Uvumilivu huu wa Mungu unatupata nafasi kuifaidi huruma yake kwa kufanya toba kwa wakati ili hukumu ya mwisho isitutie hatiani. Uvumilivu huu wa Mungu unatupata nafasi kuifaidi huruma yake kwa kufanya toba kwa wakati ili hukumu ya mwisho isitutie hatiani.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 16 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukuu wa Huruma ya Mungu: Uvumilivu!

Masomo ya Dominika hii ya 16A yanaendelea kutufundisha ukuu wa huruma ya Mungu na uvumilivu wake kwa kule kutokuwa na haraka kutuadhibu tunapomkosea kwa kutenda dhambi. Anatuacha tuendelee kuishi pamoja na walio wema mpaka wakati wa hukumu ya mwisho. Uvumilivu huu wa Mungu unatupata nafasi kuifaidi huruma yake kwa kufanya toba kwa wakati ili hukumu ya mwisho isitutie hatiani. Hiki ni kielelezo cha ukuu wa huruma ya Mungu kwa binadamu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 16 mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Kwa anguko la Adamu na Eva mahusiano kati ya Mungu na mwandamu yanaelezwa katika uhusiano wa huruma na upendo Mungu kwa mwanadamu. Huruma hii inaelezwa kwa namna mbalimbali ili mwanadamu aweze kuilewa na kuipokea. Masomo ya dominika ya 15A yalieleza uhusiano wa huruma na uvumilivu wa Mungu kwa kuhusianisha Neno lake na maji ya mvua, na mbegu alizopanda mpanzi. Masomo ya Dominika hii ya 16A yanaendelea kutufundisha ukuu wa huruma ya Mungu na uvumilivu wake kwa kule kutokuwa na haraka kutuadhibu tunapomkosea kwa kutenda dhambi. Anatuacha tuendelee kuishi pamoja na walio wema mpaka wakati wa hukumu ya mwisho. Uvumilivu huu wa Mungu unatupata nafasi kuifaidi huruma yake kwa kufanya toba kwa wakati ili hukumu ya mwisho isitutie hatiani. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 12:13, 16-19). Somo hili linatueleza kuwa Mungu anaweza kuadhibu mabaya na kulipa mema; anaweza kutuangamiza kwa uovu wetu lakini kwa hekima na huruma yake anatupatia nafasi ya kutubu. Ndiyo maana Sulemani anasema; “Walakini, desturi yako unauzuia hata uwezo wako, na kuhukumu kwa upole, na kututawala kwa uvumilivu mwingi. Yaani uwezo unao, wakati wote utakapo kuutumia…lakini endapo watu wametenda dhambi unawajalia toba.” Hulka hii ya Mungu ilimfanya mzaburi atafakari na kuandika maneno ya wimbo wa mwanzo dominika hii akisema; “Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; Ee Bwana, nitalishukuru jina lako maana ni Jema” (Zab. 54:4,6) na katika wimbo wa katika tunaimba na kusema; “Kwa maana wewe, u mwema, umekuwa tayari kusamehe” (Zab. 86:5).

Mfano wa magugu na ngano: Uvumilivu wa Mungu
Mfano wa magugu na ngano: Uvumilivu wa Mungu

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:26-27). Katika somo hili mtume Paulo anatumbua kuwa hali yetu sisi binadamu ni dhaifu, hali kadhalika na sala zetu. Lakini kwa sababu Roho wa Mungu yu ndani yetu, sala zetu zinapata mastahili na kusikilizwa na Mungu. Hapa msisitizo ni huruma ya Mungu ndiyo inayotujalia Roho wake awe msaada kwetu. Kwa kuwa maneno ya Mtume Paulo ni mazito mno ni vyema kuyanukuu, anasema: “Roho hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu wa Mungu tunazidishiwa kwa wema baraka za neema za Mungu. Hivyo tunakuwa na uwezo wa kuzishika daima amri zake kwa moyo wa matumaini, imani na mapendo. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 13:24-43). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anatumia mifano mitatu: Mfano wa ngano na magugu, mfano wa punje ya haradali na mfano wa wa chachu ya mwanamke. Mifano hii mitatu inahusu kukua na kuenea kwa ufalme wa Mungu katika moyo wa kila mtu na katika ulimwengu kwa ujumla.  Lakini mifano ya punje ya haradali na chachu ya mwanamke, inasisitiza zaidi hatua na hali mbalimbali inazozipitia Kanisa katika kuusimika ufalme wa huruma ya Mungu. Licha ya kuwa mwanzo wake ni mdogo na duni na haujulikani sana; daima huambatana na matatizo, lakini mwishowe litakuwa kubwa, lenye ustawi na kujulikana. Na mfano wa ngano na magugu unafunua huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu dhaifu na wadhambi.

Huu ni muda wa toba na wongufu wa ndani
Huu ni muda wa toba na wongufu wa ndani

Huruma ya Mungu inafumbatwa katika uvumilivu wake na imani aliyonayo kwa mwanadamu ya kubadilika na kumrudia yeye akitumia sera ya viache vyote vikue pamoja hata wakati wa mavuno. Tunasali vyema katika sala ya imani kuwa Mungu hadanganyiki wala hadanganyi na mafundisho ya Kanisa yatueleza kuwa Mungu ajua yote hata mawazo yetu. Kumbe mwovu yeyote kunawiri si kwa sababu Mungu haoni uovu wake bali ni huruma yake na uvumilivu wake Mungu ndivyo vinayompa mdhambi nafasi ya kutubu na kubadilika. Basi tutumie vizuri huruma na uvumilivu huu tusingoje hata siku ya mwisho, siku ya hukumu. Tusidhani na kujiaminisha kuwa tunapoendelea kufanikiwa licha ya matendo yetu maovu kwamba Mungu haoni au hana nguvu ya kutuadhibu. Kinyume chake ni kweli, Mungu anajua na anaona yote na uwezo anao ila anatupatia nafasi ya kutubu na kubadilisha mwenendo wetu. Tutumie vizuri Sakramenti ya kitubio ambayo kwayo Mungu anapitishia huruma yake kwetu wadhambi. Mfano wa ngano na magugu unatutahadharisha kujikinga dhidi ya wapanda magugu. Shamba/konde linaweza kulinganisha na nafsi ya mtu. Kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kila alichokiumba Mungu na tazama ni chema sana. Kwa njia ya uumbaji Mungu amepanda ndani ya kila nafsi ya mtu kila lililojema kwa maisha yake. Lakini katika kukua kwetu tubadilika na kujifunza tabia mbalimbali na tofauti tofauti kutoka kwa watu wengine. Kwa wema tunajifunza tabia njema. Kwa waovu tunajifunza tabia mbaya ndiyo maana “marafiki wabaya huharibu hata watu wema."

wazazi wana wajibu wa malezi na makuzi bora kwa watoto wao.
wazazi wana wajibu wa malezi na makuzi bora kwa watoto wao.

Ni adui shetani anayefanya kazi ya kupanda magugu ndani ya nafsi zetu kupitia kwa marafiki waovu. Kumbe kila mmoja ana wajibu wa kujilinda na yule mwovu asije kupanda ndani mwake uovu wake. Wazazi wana wajibu wa kuwalinda na kuwaelekeza vyema watoto wao ili asiwepo yeyote wa kupanda magugu ndani ya nafsi zao. Tukumbuke kuwa mtoto asipokuwa na msingi nzuri wa maadili toka nyumbani, ni rahisi kwa yule mwovu kupanda yaliyo mabaya ndani mwake. Mfano wa ngano na magugu unatuasa kuacha tabia ya kuwahukumu wengine kwa sababu ya udhaifu wetu, ni vigumu kutambua nani mwema na nani ni mbaya. Hivyo, tusiwahukumu watu na kuwawekea alama kwamba huyu ni mwema na huyu ni mbaya kwa kuangalia tu mwonekano wa nje. Mtu anaweza kuwa anaonekana mwema kwa macho au maneno, lakini ni mwovu ndani mwake. Mwingine anaweza kuwa anaonekana kwa watu kuwa ni mwovu, lakini ni mwema ndani mwake. Tatizo linaweza kuwa wapo waliomsema vibaya kwa maslahi binafsi au kwa sababu tu haeleweki. Tuache hukumu kwa Mungu anayejua mioyo ya watu. Mtume Paulo anatuonya akisema : “Basi msihukumu kabla ya wakati wake ; acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yalofichika, na kuonesha wazi nia za mioyo ya watu” (1Kor 4 :5). Hii haimaanishi kuwa watu wakikosea tusiwakosoe, la hasha. Kinachokatwaza hapa ni kukata tamaa kwamba mtu huyu hawezi kubadilika. Muache atabadilika. Hata kumkemea au kumuadhibu aliyekosa inaonesha kuwa bado tuna matumaini katika mtu huyo kuwa anaweza kubadilika.

Huruma ya Mungu imefunuliwa katika Kiti cha Maungamo.
Huruma ya Mungu imefunuliwa katika Kiti cha Maungamo.

Pasingekuwa na matumaini pasingekuwa na haja ya kumuadhibu. Mfano wa ngano na magugu unatuasa tusiwe wabaguzi kwa watu wasio na uwezo. Watumishi walitaka kung’oa magugu ili ngano ikue vizuri. Utamaduni wa kifo umeanza kwa dhambi ya ubaguzi kwa kuwanyanyasa, kuwatenga na pengine kuwatokomeza kabisa kwa kukatisha maisha ya wasiojiweza na wanyonge kama walemavu, vikongwe, wagonjwa mahututi au hata ambao bado hawajauona mwanga wa jua wasio na hatia wala uwezo wa kujitetea, ili mradi tu walio wazima waishi vizuri. Viacheni vyote vikuwe hata wakati wa mavuno. “Hapo ndipo mtakapotambua tena tofauti iliyopo kati ya waadilifu na waovu, naam, kati ya mtu anayemtumikia Mungu na asiyemtumikia” (Mal 3 :18). Tusipojifunza kuacha taratibu kwa hiari, tutalazimika kuacha kwa lazima tutakapo kufa. Kifo kikitufikia tutaacha yote. Basi tumwombe Mungu kupitia huyo Roho atujalie kuwavumilia watu wabaya huku tukiwaombea na kuwaonyesha mfano mzuri wa maisha ili nao waachane na uovu wabadilike na kumrudia Mungu. Pia Mungu atujalie tutumie vyema uvumilivu wake wa kutuacha tuendelee kuishi hata kama tunatenda mabaya kwani si kwamba haoni bali anatupatia muda wa kutubu. Atujalie tuwe na moyo wa toba na kubadilika ili hukumu ya mwisho itukute tukiwa ngano bora na hivyo, tukusanywe katika ufalme wa mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 16 Mwaka A

 

 

19 July 2023, 08:28