Tafuta

Tafakari Dominika 28 ya Mwaka A wa Kanisa: Mwaliko wa kushiriki karamu ya maisha ya uzima wa milele: Sharti msingi ni vazi la arusi, yaani neema ya utakaso. Tafakari Dominika 28 ya Mwaka A wa Kanisa: Mwaliko wa kushiriki karamu ya maisha ya uzima wa milele: Sharti msingi ni vazi la arusi, yaani neema ya utakaso.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 28 Mwaka A wa Kanisa: Karamu ya Uzima wa Milele

Masomo ya dominika hii yanatilia mkazo kuwa mwaliko wa kushiriki karamu ya uzima wa milele mbinguni ni kwa wote. Ni mwaliko wa kuwa raia wa ufalme wa Mungu na kushiriki furaha za mbinguni. Kila binadamu amejaliwa akili, utashi na uhuru kamili. Hivyo kila mmoja yuko uhuru kukubali au kuukataa mwaliko huu. Kuishi maisha ya dhambi ni kuukataa mwaliko huu. Lakini Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 28 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatilia mkazo kuwa mwaliko wa kushiriki karamu ya uzima wa milele mbinguni ni kwa wote. Ni mwaliko wa kuwa raia wa ufalme wa Mungu na kushiriki furaha za mbinguni.  Kila binadamu amejaliwa akili, utashi na uhuru kamili. Hivyo kila mmoja yuko uhuru kukubali au kuukataa mwaliko huu. Kuishi maisha ya dhambi ni kuukataa mwaliko huu. Lakini Mungu ni mwenye huruma na upendo wake ni mkuu kwa kila binadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake. Hivyo kila anayeamua kuuupokea mwaliko huu kwa kutubu na kukiri makosa yake, Mungu atamsamehe na kutokumhesabia kabisa uovu wake kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Bwana, kama wewe ungehesabu maovu yetu, nani angesimama mbele zako? Lakini kwako kuna msamaha, Ee Mungu wa Israeli” (Zab. 130:3-4). Huu ndio ujumbe wa faraja kwetu wa kutubu na kuomba msamaha ili kujaliwa nguvu za kutenda mema kwa neema zake Mungu ndiyo maana katika sala ya mwanzo tunasali nakuomba neema ya Mungu itusaidie tukisema; “Ee Bwana, tunakuomba neema yako ituongoze daima na kutusindikiza, itutie siku zote moyo wa bidii wa kutenda mema.”

Vazi la arusi ni neema ya utakaso
Vazi la arusi ni neema ya utakaso

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 25:6-10). Somo hili linahusu karamu ambayo Mungu anatualika kuishiriki ili tupate wokovu na furaha ya milele. Katika karamu hii watu wa mataifa yote wamealikwa. Kuna vyakula na vinywaji vyenye uzima na uhai wa kimungu. Wanaokubali mwaliko wanakuwa na mang’amuzi mapya; hawana huzuni, hawataonja mauti, watamwona Mungu uso kwa uso, kwani kilema cha huzuni na hofu ya kifo vyote vitaondolewa. Kwa kuwa watafanyika wana wa Mungu, na kazi yao itakuwa ni moja tu, kumsifu na kumwabudu Mungu; wataimba oneni huyu ndiye Mungu wetu tunayemtumainia ndiye wokovu wetu. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa katikati alipotafakari juu ya wema huu wa Mungu aliimba kwa furaha akisema; “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu, huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya: Kwa maana Wewe Bwana upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele” (Zab. 23). Kinyume chake kukataa mwaliko huu ni kujipalia makaa ya moto kichwani ndiyo kujiingiza katika hukumu ya mauti milele yote.

Watu wote wanaalikwa kwenye karamu ya uzima wa milele
Watu wote wanaalikwa kwenye karamu ya uzima wa milele

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Flp. 4:12-14, 19-20). Katika somo hili Mtume Paulo anatuasa wakristo kumshukuru na kumtukuza Mungu daima katika hali zote, katika taabu, mateso na furaha. Tutaweza kufanya hivyo sababu katikati yetu yupo atutiaye nguvu, Yesu Kristo mkuu wa karamu ya uzima wa milele anayetufundisha kujua kudhilika na kufanikiwa, kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa, kuwa yote katika hali yoyote. Yeye Kristo ni mfano hai na halisi maana “alikuwa yu namna ya Mungu lakini aliachilia yote akawa mtii hata mauti naam mauti ya msalaba” (Flp. 2:6ff). Na kwa kuwa Yeye aliye mfano wetu hakuishia katika mauti bali katika uzima wa milele. Ndivyo itakavyokuwa na kwetu sisi tunaomwamini. Hata waswahili wanasema; “Baada ya dhiki ni faraja na Mchumia juani hulia kivulini”. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 22:1-14). Katika sehemu hii ya Injili Yesu kama Nabii Isaya katika somo la kwanza anatupa mfano wa karamu unaotufundisha kuwa katika karamu ya uzima wa milele watu wote wanaalikwa bila ubaguzi na kadi ya mwaliko ni moja tu, ubatizo ulio mlango wa sakramenti zingine zote na kuziishi ahadi tulizoweka mbele za Mungu. Katika mfano huu wa karamu Yesu anasema kuwa mfalme aliwatuma watumwa wake wawaite walioalikwa arusini maana maandalizi yote yalikuwa tayari, nao wakakataa kuja. Akatuma tena watumishi wengine kuwaita walioalikwa lakini hawakujali kila mmoja akaendelea na shughuli zake na waliosalia wakawakamata wale watumwa wakawapiga na kuwaua. Basi yule mfalme akapeleka jeshi akawaangamiza wale wauaji, akawaambia watumwa wake waende hata njia panda na wote watakaowaona wawaite arusini. Wakafanya hivyo arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia mfalme ili kutazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiye na vazi la arusi, naye alipomuuliza aliingiaje bila vazi la harusi, hakuwa na jibu, alikaa kimya. Basi mfalme akawaamuru watumishi wake wamtoe na kumtupa nje gizani.

Mwaliko wa kushiriki karamu ya uzima wa milele
Mwaliko wa kushiriki karamu ya uzima wa milele

Maana ya mfano huu ni hii: Mfalme aliyemfanyia mwanae arusi ni Mungu. Huyu mwana ni Yesu Kristo. Bibi arusi ni taifa teule na Israeli, nyakati zetu ni Kanisa, watumishi ndio manabii, waalikwa ni watu wa mataifa yote, kwanza Taifa teule la Israeli walioalikwa kwanza na walioalikwa mwishoni ni watu wote waliohubiriwa Injili au Habari Njema wakaamini na kubatizwa. Yule aliyeingia bila vazi la arusi anawakilisha wadhambi au wakosefu. Kumbe tunaona kuwa kuna makundi matatu ya watu; kwanza wapo wale waliokataa mwaliko wakaendelea na shughuli zao, pili waliokubali mwaliko na kuingia katika arusi kadiri ya masharti wakachukua vazi la arusi na tatu aliyeitikia mwaliko akawa tayari kuingia katika arusi lakini hakufuata masharti hakuchukua vazi la arusi. Mungu ametuandalia na kutualika twende kwenye karamu ya ufalme wake. Kuwa mkristo, ni ishara ya kukubali huu mwaliko. Lakini ili kuingia katika sherehe hii tunahitaji vazi rasmi. Tulipobatizwa tulipewa vazi kama wale waliokuja arusini walivyopewa vazi la arusi. Tulipewa kitambaa cheupe, tukaambiwa kitambaa hiki ndilo vazi la arusi na tukifikishe katika ufalme wa Mungu kama kilivyo bila doa lolote. Vazi hili ni neema ya utakaso. Ingawa tumeitikia mwaliko na vazi tunalo kwa dhambi zetu tunawezalichafua na hivyo kutotambulika kama vazi la arusi. Ni wajibu wetu wa kulifua vazi hili mara kwa mara kwa toba katika sakramenti ya upatanisho ili Bwana arusi atakapokuja atukute tumevaa vazi hili likiwa safi tupate kustahili kuingia katika karamu ya uzima wa milele mbinguni. Tukifanya hivyo sala ya kuombea dhabihu inayosema; “Ee Bwana, pokea sala za waamini pamoja na dhabihu tunayokutolea, ili kwa ibada hii takatifu tupate kuufikia utukufu wa mbinguni”, itakuwa na maana. Nayo antifona ya komunyo inayosema; “Bwana atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yoh. 3:2), na sala baada ya komunyo inayosema; “Ee Bwana mtukufu, sisi unaotulisha Sakramenti ya Mwili na Damu takatifu tunakusihi utushirikishe pia umungu wako”, vitadhihirika wazi wazi kwetu huko mbinguni.

Tafakari Dominika 28
10 October 2023, 14:29