Tafakari Neno la Mungu Dominika 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Mungu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu katika dominika ya 15 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika ya kumi na tano ya Mwaka A wa Kanisa yanatufundisha na kutukumbusha juu ya nguvu ya Neno la Mungu kwa wale wanaolipokea na kuliishi na wajibu wa kila mwanadamu katika kulipokea, kulitunza na kuliishi neno hili linalopandwa katika mioyo yetu ili litupatie matunda yake ya ukombozi wetu. Neno hili ni kama maji ya mvua yalowanishapo ardhi na mimea kuota. Lakini kama ilivyo kwa mbegu nzuri na iliyo bora ikipandwa katika udongo wenye rutuba inavyozaa mazao mengi na bora zaidi ndivyo lilivyo neno la Mungu linavyohitaji kupokelewa, kutunzwa na kuliishi ili kupata mafao yake. “Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina makali kuliko upanga uwao wote wenye makali kuwili, tena linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” (Ebr. 4:12). Somo la kwanza ni la kitabu cha nabii Isaiya (Isa. 55:10-11). Hizi ni aya tatu zinazihitimisha kitabu cha pili cha Nabii Isaya kinachoanzia sura ya 40 mpaka sura ya 55. Katika somo hili Nabii Isaya anashuhudia nguvu ya Neno la Mungu kuwa haliwezi kurudi nyuma au kubadilika kama vile mvua inyeshavyo haina budi kustawisha mimea. Nabii Isaya anatumia lugha ya picha katika mazingira ya mkulima.
Kama vile mkulima anavyongojea kwa hamu mvua kunyesha ndivyo walivyosubiri kwa hamu wana wa Israeli kutimia kwa ahadi za Mungu za kuwakomboa kutuma uhamisho wa Babeli. Kwa lugha hii ya faraja na matumaini ya mkulima Nabii Isaya anawadhihirishia Waisraeli kwamba watarudi katika nchi yao kwa sababu Mungu aliahidi hivyo. Kama vile mvua inyeshapo haina budi kuilainisha ardhi, na kuichipusha, kustawisha na kuizalisha mimea ikampa mtu apandaye mbegu chakula chake, ndivyo lilivyo neno litokalo katika kinywa cha Mungu kwa njia ya watumishi wake haliwezi kurudi bure lazima litimize mapenzi ya Mungu aliyoyatamka nalo na kuahidi kuyatenda. Neno la Mungu linaonya, linakaripia, linafundisha, linarekebishwa na ana heri yule aonywaye na kuonyeka, akaripiwapo na kukaripika, afundishwapo na kufundishika, arekebishwapo na kurekebeshika, kwani ataishi kwa furaha maisha ya hapa duniani na kupata heri ya milele mbinguni. Ndivyo ilivyokuwa kwa Waisraeli walipolipokea Neno la Mungu, Mungu aliwakomboa kutoka utumwani Babeli na kuwarudisha katika nchi yao. Na kinyume chake ni kweli kwa wasiolipokea na kulikubali neno la Mungu adhabu ya milele ni yao.
Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:18-23). Katika somo hili Mtume Paulo anatueleza kuwa mateso na mahangaiko ya wakati huu ni ya kitambo kidogo tu na sio mateso yaletayo kifo cha umilele bali ni maandalizi ya mwanzo wa maisha mapya na ya umilele huko mbinguni. Baada ya faraja hiyo ya mwisho wa mateso kwa binadamu, mateso yaliyosababishwa na dhambi ya mwanadamu mwenyewe. Mtume Paulo anaelezea pia mtokeo na madhara ya dhambi na udhalimu wa mwanadamu kwa viumbe vingine na ulimwengu wote unavyoteseka kwa matokeo yake akisema kuwa: “Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa.” Kumbe, uchoyo na ulafi wa mwanadamu wa kutaka kutumia zaidi ya kile anachopaswa kutumia kutoka kwa viumbe vingine na mbaya zaidi mchango wake wa kuutunza na kuutiisha ulimwengu kuwa ni kidogo kuliko kule kuuharibu zinavifanya viumbe vingine viugue na kuteseka. Lakini zaidi sana kwa uharibifu huu binadamu mwenyewe anateseka zaidi kama Mtume Paulo anavyosema; “Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu.” Kumbe somo hili linaweka wazi madhara ya uharibifu wa mazingira sio tu kwa viumbe vingine lakini pia kwetu sisi wanadamu. Sisi wenyewe tunashuhudia ukweli huu kwa mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa yanavyotufanya tuteseke kwa ongezeko la joto, ukame na mafuriko, viumbe hai wengine kutoweka, hata mahusiano ya binadamu na viumbe vingine yanakuwa hatarishi kwa afya zetu kwa kuibuka kwa milipuko ya magonjwa yasiyo na tiba. Tunaalikwa kuyatunza mazingira pamoja na viumbe vingine vyote ili tuweze kunufaika navyo kwa kuishi kwa furaha na amani.
Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 13:1-23) nayo inahusu mfano wa mpanzi. Somo hili linasisitiza kuwa kama vile mbegu iwezavyo kutoa mavuno makubwa licha ya mapingamizi na vikwazo vingi, vivyo hivyo Neno wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo anavyoleta matunda mema na mengi katika maisha yetu licha ya uwepo wa maadui wanaopinga kazi yake. Mtakatifu Yohane Christostom anasema kuwa katika mfano wa mpanzi Yesu anaeleza upendo na huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika kazi na matendo yake katika kumkomboa mwanadamu kutoka katika mahangaiko na utumwa wa dhambi. Yesu anaposema mpanzi alitoka, ni kile kitendo cha Mungu muweza wa yote aliyeko mahali pote kujishusha, kuchukua hali yetu ya kibinadamu katika fumbo la umwilisho akawa mwanadamu na kuja kukaa nasi kwa kuwa sisi hatukuwa na uwezo wa kumwendea yeye aliye mkatatifu kwa sababu ya dhambi zetu. Kumbe, Mungu kwa upendo wake, huruma yake na uvumilivu wake, akashuka kuja kukaa nasi na kupanda ndani mwetu Neno la uzima. Uvumilivu wa Mungu katika kupanda Neno lake mioyoni mwetu bila ubaguzi, bila kuangalia mapungufu na dhambi zetu, akiheshimu uhuru wa kila mmoja wetu ni kama uvumilivu wa mkulima ambaye anapanda mbegu mahali popote shambani mwake bila kubagua maeneo akiwa na matumaini kuwa zitamea na kutoa mazao. Uvumilivu na matumaini ya Mungu yanafananishwa na ya mkulima ambaye licha ya kuwa kuna mambo ya kukatisha tamaa katika kazi yake kwa ishara za kupata mazao kidogo kwa sababu ya ndege kuvamia na kula mbegu kabla ya kuota, miamba kuzuia mizizi ya mimea iliyoota kukua na hivyo mimea inapigwa na jua na kukauka, miiba kuisonga mimea iliyoota hivyo kushindwa kuzaa vyema, mkulima huyu hakati tamaa, anavumilia na kuweka matumaini yake katika sehemu ndogo ya udongo mzuri ambapo mbegu zilimea na kuzaa mazao mazuri na mengi. Ndiyo yalivyo matumaini ya Mungu kwa mwanadamu katika kazi ya kumkomboa.
Kama ilivyo kwa mbegu bora inavyotegemea udongo mzuri wenye rutuba ili imee, ikuu, ikomae na kuzaa mazao mengi na mazuri, ndivyo ilivyo kwa neno la Mungu ili, liingie na kupenya mioyo yetu, likue, likomae na kuzaa matunda bora ndani ya maisha yetu linahitaji utayari wetu, imani yetu, upendo wetu, matumaini yetu na ujasiri wetu katika kulipokea, kulipa nafasi ndani mwetu na kuliacha litubadilishe. Neno hili lapita uwezo wa ufahamu wetu, kumbe imani, matumaini, upendo, uvumilivu na usikivu vyahitajika ili liweze kuzaa matunda yake ndiyo maana Yesu katika mfano huu wa mpanzi anasisitiza umuhimu wa wenye masikio kusikiliza na kusikia Neno la Mungu ili liweza kuwapa matunda yake. Katika ulimwengu mamboleo kuna sauti nyingi nzuri, tamu na za kupendeza masikioni zinazoweza kutufanya tusikie lakini tusisikilize na hivyo tusilielewe Neno la Mungu. Lakini pia kuna vitu vingi vya kupenda mbele yetu na kuyafumba macho yetu yasiuone wema wa Mungu kwa kuifanya mioyo yetu iwe mizito. Haya yote ni kama ndege wala mbegu, miamba, miiba na jua kali, vikwazo kwa Neno la Mungu kuzaa matunda yake ndani mwetu. Kumbe tuna wajibu na tunahitaji kujifunza kwa bidii, kulisoma, kulisikiliza na kulitafakari Neno la Mungu, ili kwamba hawa ndege wasilile, miamba isilizuie kuzama mioni mwetu, jua lisiikaushe na miiba isilisonge na kulizuia lisizae matunda yake ndani mwetu. Basi tumwombe Mungu atuonyeshe uso wake katika haki kama wimbo wa mwanzo unavyotuasa ili tuamkapo tushibishwe kwa sura yake (Zab. 17:15), ambapo Mungu mwenyewe anatuonyesha mwanga wa ukweli wake kama tukiishika imani yetu na pale tunapodanganyika na yule mwovu kwa kulinyakua Neno la Mungu ndani mwetu, Roho Mtakatifu atusaidie kurudi katika njia ya haki, udhia au dhiki ikitokea kwa ajili ya Neno la Mungu tusichukizwe na kuliacha na shughuli za dunia hii na udanganyifu wa mali usitusonge kiasi kwamba tukalisahau Neno la uzima wa milele.