Jubilei ya Miaka 50 Parokia ya Itigi, Jimbo Katoliki Singida!
Na Ndahani Lugunya, Singida na Pd Richard A. Mjigwa, C.PP.S., -Vatican.
Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, sehemu muhimu ya uinjilishaji wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa linaloinjilisha na huku likiendelea kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni msanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili, ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji. Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji!
Parokia ni mahali muafaka pa waamini kujisikia kupenda na kupendwa; mahali pa kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara yaani wa kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, wanapewa malezi na makuzi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha na utume wake. Watu wote wa Mungu wanaitwa, wanatumwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko mpya wa kimisionari.
Ni katika muktadha huu, Parokia ya Damu Azizi ya Yesu, Itigi, Jimbo Katoliki la Singida nchini Tanzania inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, tarehe 2 Februari 1973 na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mintarafu Maandiko Matakatifu, Jubilei ni kipindi cha kumbukumbu, toba na wongofu wa ndani; muda muafaka wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni muda wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida ndiye aliyehitimisha kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Damu Azizi ya Yesu, Itigi, Jimbo Katoliki la Singida. Amesema, Jubilei ni wakati muafaka kwa Wakristo kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pasipo kutafuta sifa wala masilahi binafsi, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa uhuru kamili na kwamba, hii ni sehemu ya wajibu wao unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, ili watu wote waweze hatimaye, kuifahamu njia ya Wokovu. Kumbe, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 iwe ni fursa kwa watu wa Mungu Parokia ya Itigi kujikita katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili, wakati wote tena bila kuchoka wala kukata tamaa. Hiki ni kipindi muafaka cha kufanya tafakari ya kina juu ya mienendo ya maisha yao, tayari kutubu na kumwongokea Mungu ili aweze kuwakirimia neema na baraka za kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Askofu Edward Elias Mapunda amewapongeza waamini pamoja na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi, C.PP.S.
Parokia ya Itigi imekuwa ni chemchemi ya neema na baraka; ustawi, maendeleo na mafao kwa watu wa Mungu katika ujumla wao. Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wakisukumwa na kauli mbiu ya “Elimisha, Tibu na Fariji” walianza rasmi kutoa huduma za afya hapa Itigi 15 Septemba 1987. Lengo kuu likiwa ni kutoa huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Nia hii njema ilizidi kukuwa na baada ya miaka miwili huduma hii ilipanuka na hivyo kufunguliwa rasmi kwa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar na Mzee Ali Hassan Mwinyi tarehe 15 Mei 1989 pamoja na kuanzishwa kwa Chuo cha Uuguzi. Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida amemkumbuka na kumshuhuru Hayati Askofu Bernardo Mabula, Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Singida kwa maongozi ya Roho Mtakatifu akaona hitaji la kuanzishwa kwa Parokia, Itigi, leo hii imegota miaka 50 ya uwepo wake.