Wazo Kuu: Uadilifu na uwajibikaji ni tunu za kimisionari Wazo Kuu: Uadilifu na uwajibikaji ni tunu za kimisionari  (REUTERS)

Tafakari Dominika 29 ya Mwaka A wa Kanisa: Uadilifu na Uwajibikaji: Tunu Msingi za Kimisionari

Kwa ubatizo sisi sote tunafanywa kuwa wana wa Mungu. Pia tunakuwa vyombo vyake vya kutangaza habari njema ya ufalme wa Mungu kwa watu. Kwa ubatizo tunafanywa kuwa makuhani. Kila mmoja kwa ubatizo anaitwa kwa jina lake kuwa chombo kiteule katika taifa lake Mungu, kutangaza Habari Njema na kuwafungulia wale waliofungwa katika giza la utumwa wa dhambi kwa maneno na matendo yake. Magumu ni mengi lakini tumaini letu ni Kristo siku zote.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Maingilio: Kwa ubatizo sisi sote tunafanywa kuwa wana wa Mungu. Pia tunakuwa vyombo vyake vya kutangaza habari njema ya ufalme wa Mungu kwa watu. Kwa ubatizo tunafanywa kuwa makuhani. Kila mmoja kwa ubatizo anaitwa kwa jina lake kuwa chombo kiteule katika taifa lake Mungu, kutangaza Habari Njema na kuwafungulia wale waliofungwa katika giza la utumwa wa dhambi kwa maneno na matendo yake. Magumu ni mengi lakini tumaini letu ni Kristo siku zote. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 22 Oktoba 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Mioyo inayowaka moto, na miguu inayotembea. (Lk 24:13-35). Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anabainisha jinsi ambavyo katika kazi ya kimisionari Neno la Mungu huangaza na kubadili mioyo ya waamini. Kristo Mfufuka bado anabaki na kutembea na wafuasi wake ili wasikate tamaa. Umuhimu wa kulifahamu Neno la Mungu, Sakramenti ya Sadaka ya Yesu Msalabani, ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wawe tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kwanza kabisa kwa kujikita katika wongofu wa kimisionari tayari kushuhudia upendo wa Kristo kwa waja wake. Waamini wanaalikwa kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa uenezaji wa imani tayari kujikita katika safari ya kisinodi inayonogeshwa na maneno makuu matatu: umoja, ushiriki na utume. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuianza safari hii kwa mioyo inayowaka moto ili kuifanya mioyo mingine iwake kwa Neno la Mungu, ili kuifungua mioyo ya wengine kwa Kristo katika Ekaristi sanjari na kukoleza njia ya amani na wokovu ambao Mwenyezi Mungu, katika Kristo Yesu, amewakirimia binadamu wote.

Ibada ya Misa Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ibada ya Misa Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Ufafanuzi: Uadilifu ni hali ya kuwa na tabia au namna zenye kufaa  na kukubalika kadiri ya mfumo wa jamii husika. Hali hiyo humwambata mtu. Naye huyo anayeambatwa na uadilifu huitwa mwadilifu. Mwadilifu ni mtu mwenye kuwa na mwenendo mwema wenye kukubalika na watu walio wema. Mtu mwadilifu ni yule mwenye kuwa na maadili mema yenye kukubalika na watu wanaopendwa na Mungu. Na uwajibikaji ni hali ya kuishi na kuukubali ukweli na uhalisia wa jambo fulani iwe ni hali fulani au tendo fulani katika kuhakikisha haki na amani vinapatikana vikitanguliwa na uadilifu na uwajibikaji wa kila mtu katika jamii husika. Katika somo la kwanza, tunaletewa simulizi la kuitwa na kutumwa kwa Koreshi. Koreshi alikuwa mpagani, mwenye imani ya kipagani, mtu asiye mwisraeli, lakini Mungu anamwona anafaa kwa imani yake na matendo yake anamwita na kumpa wajibu wa kwenda kuwakomboa waisraeli walioutumwani na pia afanyapo kazi hiyo anapewa wajibu ulioambatanishwa wa kumtangaza Mungu wa kweli kwa hayo mataifa yasiyomjua Mungu bado, ‘Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi hapana Mungu,… ili wapate kujua toka maawio ya jua, na toka maghariibi, ya kuwa hapana mwingine zaidi ya mimi’Isa 45:5-6. Mungu pia anamwahidia Koreshi (chombo chake cha kuwakomboa waliofungwa kati ya wafalme) kuwa pamoja naye katika kazi hiyo.

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu
Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu

Katika Injili, kwa ufupi mawazo yanayojitokeza katika somo la kwanza la utumishi wa Neno la Mungu na katika somo la pili mafanikio katika utumishi wa Neno la Mungu yanaonekana vizuri kabisa kwa Yesu Kristo mwenyewe. Yeye aliyekuja kutangaza ufalme wa Mungu hapa duniani, katika kazi hiyo anaonekana kuchukiwa na kupingwa pingwa na wale wote ambao hawakuuelewa utume wake wala hawakuupenda ujumbe wake hata kidogo kwa kuwa walijiona upo kinyume kabisa na matendo yao Mafarisayo walimtafuta Yesu kwa kila namna sababu alifanya mambo wasiyoyapenda na wasiyoyaweza na hivi kujikuta wakipoteza umaarufu wao mbele ya jamii. Mara nyingi walimweka katika njia panda na leo wanamtega kwa swali baya kabisa. Wanaanza na maneno mazuri ya kumsifu kuwa ni mtu mzuri, mtu wa kweli, hajali cheo cha mtu na hatazami sura za watu, halafu wanamtega (Mt 22:15-21). Mara si haba tumefanana na hawa wanaomtega Yesu. Jibu hili la Yesu linaweza kutafsiriwa vibaya na wanasiasa kuwa viongozi wa dini wasiingilie mambo ya siasa, wasiambiwe hata kama hali si hali, hata kama hakuna ukweli, hakuna maadili, kuna kashfa, rushwa, uonevu, ukosefu wa haki na uhuru iwe ni kimya sababu kuyasemea hayo ni kuchanganya dini na siasa, tumpe Kaisari vilivyo vya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu. Viongozi wa dini nao watasema viongozi wa serikali wasiingilie mambo ya dini, hasa mifumo na taratibu zake... Ukweli ni kuwa mwanadamu sio siasa pekee (mwili) na sio dini peke yake (roho) ila ni vyote, mwili na roho… vikitengana ni mtu amefariki. Hali ya kisiasa na aina ya siasa ya nchi huathiri namna ya kuabudu na shughuli za uinjilishaji na wakati huohuo shughuli za kidini na uinjilishaji huathiri utendaji na maisha ya wanasiasa… ngumu kutenganisha! Viongozi wa dini kama raia wa nchi wanaowaongoza watu kumwendea Mungu wana wajibu wa kuwafundisha waamini juu ya siasa na hata kukemea ikibidi hali inapokuwa kinyume na utu na maadili ya kimungu. Tumeendelea kusikia katika vyombo ya habari vita ikiendela baina ya mataifa yaliyotofautiana kimitazamo na itikadi kusababisha maelfu ya watu kukosa makazi na watu wengi kuuwawa, hii ni ishara kuwa binadamu sasa hana hofu ya Mungu ndani yake na upendo kwa jirani umetoweka.

Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni kwa mwaka 2023
Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni kwa mwaka 2023

Leo Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni. Tunapomshukuru Mungu kwa ajili ya shughuli za kimisionari za Mama Kanisa kila mmoja wetu aonje yeye ni mmisionari. Kwa ubatizo wetu Mungu anatuita kwa majina yetu. Tukiongoza na ujumbe wa siku hii ya umisionari “mioyo inayowaka na miguu inayotembea” pale wanafunzi wa Emau walipomtambua Kristo na wakaanza uwajibikaji na kupeleka Habari Njema za ufufuko mintarafu amani kwa watu wengine, tukiwa Mama Kanisa Mtakatifu akiwa katika Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” tujitahidi kuwasindikiza Mababa wa Sinodi kwa sala. Tunapoadhimisha dominika hii ya misioni ni ishara wazi kabisa umisionari ni uti wa mgongo wa uinjilishaji wakati wote hivyo waamini wote wenye mapenzi mema tunaalikwa na mama kanisa kuwa na mioyo inayowaka mapendo kwa Mungu na jirani na kutembea na kupeleka na kuwa wajumbe na mawakala wa habari njema kwa kila kiumbe Katika somo la pili, tunapewa furaha ya Mtume Paulo kwa Kanisa la Thesalonike akifurahia kazi ya uinjilishaji ilivyofanikiwa kwa nguvu na uwezo wa Roho Mtakatifu. Paulo anatuonesha kuwa kazi yake ya kutangaza Habari Njema inapata mafanikio kwakuwa imefanyika katika maongoza ya Roho Mtakatifu. Hivyo basi Paulo anatukumbusha kusali na kumshukuru Mungu daima kwa neema mbalimbali anazotujaliwa katika utume wetu na wa kanisa lote na pia anatuonesha kwamba kazi yeyote ya uinjilishaji wa habari njema inayofanyika kwa nguvu na uwezo wa mwenyezi Mungu huzaa matunda. Mungu ndiye anayetufanikishia utume wetu. Nasi tunaalikwa pia kama wabatizwa kuwa na furaha na amani pale tunapotimiza wajibu wetu wa kimisionari, kwa kushirki kila mmoja, kushirikiana na kanisa popote pale alipo na kufanya umisionari. Tukiongozwa na mioyo inayowaka moto na miguu inayotembea hasa kwa kuchangia kazi hii inayotuhusu sote wabatizwa na wafuasi wa kristo. Na kwa hakika hayo ndio mapato ya maisha ya fadhila za kiutu tunazotafakalishwa leo na mama kanisa yaani. Uadifu na uwajibikaji ni tuzu za kimisionari.

Liturujia Dominika 29
20 October 2023, 16:01