Tafuta

Liturujia imetenga siku maalumu, tarehe 6 Agosti kila mwaka kuadhimisha Kung’ara sura kwa Yesu katika hadhi ya sikukuu. Liturujia imetenga siku maalumu, tarehe 6 Agosti kila mwaka kuadhimisha Kung’ara sura kwa Yesu katika hadhi ya sikukuu.   (ANSA)

Sherehe ya Kung'ara Bwana Wetu Yesu Kristo 6 Agosti 2023

Dominika hii ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni inayoongozwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa B. Maria katika maisha ya Kanisa. Kanisa la Tanzania linaadhimisha Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2023. Ujumbe wa Papa Francisko unanogeshwa kwa kauli mbiu: “Zungumzeni Ukwe katika upendo"

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tarehe 6 agosti kila mwaka, Kanisa huadhimisha sherehe ya Kung’ara Sura Bwana wetu Yesu Kristo. Mwaka huu siku hii imeangukia siku ya Jumapili, kwa hiyo inachukua nafasi ya ambayo ingekuwa dominika ya 18 ya mwaka A. Kumbe, masomo ya Misa tunayosoma dominika hii na ambayo tunayatafakari katika kipindi hiki sio yale ya dominika ya kawaida bali ni masomo ya Sherehe ya Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo. Dominika hii ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, Ureno inayoongozwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Katika dominika hii, Kanisa la Tanzania linaadhimisha Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2023. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unanogeshwa kwa kauli mbiu: “Zungumzeni Ukweli Katika Upendo”: Veritatem facientes in caritate. “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Efe 4:15.

Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Unabii. Torati na Ushuhuda
Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Unabii. Torati na Ushuhuda

Kung’ara sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo: Tukio la Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo linaelezwa na Injili tatu: Marko, Mathayo na Luka, kila moja ikilenga kuweka msisitizo katika eneo lake bila kuwa na utofauti mkubwa kati yao. Kusimuliwa na injili zote tatu tena bila tofauti kubwa kunaonesha umuhimu ambao wainjili wamelipa tukio hili la Yesu kugeuka sura. Umuhimu wa tukio hili unaonekana pia katika liturujia. Injili ya kugeuka sura husomwa katika kipindi cha Kwaresima, kila dominika ya 2 ya Kwaresima. Zaidi ya hapo Liturujia imetenga siku maalumu, tarehe 6 Agosti kuadhimisha Kung’ara sura kwa Yesu katika hadhi ya sikukuu. Tukio lenyewe lilikuwaje? Kutoka katika masimulizi ya Wainjili tunapata kujua kuwa Yesu aliwachukua wanafunzi wake watatu: Petro, Yakobo na Yohane akapanda nao mlimami kusali. Akiwa anasali sura yake ikageuka, ikang’ara na mavazi yake yakawa meupe sana. Kumbe, mazingira ambamo tukio hili linatendeka ni mazingira ya sala, sala ya Yesu. Sasa, akiwa katika hali hiyo wanatokea Musa na Eliya. Hawa ni watu muhimu sana katika historia ya wayahudi. Musa ndiye anayewakilisha Torati, yaani sheria na taratibu zinazoongoza maisha yote ya Wayahudi. Eliya yeye anawakilisha Manabii. Zaidi ya hapo kuweka pamoja Musa na Eliya, yaani Torati na Manabii, katika lugha ya kibiblia maana yake ni ufunuo wa Maandiko Matakatifu. Torati na Manabii ni neno lililotumika kumaanisha Maandiko Matakatifu katika Agano la Kale. Simulizi linaendelea kutuonesha kuwa Petro anapoona hali hiyo ya utukufu anamwambia Yesu “ni vizuri kuendelea kuwa hapa, tujenge vibanda vitatu kimoja cha kwako, kimoja cha Musa na kimoja cha Eliya.”

Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Utimilifu wa Unabii na Torati
Sikukuu ya Kung'ara Bwana: Utimilifu wa Unabii na Torati

Kwa nini Petro anazungumza habari ya vibanda? Petro anazungumza habari ya vibanda kwa sababu tukio hilo la Yesu kugeuka sura lilitokea katika kipindi ambacho Wayahudi walikuwa wakiadhimisha sikukuu yao ya kila mwaka iliyofahamika katika sikukuu ya vibanda. Hii ilikuwa ni sikukukuu ambayo walikumbuka kuwa kwa miaka 40 waliishi jangwani kwenye vibanda baada ya kutoka Misri wakiwa wanaelekea nchi ya ahadi. Sikukuu ya vibanda ilidumu kwa juma zima. Hii ndiyo namna zinavyotafsiriwa siku sita wanazoongelea Wainjili Mathayo na Marko na siku nane anazoongelea Mwinjili Luka. Mwisho wa tukio hilo ni kwamba linashuka wingu na ndani ya wingu hilo inasikika sauti: huyu ni mwanangu mpendwa msikieni yeye”. Wingu na sauti hii ni ile ile iliyosikika siku ya ubatizo wa Yesu. Wingu ni alama ya uwepo wa Mungu kumbe sauti hiyo inayosikika inaonekana moja kwa moja kuwa ni sauti ya Mungu. Tukio hili ni tukio lenye mafundisho mengi na tena lina alama nyingi sana. Linaonesha mabadiliko ambayo Yesu aliyapata daima alipokuwa akisali, akizungumza na Baba; linaonesha utukufu wa Mungu ambao daima Yesu aliuficha katika ubinadamu wake na linaonesha utukufu ambao Yesu na wote wanaomwamini wataupata baada ya adha ya Msalaba na mahangaiko ya maisha ya duniani; linaonesha Yesu kama utimilifu wa Torati na Manabii na linaagiza kumsikiliza yeye, yaani kulipokea Neno lake na kuliishi kama wafuasi wake.

Siku ya kuhitimisha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni
Siku ya kuhitimisha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni

Tafakari ya Masomo: Tukiyaangalia kwa pamoja masomo ya Misa ya sherehe hii kwa namna ya pekee somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Danieli tunaona kuwa msisitizo wa liturujia ya leo ni kutuelekeza kumtambua Yesu kama masiya aliyetabiriwa na aliyekuwa akisubiriwa. Somo la nabii Danieli (Dan. 7:9-10.13-14) linazungumzia ujio wa mwana wa mtu, ujio wa Masiha. Linaamsha matumaini ya watu wa Mungu kuhusu ujio wa mkombozi na linaeleza huyo mkombozi atakayekuja atakuwa wa namna gani. Katika mwanga wa somo hili la kwanza, tunaona kuwa kitendo cha Yesu kuwachukua hao Mitume watatu na kugeuka sura mbele yao tena katika namna ambayo Danieli na Manabii wengine walieleza itakavyokuwa sura ya masiha, maana yake ni kuwa Yesu alitaka kuwaonesha kuwa wakati wa masiya umefika na kwamba Yeye ndiye masiya aliyekuwa akisubiriwa. Ni katika mwanga huu tunaona kuwa alama ambazo zinazindikiza tukio la kugeuka sura kwa Yesu kuwa ni alama za kimasiya. Musa na Eliya wanaonekana pamoja kama uthibitisho kuwa yale waliyotaka watu wayaishi katika Torati na yale ambayo manabii waliyatabiri, yote yanaunganika katika Kristo. Ni yeye anayeyaunganisha yote katika nafsi yake na ni yeye anayeyapatia yote hayo ukamilifu wake. Hii ndiyo sababu ya ile sauti inayosikika ikisema “msikieni yeye.” Kwa vile yeye ndiye utimilifu, Yesu haafiki swali la Petro kujenga vibanda vitatu. Ni yeye kwa ujio wake na kwa kutwaa mwili amejenga kwetu maskani yake, au kibanda kama ile hema ya mkutano na Mungu wakati wa Musa.  Kila anayempokea na kila anakubali kuishi kwa ajili yake anakuwa maskani hai, au vibanda hai vya uwepo wa Mungu.

Vibanda vya maungamo: Mahakama ya huruma ya Mungu
Vibanda vya maungamo: Mahakama ya huruma ya Mungu

Katika maisha ya kila siku: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kupata ufafanuzi wa fumbo tunaloliadhimisha katika sherehe ya kugeuka sura Bwana wetu Yesu Kristo na baada ya kuyaangalia masomo ya Misa katika mwanga waa fumbo hilo, ni wakati sasa wa kujitafakari fumbo la sherehe hii pamoja na fundisho la Neno la Mungu linaniambia nini katika maisha yangu ya kila siku. Ni muhimu daima kujiuliza swali hili kila tunaposoma na kutafakari Neno la Mungu ili Neno lisibaki nje ya maisha yangu bali ujumbe wake unisaidie kuyaelewa vema yale ninayoishi hasa yale ambayo Mungu anataka niyaishi. Leo tumelipokea hili neno kwamba Yesu anapogeuka sura anadhihirisha kuwa ndiye masiha aliyeahidiwa na ndiye utimilifu wa ahadi za Mungu kwa watu wake. Na mimi ninajiuliza, ninamwona Yesu kama ndio utimilifu wa yale ninayomwomba Mungu kila siku? Au kwangu kuwa mfuasi wa Yesu, kwenda Kanisani, kuishi Sakramenti na kuyatoa maisha yangu kwa ajili ya wengine kama anavyofundisha yeye ni vitu ambavyo kwangu vimepitwa na wakati na havina nafasi tena? Yesu anapogeuka sura na kuuonesha utukufu wake wa kimungu ananionesha mimi na wewe kuwa kwanza tumeitwa kuufikia utukufu. Wito wetu ni kuufikia utukufu wa Mungu mbinguni. Pili utukufu wa Yesu anatuonesha ule utukufu ambao Mungu ameuweka ndani yetu, utukufu ambao kwa njia ya ufuasi wetu, kwa njia ya sadaka zetu na kwa njia ya huduma tunazozitoa utukufu huo unaendelea kung’ara, unayaangaza maisha yetu na ulimwengu nuru ya Kristo. Nakutakia tafakari njema ya Sherehe ya Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo.

Kung'ara Bwana

 

05 August 2023, 15:30