Tafakari Dominika ya 30 ya Mwaka A wa Kanisa: Upendo kwa Mungu na Jirani
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 30 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tunapokaribia mwisho wa mwaka wa kiliturujia wa Kanisa, Mama Kanisa anatukumbusha namna tunavyopaswa kuishi hapa duniani ili tuweze kuwa warithi wa uzima wa milele. Na kumpenda jirani ndiyo namna pekee ya kupata furaha ya moyo hapa duniani na mbinguni maana ndiyo namna ya kumtafuta Mungu aliye asili ya furaha kama wimbo wa mwanzo unavyoimba kusema; “Ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake sikuzote” (Zab. 105: 3-4). Ndiyo maana katika sala ya mwanzo tunasali na kuomba tukisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuzidishie imani, matumaini na mapendo. Utuwezeshe kupenda unayoamuru, tustahili kupata na hayo unayoahidi.” Somo la kwanza ni la kitabu cha kutoka (Kut. 22:21-27). Somo hili ni sehemu ya mkusanyo wa sheria zinazoeleza namna ya kuishi maisha yampendezayo Mungu. Na baadhi ya maongozi ni haya: kutokuwaonea wageni wala kuwatendea jeuri, kutowatesa wajane wala yatima. Maana matendo haya mabaya dhidi yao ni dhambi ambazo kilio chake kinafika moja kwa moja kwa Mungu kama anasema mwenyewe; “Ukiwatesa watu hao nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto juu yenu”. Zaidi sana tunaaswa kuwa ukimkopesha mtu aliye maskini, usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala usimwandikie faida. Ikiwa wewe kwa njia yoyote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima umrudishie kabla ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake ya kulalia. Mungu anaahidi kuwa itakuwa hapo atakapomlilia, atasikia kilio chake kwa kuwa Yeye ni mwenye rehema.
Ijapokuwa sheria ya Musa ilikataza kuchukua riba katika mali waliyowakopesha ndugu zao, lakini bado wapo waliowatoza riba ndugu zao. Watu maskini walinyonywa haki zao, wajane walinyang’anywa urithi wao, na yatima waliuzwa na kuwa watumwa kama Nehemia anavyoelezea uhalisia huu akisema; “Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao juu ya ndugu zao Wayahudi. Maana walikuwako watu waliosema: Sisi na wana zetu na binti zetu, tu wengi, na tupate ngano, tukale tukaishi. Tena walikuwako wengine waliosema: Tumeweka rehani mashamba yetu na mizazibu yetu na nyumba zetu tupate ngano kwa sababu ya njaa. Tena walikuwako wengine waliosema, tumekopa fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa kuweka rehani mashamba yetu na mizabibu yetu. Lakini miili yetu ni kama miili ya ndugu zetu, na watoto wetu kama watoto wao; kumbe tunawatia utumwani wana wetu na binti zetu kwa utumishi na baadhi ya wenzetu wamekwisha kutiwa utumwani, wala hatuwezi kujiepusha na hayo, maana watu wengi wana mashamba yetu na mizabibu yetu” (Neh 5:1-5). Nasi tujiulize mioyoni mwetu, uovu huu katika jamii zetu, jumuiya zetu na familia zetu haupo? Je sisi nasi hatushiriki katika uovu huu? Basi tunaonywa tusishiriki katika uovu huu, ili hasira ya Mungu isijewaka juu yetu watakapomlilia Mungu akawasikiliza kama Mzaburi anavyoimba katika wimbo wa katikati; “Wewe Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana; Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu. Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, hivyo nitaokoka na adui zangu. Bwana ndiye aliye hai, na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu. Ampa mfalme wokovu mkuu. Amfanyia fadhili Masihi wake” (Zab. 18:1-3, 46, 50).
Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (1Thes. 1:5-10). Katika somo hili mtume Paulo anaeleza jinsi Wathesalonike walivyoipokea Injili kwa furaha licha ya upinzani mwingi hata wakapata sifa sehemu zote za Ugiriki. Paulo anasema kuwa wao wamekuwa kielelezo kwa watu wote waaminio. Maana kutoka kwao neno la Mungu limevuma kila mahali ambapo imani yao kwa Mungu imefika na kuenea. Paulo anashuhudia kuwa Wathesalonike walipomwongokea Mungu, waliziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli wakiingojea hukumu ya mwisho. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwa kila mbatizwa, kumwongokea Mungu kwa moyo wote na kuachana na sanamu za miungu mingine na kusubiri kwa matumaini hukumu ya mwisho kwa furaha. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 22:34-40). Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi Mafarisayo walivyofanya shauri na kupanga kumuuliza Yesu swali la kumjaribu kuhusu amri iliyo kuu katika torati ili wapate mashitaka juu yake. Ni wazi kuwa Mungu kupitia Musa aliwapa Waisraeli Amri 10. Lakini hadi ujio wa Kristo Viongozi wa Dini walizinyumbulisha amri hizo hadi kufikia 613, ambapo amri 248 zilihimiza wanayopaswa kufanya na amri 365 – idadi ya siku katika mwaka – zilitoa makatazo ya mambo ambayo hawapaswi kuyafanya. Sheria hizi zilikuwa kama mzigo mzito kwa watu wa kawaida kuzishika na kuziishi na hivyo maisha yao yalikuwa magumu sana. Ndiyo maana Yesu alisema hivi juu yao; “wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, wasitake wenyewe kuigusa hata kwa ncha ya kidole chao” (Mt. 23:4).
Yesu anatoa jibu kwa swali lao kuwa kumpenda Mungu, na jirani ni msingi wa amri zote. Yesu anaziweka amri zote 613 katika amri moja ya kumpenda Mungu na jirani. Sehemu ya kwanza ya jibu la Yesu ni sehemu ya sala ya Wayahudi ambayo ilikuwa kama kanuni ya imani kwao iliyojulikana kama “shema” – “Silikiliza ee Israeli”. Watoto walifundishwa sala hii na kuisali mara mbili kwa siku wakiibeba kifuani pao kama scapulari na ilionekana kuwa kinga kwa walioivaa. Yesu ananukuu mstari wa kwanza wa sala hii unaosema; “Sikiliza ee Israeli; Bwana Mungu wako ni Mungu mmoja; Nawe Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote”. Kisha akaongeza sehemu muhimu katika amri hiyo; “mpende jirani yako kama nafsi yako” (Wal 19:18). Akamalizia; “Katika amri hizi mbili hutegemea Torati yote na Manabii”. Kwa kuwa Wayahudi walifikiri jirani yao ni Myahudi swali lililofuata lilikuwa na jirani yangu ni nani? Ndipo hapo Kristo alipofundisha kuwa jirani yako ni mtu yeyote yule mhitaji kwa kutoa mfano wa msamaria mwema. Mwishoni mwa maisha yake hapa duniani, Yesu aliwaalika wafuasi wake kuweka maisha yao katika kiini cha upendo kwa Mungu na jirani. Tena akasema hii ni amri mpya tena akaiweka kwa maneno machache kabisa, “pendaneni kama nilivyowapenda ninyi” (Yn 13:34), akasisitiza; “mkipendana watu watawatambua kuwa mu-wanafunzi wangu”. Kumbe upendo ni kitambulisho cha ufuasi wetu kwa Kristo. Mtume Paulo anainukuu amri hii katika barua yake kwa warumi akisema; “ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika neno hili; mpende jirani yako kama nafsi yako” (Rum 13:9).
Kumbe, tukumbuke kuwa dini iliyo safi mbele ya Mungu Baba ni hii; “kuwatazama yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda na dunia pasipo mawaa” (Yak 1:27). Haya ni makundi dhaifu yasiyo na usalama. Kilio chao chasikika mbele ya Mungu maana hawana mtetezi ila Mungu. Tukiwatesa katika neno lolote; Mungu atasikia kilio chao, hasira yake itawaka moto juu yetu. Basi tufuate wosia wa Tobiti akisema; “Wenye njaa uwape baadhi ya chakula chako, walio uchi uwape baadhi ya nguo zako. Sawa sawa na wingi wako utoe sadaka. Utoapo sadaka jicho lako lisiwe na choyo” (Tob 4:16). Huu ndio upendo tunaopaswa kuwa nao kwa ndugu zetu ambao ndio kipimo cha maisha yetu ya ukristo na cha hukumu ya mwisho. Tukifanya hivyo sala ya kuombea dhabihu zetu inayosema; “Ee Bwana, tunakuomba upokee dhabihu tunazokutolea wewe mtukufu, ili ibada tunayofanya iwe hasa kwa ajili ya utukufu wako”, itakuwa na maana. Nasi wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu tutaweza kuimba kwa furaha na amani antifona ya komunyo inayosema; “Kristo ametupenda, akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato” (Efe. 5:2). Nayo sala baada ya komunyo inayosema; “Ee Bwana, tunaomba neema ya Sakramenti zako zitukamilishe, ili hayo tupokeayo katika maumbo, tufahamu ukweli wake”, itatimizwa kwetu. Tumsifu Yesu Kristo.