Tafuta

Majandokasisi watakwenda kufanya mazoezi ya Mwaka wa Kichungaji mara baada ya kumaliza Mwaka wa Tatu wa Taalimungu Majandokasisi watakwenda kufanya mazoezi ya Mwaka wa Kichungaji mara baada ya kumaliza Mwaka wa Tatu wa Taalimungu  

Mwaka Mmoja wa Mazoezi ya Kichungaji Nchini Tanzania

Bodi ya Kitaifa ya Seminari kuu Tanzania katika kikao chake kilichofanyika kati ya tarehe 6 na 7 Septemba 2023, kiliamua kwamba, kuanzia Mwaka wa Masomo 2024/2025 Majandokasisi watakwenda kufanya mazoezi ya Mwaka wa Kichungaji mara baada ya kumaliza Mwaka wa Tatu wa Taalimungu na mazoezi haya yatafanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwamba, Majandokasisi walioko mwaka wa tatu 2023/2024 ndio watakaofungua zoezi hili rasmi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia! Mwongozo huu ni matunda ya ushirikiano mkubwa kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican, kazi iliyoanza kutimua vumbi kunako mwaka 2014. Mwongozo unatoa kwa muhtasari sheria, kanuni na mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya Seminari moja moja. Mwongozo huu inapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unagusia misingi ya malezi ya Kipadre. Hapa wahusika wakuu ni majandokasisi na kiini cha malezi haya ni utambulisho wa Padre mintarafu mafundisho ya kitaalimungu kwa kutambua kwamba, Padre ni Sadaka hai na takatifu inayompendeza Mungu na Sakramenti hii inapata chimbuko lake katika Ubatizo, lakini Wakleri wanapakwa Mafuta matakatifu ili kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na Kusamehe dhambi za waamini wanaokimbilia: wema, huruma na upendo wa Mungu.

Daraja Takatifu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa
Daraja Takatifu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa

Sura ya Nne inajikita katika Malezi ya awali na endelevu. Malezi ya awali ni yale yanayotolewa kwa majandokasisi Seminarini kabla ya kupewa Daraja Takatifu ya Upadre. Malezi endelevu ni nyenzo msingi zinazomwezesha Padre kupyaisha maisha na utume wake, kwa kuwa na wongofu endelevu wa kimisionari na kichungaji, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati katika mwanga wa imani, upendo wa kichungaji na sadaka binafsi. Malezi haya ni wakati wa masomo ya falsafa ili kujenga dhana ya Ufuasi wa Kristo na masomo ya taalimungu ni kumwezesha jandokasisi kujifananisha zaidi na Kristo mtumishi na mchungaji mwema na hatima ya safari hii ya malezi ni Daraja ya Ushemasi na hatimaye Daraja takatifu ya Upadre. Majiundo endelevu kimsingi yanajikita katika upendo wa shughuli za kichungaji unaofumbatwa katika maisha na utakatifu wa Wakleri. Ni wajibu wa Maaskofu kuwa makini kwa maisha na wito wa Mapadre wao vijana, ili wasijikute wanaingia katika mazingira magumu na hatarishi katika maisha na wito wao wa Kipadre. Watambue mapungufu yao ya kibinadamu na kwamba, wao ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa na wala si wafanyakazi wa mshahara. Wawe makini katika kupambana na changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kukuza umoja na udugu katika maisha ya Kipadre sanjari na Mashauri ya Kiinjili.

Askofu Joseph Roman Mlola, Mwenyekiti wa NBMS.
Askofu Joseph Roman Mlola, Mwenyekiti wa NBMS.

Ni katika muktadha huu Bodi ya Kitaifa ya Seminari kuu Tanzania katika kikao chake kilichofanyika kati ya tarehe 6 na 7 Septemba 2023, kiliamua kwamba, kuanzia Mwaka wa Masomo 2024/2025 Majandokasisi watakwenda kufanya mazoezi ya Mwaka wa Kichungaji mara baada ya kumaliza Mwaka wa Tatu wa Taalimungu na mazoezi haya yatafanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwamba, Majandokasisi walioko mwaka wa tatu 2023/2024 ndio watakaofungua zoezi hili rasmi. Baada ya Mwaka wa Kichungaji, Majandokasisi watapaswa kurejea tena Seminari kuu ili kuendelea na masomo ya Mwaka wa Nne wa Taalimungu, ambao kimsingi ni mwaka wa mwisho na kwamba, Daraja ya Ushemasi itatolewa kwa wale Majandokasisi watakaokuwa wamehitimu Mwaka wa Kichungaji na kwamba, Daraja hii itatolewa Majimboni mwao wakati wa Kipindi cha Mapumziko ya Noeli. Tarehe ya Daraja ya Ushemasi itatolewa na Askofu Jimbo na Mashemasi watakuwa na mapumziko ya Kipindi cha Noeli kuanzia tarehe 26 Desemba hadi tarehe 10 Januari kadiri ya maelezo yaliyotolewa na Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Seminari kuu Tanzania: “The National Board of Major Seminaries, NBMS.)

Mwaka wa Kichungaji
25 November 2023, 07:33