Tafakari Dominika 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Nafasi ya Neno la Mungu katika Maisha ya Mwamini
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika ya 15 ya mwaka A wa Kanisa inatupatia tafakari juu ya Neno la Mungu. Masomo yote matatu ya dominika hii yanajikita kuonesha nafasi ya Neno la Mungu katika maisha ya mwamini na kwa namna ya pekee kabisa yanatuonesha kuwa Neno hilo kimsingi sio maandishi yanayohifadhiwa katika kitabu kitakatifu bali ni nafsi hai ya Mungu ambayo kupitia maandishi hayo inakutana na nafsi yenye kiu ya mwanadamu. Masomo kwa ufupi: Kama kawaida ya kipindi hiki, tunaanza kwa kuyapitia kwa kifupi masomo yote matatu ili kuona kile ambacho yanazungumzia. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Nabii Isaya (Is 55, 10-11). Somo hili linaonesha kuwa Neno la Mungu lina nguvu ya kuleta mabadiliko katika nafsi ya mtu anayelipokea. Kwa kinywa cha nabii Isaya Mungu mwenyewe anasema: kama ambavyo mvua inainyeshea ardhi, hairudi juu bila kuirutubisha na kuchipusha mbegu basi ndivyo hivyo na Neno langu. Halirudi hadi litakapotimiza kile nitakacho”. Neno la Mungu lina nguvu. Nguvu hii inatoka wapi? Nguvu hii inakuja kwa sababu Neno la Mungu ni nafsi hai ya Mungu. Kila anayelisoma, kila anayelitangaza, kila anayelisikiliza kwa imani, hakutani tu na maandishi bali anakutana na nafsi hai ya Mungu. Ni hiyo nafsi hai ya Mungu inayokwenda kutenda kazi na ni hiyo nafsi hai ya Mungu inayokwenda kuleta mabadiliko katika nafsi ya yule anayelipokea.
Tukiingia katika somo la pili, tunasoma kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 8: 18-23) kuhusu hali ya mahangaiko iliyopo duniani. Mtume Paulo anachora picha ya viumbe vyote na dunia kwa ujumla. Anasema dunia nzima inahangaika, ina kiu. Viumbe vyote vipo katika hali duni ya udhaifu na ya uharibifu, kama viumbe vinavyosubiria ufunuo wa ukombozi. Picha anayoichora mtume Paulo ni ile inayoonesha kuwa katika maisha ya mwanadamu daima kuna kitu kinakosekana, kuna kitu hakijakamilika na kuna kitu kinazuia ukamilifu huo. Tukilitazama somo hili katika mwanga wa dhamira ya masomi ya dominika hii ya 15, dominika inayozungumza juu ya nguvu ya Neno la Mungu, fundisho tunalolipata ni kuwa suluhisho la hali duni ya ulimwengu na ya viumbe vyote ipo katika Neno la Mungu. Neno la Mungu ndiyo matumaini katika maisha ya mwanadamu yaliyojaa changamoto na magumu mbalimbali. Neno la Mungu ambalo ni nafsi hai ya Mungu ni msaada, ni mwanga na nguvu inayomsaidia mwanadamu na kumuongoza ajue ni nini cha kufanya na jinsi gani aishi katikati ya changamoto hizo zinazomkabili. Somo la Injili (Mt 13:1-23), lenyewe linatuletea mfano ambao unafahamika zaidi kama mfano wa mpanzi. Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu shambani. Mbegu nyingine zikaanguka njiani, nyingine kwenye miamba, nyingine kwenye miiba na nyingine kwenye udogo mzuri.
Yesu mwenyewe anatoa ufafanuzi wa mfano huu akieleza kuwa mbegu ni Neno la Mungu na mahala inapodondoka mbegu hiyo ni mazingira mbalimbali ya aina ya watu wanaolipokea Neno hilo. Njia ni moyo usioweza kulihifadhi Neno; unalisikia lakini linapotea mara moja. Mwamba ni ule moyo ambao mbegu ya Neno haiwezi kuota mizizi, haina udongo. Miiba ni ule moyo ambao umesongwa na mambo mengi, hauna muda wa kutulia ili Neno likae ndani yake. Udongo mzuri ndio ule moyo ulio tayari na unaojibidiisha kulipokea Neno nalo linazaa matunda ndani yake. Kuliko kuuona mfano huu wa mpanzi kama ni mfano unaozungumzia aina mbalimbali za mioyo inayolipokea Neno la Mungu, huenda inafaa zaidi kuuona kama ni mfano unaozungumzia nyakati au mazingira mbalimbali ya moyo wa mtu mintarafu kulipokea Neno la Mungu. Upo wakati moyo unakuwa kama njia, Neno linaingia na linatoka; upo wakati moyo unakuwa kama mwamba, haulipi nafasi Neno kuota mizizi; upo wakati moyo unakuwa na miiba, unasongwa na mambo mengi, unakuwa “bize” na mambo mengine yote isipokuwa yale ya kimungu. Upo wakati ambapo moyo unakuwa kama udongo mzuri. Unalipokea Neno na kwa utulivu Neno linazaa matunda ndani yake. Kuliona somo hili namna hii inatusaidi kujua ni wakati gani au ni namna gani ambavyo Neno la Mungu linaweza kuzaa matunda ndani yetu.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ya 15 yamejikita katika Neno la Mungu. Yametufafanulia kwa namna tofauti tofauti nguvu ya Neno la Mungu, manufaa yake kwa kwa mwamini na mazingira mbalimbali ambayo yanaweza kulifanya Neno hilo lizae matunda ndani ya nafsi ya mtu. Mojawapo ya maswali ambayo tunaweza kujiuliza baada ya kuupokea ujumbe huu ni: tunawezaje kulipokea Neno la Mungu na kuliishi katika mazingira yetu ya kawaida? Kulijibu swali hili, kwanza ninarudia kitu ambacho tumekiona katika ufafanuzi wa masomo. Kitu hicho ni kuwa Neno la Mungu sio tu maandishi yaliyo katika kitabu kitakatifu bali ni nafsi ya Mungu. Nafsi hiyo tunakutana nayo tunapolisoma, tunapolisikiliza, tunapolitafakari na tunapolitangaza Neno la Mungu. Kumbe hatua ya kwanza ni kujenga ukaribu na Neno hilo. Mtakatifu Gregori Mkuu alifundisha akisema “Neno la Mungu hukua ndani yake yeye anayelikaribia”. Namna nzuri ya kulikaribia Neno la Mungu ni kulisoma. Sasa nitalisomaje Neno la Mungu? Nishike Biblia na kuanza kuisoma tangu mwanzo hadi mwisho? Au niwe nafungua tu kwa kubahatisha, kile kifungu nitakachokiona kwa siku hiyo ndiyo nakisoma? Aliye na nafasi ya kusoma Biblia nzima anaweza kufanya hivyo lakini ni vizuri akawa ni mtu aliyepata maandalizi walau ya awali juu ya Biblia au awe anasoma akisaidiwa na yule aliye na ufahamu zaidi wa Maandiko Matakatifu.
Binafsi sishauri pia kufungua Biblia na kusoma kile kifungu unachokiona mbele yako. Badala yake ninashauri kuanza na masomo ya dominika. Kufuata masomo yaliyoandaliwa katika liturujia yatahakikisha kuwa zoezi la usomaji wa Neno linakuwa endelevu. Masomo hayo ya dominika, ni vizuri ukayasoma kabla ya kwenda kuhudhuria Ibada ya Misa takatifu. Utakapoyasikia kwa mara ya pili Kanisani na kusikiliza mahubiri ya Padre utapata mwanga zaidi na mkutano wako na nafsi ya Mungu iliyo katia Neno lake utakuwa hai zaidi. Usipopata nafasi ya kuyasoma kabla unaweza kuyarudia ukirudi nyumbani baada ya kuyasikiliza katika Misa. Kwa namna hii, Neno la Mungu la dominika litakuwa msaada katika juma zima ukisubiri kwa hamu kukutana nalo tena dominika ijayo. Baada ya hatua hiyo ndipo inaweza kufuata hatua ya pili ya kuyasoma masomo ya Misa ya kila siku kwa utaratibu ule ule wa dominika. Kusoma Neno la Mungu ni tofauti na kusoma kitabu cha hadithi au habari za magazetini. Anayesoma Neno la Mungu anasoma kwa imani akijua kuwa katika Neno hilo ni Mungu anayezungumza. Mwisho wa hatua za kulitafakari Neno hilo ni swali ambalo anayesoma inabidi ajilize: Neno hili linaniambia nini mimi leo na katika maisha yangu kwa ujumla? Kwa jinsi hii Neno linakuwa daima chanzo na kichocheo cha mabadiliko, ndiyo kuzaa matunda katika maisha yetu. Nakutakia tafakari njema ya dominika ya 15 ya mwaka A kwa Kanisa.