Tafuta

“Ee Mungu Mwenyezi wa milele, unatujalia kwa wema wako mkuu mema mengi kupita yale tunayoomba na kutamani." “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, unatujalia kwa wema wako mkuu mema mengi kupita yale tunayoomba na kutamani."  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 27 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukuu wa Huruma na Upendo wa Mungu

Masomo ya dominika hii yanafafanua ukuu wa upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu aliotuumba kwa sura na mfano wake. Upendo wake kwetu sisi unajidhihirisha katika vitu alivyoviumba kwa ajili yetu na anaendelea kuvitunza ili vitufae kwa maisha ya hapa duniani. Mama Kanisa anamwomba, Mwenyezi Mungu aweze kushusha huruma, awasamehe waja wake dhambi na makosa yanayowaletea hofu moyoni na kuwaongea yale wasiothubu kuomba.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 27 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanafafanua ukuu wa upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu aliotuumba kwa sura na mfano wake. Upendo wake kwetu sisi unajidhihirisha katika vitu alivyoviumba kwa ajili yetu na anaendelea kuvitunza ili vitufae kwa maisha ya hapa duniani kama wimbo wa mwanzo unavyoimba kusema: “Ee Bwana, ulimwengu wote u katika uwezo wako, wala hakuna awezaye kukupinga ukipenda. Wewe umeumba yote, mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyomo chini ya mbingu; ndiwe Bwana wa yote (Esta 13:9, 10-11). Na wazo la huruma yake kuu linaashiriwa na sala ya mwanzo inayosema: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, unatujalia kwa wema wako mkuu mema mengi kupita yale tunayoomba na kutamani. Utushushie huruma yako, utusamehe makosa yanayotuletea hofu moyoni, utuongezee na hayo tusiyothubutu kuomba”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 5:1-7). Katika somo hili ambalo lina mfumo wa shairi la upendo, Nabii Isaya anamfananisha Mungu na mkulima wa mizabibu na taifa teule la Israeli kama shamba lake kama kiitikio cha wimbo wa katikati kinavyoimba; “Shamba la mizabibu la Bwana ndilo nyumba ya Israeli” (Isa. 5:7; Zab. 80: 8, 11-15, 18-19). Jinsi mkulima anavyoitunza mizabibu katika shamba lake ili iweze kumzalia zabibu njema, ndivyo Mungu kwa upendo wake mkuu alivyolitunza Taifa teule la Israeli – aliwatoa utumwani Misri kwa mkono wa nguvu zake na maajabu mengi, aliwaongoza jangwani na kuwalisha kwa chakula kutoka mbinguni, na kuwapa nchi aliyowaahidia babu zao na kufanya nao agano na kuwapa ulinzi na usalama. Lakini kwa bahati mbaya wao walikosa moyo wa shukrani, wakasahau maagizo yake na kuacha kuzifuata amri zake na maagizo yake, wakaishi maisha ya dhambi – dhuluma, ufisadi, rushwa, uasherati na ushirikina, wakachuma laana za uasi kwa kuabudu miungu ya uwongo – wakazaa zabibu mwitu.

Shamba la Mizabibu ni Taifa teule la Mungu
Shamba la Mizabibu ni Taifa teule la Mungu

Nabii Isaya anawasihi waache uasi wao, waongoke na kutubu dhambi zao, na kumrudia Mungu naye atawasamehe. Zaidi sana Nabii Isaya anawaonya kuwa majanga mabaya ya kutisha yatawatokea kama hawatatubu na kumrudia Mungu, wataadhibiwa kwa kuondolea ulinzi na usalama na baraka zake – ndio kumea mbigili na miiba, mawingu kufunga na hivyo kukosa baraka kama maji ya mvua juu yao. Haya ndiyo yaliyotokea, maana walikaza shingo na kuziba masaikio, wakakaidi maongozi na maagizo ya Mungu, hivyo waliadhibiwa kwa kuvamiwa na maadui, wakapelekwa uhamishoni na falme zao kusambaratishwa. Katika hali hii Mzaburi alipotafakari akasali sala ya kuomba msamaha kama mashairi ya wimbo wa katikati yanavyosema; “Ulileta mzabibu kutoka Misri, ukawafukuza mataifa ukaupanda. Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, na vichipukizi vyake hata kunako mto. Kwa nini sasa umezibomoa kuta zake, wakachuma zabibu zake wote wapitao njiani? Nguruwe mwitu wanauharibu, na hayawani wa kondeni wanautafuna. Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, utazame toka juu, uone, uujilie mzabibu huu, na mche ule ulioupanda, kwa mkono wako wa kuume. Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma; utuhuishe nasi tutaliitia jina lako. Ee Bwana, Mungu wa majeshi, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka” (Zab. 80:11-15, 18-19). Ndivyo inavyokuwa hata kwetu tunapokosa uaminifu kwa Mungu na kuabudu miungu mingine, tunazaa zabibu mwitu – dhambi – tunakosa neema na baraka za Mungu na hivyo matatizo, mahangaiko na mateso yanatusonga mfano wa nguruwe mwitu na hayawani wa kondeni, mbigili na miiba kuota katika njia na mapito yetu.

Ukuu wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Ukuu wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Flp. 4:6-9). Katika somo hili mtume Paulo anatuasa tutolee mahangaiko na taabu zetu kwa Mungu katika sala zetu, tuishi kwa amani, huku tukiyafikiria na kuyatenda mambo mema ili tuendelee kujenga uhusiano mwema na Mungu. Mtume Paulo anafafanua mambo ambayo mkristo anatakiwa ayaishi ili awe jirani na Mungu ikiwa ni kudumu katika kutenda matendo mema, kutenda haki na kudumu katika sala. Tukifanya hivyo hatutakuwa na wasiwasi wala mashaka bali tutadumu daima katika furaha kwani tutakuwa tumeunganika na Mungu wetu aliye mtakatifu kwa utakatifu wetu. Na tukiwa tumeunganika na Mungu, mambo yote ni murwa na shwari kabisa. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 21:33-43). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anachukua mfano wa Nabii Isaya kuhusu shamba la mizabibu. Lakini kinyume na nabii Isaya anayesisitiza mizabibu kuzaa zabibu mwitu, Yesu anatilia mkazo uovu wa watumishi katika shamba la mizabibu wanaokataa kumpa Bwana mwenye shamba mavuno ya mizabubi kwa wakati, na mbaya zaidi wanawatenda jeuri watumwa wa Bwana mwenye shamba na wengine kuwaua kabisa na alipomtuma mwanae ambaye ni mrithi naye hawakumheshimu kabisa, wakamuua. Ikumbukwe kuwa shamba la mizabibu linawakilisha ufalme wa Mungu, wakulima ni Taifa la Israeli na viongozi wao, watumwa ni manabii na mwana pekee mrithi wa shamba ni Yesu Kristo mwenyewe ambaye wao wanapanga kumuua. Mfano huu unatufunulia jinsi huruma na upendo wa Mungu visivyo na mipaka.

Shamba la Mizazbibu la Bwana ni Nyumba ya Israeli
Shamba la Mizazbibu la Bwana ni Nyumba ya Israeli

Maana Mungu hata baada ya kuona watumwa wake – manabii – wameua na watumishi waovu katika shamba lake la mizabibu, hatumi jeshi kuwaangamiza, bali anamtuma mwanae wa pekee tena bila jeshi wala ulinzi wowote. Kwa kutompokea Yesu, Taifa la Israeli, kama wakulima katika shamba la Mungu lilinyang’anya hadhi na heshima sio tu ya kuwa shamba la mizababu, Taifa teule, bali pia hadhi ya kuwa wakulima, uteule wa kuujenga ufalme wa Mungu na kupewa wakulima wapya ndio sisi wakristo wa leo. Kwa ubatizo kila mkristo amepewa hadhi ya kuwa taifa teule la Mungu, wakulima wapya wanaopaswa kutoa matunda bora ya ujenzi wa ufalme wa Mungu hapa duniani kwa wakati wake. Ili tusizae zabibu pori – dhambi – kwa matendo maovu – wizi, ujambazi, ufisadi, ulevi, uasherati, uzinzi, ukahaba, ushirikina, uongo na ulaghai wa kiimani yanasosababisha kuachwa na mwenye shamba tuharibiwe na nguruwe mwitu na hayawani. Basi tufungue mioyo yetu, tukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu ili tuweze kuzaa zabibu bora – matendo ya huruma na upendo kwa jirani na kusulibisha tamaa zetu za kimwili. Maana matunda ya Roho Mtakatifu ni wazi; upendo, furaha, amani, uvumilivu, uaminifu, fadhili, haki, kiasi, upole na uchaji wa Mungu. Yesu anatusisitiza kuwa waaminifu katika kazi tunazokabidhiwa. Uaminifu unapotoweka katika jambo lolote lile, madhara yake ni kuvunjika kwa uhusiano mwema uliopo. Tunapokosa uaminifu kwa mwenyezi Mungu uhusiano mwema uliopo kati yetu na Mungu huvunjika. Basi tumwombe Mungu atudumishe daima katika kutenda yaliyo mema, yanayompendeza na yanayotufanya daima tuitwe watoto wake wateule. Na hivyo sala ya kuombea ya dhabihu inayosema; “Ee Bwana, tunaomba uzipokee sadaka zilizowekwa kwa amri yako. Upende kutujaza neema za ukombozi wako kwa mafumbo haya matakatifu tunayoadhimisha kwa mujibu wa utumishi wetu”, itasikilizwa. Na hivyo sala baada ya komunyo inayosema; “Ee Mungu Mwenyezi, utujalie Sakramenti hizi tulizopokea zizidi kutuburudisha na kutusitawisha tupate kuwa na uzima wake yeye tuliyempokea” itaweza kutimizwa nasi kuupokea uzima wa milele.

Tafakari Dominika 27

 

06 October 2023, 14:23