Sherehe ya Kristo Mfalme Wa Ulimwengu & Siku ya 38 ya Vijana Ngazi ya Kijimbo
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli)- Italia
Utangulizi: Leo ni Dominika ya 34 ya Mwaka “A” wa Kanisa ambayo kwa desturi huadhimishwa Sherehe ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme ambayo huitimisha mwaka wa Kanisa na kutuandaa kwa kipindi cha Majilio. Hii pia ni Dominika ya Vijana Kijimbo. Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Huu ni mwaliko kwa vijana kushirikishana matumaini. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakumbuka Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yaliyofanyika Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu anasema chimbuko la matumaini ya Kikristo linabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka; Mashuhuda wa matumaini; Matumaini yanayong’ara katikati ya usiku wa giza; Umuhimu wa kukoleza matumaini kwa kuwasha mwenge wa matumaini. Sherehe ya Kristo Mfalme iliwekwa na Baba Mtakatifu Pius XI mwaka 1925. Lengo kubwa lilikuwa kuyakumbusha mataifa yote, viongozi na watawala wao na watu wote kwa ujumla kuwa Kristo ndiye Mfalme wa mbingu na dunia.
Hii ni kwa sababu watawala na hata watu binafsi waliweka kando utawala wa Kristo na kujifanyia mambo bila kutambua kuwa madaraka yote yametoka kwa Kristo. Watawala, wafalme kwa marais, na watu wa kawaida walidiriki hata kudai jina la Yesu/Mungu lisitajwe katika katiba zao, mabunge yao na katika mikutano. Walitaka kujifanya kuwa wao ndio wafalme wa dunia hii.Baba Mtakatifu Pius XI, kwa kuanzisha sherehe hii ya Kristo Mfalme, anawakumbusha kuwa Kristo ndiye Mfalme na ya kwamba wanapaswa kuongozwa na kutawaliwa na Kristo katika kutimiza majukumu yao. Kristo ni Mfalme si kwa sababu ametumia mabavu kupata ufalme au amenyang’anya ufalme wa mtu bali kwa sababu ni Mfalme kwa asili na hulka yake (Christ is the King by essence and nature). Kwanza, Yesu Kristo ni Mungu aliyetwaa mwili, na kwa kuwa ni Mungu viumbe vyote vipo chini ya utawala wake na hivyo ni Mfalme wa vyote. Pili, kwa kifo chake ametukomboa kutoka utumwa wa shetani na kutuweka chini ya utawala wake na hivyo kuwa Mfalme wetu (Rejea 1 Kor. 6:20). Tatu, Yeye Mwenyewe anasema “nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” (Mt. 28:18) na hivyo Yeye ni Mfalme wa Mbingu na Dunia kwa kuwa amepewa ufalme na Mungu Baba.
UFAFANUZI WA MASOMO HUSIKA: Somo letu la kwanza (Eze. 34:11-12, 15-17) linamfunua Mungu wetu mfalme katika taswira ya mchungaji. Mungu ni Mfalme ambaye anatafuta kondoo wake waliotawanyika, anawalisha kondoo zake, anawatafuta kondoo waliopotea, anawahudumia kondoo wenye majeraha na kuwatibu walio wagonjwa. Hata hivyo anawaharibu kondoo wanono na wenye nguvu. Hii ndio hulka ya Mungu wetu Mfalme. Siyo Mfalme wa kisiasa, vita au majivuno. Mungu wetu ni mfalme wa namna ya pekee. Ni mfalme anayehudumia zaidi kuliko kuhudumiwa: anatutafuta sisi ambao tumetawanyika kwa sababu ya dhambi kwa kutuonesha upendo na huruma yake; anatulisha kwa Neno lake na kwa masakramenti hasa Ekaristi Takatifu; anatutibu sisi ambao tumejeruhiwa na ulimwengu na ambao tu wagonjwa kwa sababu ya dhambi kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio na Mpako wa Wagonjwa. Lakini pia Mungu huwaaribu na kuwaadhibu wale “kondoo wanono na wenye nguvu” hawa ni wale ambao wanajineemesha kwa migongo ya wengine na wanajivunia mamlaka na nguvu zao wenyewe kana kwamba hawakupata kutoka kwa Mungu. Ulimwengu umeshuhudia na unaendelea kushuhudia watu na viongozi wa namna hii wakishushwa katika viti vyao vya enzi na baadhi yao wamekuwa na mwisho wa kusikitisha sana. Swali la msingi ni je tunaambatana na mchungaji wetu, yaani Mungu? Tunatumia fursa anazotupatia vizuri ili kushiriki ufalme wake?
Somo letu la pili (1 Kor. 15:20-26,28) linatufundisha kuwa sisi sote tuna uzima katika Kristo ambaye ameangamiza mauti kwa kifo na ufufuko chake. Kama ambavyo Adam alikuwa chanzo cha mauti, kadhalika Kristo ni chanzo cha uzima. Katika Kristo watu wote watahuishwa. Ingawa tutahuishwa kikamilifu katika Kristo wakati wa ufufuo wa wafu, tunaweza kuanza sasa kuhuishwa- yaani kufufuka katika Kristo na kuanza maisha mapya tukingali hapa duniani kwa kujitahidi kuacha dhambi, kwa kuungana na Kristo kwa njia ya misalaba yetu ya maisha, masakramenti na sala, kwa kuhusiana vizuri na wenzetu na kuishi fadhila mbalimbali ya kiutu na za Kikristo. Kwa kufanya hivyo tutashiriki ufufuko wa Kristo katika Ufalme wa Kristo. Katika somo la Injili (Mt. 25:31-46) Yesu anatufunulia kuwa kigezo cha kushiriki Ufalme wa Kristo ni matendo mema tunayowatendea wenzetu: kulisha wenye njaa, kunywesha wenye kiu, kukaribisha wageni, kuvisha walio uchi, kutazama wagonjwa na kutembelea wafungwa. Je, ni wangapi tunafanya haya? Hata hivyo katika ulimwengu wa sasa watu hawana tu njaa ya chakula au kiu ya maji. Watu wengi wana njaa ya kupendwa, kuthaminiwa, kusikilizwa, kutulizwa na kufarijiwa. Wengine wana kiu ya kutendewa haki, kiu ya amani na utulivu na kiu ya kumjua Mungu. Je tunajitahidi kuwatimizia hayo? Tunapaswa kujenga mazingira mazuri ya kupatikana kwa haki, amani na utulivu na kuwasaidia watu kumjua Mungu kwa kina. Kuna watu wengi wako uchi, si kwa sababu ya kukosa nguo za kuvaa bali kwa kuwa utu wao umepuuzwa na kudharauliwa kutokana na rangi zao, jinsia zao, kabila zao, hali zao za kiuchumi au itikadi zao za kisiasa na kidini.
Tunawajibika kuwaonesha kwa vitendo kuwa utu wao ni wa thamini kwa kuwa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuna wengine ni wafungwa si kwa maana ya kuwa gerezani, lakini kwa kufungwa na dhambi na makandokando ya ulimwengu. Je, sisi ni chanzo cha wao kuwa katika utumwa huo au tu ndoano ya kuwanasua kutoka katika utumwa huo? Matendo ya kila mmoja yawe ni fursa ya kujitafiti kiroho na kibinadamu. Kila mmoja ana wajibu wa kutenda mema kwa wengine kwani kwa kufanya hivyo tunamtendea Kristo Mwenyewe. Kwa kutenda mema tunakubali kuwa Kristo ni Mfalme wetu kwani tunatii maagizo yake na amri zake. Kwa kukubali kuwa Kristo ni Mfalme wetu ni lazima kukubali kuwa maisha yetu yote na vitivo vyetu vyote vinapaswa kutawaliwa na Kristo- (1) akili zetu zinapaswa kutawaliwa na Kristo ili tuweze kuwa na utii kamili kwake na kuwa na imani thabiti kwa kweli zote zilizofunuliwa kwetu na kwa mafundisho ya Kristo; (2) Kristo lazima atawale mioyo yetu ili iwe na upendo kwa Mungu zaidi ya vyote na kuambatana naye daima; (3) Kristo lazima atawale miili yetu ili iendelee kuwa vyombo vya utakatifuzo wa ndani wa roho zetu. Tukimtambua Kristo kama Mfalme wetu katika maisha yetu ya binafsi na ya hadhara tutaweza kuwa na uhuru wa kweli, amani na utulivu wa kweli na mwisho tutaurithi Ufalme wa Kristo mbinguni. Dominika Njema