Tafuta

Mimi ndimi nuru ya ulimwengu;yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yn. 8:12). Mimi ndimi nuru ya ulimwengu;yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yn. 8:12). 

Dominika ya 23 Mwaka A:Maonyo na msamaha katika jumuiya kikristo

Ili kuonesha jinsi msamaha wa kindugu ulivyo muhimu,Yesu anasisitiza na kusema;“Yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni” (Mt. 18:18).Na Kristo akiwa katikati yetu tutaweza kuona kila lililojema na kulifanya maana Bwana ni nuru ya ulimwengu.

Na Padre Paschal Ighondo; –Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 23 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika hii yanatukumbusha wajibu wa kila mbatizwa katika kuishuhudia injili kwa maneno na matendo katika maisha ya kila siku. Wajibu huu ni pamoja na kuwaongoza wakosefu ili wapate kutambua na kutubu makosa yao na kurudi katika njia ya haki ya kumpendeza Mungu na jirani. Mwongozo wa kutimiza wajibu huu unatolewa na Yesu mwenyewe akisema; “Ndugu yako akikukosea, mwonye, patana naye na umrudishe kwa Mungu” hakimu mwenye haki kama mzaburi anavyotutafakarisha katika wimbo wa mwanzo akisema; “Ee Bwana, wewe ndiwe mwenye haki, na hukumu zako ni za adili. Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako” (Zab. 119:137, 124).

Somo la kwanza ni kitabu cha Nabii Ezekieli (Eze. 33:7-9). Mungu alimwita nabii Ezekieli kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli wakati wa utumwa wa Babeli. Somo hili linaeleza wazi kazi aliyopewa nabii Ezekieli na Mungu - kuwaonya na kuwaongoza wakosefu waache njia zao mbaya wawe watu wema. Nabii Ezekiele alipaswa kuwaonya watu waovu waziache njia zao mbaya. Kwa upande wake Nabii asipomwonya mtu mwovu aiache njia yake na mtu huyo akifa katika uovu wake, Mungu atamdai damu yake mtu huyu. Lakini akimwonya mtu mbaya kusudi aiache njia yake mbaya, na huyo mtu mbaya akakaza shingo, asiiache njia yake mbaya, basi atakapokufa katika uovu wake, atahukumiwa, lakini nabii ataiokoa roho yake. Hii ndiyo kazi ambayo Mungu alimwitia nabii Ezekieli aikamilishe, kuwaonya na kuwaongoza wakosefu wa taifa la Israeli watubu.

Ndivyo anavyoitwa kufanya kila mbatizwa kwani kwa sakramenti ya ubatizo kila mkristo anashirikishwa ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Hivyo tunapaswa kuwa wasikivu kwa mwito huu kama wimbo wa katikati unavyotuusia ukisema: “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu” (Zab. 95:7-8). Tutimize basi wajibu huu wa kinabii wa kuonyana sisi kwa sisi kwa moyo wa upendo ili maisha yetu yawe ya kumpendeza Mungu ndipo tutaweza kuimba kwa pamoja na mzaburi tukisema; “Njoni tumwimbie Bwana, tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele yake kwa shukrani, tumfanyie shangwe kwa zaburi. Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba. Na sisi tu watu wa malisho yake, na kondoo za mkono wake (Zab. 95:1-2, 6-9).

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 13:8-10). Somo hili linaweka wazi ukweli kuwa kiini cha maisha yetu ya kikristo ni kuonyeshana daima mapendo kwa matendo. Tukifanya vile tunatimiza sheria zote kama anavyosema Mtume Paulo: Ndugu zangu; “Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani, na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Kwa kuwa pendo halimfanyii jirani neno baya, basi pendo ndilo utimilifu wa sheria” (Rum. 13:8-10). Mtume Paulo aliwaandikia wakristo warumi barua hii akiwaasa watambue kuwa ni kwa upendo na huruma kuu ya Mungu wao wamekuwa wakristo kwa gharama ya damu azizi ya Yesu. Hivyo watambue deni walilonalo kwa Kristo aliyewakomboa kutoka utumwa wa dhambi na kuwapa Roho Mtakatifu na kuwafanya kuwa watoto wa Mungu na kuwaweka katika njia ya kufika mbinguni kwenye uzima wa milele. Na namna ya pekee ya kulipa deni hili ni kutenda matendo ya huruma kwa jirani zao kwa moyo wa upendo.

Ujumbe huu wa Mtume Paulo kwa wakristo wa Roma wa kuishi maisha ya jumuiya kindugu na kwa kupendana, unamhusu kila mkristo wa nyakati zote, kwani kila aliyebatizwa kwa jina la Yesu Kristo amewekwa huru kutoka utumwa wa dhambi kwa kulipiwa deni lake kwa damu azizi ya Yesu iliyomwagika msalabani. Na namna ya pekee ya kulipa deni hili ni matendo ya huruma kwa ndugu zetu wahitaji yanayopaswa kuongozwa na moyo wa upendo kwao (Yoh 13:34). Tukumbuke kuwa yote tunayofanya kama hakuna upendo, ni bure (1Kor 13:1-3). Upendo unadai kuwapokea, kuwaonya na kuwasamehe wanaotukosea, upendo unatudai kuwajali maskini, kushiriki furaha na machungu yao, kuwa na amani na watu wote, kutokulipa kisasi, kulipa ovu kwa jema (Rom 13:14-21). Hivi ndivyo tunavyopaswa kuishi katika jumuiya zetu za kikristo.

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 18:15-20). Sura ya 18 ya Injili ya Mathayo imebeba mafundisho, mawaidha na mausia ya namna tunavyopaswa kuishi maisha ya kijumuiya. Kwa kuwa jumuiya ya wakristo si kwa ajili ya watakatifu bali kwa ajili ya wakosefu wanaouendea utakatifu, aliyoianzisha Yesu aliyekuja kwa ajili ya wenye dhambi. Basi, moja ya mausia muhimu sana katika maisha ya kijumuiya ni kuonyana kindugu pale tunapokoseana na kusameheana. Yesu anaitilia msisitizo suala la kuonyana na kusameheana kidugu kwa kuwa mambo haya mawili ni ya muhimu sana kwa maisha ya kikristo na anatoa mwongozo wa namna, jinsi na hatua za kuonyana. Jambo la muhimu kabisa katika kumwonya ndugu aliyekosa, tunapaswa kufanya hivyo kwa upendo na kwa hatua. Hatua ya kwanza inatudai kumsahihisha mtu aliyekosa kwa faragha, tukiheshimu hadhi na utu wake, pamoja na kulinda jina lake hata kama ni mkosaji ili mkosefu huyu atambue na kuonja upendo wa kindugu. Hatua hii ya kwanza ikishindikana tunapaswa kuomba msaada kutoka kwa mtu mwingine anayeweza kumshauri mkosefu kwa upendo. Na kama hatua hii ya pili ikishindikana ndipo hapo tunapaswa kuripoti kwa mzee wa Kanisa. Kama mkosaji huyu atakaza shingo na kuziba masikio yake basi jumuiya ina haki ya kumtenga.

Kumbe ili kumsaidia mkosaji hatupaswi kuwa wepesi wa kueneza uovu na makosa yake kwa kuwatangazia wengine na kukimbilia adhabu. Kutangaza makosa ya mkosaji hata kabla ya kumuonya na kumsahihisha ni dalili wazi kuwa mwenendo wetu hauongozwi na upendo wa kindugu. Hivyo basi kama Mungu alivyomweka nabii Ezekieli kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli ili kuwaonya wakosefu watubu, nasi pia kwa ubatizo tumewekwa kuwa walinzi wa ndugu zetu, kuwaonya wanapokosea na kuwasamehe wanapoomba msamaha. Tuwaonye na kuwaongoza wakosefu wapate kutubu. Sisi tulipobatizwa, tulipewa jukumu la kushuhudia injili kwa maneno na matendo yetu mema kila siku ili watu wakiyaona wamtukuze Mungu Baba yetu aliye mbinguni, wawe na hamu ya kuwa kama sisi ili siku moja tukaufurahie uzima wa milele pamoja mbinguni. Na kwa kuwa kwa ubatizo tulifanywa kuwa walinzi wa imani, manabii wa kuonya na kuwaongoza wakosefu ili watubu na kumrudia Mungu, tusipofanya hivyo tutakuwa na lawama mbele ya Mungu kama Mungu alivyomwambia nabii Ezekieli. Mungu atatudai kwa nini tumeacha roho ya mkosefu ipotee. Lakini kazi hii si rahisi, inadai sadaka. Katika kuifanya tutapata madhulumu na mapingamizi. Wakati mwingine wakosefu wanavichwa na shingo ngumu na masikio yao hayasikii. Sisi hatupaswi kukata tamaa, bali kuendelea kuwaonya mpaka kielewe.

Ili kuonyesha jinsi msamaha wa kindugu ulivyo muhimu, Yesu anasisitiza na kusema; “Yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni” (Mt. 18:18). Na akakaza kusema; “wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwa na Mungu kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu mimi nipo kati kati yao”. Na Kristo akiwa katikati yetu tutaweza kuona kila lililojema na kulifanya maana “Bwana asema: Mimi ndimi nuru ya ulimwengu; yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yn. 8:12). Na hili ndilo tumaini letu – kushirikishwa uzima wa kimungu kwa njia ya Yesu Kristo kama sala baada ya komunyo inavyohimisha kusema; “Ee Bwana, sisi waamini wako umetulisha neno lako na kututia uzima kwa chakula cha sakramenti hii takatifu. Utuwezeshe kuendelea kutenda mema kwa msaada wa neema nyingi za Mwanao mpenzi, hata tustahili kushirikishwa daima uzima wake”.

Tafakari ya Dominika ya 23 ya Mwaka A
07 September 2023, 09:31