Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC., Wanamwimbia Mungu Utenzi wa Sifa na Shukrani
Na Sr. Lucina John Gadiyet, ASC., Roma, - Italia.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Ni katika muktadha huu, katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, Dominika tarehe 6 Agosti 2023, Wanovisi wanne wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC wanafunga nadhiri zao za kwanza mjini Acuto, nchini Italia. Tarehe 19 Agosti 2023, Masista watatu wataweka nadhiri zao za daima sanjari na Jubilei ya Miaka 25 ya Maisha ya Kitawa kwa Masista wanne, matendo makuu ya Mungu. Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC walifanya mkutano mkuu wa XXI wa Shirika huko Lima –Peru kuanzia tarehe 5 Julai hadi tarehe 28 Julai 2017. Kati ya maamuzi na mapendekezo ya utekelezaji wa hati ya mkutano mkuu, mojawapo ni kuanzisha Jumuiya ya Wanavosi wa Shirika Kimataifa.
Mnamo mwaka 2019 tulithubutu kuanzisha jumuiya ya kimataifa iliyoundwa Masista wanne (4), wenye mwingiliano wa tamaduni mbalimbali kutoka Italia, India, Tanzania na Croatia Ili kwa pamoja waweze kuwasindikiza walelewa katika safari ya utafiti juu ya wito wao, na mwaka huohuo waliingia wanovisi saba (7) na wao kutoka Mataifa yenye mwingingiliano wa utamaduni tofauti, Italia, India na Croatia, hao ndio waliokuwa wanovisi wa kwanza kufungua Jumuiya ya Wanovisi Kimataifa. Kati ya wanovisi walioingia awamu ya pili mwaka 2021 ni wanovisi watano (5) kutoka Tanzania, india na Italia. Wanovisi hao, baada ya kumaliza mwaka wao wa mazoezi ya kichungaji ambao waliofanyia hapa Italia, kati yao waliokuwa tayari kufanya maamuzi ya kuendelea walituma maombi yao kwa Mama Mkuu wa Shirika kuomba kufunga nadhiri za kwanza kwa pamoja kama kundi hapa Italia. Baada ya ombi lao kukubaliwa kwa mapenzi ya Mungu hapo tarehe 06/08/2023 Mnovisi Rashma Denish- kutoka India, Mnovisi Agnes Andrea, Angelista Shirima na Pia kutoka Tanzania watafunga Nadhiri zao za kwanza Siku ya Sherehe ya kung’ara Bwana sura, katika kikanisa cha Nyumba Mama- Acuto. Nyumba ya kwanza alipoanzisha Shirika Mtakatifu Maria De Mattias kunako mwaka 1834.
Katika Historia ya Shirika Masista hao ni wa kwanza kama wanovisi wa Shirika Kimataifa kufunga nadhiri zao wakiwa wote kwa pamoja na hasa katika nyumba ya kwanza ya Mwanzilishi. Pamoja na Changamoto mbalimbali zilizokuwepo mfano, janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 lakini bado Mungu ameweza kufanikisha, hatimaye leo hii tunaposherehekea tena mkutano wa XXII tayari tuna matunda ya utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliotangulia yaani mkutano mkuu wa XXI wa Shirika uliofanyika Lima, nchini Perù. Tunamshukuru sana Mungu kwa zawadi ya hawa Masista Wanne kuitikia wito wa Mungu katika Kanisa kuptia Shirika letu la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Kristo. Tunawakaribisha na kuwaombea neema na baraka ili kudumisha hamu na moyo wa huduma ya kuwaendea wahitaji na kwa pamoja tuweze kushiriki na Kristo Yesu katika kazi ya ukombozi.
Wakati huo huo, Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu Kanda ya Tanzania” tunamshukuru Mungu, ndani ya mwaka huu tunaposherehekea Mkutano mkuu wa Shirika, kwetu sisi umeambatana na neema nyingi za kusherehekea miito ya masista wetu ambao wanaendelea kuitikia wito wa Mungu katika hatua mbalimbali za maisha yao ya kitawa. Mnamo tarehe 19/08/2023 siku ambayo kwetu sisi Masista Waabuduo Damu ya Kristo tunafanya kumbukizi ya kifo cha Mt. Maria De Mattias 20/08/1866, tutakuwa na Ibada ya Misa Takatifu katika Kikanisa cha nyumba ya Makao makuu ya Shirika Kanda ya Tazania, Itakayoadhimishwa na Mhashamu Askofu mkuu Beatus Kinyaia wa Jimbo kuu la Dodoma Shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya tukio hili kubwa la Masista wetu watatu ambao ni Sr. Magdalena George, Sr. Mary Malele na Sr. Rosemary Malele hawa ni watoto mapacha kufunga nadhiri zao daima na Masista wetu wanne Sr. Fortunata Shabani, Sr. Laura William, Sr. Magdalena Pantaleo na Sr. Yohana Maley kumshukuru Mungu kwa kusherehekea Jubilei ya fedha ya maisha ya kitawa yaani Jubilei ya Miaka 25 ya Maisha ya Kitawa. Tunawashukuru sana Masista hawa kwa kuendelea kuitikia wito wao na moyo wa kujitoa katika kumtumikia Mungu na wapendwa jirani ndani ya Kanisa kupitia Shirika letu, tukiendelea kutgemezana Katika Maisha ya Jumuiya na Kuishi kwa hiari mashauri ya Injili.