Jumuiya ya Mt.Egidio:Vijana wa amani 1000 wa Ulaya huko Padova na Venezia
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
“Urafiki wa Ulimwenguni kwa Wakati Ujao wa Amani" ndiyo kauli mbiu ambayo inaongoza mkutano wa kimataifa wa vijana 1000, ambao ni wanafunzi wa shule za Sekondari na vyuo vikuu, kutoka nchi 13 za Ulaya ili kukutana kuanzia tarehe 25 hadi 27 Agosti 2023 huko Padova na Venezia nchini Italia. Huu ni mkutano wa Amani, kama Harakati ambayo inahusiana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambayo inajishughulisha kila siku katika vitongoji na watoto walio na shida, wasio na makazi, wazee peke yao, na imehamasisha hata likizo za mshikamano na wakimbizi na mitaa katika kambi za Ugiriki na Cyprus kwenye miezi ya kiangazi.
Ni tukio kubwa la Ulaya kwa ajili ya amani, lililohisiwa sana, katika wakati huu uliowekwa na vita vya kutisha nchini Ukraine. Na hasa kutoka Ukraine ambapo Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaendelea kusaidia idadi kubwa ya watu kwa usambazaji wa vyakula, usafirishaji wa vifaa vya matibabu na imefungua vituo vya elimu kwa watoto na vijana, pia shukrani kwa msaada wa wakimbizi wengi ambao wamejiunga na Jumuiya hiyo katika kazi yake ya kibinadamu. Kwa njia hiyo Wasichana 70 na wavulana kutoka Kiev, Lviv, Ivano-Frankivsk wamefika Mkoa wa Veneto. Kwa pamoja na wenzao kutoka nchi nyingine za Ulaya, wametaka kutoa sauti kwa ajili ya matumaini ya kizazi chao ya amani na kujadili masuala mbalimbali kama vile ya ikolojia, uhamiaji, umaskini na zaidi katika kueneza utamaduni wa mshikamano, ushirikiano na ufungamanishwaji.
Siku ya uzinduzi ilikuwa ni siku ya Ijumaa tarehe 25 Agosti kwa kuanza na mkutano ulioongozwa na Mario Giro, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Italia uliopewa mada: “Vijana Ulimwenguni:kuuelewa ulimwengu wetu tata” na ulifunga kwa mkesha wa maombi ya amani ulioongozwa na Kardinali Matteo Zuppi, rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Italia (CEI) na mjumbe maalum wa Papa Francisko kwa nchi ya Ukraine na Urussi aliyofanya hivi karibuni. Jumamosi asubuhi tarehe 26 Agosti 2023 vijana walishiriki katika mkutano na Marco Impagliazzo, rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye kichwa: “Kila kitu kinaweza kubadilika.” Mkutano utahitimishwa Dominika alasiri, tarehe 27 Agosti 2023 huko Venezia, na umati wa watu wanaotafuta amani katika Uwanja wa Mtakatifu Marco.