Tafakari Dominika ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukarimu wa Mungu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 18 mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yamejikita katika kuidhihirisha ukarimu wa Mungu kwa mwanadamu unayofumbatwa katika upendo wake wa kumtoa Mwanae wa pekee ili kila amwaminiye na kumfuata apate uzima wa milele. Katika mahangaiko yetu ya kila siku Mungu ndiye ngao na kinga yetu. Yeye daima atazima njaa zetu za kila aina naye anataka nasi tuwatendee wenzetu hivyo hivyo. Anayemtendea mwenzake kwa ukarimu, Mungu pia atamtendea kwa ukarimu kwa sababu kipimo tupimacho ndicho tutakachopimiwa. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 55:1-3). Somo hili ni mwaliko wa kuingia katika Ufalme wa Mungu unaofananishwa na karamu nono pasipo malipo. Mwaliko huu ulielekezwa kwa wana wa Israeli walipokuwa wamegubikwa na njaa na mahangaiko mbalimbali wakiwa utumwa na kuteseka mateso mengi ya kila aina. Katika hali hiyo Mungu anawapelekea ujumbe wa faraja. Kwa kinywa cha Nabii Isaya anawafariji watu wake akiwalika wajongee katika karamu ya meza ya Bwana ambayo kuna vyakula na vinywaji tele vilivyoandaliwa kwa ajili yao akisema: “Kila aonaye kiu, njooni majini, naye asiye na fedha; nunueni mle; naam, njoni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila thamani. Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema. Na kujifurahisha nafsi zenu, kwa unono, tegeni masikio yenu, na kunijia. Sikieni, na nafsi zenu zitaishi, nami nitafanya nanyi agano la milele, naam, rehema za Daudi zilizo imara”. Baadaye Wayahudi waliruhusiwa kurudi Yerusalemu na utabiri wa Nabii Isaya ulitimia hekalu lilipojengwa nao wakaanza kumwabudu Mungu wa kweli.
Faraja hii anayowapa Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya ni ya kiroho zaidi ambapo utabiri huu wa kununua bila gharama unatimizwa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu ambaye kwa upendo wake kwetu anatoa maisha yake kulipia gharama ya adhabu ya dhambi zetu na kujitoa mwenyewe kuwa chakula chetu cha kiroho yaana Ekaristi Takatifu. Yesu mwenyewe anasema; “Mimi ni mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni” (Yoh 6:51) na maji ya uzima wa milele naye anayenywa hatasikia kiu kamwe tena (Yn 4:10,14). Ndivyo kiitikio cha wimbo wa katikati kinavyosisitiza; “Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake” (Zab. 144: 8-9, 15-18, (K) 16). Na wimbo wa mwanzo nao unatilia mkazo ukisema; “Ee Mungu, uniokoe, ee Bwana, unisaidie hima. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, ee Bwana, usikawie” (Zab. 70:1, 5). Nayo sala ya mwanzo inasema; “Ee Bwana, uwe nasi watumishi wako, utukirimie mema yako yasiyo na mwisho sisi tuombao. Uyatengeneze na kutuhifadhi mema hayo, kwa vile tunaona fahari kwamba wewe ndiwe mwumba na mfalme wetu”. Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8: 35, 37-39). Katika somo hili Mtume Paulo analisitiza jinsi pendo la Mungu lilivyodhihirishwa kwetu katika Kristo Yesu. Nasi tukikubali kuongozwa na hilo pendo, hakuna hatari wala matatizo yawezayo kututisha, “wala dhiki, wala shida, wala adha, wala njaa, wala uchi, wala hatari, wala upanga, wala mauti, wala uzima wala malaika, wala wenye mamlaka wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”. Lakini kinyume chake ni kweli, kwa wale ambao wanaukataa upendo wa Kristo na kuutupilia mbali, dhiki, shida, adha, njaa, uchi, hatari, upanga na mauti ndio chakula chao.
Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt.14:13-21). Sehemu hii ya Injili inatueleza kuwa Kristo ni Masiha, mfano wa Musa aliyewalisha Waisraeli; tena inadokeza matayarisho ya karamu ya Ekaristi takatifu; na mwishowe inaonyesha upendo wa Mungu anayetualika wote kwenye karamu mbinguni. Dokezo la matayarisho ya karamu ya Ekaristi Takatifu ni ishara ya upendo wa Mungu kwetu unaojidhihirisha kwa njia ya Yesu anayetualika sote kwenye karamu ya mbinguni kwa kuibariki na kuimega mikate mitano na samaki wawili na watu wote wakala wakashiba. Kwa njia ya Yesu huruma ya Mungu inayofumbatwa katika upendo inajifunua kwa Yesu kuwaonea huruma kwa watu walio kama kondoo wasio na mchungaji hivyo anawalisha kwa neno lake kwa mafundisho yake, anawaponya magonjwa yao, anawashibisha njaa zao kwa kuwapa chakula kwa muujiza wa kuongezeka idadi ya mikate na samaki. Muujiza huu ni mwangwi wa kuwekwa kwa Ekaristi Takatifu katika karamu ya mwisho, kwa sababu matendo haya mawili yanafanana: “Kisha atachukua mikate mitano na samaki wawili, akainua macho yake mbinguni na kubariki, akaimega na kuwapa wafuasi wake nao wakawapa makutano” (Mt. 14:19). Wakati walipokuwa wanakula, Yesu alichukua mkate na baada ya kuubariki, aliumega na kuwapa wanafunzi wake akisema; “Twaeni, mle, huu ni mwili wangu” (Mt. 26:26).
Nasi kila mara tunapokusanyika katika adhimisho la Ekaristi Takatifu muujiza huu unafanyika, kwanza Yesu anatuponya magonjwa yetu kwa kutusamehe dhambi zetu ndiyo maana tunaanza maadhimisho ya Ekaristi Takatifu kwa kumwomba msamaha Mungu na wenzetu, pili tunalisha kwa Neno lake katika liturujia ya Neno kisha tunashibishwa kwa Ekaristi Takatifu. Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu kwa pamoja vinafanya mlo kamili wa kiroho. Na kupokea kimoja na kuacha kingine hakukidhi mahitaji ya kiroho. Yesu angeweza kuandaa chakula kwa ajili ya mkutano bila kuwa na kitu chochote. Badala yake alichagua kutumia mikate mitano na samaki wawili alivyokuwanavyo mtoto. Hii inatuonyesha umuhimu wa majitoleo yetu wakati wa Sadaka ya Misa Takatifu ambapo sala na majitoleo yetu ya vipaji mbalimbali vinageuzwa kuwa hazina yenye thamani inayotusaidia kupata uzima wa milele baada ya maisha haya. Ndivyo inavyosisitiza sala ya kuombea dhabihu ikisema; “Ee Bwana, tafadhali uzitakatifuze dhabihu hizi kwa wema wako. Uikubali sadaka hii ya roho zetu, na kutufanya sisi wenyewe tuwe kwako sadaka ya milele”. Zaidi sana inatunyesha umuhimu wa kila mmoja kuchangia chochote kwa ajili ya manufaa ya mwingine. Tusiwe wachoyo na kujilimbikizia vitu ambavyo hata kama tukivitumia kila siku hatuwezi kuvimaliza. Kujilimbikizia vitu vingi ambavyo havitumii wakati wapo wanaokufa kwa njaa na kiu ni dhambi kubwa mno. Ni katika hili tutahukumiwa siku ya mwisho.
Kiujumla masomo ya dominika hii yanatambua wazi kuwa kila mwanadamu anahitaji chakula na kinywaji ili aweze kuishi. Mahangaiko yote ya hapa duniani ni kutafuta chakula cha kuzima njaa yake na kinywaji cha kukata kiu yake. Lakini mahangaiko haya yote ni kutafuta furaha ambayo hawezi kuipata katika utimilifu wake mpaka pale atakapouona uso wa Mungu. Ni wazi kuwa moyo wa mwanadamu unatafuta furaha katika vitu vilivyoumbwa. Lakini kati ya vitu vilivyoumbwa hakuna chochote kinachoweza kumpa mwanadamu furaha ya kweli na ya kudumu. Mtakatifu Agustino alilitambua hili baada ya wongofu wake na kusema: “Umetuumbwa kwa ajili yake ee Bwana na mioyo yetu haiwezi kutulia mpaka itakapotulia ndani yako”. Furahi hii inaanza kujifunua kwetu kwa kuwahudumia wengine kwa upendo na bila uchoyo. Kama Kristo alivyojitoa mwenyewe kwa ajili yetu, sisi nasi tunawajibu wa kujitoa wenyewe kuwahudumia wengine kwa maisha yetu. Haitoshi kutoa vitu kwa ajili ya wengine bali kujitoa wenyewe katika kuwahudumia kwa vile tulivyonavyo. Tukifanya hivyo tutaanza kuionja furaha ya kweli hapa hapa duniani. Basi tuombe neema za Roho Mtakatifu ili tuweze kuwa na moyo wa kutokuchoka kuwahudumia ndugu zetu wahitaji ikibidi kuwaandalia karamu za vinono tena bure ili tupate kustahilishwa nasi kuingia katika karamu ya uzima wa milele mbinguni ambapo hatutaona tena njaa kamwe maana tutakuwa pamoja na Kristo aliye shibe yetu kama antifona ya wimbo wa komunyo inavyosema; “Bwana asema: Mimi ndimi mkate wa uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe” (Yn. 6:35). Nayo sala baada ya komunyo inahitimisha ikisema; “Ee Bwana, utulinde daima na popote sisi uliotutia nguvu kwa chakula cha mbinguni. Utufadhili siku zote ili tustahili ukombozi wa milele”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo.