasa anawajulisha watu wake kuwa Mfalme huyu ni amani na ni wa watu wote na mamlaka yake hayana mipaka wala mwisho. Huyu si mwingine ila Yesu Kristo aliyekuja katika hali ya unyenyekevu kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Ndiyo maana sala ya mwanzo inatilia mkazo ikisema: “Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wake Mwanao umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu; uwapatie furaha za milele hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi."
Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:9, 11-13). Katika somo hili kadiri ya Mtume Paulo kuishi kwa mwili tu maana yake ni kuishi katika hali ya dhambi; lakini kuishi kwa roho ni kuishi katika imani na ubatizo na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kwa hivi tukiishi kwa mwili tu tutapotea, bali tukiishi kwa roho tutaokoka. Hivi ndivyo Mtume Paulo alivyowaasa Warumi kuwa Roho wa Mungu yu ndani yao hivyo waishi kiroho yaani maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu. Hivyo nao wataishi milele na Kristo huko Mbinguni. Mtume Paulo anatueleza matunda ya Sakramenti ya ubatizo katika maisha yetu ya kiroho. Kuwa kwa ubatizo tumefufuliwa pamoja na Kristo. Maisha yetu yamebadilika. Hatufungwi na maisha ya kimwili bali tunaongozwa na Roho Mtakatifu tuliyempokea katika Kristo Yesu. Maana wale walio wa Kristo wamezisulubisha tamaa za kimwili na hivyo wanakuwa na uwezo wa kuishi kwa kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu. “Na tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria...Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu” (Gal 5:22-25).
Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 11:25-30). Katika sehemu hii ya Injili ambayo ni kama wimbo wa sifa tunajifunza kwanza kabisa namna ya kuutambua ufalme wa Mungu na mpango wake wake wa ukombozi kuwa njia ya Yesu Kristo kuwa unajidhihiisha na kujifunua kwa walio wanyenyekevu na maskini wa roho. Hili Yesu mwenyewe analidhihirisha kwa sala yake ya shukrani kwa Mungu Baba wa mbingu na dunia. Pili katika sala hii Yesu anajifunua kwetu ya kuwa yeye ni Mwana halisi wa Mungu ambaye kwa kupitia yeye Mungu anajifunua kwetu. Mungu anamtambua Yesu kuwa mwanae mpendwa na Yesu anamtambua Mungu kuwa Baba kwake. Kumbe tunaona uhusiano wa upendo uliopo kati ya Mungu Baba na Mungu mwana ambao Yesu Mwenyewe anaufunua na kuudhihirishwa kwa wanyenyekevu na maskini wa roho. Na tatu ni mwaliko wa Yesu wa kuwa tayari kuwapokea na kuwasaidia wote wanaosumbuka na kulemewa na matatizo mbalimbali katika maisha yao. Kumbe, Yesu anatudhihirishia kuwa yeye ndiye masiya aliyetabiriwa na manabii. Amekabidhiwa yote na Mungu Baba, anayemjua yeye amemjua pia baba. Yeye ni njia pekee ya kufikia mbinguni kwa baba, wote wenye shida wamfuate yeye naye atawapumzisha. Ugumu wa maisha kwa watu sababu ya sheria nyingi zilizowekwa na Walimu wa sheria na Mafarisayo ulikuwa ni mzigo mzito uliowatesa na kuwaumiza watu na kuwalemea ndiyo maana Yesu anawaambia; “Njoni kwangu ninyi yote mnaosumbuka na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha”. Sheria zilikuwa zimewafanya watu kama punda waliofungwa nira (kamba) na kubebeshwa mizigo mizito. Ndiyo maana anasema “Nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi."
Kumbe, tunaona kuwa masomo yote matatu yanasisitiza juu ya kumkubali Yesu kuwa yeye ndiye Masiha, mkombozi wetu aliyeshuka duniani kutukomboa kama manabii walivyoagua. Waisraeli walitegemea pengine huyo masiya angekuwa ni mtawala wa kidunia, angekuwa tajiri, mwenye mali nyingi, mfalme mwenye jeshi kubwa ambalo lingeweza kuwashambulia na kuwaua adui zao iliwaangamie kabisa. Lakini Yesu alikuja kwa namna tofauti ambayo wao hawakutegemea, alikuja kama mtu masikini, tena alizaliwa katika zizi la ng’ombe. Alishirikiana na watu walitengwa na jamii wadhambi kama watoza ushuru na makahaba, wagonjwa, maskini na wafungwa. Hata nyakati zetu kuna ugumu wa maisha tuna mizigo mingi tunaliyobeba; magonjwa, njaa, kukosa fedha, kukosa kazi, tabia ngumu za wale tunaoishi nao, wenzi wetu, watoto, wanafamilia, hata majukumu kama kiongozi katika jumuiya na katika kanisa, udhaifu wetu wa kimwili au kiroho, Yesu anasema; “Njoni kwangu niwapumzishe”. Yeye anatupatia mtazamo mpya kuhusu sheria, kutusamehe dhambi zetu, kutufundisha maana mpya ya mateso katika maisha yetu, kutuahidia uzima wa milele. Analeta mtazamo mpya kuhusu sheria. Kristo anasema “Sikuja kutangua sheria bali kuikamilisha.” Kristo amekuja kuikamilisha sheria yaani kuipatia maana mpya. Mtu asiwe kwa ajili ya sheria bali sheria kwa ajili ya mtu. Tunapaswa kuongozwa na amri ya mapendo Pendaneni kama nilivyowapenda mimi asema Bwana maana; “Sheria yote ya Musa na Manabii zinategema amri hizi mbili: Kumpenda Mungu na Jirani” (Mt 22:40).
Mtazamo huu unatusaidia kwa namna mbili: Kwanza sisi tutazielewa amri za Mungu na za Kanisa kwamba hazikuwekwa ili kututesa bali kutulinda na tukizifuata vizuri basi tutakuwa na raha nafsi mwetu. Sheria ipo ili kutulinda. Itunze sheria na sheria ikutunze. Katika matendo yetu yote kwa wenzetu tuzingatie upendo. Kila tunalotenda tujiulize swali hili; Je, ninachotaka kumtendea mwenzangu ni tunda la upendo? Wakati mwingine ili kuisha kwa furaha na amani inabidi kujisadaka na kusamehe pale tunapokosewa hata kama hatujaombwa msamaha. Hata pale sheria inapokuruhusu kulalamika, potezea usilalamike. Hata pale sheria inapokupatia haki ya kulipwa na mnyonge maadamu kule kutokulipwa hakukupunguzii chochote, achilia yote kwa ajili ya amani kuiishi amri ya upendo kwa Mungu na jirahi nawe utakuwa na raha nafsini mwako. Wakati mwingine hata pale sheria inapokuruhusu kushtaki na kulipiza kisasi jitahidi kuongozwa na upendo, kumbuka sala ya Baba Yeu, hasa sehemu inayosema; “utusamehe makosa yetu kama na sisi tunavyowasamehe waliotukosea”. Basi hiyo ahadi tunayoitoa kwa Mungu itupe nguvu ya kuwaachilia na kuwasamehe kweli waliotukosea nawe utakuwa na raha na amani nafsi mwako. Kwa jinsi hii tutaweza kutua mizigo na masumbuko yanayosababishwa na makovu ya kutunza hasira na sumu ya kutaka kulipiza kisasi kwa sababu ya kutendewa vibaya na wengine.
Kristo anasisitiza kusema; “jifunzeni kwangu maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo”. Na mzaburi katika wimbo wa katikati anakaza kusema; “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema”. Yeye “alipotukanwa hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki” (1Pet 2:23). Haya ndiyo mambo ambayo Yesu anasema Mungu Baba amewaficha wenye hekima na akili akawafunulia watoto wachanga. Maana wenye hekima na akili za ufahamu wa kupata haki kwa sheria tu hawawezi kujua namna ya “kuyaweka matumaini yao kwa Mungu, hakimu mwenye haki”. Hawa hawewezi kuelewa wala kukubali kuwa kuwa nyakati ni vizuri kukubaliana na fundisho hili; “akupigaye shavu la kulia mgeuzie na la kushoto” wao kila kitu ni “jino kwa jino” na jicho kwa jicho. Familia ya namna hii, jumuiya ya namna hii nchi ya namna hii haiwezi kuwa na amani kamwe. Kumbe kuna nyakati tunapaswa kusema kama mtume Paulo kuwa; “Na sasa nafurahia kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake yaani Kanisa” (Kol 1:24). Haya ndiyo matunda ya kuwa wanyenyekevu, wapole na maskini wa roho. Fadhila hizi zinatuapa nafasi ya kupokea matunda ya Sakramenti ya Kitubio kwa kusamehewa na kutuondolea dhambi ztu. Zaidi sana kupokea na kupata matunda ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu yaani kutiwa nguvu za kiroho za kupambana na nguvu ya dhambi na udhaifu wa kimwili. Basi tutiwe nguvu na kupewa faraja na maneno haya ya Yesu: “Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake” (Yn.14:21) na zaidi sana kuupokea uzima wa milele Mbinguni.