Tafakari Dominika 31 ya Mwaka A wa Kanisa: Ushuhuda Katika Vitendo na Maisha Adili
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia
Utangulizi: Maneno yetu na mwenendo wetu wa maisha havipaswi kutenganishwa, bali vinapaswa kuwa na ulinganifu. Kukiwa na utofauti kati ya maneno yetu na mwenendo wetu wa maisha tunageuka kuwa wanafiki. Tusifanye mambo kwa ajili ya kutafuta sifa bali kwa ajili ya kumtukuza Mungu na kwa ajili ya wokovu wetu. Katika Injili ya leo (Mt. 23:1-12) Yesu Kristo anakemea tabia ya unafiki na kufanya mambo ili kutafuta sifa. Leo Yesu anawazungumzia Waandishi na Mafarisayo. Yesu anawaambia makutano na wanafunzi wake kuwa “wafuate wanayofundishwa na Waandishi na Mafarisayo lakini wasifuate matendo yao.” Hii ni kwa sababu Waandishi na Mafarisayo walifundisha mambo mazuri na ya kweli kuhusu imani ya Kiyahudi kwa kadiri ya torati lakini wao wenyewe wakashindwa kuyaishi na hivyo kuwa wanafiki. Walichofundisha sicho walichoishi. Walikuwa kama “kinyonga, ambaye anabadilika kulingana na mazingira.” Katika Injili Yesu anakemea dhambi tatu za Waandishi na Mafarisayo: Kwanza, hawatendi wanachofundisha. Wanasema hiki na wanatenda kingine kabisa ambacho hakiendani na wanachosema au kufundisha. Pili, wanafanya mambo kutafuta sifa mbele za watu: walivaa hirizi kwenye paji la uso na katika mkono wa kushoto (hirizi zilikuwa ni visanduku vidogo vya ngozi ambavyo ndani yake waliandika mojawapo ya vifungu vinne kutoka kwenye vitabu vya Torati. Mojawapo ya vifungu hivyo vinne ni kifungu kutoka Kumb. 6:4-9 ambacho kinaitwa “Shema Israeli” yaani “Sikiza, ee Israeli…”. Walivaa hizi hirizi hizi ili kutafsiri kwa vitendo agizo lililoandikwa katika kitabu cha Kutoka 13:9 na waliweka matamvua/vishada kwenye pindo nne za mavazi yao ili kuwakumbusha juu ya amri za Mungu na wajibu wao wa kuzishika (Rejea Hes. 15:37-41 na Kumb. 22:12).
Waandishi na Mafarisayo walivaa hirizi na nguo zenye matamvua kwa lengo la kujionesha kwa watu kuwa wao ni wacha-Mungu ilihali matendo yao mengi hayakuwa ya kumcha Mungu. Lakini pia ili kutafuta sifa mbele za watu walipenda kukaa nafasi za mbele kwenye sherehe na katika masinagogi na walipenda sana kusalimiwa hata wakiwa masokoni na kuitwa majina yenye kuonesha kuheshimiwa kama “Rabbi” yaani Bwana/Mwalimu, “Baba” na mengineyo. Kwa kuwa Waandishi na Mafarisayo walikuwa ni viongozi wa dini walitumia dini kwa lengo la kutafuta heshima, sifa, vyeo na kujitukuza wenyewe badala ya kumtukuza Mungu. Tatu, wanatafsiri sheria kwa mtazamo finyu ambao unageuka mzigo kwa wengine: walizivunjavunja amri kumi za Mungu na kupata jumla ya sheria 613. Wingi wa sheria hizi uligeuka kuwa mzigo mzito, hasa kwa watu wa kawaida. Badala ya sheria kumfanya mtu awe karibu na Mungu zikamweka mbali na Mungu. Kwa dhambi hizi tatu Waandishi na Mafarisayo wanageuka kuwa wanafiki na watafuta sifa na wenye kujitukuza wenyewe. Hata sisi katika ulimwengu wa leo tunatenda dhambi kama za Waandishi na Mafarisayo. Sisi ni wanafiki kwa kuwa hatutendi tunachosema. Maneno yetu hayarandani na matendo yetu. Tumekuwa kama popo. Unafiki ni kuvaa hulka mbili kwa wakati mmoja. Mtu mnafiki akiwa mbele ya uso wako anakusifia lakini akiwa nyuma ya mgongo wako anakuponda. Wengi wetu ni wanafiki kwa kuwa tunafanya vitu si kutoka moyoni na kwa nia njema bali kutafuta sifa na utukufu mbele za watu, yaani kutafuta “makomeo.” Je, tunapotoa michango mikubwa na majitoleo binafsi makanisani tunatoa kwa lengo la kumtukuza Mungu au kwa lengo la kusifiwa na watu na kutafuta mafaa binafsi? Matendo yetu ya kiibada yanatoka moyoni au tunafanya ili kujionesha kuwa tu wacha-Mungu?
Wengi wetu tunavaa visakramenti kama vile rozari, medali na skapulari si kwa sababu tunatambua umuhimu wake bali kujionesha kwa watu kwamba tu watakatifu sana. Ni waamini wangapi kwa nje wanajionesha kuwa wanasali sana lakini ndani ya mioyo yao wamejaa ushirikina, visasi, chuki, dhuluma na mengineyo kama hayo? Huu ni unafiki na kutafuta tu sifa za nje. Je, imani tunayofundisha na kuikiri ndiyo tunayoiishi? Wazazi wengi wanawafundisha kwa maneno matupu watoto wao kuwa na fadhila kama kujiheshimu na kuheshimiana, upendo, kiasi, kujitawala na mengineyo lakini wakati huo huo wao wenyewe hawaheshimiani, wanapigana kila uchao, ni walevi kupindukia, makahaba na wahuni. Wengi wetu tunapenda sana kuitwa kwa majina yenye kuashiria kuheshimika kama vile “Mheshimiwa,” “Mwalimu,” “Mkuu,” “Bosi” “Tajiri”. Je, jina “Mheshimiwa” ni kilelezo kuwa tunajiheshimu wenyewe mpaka kuitwa “Mheshimiwa’? Je, tunapoitwa “Mwalimu” ni kielelezo kuwa ni tunawafundisha wengine kwa matendo yetu? Je, tukiitwa “Tajiri” ni kiashiria cha utajiri wa mali au utajiri wa fadhila za Kikristo? Je, tukiitwa “Mkuu” ni kiashiria cha kutumikiwa au ni ukuu wa kuwatumikia watu? Tujitafakari na kuchukua hatua. Je, sheria tunazotunga na kuzipitisha ni kwa lengo la kuwasaidia watu kuishi vizuri au ni kwa lengo la kuwatwisha watu mizigo? Lengo la sheria ni kuwawezesha watu kuishi vizuri na mwisho kupata ustawi wa kiroho na kimwili. Sheria zinapaswa kuwa chachu ya upendo kwa Mungu na binadamu. Baadhi yetu sisi Mapadre kwa bahati mbaya tunawawekea waamini wetu vijisheria vingi kwenye maparokia ambavyo hata havitambuliwi rasmi na Kanisa. Matokeo yake kondoo wetu wanakata tamaa na kuacha kusali. Tujitahidi kuwapunguzia waamini wetu mizigo ili jitihada zao za kumtafuta Mungu zifanikiwe. Vinginevyo hatutatofautiana na Waandishi na Mafarisayo ambao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Amani ya Bwana iwe nawe!