Tafuta

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu ndio kilele cha Mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa. Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu ndio kilele cha Mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa.   (Vatican Media)

Sherehe ya Kristo Mfalme na Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni: Furaha na Matumaini

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu ndio kilele cha Mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa. Sherehe hii iliwekwa katika kalenda ya Liturujia ya Kanisa na Papa Pio XI, mwaka 1925, miaka michache baada ya kumalizika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ilikazia: matumaini kwa Yesu, Mfalme wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli! Yesu ni Mfalme wa amani anawapa wafuasi wake na kuwaimarisha kwa kusema amani kwenu, mwaliko kwa kuwa ni vyombo vya amani.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, leo ni Jumapili ya 34 ya mwaka A. Hivyo basi, ni Jumapili ya mwisho wa mwaka wa Kanisa. Kadiri ya utaratibu Liturujia ya mwaka wa Kanisa, Jumapili hii huwa tunaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa amani. Baba Mtakatifu amechagua mada za Maadhimisho ya Siku mbili za Vijana Ulimwenguni ambazo zitaadhimishwa katika Makanisa mahaliai kwa Mwaka 2023 na 2024, wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme, na kama sehemu ya Maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 ambayo yananogeshwa na kauli mbiu: “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” Kumbe maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Furahini katika tumaini” Rej. Rum 12:12. Na siku ya 39 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2024 itaongozwa na kauli mbiu "Wale wanaomtumaini Bwana watapiga mbio wala hawatachoka" (taz. Is 40:31). “Furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya wanaume na wanawake wa siku hizi, hasa wale walio maskini au wanaoteseka kwa njia yoyote ile, hizi ni furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya wafuasi wa Kristo” Rej. Gaudium et spes (n. 1). Mama Kanisa anataka kufufua matumaini kwa walimwengu hasa kwa kuwekeza kwa vijana ambao wanapaswa kuwa ni wamisionari wa furaha na matumaini. Hii ni changamoto kwa vijana kuongeza uelewa wao wa tumaini la Kikristo na hivyo kushuhudia kwa furaha kwamba, Kristo Yesu yu hai!

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni 2023
Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni 2023

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Huu ni mwaliko kwa vijana kushirikishana matumaini. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakumbuka Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yaliyofanyika Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu anasema chimbuko la matumaini ya Kikristo linabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka; Mashuhuda wa matumaini; Matumaini yanayong’ara katikati ya usiku wa giza; Umuhimu wa kukoleza matumaini kwa kuwasha mwenge wa matumaini. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu ndio kilele cha Mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa. Sherehe hii iliwekwa katika kalenda ya Liturujia ya Kanisa na Papa Pio XI, mwaka 1925, miaka michache baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ilikazia kwa namna pekee, matumaini kwa Kristo Yesu, Mfalme wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli na watu wote! Injili inafafanua kamaYesu Kristo ni Mfalme wa amani anawapa wafuasi wake na kuwaimarisha kwa kusema amani kwenu, Katika kuungana na Wakristo wote duniani kuadhimisha sherehe hii, naomba tutafakari wazo hili kuwa, “Mfalme wa Amani anatutuma tuwe wajumbe wa amani kwa kila kiumbe.”

Kristo Yesu ni Mfalme wa Haki na Amani; Upendo na Huruma
Kristo Yesu ni Mfalme wa Haki na Amani; Upendo na Huruma

UFAFANUZI: AMANI ni “hali ya usalama, kinyume cha ghasia, fujo au vita; ni utulivu, ni suluhu.” Amani ya kweli ipo ndani ya mtu katika moyo wake. Mmoja aweza kujaliwa kila kitu; fedha, nyumba, familia, elimu, ulinzi, usafiri, tiba, cheo, mamlaka, elimu nk lakini bado akaikosa amani nafsini mwake. Amani ni tunu bora kabisa kwa sababu mmoja anapoikosa huwa mnyonge na huweza kujidhuru. Mungu wa amani anatuagiza kudumisha amani kwa daima kwa vile sio lengo lake wanawe kukosa amani. Hili ndilo wazo tunaloliona katika somo la I (Eze 34:11-12, 15-17) ambapo Mungu anachukua hatua ya kuwatafuta kondoo wake na kuwatunza Yeye Mwenyewe. Wengi tunao kondoo wa kuwatunza mfano ni viongozi wa kada na ngazi zote na wazazi. Kondoo hao ndio raia, wanakijiji, waamini, wanajumuiya, wanafamilia, watoto, wanafunzi nk. Mungu anatutaka tuwatunze hao kimwili na kiroho kwa kuwapatia mahitaji na kuwafundisha dini na maadili. Tuwapiganie wanapoonewa na kuwaganga dhiki zao.  Tusipofanya hivyo Mungu Mwenyewe atainuka ili kuwachunga kondoo wake. Kristo alishuka duniani akatuokoa kutoka utumwa wa shetani, dhambi na mauti ili atupatie amani. Wanadamu tulipoteza amani kwa dhambi ya asili na dhambi nyingine. Shetani akawa mkuu wa Ulimwengu akiuendesha apendavyo. Mungu akamwita Abrahamu na kuunda taifa la Israel na kutoka taifa hilo alizaliwa Yesu Kristo Mwokozi wa Ulimwengu ili tu aturudishie amani tuliyopoteza. Alipozaliwa tu malaika walishangilia “utukufu kwa Mungu juu na amani duniani…” alihubiri amani, akiponya magonjwa na udhaifu wa kila namna, alitoa pepo, akafufua wafu, alikamilisha sheria yote na manabii akivijumlisha vyote katika amri ya mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Mwisho aliteswa, akafa na kufufuka mtukufu. Alipowatokea Mitume aliwaambia “Amani iwe kwenu” (Yn 20:19, 26b) na halafu akawapa uwezo wa kuondoa dhambi ili ulimwengu wote upate amani (Yn 20:21-23). Alimpeleka Roho Mtakatifu anayeliangazia Kanisa kusudi amani ya Kristo ienee kizazi kwa kizazi hadi mwisho wa nyakati, “hakika Yesu Kristo ni Mfalme wa amani.”

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na mapendo
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na mapendo

Injili ya leo (Mt 25:31-46) inadhihirisha faida iliyosheheni katika kusaidiana. Ufalme wa Kristo upo katika wanyonge, watu wa kawaida, masikini wanaohitaji msaada wetu. Siku ya Bwana ikifika vigezo vitakuwa “Nilikuwa mgonjwa, mgeni, uchi, njaa, kiu, mfungwa… kadiri msiyowatendea wadogo hamkunitendea mimi…” tunapofunga mwaka wa Kanisa tujiulize tumeyafanya haya kwa kiasi gani na kama bado basi mwaka mpya uanze kwa matendo ya huruma na ya upendo… hapo tutaviweka vyote chini ya miguu ya Kristo, na katika Yeye sote tutahuishwa (Somo la II - 1Kor 15:20-26, 28) na kukaa katika amani. Tunafanya mengi yanayotufunga, kututesa wenyewe na kutuondolea amani. Mfano ni imani ya ushirikina, kwa wakristo ni mchanganyo mgumu kabisa kumeza. Pili, ni vifua vilivyajaa visasi, lawama, kutoaminiana, hofu, wivu, masengenyo nk. Haya yanaleta ugumu wa kusamehe na hivi kutukosesha amani. Hii mizigo ni mizito, tukae chini ya mbawa za Kristo naye atatupa amani ya kweli. Ulimwengu wetu leo hii umejeruhiwa. Licha ya maendeleo kisayansi na kiteknolojia lakini bado hatuna amani. Maana thamani ya maisha imepotea na watu wanakata tamaa. Tunajali maendeleo na sifa za kuonekana wenye nguvu zaidi kuliko wengine kwa hasara ya haki na utu. Wapo wanaohamia mijini wakidhani ni kuzuri na kuna ajira, matokeo yake wengi hasa vijana akina maman na watoto hasa kwa mataifa masikini hukosa kazi sababu hawana elimu, ujuzi na hawana “connection-wajuani” wanaishia kuwa wezi, ombaomba, watoto wa mitaani tukilala kwenye sehemu za maegesho ya magari na kwenye mashimo na sehemu nyingine hatarishi” wakijifunika maboksi na kuwafaidisha mbu. Wasichana wanashawishika kujiuza ili kuishi na matokeo ya mwisho ni kurudi kijijini wajawazito au wagonjwa na kuleta misiba na huzuni nyumbani badala ya furaha na amani. Hapa familia inakosa umoja, matumaini yanapotea, imani kwa Mungu inafifia na amani inatoweka.

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni Ngazi ya Kijimbo
Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni Ngazi ya Kijimbo

Wengine hudhani amani ipo katika madaraka, mali, umaarufu, ngono, ulevi nk, hili ni suluhisho bandia. Amani ya kweli ipo katika Kristo Mfalme. Tunakutana naye katika neno lake, katika sala, katika masikini na katika sakramenti hasa Kitubio ambacho kwa wengi kimepoteza mvuto, wanaoungama ni wachache na pengine hawaungami vizuri, Ekaristi Takatifu na Ndoa vile wengi hawapendi kufunga wakitaka uhuru kuishi wanavyotaka. Tunapomfurahia Kristo Mfalme wa amani tuwaombee watawala wetu wadumishe amani duniani kote sote tunashuhudia kupitia vyombo vya habari duniani kote tawala na tawala zikigombana maelfu ya watu kupoteza uhai na makazi hakuna amani. Si rahisi kuwa na amani ya kweli, labda kwa unafiki tu, ikiwa hakuna haki, usawa, kujali, uaminifu na kuheshimiana kwa wote… Kristo anatutuma kuipeleka amani yake kwa watu wote. Tumwombe Kristo atujalie amani yake katika maisha yetu ya kila siku... Tuziombee nchi zetu zidumishe haki, amani na maridhiano. Familia zetu zistawishe amani ya Kristo Mfalme, na kila mmoja wetu awe balozi mwema wa amani. Mama Maria, Malkia wa amani, atuombee kusudi Mungu Mkuu atusikie na atusaidie… Amina! KRISTO MSHINDA, KRISTO MTAWALA, KRISTO MFALME, TENA WA AMANI.

Kristo Mfalme
24 November 2023, 15:06