Tanzania:Jubilei ya miaka 25 ya Padre M.Mutasingwa,tudumishe imani!
Na Patrick P.Tibanga, - Radio Mbiu, Bukoba Tanzania.
Wazazi na walezi wametakiwa kuwafundisha watoto wao maadili na kuwalea katika misingi Imara ya kumpendeza Mungu na kuwafundisha watoto kazi za mikono. Wito huo umetolewa na Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Mateso saba Kashozi, Padre Samwel Muchunguzi katika homilia yake tarehe 18 Agosti 2023 katika adhimisho la Misa takatifu ya Shukrani kwa miaka 25 ya Upadre wa Padre Maxmillian Mutasingwa, Misa iliyofanyika, huko Kagondo Jimboni Bukoba, Tanzania kwa kuudhuriwa na maaskofu, mapadre, watawa .
Katika homilia yake Padre Muchunguzi alisema kuwa ni wajibu wa kila mzazi kumlea mtoto katika misingi ya maadili, sala na kuwafundisha kazi na kusema kuwa Mtoto anatakiwa kupewa malezi tangu tumboni, na kuwasisi wazazi kuwa walimu wa kwanza kabla ya kuwapeleka watoto shuleni na wale wanaojenga shule alisema “ninawaomba lengo liwe malezi na sio biashara kama ilivyo kwa baaadhi ya shule.”
“Mtoto anatakiwa kupewa malezi bora kabla hajazaliwa, yaani akiwa tumboni kwa mama, hiyo ndio shule kubwa kuliko zote, hivyo mzazi anza wewe kuwa mwalimu mkuu wa mtoto akiwa bado tumboni, ninawasihi wazazi baba na mama, familia yenu ndio iwe Day Care na sio kuwapeleka watoto katika shule hizo na kuwaacha huko siku nzima, au kuleta wawekezaji wa nje kwaajili ya kuwalea watoto wenu,” Alisema Padre Samwel Muchunguzi katika homilia yake.
Akiendelea na homilia yake Padre Samwel aliongeza: “Tunawaachia watu walee watototo wetu, tunaposema wawekezaji wengi tunawaza kutoka nje ya nchi, kila kitu sasa tunawaza wawekezaji na sasa hivi familia zilizo nyingi zinalelewa na wawekezaji tunawaachia watu wa mshahara walee watoto wetu. Jiulize mtoto wako analelewa na nani? Na mtoto ili awe mzuri inategemea na muwekezaji wako, na ubora wa malezi utategemea na kiasi anacholipwa mwekezaji wako, hayo ni majanga alafu tunauliza ni nani katuloga, na watoto waliolelewa na wawekezaji wakipewa idara waziongoze wanashindwa.” Katika tafakari yake pia aliitaka Serikali na wadau wa mazingira kufadhili wadau wa misitu kwa kuwasaidia pembejeo husika wanapohudumia misitu na sio kusubiri kutoza miti ushuru au mbao kwa kisingizio cha kutunza mazingira na sio kudai kodi ya ukataji wa miti baada ya miti kustawi.
“Tujifunze kwake Padre Maxmillian kupanda na kutunza mazingira, hii ni kwa wadau wa mazingira na ninajua serikali mpo hapa wahusika tusiwe watu wakusubiri kutoza watu ushuru katika miti kwa kigezo cha kutunza mazingira na mbao, bali tuwafadhili wadau wa misitu tulionao kwa kuwasaidia pembejeo husika wakati wanahudumia misitu yao, mtu anaanza kupanda mti, anakuza na kumwagilia, wakati wa kuikata eti apate ruhusa kwanini? Wakati wa kukata ndio mnakuja kuchukua tozo na ushuru hapana! Sawa mnalinda misitu lakini mkumbuke na kuwasaidia ili mtu huyo anapokuja kulipa tozo na makato yote baada ya miti yake kukua na nyie mseme mmesaidia.”Alifafanua Padre Muchunguzi.
Padre Samwel Muchunguzi aidha amewataka waamini kuiga mfano wa msimamo thabiti wa Imani alionao Padre Maxmillian, hasa kwa nyakati hizi za wachungaji feki na wajanja wa kuwahadaa waamini na kwamba, “kati ya sifa kuu za manabii ni kupambana na Imani za kishirikina na Imani potofu na ushabiki wa imani hizo” na kuwasihi waamini kuwa watu wa shukrani kwa kurudisha fadhila kwa walipotokea.
Kwa kutilia mkazo, kuhani huyo alisema: “ibilisi hajalala anazunguka kama simba kwa kutafuta mawindo (1Pet 5:8-9), hivyo wakiwa watu wa kutangatanga watatekwa na wachungaji wasio na misimamo hivyo kuwa imara katika Imani yako na kuwa watu wa kurejesha shukrani kwa yote waliyopitia.”