Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme. Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Siku ya 38 ya Vijana Ngazi ya Kijimbo

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Huu ni mwaliko kwa vijana kushirikishana matumaini. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakumbuka Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana 2023

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 34 ya mwaka A wa Kanisa kipindi cha kawaida. Hii ni Dominika ya mwisho wa mwaka A wa kiliturujia na dominika ijayo inakuwa ya kwanza ya Kipindi cha Majilio mwaka B. Kadiri ya utaratibu wa Mama Kanisa, katika dominika hii tunaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme sanjari na maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo. Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Huu ni mwaliko kwa vijana kushirikishana matumaini. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakumbuka Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yaliyofanyika Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu anasema chimbuko la matumaini ya Kikristo linabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka; Mashuhuda wa matumaini; Matumaini yanayong’ara katikati ya usiku wa giza; Umuhimu wa kukoleza matumaini kwa kuwasha mwenge wa matumaini.  Itakumbukwa kuwa katika Kanisa kuna baadhi ya sherehe, kadiri ya utaratibu wake zilipaswa ziadhimishwe ndani ya Juma Kuu. Lakini kwa sababu za kichungaji, sherehe hizo zinahamishiwa katika kipindi mara baada ya Pasaka au katika kipindi cha mwaka. Moja ya sherehe hizo ni Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme iliyopaswa kuadhimisha siku ya Dominika ya Matawi. Lakini kutokana na mazingira ya Liturujia ya siku ya Dominika ya Matawi yalivyochanganyika kwa furaha na huzuni ambapo katika sehemu ya kwanza ni maandamano ya Yesu Kristo kuingia Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme, umati mkubwa wa watu ukimshangilia na kumlaki, wakishika matawi mikononi na kama walivyofanya nyakati zile kule Yerusalemu. Sehemu ya pili inahusu historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo inayoonesha jinsi alivyokamatwa na kutiwa nguvuni, mchakato mzima wa kesi yake ulivyoendeshwa hadi kuhukumiwa na kuteswa mpaka kufa kifo cha aibu Msalabani.

Siku ya Vijana Duniani Ngazi ya Kijimbo: Ushuhuda wa Furaha ya Injili
Siku ya Vijana Duniani Ngazi ya Kijimbo: Ushuhuda wa Furaha ya Injili

Na sehemu ya tatu ni Liturujia ya kawaida kama Dominika ya Kwaresima. Kutokana na mwingiliano huu wa furaha na huzuni katika siku ya Dominika ya Matawi, Kanisa limeihamishia sherehe hii kutoka Dominika ya Matawi na kuiweka katika Dominika ya 34 ya mwaka ili kupata wasaa mzuri wa kumtafakari Kristo kama Mfalme wetu wa kweli, Mfalme asiyeeleweka kwa watu wake, ndiyo maana alihukumiwa, akateswa, akasulubiwa na kuuawa kwa kifo cha aibu msalabani. Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha ajabu watu walishuhudia na kukiri ukuu wa ufalme wake na kusema hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Kihistoria sherehe hii iliidhinishwa na Baba Mtakatifu Pius wa XI mwaka 1925 akiuambia ulimwengu kwamba: “Dunia haiwezi kuuepa utawala wa Kristo kama inataka kubaki salama.” Kwa kuwa tangu mwanzo wakristo waliogopa kumwita Kristo Yesu Mfalme, kwa kuhofia kumfananisha na wafalme wa dunia hii, Baba Mtakatifu alisisitiza kuwa; “Wakristo tusiogope wala tusione aibu juu ya kumkiri Kristo kuwa Mfalme, Mwokozi na Mkombozi wetu kwani Pilato alipomwambia; “Wewe u Mfalme basi?” Yesu alijibu; “Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme” (Yn.18:37). Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali na kukiri ufalme wake akisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, umependa kutengeneza upya mambo yote katika Mwanao mpenzi, Mfalme wa ulimwengu. Utujalie kwa wema wako, viumbe vyote vilivyokombolewa utumwani vikutumikie na kukusifu bila mwisho.” Kwa mwaka mzima Kanisa limetukumbusha ya kwamba: Kristo ni Mfalme na Mchungaji mwema wa wanadamu wote kwa maisha ya sasa hapa duniani na maisha yajayo mbinguni baada ya kifo. Kumbe, iwe tu hai au tumekufa, kama anavyotuambia Mtume Paulo katika waraka wake kwa warumi, tu mali yake Kristo. Tunapoadhimisha sherehe ya Kristo Mfalme mama kanisa anatutaka tutafakari na kujiuliza kama kweli maisha yetu yanaakisi utawala wake Kristo ndani mwetu, kama kweli tunamtumikia, kama kweli tumejiweka chini ya utawala wake au tuko chini ya tawala za falme zingine ambazo kwazo kwa maisha yajayo zitatuacha solemba milele yote.

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu

Kumbe kwa sherehe hii tunahimizwa kumfuata Kristo mfalme wetu, kusudi mwishowe, atukaribishe katika ufalme wake wa milele yote mbinguni maana Yeye ni mfalme wa mbingu na dunia na ni muweza wa yote kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele” (Ufu. 5:12, 1:6). Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Ezekieli (Eze. 34 :11-12, 15-17). Somo hili linaonyesha ukuu, ufalme na utawala wa Mungu kwa watu wake. Taifa la Israeli lilipochukuliwa mateka lilikuwa kama kundi lisilo na mchungaji kwa sababu viongozi nao waliwekwa chini ya utumwa na chini ya wafalme waovu huko Babeli. Nabii Ezekieli anatangaza kuondolewa kwa Wafalme hao waovu na Mungu mwenyewe kuliongoza taifa lake. Hii ilitokea baada ya maaskari wa Babiloni kuvamia nchi ya Israeli, mji wa Yerusalemu na Hekalu lake vilibomolewa na kufanywa kuwa magofu na watu walichukuliwa mateka. Huko uhamishoni waliteseka sana kwa utumwa kwa kufanyishwa kazi nzito. Viongozi wa dini na wazee wao hawakuwa tena na sauti ya kuwaelekeza wala kuwaongoza watu wao kwani wote pamoja walikata tamaa kabisa na kuona kuwa Mungu amewaacha waangamie kwa sababu ya dhambi zao. Mwenyezi Mungu alisikia kilio chao, akamtuma Nabii Ezekieli kuwatangazia ujio wa siku ya wokovu ambapo Mungu mwenyewe atakuwa Mfalme na mchungaji wa watu wake. Ujumbe huu ni faraja kwetu kwani Mungu mwenyewe anaahidi kumtafuta na kumuulizia kila anayepotea kwa dhambi kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake waliopotea ili kumrudisha kwake na kumuongoza katika malisho yake kama tunavyoimba kwa matumaini katika wimbo wa katikati tukisema; “Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu, katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza; hunihuisha nafsi yangu, na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake, waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata, siku zote za maisha yangu. Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele” (Zab. 23:1-3, 5-6).

Ukuu na utukufu wa Kristo Yesu vimetundikwa Msalabani.
Ukuu na utukufu wa Kristo Yesu vimetundikwa Msalabani.

Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 15:20-26, 28). Mtume Paulo anatueleza wazi kuwa kwa kifo na ufufuko wake, Yesu alishinda dhambi na mauti; na kwa njia hiyo Mungu Baba amemtukuza. Baada ya kifo cha kila mwanadamu, utawala wa shetani unafika kikomo chake, Yesu Kristo Mchungaji na Mfalme anachukua milki na kutoa hukumu. Ndiyo maana Paulo mtume anasisistiza; “Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake, limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki Yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.” Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 25:31-46). Sehemu hii ya Injili inahusu hukumu ya mwisho inayotolewa na Yesu Kristo mwana wa Mungu kwa mamlaka aliyopewa na Mungu mwenyewe. Hukumu hii ni ya haki maana inatolewa kwa kila mmoja kadiri alivyoishuhudia imani yake siku kwa siku kwa kutenda matendo ya huruma kwa jirani zake na kuiishi amri ya mapendo kwa Mungu na Jirani. Na upendo kwa jirani ni kipimo cha upendo wetu kwa Mungu. Kadiri tunavyoyatendea makundi maalumu ya ndugu zetu kwa mahitaji yao – wenye njaa, wenye kiu, maskini, wageni, wagonjwa, wafungwa, na walio uchi – ndivyo tunavyomtendea Kristo na ndicho kipimo cha hukumu yetu. Ndiyo maana Yesu anasema; “Kadiri mlivyomtendea mmoja wa wadogo hawa mlinitendea Mimi”. Na kadiri tunavyomtenda jeuri na kumdharau mhitaji, ndivyo tunavyomtendea jeuri na kumdharau Mungu. Na ni kwa namna hiyo tunajiandalia wenyewe mashahidi na ushahidi wa hukumu ya mwisho. Waswahili wanasema; “mdharau mwiba mguu huota tende."

Matendo ya huruma:kiroho na kimwili ni ufunguo wa Ufalme wa Mbingu
Matendo ya huruma:kiroho na kimwili ni ufunguo wa Ufalme wa Mbingu

Mama Kanisa daima anatukumbusha juu ya matendo ya huruma:kiroho na kimwili kila kukicha. Tukiyadharau na kutoyatendea kazi kwa kuyaishi, mwisho wake ni kuangamia kwenye moto wa milele. Kumbe, basi, tutumie muda tulionao kujitengenezea mbingu kwa kuwatendea matendo ya huruma ndugu zetu wahitaji ili nasi tukaipokee mda wetu ukifika. Tukumbuke kuwa amri ya mapendo ni sheria na ndio kipimo cha hukumu yetu. Mungu ametupa uhuru, tuutumie kwa busara na kwa faida ya wokovu wetu. Hata kama Mungu wetu ni mwema kiasi cha kuwaangazia jua lake wote na kuwanyeshea mvua yake wema na wabaya, waaminifu na wasiowaaminifu, anayaacha magugu na ngano vikue pamoja, lakini mwisho wa yote atatenda haki kwa kila mmoja kadiri alivyotumia uhuru wake na kuishi vyema au vibaya. Basi tujikabidhi kwa Kristo mchungaji mwema, mfalme wetu mtukufu, ili tuumalizie vyema mwaka huu A wa kiliturujia na kuanza vyema mwaka B wa kiliturujia kwa kipindi cha majilio tutakapojiandaa kuzaliwa kwake mkombozi wetu Yesu Kristo katika maisha yetu. Na hapo tutaweza kuimba kwa furaha antifona ya wimbo wa komunyo tukisema; “Bwana Mfalme ameketi milele, Bwana atawabariki watu wake kwa amani” (Zab. 28:10, 11). Nayo sala baada ya komunyo anayotuombea mama kanisa akisema; “Ee Bwana, sisi tuliopokea chakula cha uzima wa milele tunaona fahari kuzitii amri za Kristo Mfalme wa ulimwengu. Tunakuomba utujalie tuishi milele pamoja naye katika ufalme wa mbingu”, itasikilizwa na kutimizwa kwa sisi kuupokea uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Kristo Mfalme
22 November 2023, 15:08