Tafuta

Viongozi wa kiraia wanapaswa kuwa vyombo vya kutimiza mpango wa Mungu na si vinginevyo. Kielelezo ni mfalme Koreshi! Viongozi wa kiraia wanapaswa kuwa vyombo vya kutimiza mpango wa Mungu na si vinginevyo. Kielelezo ni mfalme Koreshi!  (Vatican Media)

Tafakari ya Dominika 29 Mwaka A wa Kanisa; Mpeni Mungu Yaliyo ya Mungu

Wajibu kwa mamlaka ya kiraia unapaswa kufungamanishwa na wajibu wetu kwa Mungu ili kupata ukamilifu wake. Dini isiwe kisingizio cha kutotimiza wajibu wetu kwa serikali; na wala majukumu ya kiraia yasiwe kisingizio cha kutokutimiza wajibu wetu kwa Mungu. Viongozi wa kiraia wanapaswa kuwa vyombo vya kutimiza mpango wa Mungu na si vinginevyo. Kielelezo ni mfalme Koreshi! Mwenyezi Mungu apewe haki yake na mamlaka za kiraia halali ziheshimiwe na raia!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Jimbo Kuu Katoliki Mwanza

Wajibu wetu kwa mamlaka za kiraia ni wajibu msingi kwa maendeleo ya mwanadamu. Hata hivyo, wajibu kwa mamlaka ya kiraia unapaswa kufungamanishwa na wajibu wetu kwa Mungu ili kupata ukamilifu wake. Dini isiwe kisingizio cha kutotimiza wajibu wetu kwa serikali; na wala majukumu ya kiraia yasiwe kisingizio cha kutokutimiza wajibu wetu kwa Mungu. Viongozi wa kiraia wanapaswa kuwa vyombo vya kutimiza mpango wa Mungu na si vinginevyo. Kielelezo ni mfalme Koreshi! Somo la Kwanza (Isa. 45:1,4-6) linatuletea ujumbe kuwa sisi sote ni vyombo vya Mungu katika kutimiza mpango wake, bila kujali makandokando yetu. Koreshi, mfalme wa Uajemi anafanikiwa kuivamia nchi ya Babel na kumwondoa mtawala wa Babeli. Wakati Koreshi anaivamia Babeli wana wa Waisraeli walikuwa uhamishoni katika nchi hiyo. Licha ya kuwa mpagani, Koreshi baada ya kuitawala Babeli anawaruhusu Waisraeli waliokuwa uhamishoni Babel kurejea Yerusalemu na kulijenga upya hekalu lao. Koreshi anarejesha matumaini ya Waisraeli. Lakini aliyewezesha hayo yote kufanyika ni Mungu Mwenyewe. Mfalme asiye Myahudi anatumika kutimiza mpango wa Mungu kwa taifa lake teule la Israeli. Koreshi alikuwa hajamjua Mungu (Isa. 45:4). Hata sisi tu vyombo vya Mungu katika kutimiza mipango yake. Licha ya kutomfahamu Mungu vizuri, licha ya kuwa wapagani katika mwenendo wetu, na licha ya madhaifu yetu ya kibinadamu bado tuna nafasi katika kutimiza mpango wa Mungu. Kama Koreshi alivyotumika kuwaondoa Waisraeli uhamishoni Babeli na kuwarejesha Yerusalemu, ndivyo nasi tunapaswa kutumika kuwatoa watu katika ulimwengu wa dhambi (ambao ni sawa na uhamishoni Babeli) na kuwaleta kwa Mungu (Yerusalem mpya). Tutaweza kutimiza hayo kwa kukemea uovu, kwa kuhangaikia wokovu wa wadhambi, kwa kuonesha mwenendo bora wa maisha ya fadhila na kwa kumhubiri Mungu wa kweli.

Tafakari Dominika 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Mungu na Kaisari
Tafakari Dominika 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Mungu na Kaisari

Somo la Pili (1 Thes. 1:1-5) linatukumbusha juu ya umuhimu wa kumshukuru Mungu na umuhimu wa kuwaombea watu wengine. Paulo na wenzake wanamshukuru Mungu kutokana na neema nyingi alizowatendea Wakristo wa Thessalonike hasa neema za imani, mapendo na matumaini. Lakini pia wanazidi kuwaombea katika sala zao. Baadhi yetu hukumbuka kumshukuru Mungu kwa mema anayotutendea sisi wenyewe, lakini kwa hakika wengi hatukumbuki kumshukuru Mungu kwa mema mengi anayowatendea watu wengine. Mara nyingi tunajiombea wenyewe tu. Ni mara ngapi katika sala zetu za kila siku tunakumbuka kuwaombea wengine- wazazi wetu, watoto wetu, viongozi wetu wa kiroho na kiserikali, adui zetu, wagonjwa, yatima, wajane na wagane, wafungwa, wakimbii, ndugu, jamaa na marafiki? Sala zetu nyingi zimejaa ubinafsi na umimi. Paulo pia anatufundisha jambo zito: maneno (mahubiri) yake pekee hayajawafanya Wakristo wa Thessalonike wawe na imani, mapendo na matumaini, bali kuna nguvu ya Roho Mtakatifu: “injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali katika Roho Mtakatifu”. Hivyo havijunii mahubiri yake. Mara nyingi tunapofanikiwa katika shughuli zetu tunafikiri kuwa ni jitihada zetu binafsi- nguvu zetu, umahiri wetu wa kuhubiri, akili zetu, elimu zetu, pesa zetu, uzuri wetu au haiba zetu. Tunasahau kuwa hayo yote tumewezeshwa na Roho Mtakatifu.

Mpeni Mungu yaliyo ya Mungu
Mpeni Mungu yaliyo ya Mungu

Katika somo la Injili (Mt. 22:15-21) Yesu anatufundisha kuwa tunapaswa kuheshimu na kutimiza wajibu wetu kwa mamlaka za kiserikali/kiraia bila kusahau wajibu mkubwa zaidi tunaopaswa kutimiza kwa Mungu. Awali ya yote kuna mambo matatu ya kujifunza kutoka Injili ya leo. Kwanza, Mafarisayo hawaendi moja kwa moja kumuuliza Yesu swali juu ya ulipaji kodi kwa Kaisari, bali wanawatumia wanafunzi wao. Mafarisayo hawataki waonekane wabaya; hawataki waonekane kuwa wanahusika kwenye mpango huu wa kutafuta njia za kumwangamiza Yesu. Wanawatumia watu wengine kutimiza nia zao mbaya. Hata katika ulimwengu wa sasa wapo watu wanaowatumia watu wengine kutimiza nia zao mbaya ili wao wenyewe waendelee kuonekana wema/wasafi. Pili, kwa kawaida Mafarisayo na Maherodi walikuwa hawapatani kabisa. Mafarisayo walikuwa wana hisia kali za chuki dhidi ya utawala wa Kirumi na hivyo walikuwa wanapinga sera nyingi za Warumi. Marehodi walikuwa ni washirika wa Herode Antipas na ukoo wake wa kifalme. Licha ya kuwa Wayahudi, Maherodi walikuwa na uhusiano mzuri na Warumi kwa kuwa walikuwa wanapata mafaa mengi kutoka kwa Warumi kama vile vyeo, pesa, usalama na upendeleo mwingine. Hivyo Maherodi waliwaunga mkono Warumi pamoja na sera zao. Kitendo cha Marehodi kuwaunga mkono Warumi kiliwachukiza sana Mafarisayo na hivyo kujenga uhasama kati yao. Katika Injili ya leo ni ajabu sana kuona mahasimu wawili (Mafarisayo na Maherodi) wanaungana kumtega Yesu ili wapate kumwangamiza. Hapa tunajifunza kuwa hata watu ambao ni maadui wanaweza kuwa marafiki kwa muda ili kutimiza nia zao mbaya dhidi ya mtu mwingine ambaye ni adui yao. Tuwe makini. Tatu, Mafarisayo na Maherodi wanaanza kwa kumsifia Yesu kabla ya kurusha kombora lao: “Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.”

Kodi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Kodi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Mafarisayo na Maherodi wanamsifia kwa unafiki maana kama kweli wangekuwa hawana hila katika mioyo yao wangemwamini kutokana na hayo mazuri wanayomsifia. Katika maisha wapo watu ambao daima hukusifia kwa unafiki lakini lengo lao ni kukulainisha ili ukishabweteka kwa wingi wa sifa watumie mwanya huo kukuangamiza. Hata sisi Mapadre husifiwa sana na waamini wetu na hata wasio waamini: wewe ni mhubiri mzuri, wewe ni padre mwema, una roho nzuri n.k. Lakini hao hao wanaotusifia ndiyo wa kwanza kutuchafua kwenye mitandao, kutugombanisha na waamini wengine, kuanzisha migogoro Kanisani na mengineyo. Tabia hii ya kusifia wakuu kwa unafiki na kisha kuwaponda ipo miongoni mwa waajiriwa na wafanyakazi wa kawaida Mafarisayo (kupitia wanafunzi wao) na Maherodi wanamwuliza Yesu swali la mtego ambalo ni la kidini na pia ni la kisiasa ili wapate sababu ya kumshitaki: Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? Swali hili ni la kidini kwa sababu Wayahudi waliamini kuwa mtawala wao pekee ni Mungu, na ndiye anapaswa kulipwa kodi. Hivyo kulipa kodi kwa mtawala mwingine ni kuabudu mungu mwingine. Na pia pesa ya kulipia kodi ilikuwa na sanamu ya mtawala wa Kirumi na hivyo kwa Wayahudi ilikuwa ni kuvunja amri ya Mungu isemayo “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia” (Kut. 20:4). Pia lilikuwa ni swali la kisiasa maana liligusa moja kwa moja mamlaka ya kisiasa ya Warumi. Kipindi hiki Waisraeli walikuwa wanatawaliwa na Warumi kisiasa na kiuchumi na hivyo Waisraeli wengi walikuwa na chuki ya waziwazi dhidi ya Warumi. Hivyo kama Yesu angesema “Ndiyo, ni halali” basi angeonekana msaliti kwa Waisraeli wenzake kwa kuunga mkono utawala wa Warumi na ya kwamba anaridhika na uonevu unaoambatana na utozaji kodi unaofanywa na Warumi.

Vipaji vitumike kwa sifa na utukufu wa Mungu
Vipaji vitumike kwa sifa na utukufu wa Mungu

Wayahudi waliamini kuwa Mungu peke yake ndiye anapaswa kupewa kodi, na si mtu mwingine. Hivyo, kama Yesu angesema moja kwa moja kuwa ni halali kulipa kodi kwa Kaisari ingeonekana ana utii kwa mungu mwingine (yaani Kaisari) na hivyo amevunja amri ya Mungu inayokataza kuabudu miungu mingine. Kama Yesu angesema “Hapana, siyo halali” angeonekana anapinga utawala wa Warumi na anataka kusababisha mapinduzi na ukiukwaji wa sheria na hivyo Warumi wangemshughulikia barabara. Kwa kujua nia yao ovu Yesu anajibu kwa maarifa makubwa akiwaomba wamuoneshe dinari iliyotumika kulipa kodi. Dinari hiyo ilikuwa na picha/sanamu ya Kaisari (mtawala wa Kirumi) aitwaye Agusto Tiberius pamoja na maneno “Agusto Tiberius, mwana wa mungu Agusto”. Wote wanakiri kuwa dinari hiyo ni mali ya Kaisari kwa kuwa ina picha na anuani ya Kaisari. Kisha Yesu anasema “mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu”. Kaisari anawakilisha utawala wa kiserikali/kiraia na Mungu anawakilisha utawala wa kiroho. Kwa kauli hiyo Yesu anatufundisha kuwa tuna wajibu kwa Mungu, kwa Kanisa na jamii kwa sababu tu raia pacha wa ufalme wa Mungu na wa hapa duniani. Yesu analenga kufundisha kuwa sisi sote tunapaswa kutimiza wajibu wetu kwa serikali bila kusahau wajibu wetu mkubwa zaidi kwa Mungu ambaye hata tawala za kiserikali zimetoka kwake. Dini isiwe kisingizio cha kutotimiza wajibu wetu kwa serikali; na wala majukumu ya kiserikali/kisiasa yasiwe kisingizio cha kutokutimiza wajibu wetu kwa Mungu. Tunapaswa kuheshimu mamlaka halali za kiraia kwa kuzitii, kushika sheria njema zinazotungwa na kutimiza wajibu wetu za kiraia ikiwemo kulipa kodi kwa ustawi wa taifa. Hata hivyo tukumbuke kuwa “Raia analazimika katika dhamiri yake kutofuata sheria za serikali zinapokuwa kinyume cha mpango wa maadili, haki za msingi za binadamu au mafundisho ya Injili” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba. 2242). Hata hivyo, wajibu mkubwa wa waamini ni kwa Mungu: “mpeni Mungu yaliyo ya Mungu”. Dinari ilikuwa na sura na anuani ya Kaisari, na hivyo kuonesha kuwa ni mali binafsi ya Kaisari. Nasi binadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tu mali binafsi ya Mungu. Yesu anasema “mlipeni Mungu yaliyo ya Mungu”. Ya Mungu ni yapi? Maisha, miili, karama na vipawa tulivyonavyo, nguvu, akili, uzuri na mali zote tulizonazo ni mali ya Mungu. Tunapaswa kuvitumia kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Dominika njema.

19 October 2023, 11:36