Tunapokea katika Injili mfano wa magugu na ngano vinavyomea pamoja katika shamba. Tunapokea katika Injili mfano wa magugu na ngano vinavyomea pamoja katika shamba.  

Tafakari Dominika 16 Mwaka A wa Kanisa: Upole na Uvumilivu wa Mungu Kwa Wadhambi

Dominika 16 Mwaka A inatuletea fundisho juu ya uvumilivu wa Mungu katika mapungufu ya maisha ya mwanadamu. Tunapokea katika Injili mfano wa magugu na ngano vinavyomea pamoja katika shamba. Mwenye shamba ambaye ni Mwenyezi Mungu haondoi maramoja magugu hayo bali huvuta subira akisema viacheni vyote vikue hadi wakati wa mavuno. Hapo ndipo magugu yatakusanywa upande wake yakachomwe bali ngano itakusanywa na kuwekwa ghalani pake.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika ya 16 ya mwaka A wa Kanisa ambayo tunaiadhimisha juma hili, inatuletea fundisho juu ya uvumilivu wa Mungu katika mapungufu ya maisha ya mwanadamu. Tunapokea katika Injili mfano wa magugu na ngano vinavyomea pamoja katika shamba. Mwenye shamba ambaye ni Mwenyezi Mungu haondoi maramoja magugu hayo bali huvuta subira akisema viacheni vyote vikue hadi wakati wa mavuno. Hapo ndipo magugu yatakusanywa upande wake yakachomwe bali ngano itakusanywa na kuwekwa ghalani pake. UFAFANUZI WA MASOMO: Fundisho tunalolipokea katika Injili ya dominika hii, linatanguliwa na kuandaliwa na somo la kwanza linalotoka Kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 12:13, 16-19) na somo la pili linalotoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (8: 26-27). Kitabu cha Hekima ya Sulemani kinahifadhi mang’amuzi mbalimbali ambayo taifa la Mungu liliyafikia baada ya kuangalia upande mmoja yale lililoyapitia kama taifa na upande mwingine yale ambayo Mungu aliyatenda na anayoendelea kuyatenda kwao. Katika yote hayo, mwandishi wa kitabu hicho kwenye somo la leo anakiri akisema Mungu huhukumu kwa upole na kutawala kwa uvumilivu mwingi. Na si kwamba kwa kufanya hivi Mungu anapunguza uwezo wake, la hasha. Ni katika upole na uvumilivu ndipo anapoonesha uwezo wake mkubwa alionao. Tunapolisikia somo hili na kulitafakari pamoja na ujumbe mbalimbali wa manabii, tunaona kuwa upole na uvumilivu wa Mungu una lengo moja tu, kumvuta mwanadamu mkosefu katika toba, abadili njia isiyofaa ili apate wokovu. Ndicho alichokifupisha nabii Zakaria alipotoa maneno ya Mungu akisema “sifurahii kifo cha mtu mwenye dhambi bali aaiche njia yake mbaya apate kuishi” (Zak 33:11).

Acheni magugu na ngano vikue pamoja.
Acheni magugu na ngano vikue pamoja.

Somo la pili, ambalo katika dominika hii ni fupi sana, linaongeza neno muhimu katika dhana ya somo la kwanza. Mtume Paulo anaeleza kuwa Mwenyezi Mungu hamwachi mwanadamu peke yake katika njia ya udhaifu. Humtuma Roho wake ili amsaidie kurudi kwake. Somo linasema “Roho hutusaidia katika udhaifu wetu”. Tena na hata pale ambapo hatujui namna ya kusali, namna ya kutafuta njia ya kurudi kwa Baba ni Roho huyo ambaye husali ndani yetu kwa uchungu mkubwa usioelezeka ili kuifanya sala yetu ipokelewe kwa Mungu. Mungu anachokifanya tunaweza kukieleza katika maisha ya kawaida kama mwajiri anayemfuata mtu asiye na ajira, anamuandikia barua ya kuomba ajira na kumpa mbinu zote za kushinda usaili na anamuwezesha kwa kumpa yote yanayotakiwa ili apate ajira. Ndivyo anavyofanya Mungu kumrudisha kwake mwanadamu dhaifu. Mungu hamkatii tamaa yeyote yule bali hufanya yote kumsaidia arudi kwake. Tukiingia sasa katika somo la Injili tunasikia mifano mitatu ambayo Yesu anaitoa. Mfano wa kwanza ndio huo wa magugu na ngano. Mfano wa pili ni wa punje ya haradali ambayo ni ndogo kabisa kama punje ya mchicha lakini ikipandwa inazaamti mkubwa ambao ndege huja na kuweka viota. Mfano wa tatu na wa mwisho ni wa hamira ambapo kiasi kidogo tu kinatosha kuumua kiasi kikubwa cha unga uliokandwa.

Tafakari: Upole na uvumilivu wa Mungu kwa wadhambi
Tafakari: Upole na uvumilivu wa Mungu kwa wadhambi

Katika mifano hii mitatu, ni ule wa kwanza, wa magugu na ngano unaobeba maana wakati ile miwili inayofuatia inafafanua kile anachokieleza Yesu katika mfano wa kwanza. Maana ya mfano wa kwanza ndio huo uvumilivu wa Mungu. Yeye amepanda mbegu njema ya ngano, adui anakuja anapanda magugu ili kuharibu ngano. Kwa nini mwenye shamba hafanyi mara moja palizi kuondoa magugu? Kwa nini Mungu haangamizi mara moja waovu wote ili duniani wabaki wema tu? Kwanza anasema palizi ya namna hiyo inaweza ikaangamiza hata baadhi ya ngano. Pili tukiangalia mifano ile miwili inayofuata, mifano inayoonesha kuwa kutoka mbegu ndogo ya haradali unazaliwa mti mkubwa na kwamba kiasi kidogo tu cha hamira kinaumua pishi kubwa, Mungu anaonesha matumaini kuwa hata katika mwovu kuna chembechembe ndogo ya wema inabaki ndani yake. Na hiyo chembechembe hata kama ni ndogo kiasi gani ina uwezo wa kumsukuma mtu afikie toba na wongofu. Uvumilivu wa Mungu ni kusubiri ili hiyo chembechembe ndogo kabisa ya wema iliyo ndani ya watu wake ikue iwafikishe wakosefu na wadhaifu katika wongofu.

Ufalme wa Mungu unakua kadiri ya mpango wa Mungu
Ufalme wa Mungu unakua kadiri ya mpango wa Mungu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuusikiliza utangulizi wa masomo na ufafanuzi wake na baada ya kuyasikiliza masomo yenyewe, ni wakati sasa wa kurudi katika mazingira ya maisha yetu ya kila siku ili kuona masomo ya dominika hii yanatualika tupige hatua ipi au tuikabili namna ipi hali mahsusi ya maisha yetu. Ili kuichokoza tafakari hiyo ninapenda kugusia vitu vitatu. La kwanza ni kujifunza maana ya uvumilivu wa Mungu katika maisha yetu. Kila mmoja wetu anapoangalia nyuma katika maisha yake anaweza kwa hakika kuona mahala ambapo Mungu amemuonesha uvumilivu huu: hajamuadhibu au kuruhusu aadhibiwe sawasawa na hatia, amempa mafanikio ambayo ni kwa neema tu na mambo mengine mengi kama hayo. uvumilivu huu wa kimungu ni mwaliko hata leo wa kumuongokea Mungu badala ya kuendelea kuishi na kutenda kana kwamba Mungu haoni au kana kwamba Mungu anahalalisha yote hayo. La pili ni kutokukata tamaa. Uvumilivu wa Mungu tunaweza kusema kuwa unasukumwa na tunu hii kuwa yeye hamkatii mtu tamaa. Sasa kama yeye hatukatii tamaa na kama anakuwa tayari kusubiri hadi dakika ya mwisho, sisi hatupaswi kujikatia tamaa na kudhani kwamba hakuna nafasi tena ya kubadilika wala ya kuongoka.

Hakuna sababu ya kukata wala kujikatia tamaa, Mungu ana saa yake.
Hakuna sababu ya kukata wala kujikatia tamaa, Mungu ana saa yake.

Vivyo hivyo hatupaswi kuwakatia watu tamaa kwa sababu mbegu ya wema ambayo Mungu ameipanda ndani yetu haifi, kuna wakati utafika itachipua. La tatu na la mwisho ni kujifunza mwelekeo huo wa kimungu dhidi ya maovu au dhidi ya wale wanaotenda maovu katika jamii zinazotuzunguka. Mwelekeo wa kikristo na mwelekeo wa kimungu si kuwatakia mabaya, sio kuwaombea au kupanga maangamizi bali ni kuwaombea kubadilika na kumwongokea Mungu. Tunao mfano katika kitabu cha Matendo ya Mitume, shemasi Stefano alipokuwa anauawa bila hatia alisali akiwaombea msamaha watesi wake. Mmojawapo wa watesi hao alikuwapo Saulo ambaye baadaye aliongoka akawa Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Bila sala hiyo ya Stefano, mtakatifu Agostino anasema, Kanisa lisingeweza kumpata mtakatifu Paulo. Mifano ya namna hii ni mingi na inakamilishwa na maneno ya Kristo mwenyewe akiwa msalabani “baba uwasamehe kwa sababu hawajui walitendalo”. Kuombea wongovu na si kulaani ndio moyo wa kimungu, ndio moyo wa kikristo. Nakutakia tafakari njema ya dominika ya 16 ya mwaka A kwa Kanisa.

Liturujia D16
22 July 2023, 14:11