Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya neno la Mungu Dominika ya 32 ya Mwaka A wa Kanisa: Wazo kuu: Hofu ya Mungu ni Hekima ya kung’amua mambo yatarajiwayo. Tafakari ya Liturujia ya neno la Mungu Dominika ya 32 ya Mwaka A wa Kanisa: Wazo kuu: Hofu ya Mungu ni Hekima ya kung’amua mambo yatarajiwayo.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 32 ya Mwaka A wa Kanisa: Hofu ya Mungu na Hekima ya Binadamu

Mfano wa wanawali kumi; watano kati yao walikuwa wenye busara na wengine watano waliosalia walikuwa ni wapumbavu.Wale watano walikuwa na busara kwa sababu walizingatia na kuweka tahadhari kwa umakini na hekima kulingana na tukiomlililokuwa mbele yao ,yaani kuwa na taa zao zinazowaka ili kumwangazia njia bibi harusi.Wamekuwa waangalifu kwa kufikiri kwamba labda watapaswa kungoja kikundi cha wavulana wafike,na hivi yafaa walete mafuta ya akiba.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa mkristo mwenzangu, katika Injili ya leo tutasikia mfano wa wanawali kumi;watano kati yao walikuwa wenye busara na wengine watano waliosalia walikuwa ni wapumbavu.Wale watano walikuwa na busara kwa sababu walizingatia na kuweka tahadhari kwa umakini na hekima kulingana na tukiomlililokuwa mbele yao ,yaani kuwa na taa zao zinazowaka ili kumwangazia njia bibi harusi.Wamekuwa waangalifu kwa kufikiri kwamba labda watapaswa kungoja kikundi cha wavulana wafike,na hivi yafaa walete mafuta ya akiba. Nao wakafanya hivyo. Waliweza kutegemewa na kuaminiwa. Wakati ulipofika walikuwa tayari. Na wale watano walikuwa wapumbavu kwa sababu walikuwa wazembe, walikosa uangalifu, hawakufikiri, hawakupanga kwa ajili ya hayo yawezayo kutokea njiani. Hawakujali kuleta vifaa vitakavyohitajika kwa safari nzima. Walipoitwa hawakuwa tayari. UFAFANUZI: Katika somo la kwanza, tunaona kuwa Waisraeli walithamini hekima kuliko utajiri na nguvu za mwili, waliheshimu watu waliojua siri za nguvu za asili, watu waliofumbua mafumbo na kutunga nyimbo na mashairi. Mtu aliyevumilia, aliyefanya mambo kwa umakini, aliyekuwa mwaminifu kwa maneno na vitendo, mnyenyekevu na mtu wa kiasi ndiye aliyekuwa na hekima. Mtu anayekubali hekima kama mwongozo wake atapata amani maishani mwake. Katika somo la pili waamini wa Kanisa la Mwanzo waliamini kuwa Yesu atarudi kwa mara ya pili mapema sana kukusanya wafuasi wake na kuwapeleka katika ufalme wa Baba yake mbinguni.

Waisraeli walikumbana na majanga mbalimbali katika maisha.
Waisraeli walikumbana na majanga mbalimbali katika maisha.

Hii ilitokana na Waisraeli kupata majanga makubwa na mateso mbalimbali. Kwa Wathesalonike mawazo kuhusu kukaribia mwisho wa dunia yallisababisha watu kutofanya kazi kwani akiba ya chakula walichokuwa nacho kiliwatosha kuwafikisha mwisho wa dunia. Muda ukapita na watu wakaanza kukata tamaa, uvumilivu ukawashinda na baadhi yao wakaacha ukristo. Ndipo hapo Mtume Paulo anawaambia wasibweteke na wakeshe kwani ujio wa Yesu ni muda wowote. Mawazo haya hadi leo yanaendelea miongoni mwa wakristo na hapa ndipo “manabii uchwara na waongo na wanachungaji” wanaotangaza Injili ya mafanikio hewa wameendelea kutapeli watu, lakini wahenga husema wajinga ndio waliwao. Maandiko yanasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa ila kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa, swali la Kristo kurudi mara ya pili ni lini aliwajibu wafuasi wake, kua sio kazi yake, kujua majira na saa bali wakeshe na kuwa tayari muda wote. Wapendwa katika Kristo Injili ya leo inatupa mfano ambao kuuelewa yatubidi tuelewe mila na desturi za Wayahudi katika kipindi cha Yesu, katika suala zima la kuoa.Kadri yao sherehe za harusi zilifanyika nyumbani kwa bwana harusi.Zilianza daima jioni na zilitanguliwa na maandamano kutoka nyumbani kwa wazazi wa bibi arusi.Na kuishia nyumbani kwa bwana arusi.Kimila bibi arusi aliwaalika marafiki wanawali wenzake wasiopungua kumi,wamsindikize na taa zao kwenye sherehe hizo.Wanawali hao walipaswa kuwa na kichupa cha akiba ya mafuta ili ikiwa sherehe zitarefuka wasitindikiwe mafuta.

Mfano na wale wanawali wajanja waliobeba mafuta ya akiba.
Mfano na wale wanawali wajanja waliobeba mafuta ya akiba.

Kama Injili isemavyo Bwana arusi alikawia kuja, kwa hiyo wanawali wakaanza kusinzia hata kulala. Ilipofika usiku ndipo ulipoonekana msafara wa bwana arusi akija kumchukua bibi-arusi.Wanawali wakaamshwa na kuambiwa waziandae taa zao,waende kumlaki bwana arusi ili waandamane naye kuja kumchukua bibi arusi.Watano kati yao walikuwa na busara hawakusahau kuchukua akiba ya mafuta.Watano wengine hawakuwa na akiba na hivyo kuanza kuwabembeleza wenzi wao wawape mafuta kidogo katika akiba yao,lakini hawakufanikiwa ikabidi waende kununua usiku huo wa manane.Waliporudi wakakuta maandamano yamekwisha,sherehe zimepamba moto na milango imefungwa.Walipogonga hodi bwana arusi hakuwatambua akawaambia waondoke. Mama Kanisa ana maana kubwa sana anapotupa mfano huu hasa tunapokaribia mwisho wa mwaka wakanisa. Mama kanisa anataka kutukumbusha mambo muhimu matatu: A) Hao wanawali marafiki wa bibi arusi ni sisi wakristo tukioitwa kushiriki harusi ya ndugu yetu Kristo.Tulialikwa siku tulipobatizwa na kuanza safari hiyo ya harusi itakayokamilika kwa ujio wa Bwana arusi siku yakufa kwetu, je tutakuwa tayari kumpokea? Ndugu zangu tuishi kama tutakaokufa kesho, tuishi maisha ya kumpendeza Mungu.

Mwaliko ni kukesha katika Sala, Neno, Sakramenti na matendo ya huruma
Mwaliko ni kukesha katika Sala, Neno, Sakramenti na matendo ya huruma

B) Hao wanawali (mabinti hapa unaweza ukaweka jina lako upo kundi gani) wapumbavu ni mfano wa wakristo waliouza ukristo wao katika kufuatilia raha na furaha batili za maisha ya sasa. Wanakesha kimwili, kiroho wako katika usingizi mzito. Tulipobatizwa tulipewa taa (mshumaa) unayowaka na tukapewa akiba ya mafuta katika Sakramenti na visakramenti. Kitubio na Ekaristi Takatifu, Misa na sala mbalimbali, amri za Mungu na za Kanisa yote hayo ndo miongozo yetu na nyenzo Madhubuti amabazo mama kanisa mtakatifu daima huliwasha Watoto wake kwa Maisha yote, lakini tulio wengi kwa hiari yetu tumeyatupilia mbali yote hayo. Mifano mizuri ya wakatifu na wenzetu wenye mapenzi mema tumeipuuza. Siku hiyo itakuja kama mwizi lakini sisi kwa uzembe wetu tumepuuza ukweli huo na kuishi kama tutakavyo sisi wenyewe. Je, mwamini mwenzangu upo upande gani? C) Chupa ya mafuta ya akiba inamaanisha vichocheo vya kulinda taa ya Neema ya Utakaso ikiwaka ndani mwetu. Lilikuwa ni sharti kwa marafiki wa bibi arusi, tukifanananisha sharti hilo na sherehe ya harusi tunaona kuwa ni jepesi sana nyakati zetu. Hali kadhalika masharti hayo ni madogo sana tukiyafananisha na karama ya uzima wa milele tunaosubiri. Lakini yanaonekana ajabu sana jinsi wengine wetu tunavyofanana na wale wanawali wapumbavu, hatuna akiba ya chupa ya mafuta. Roho zetu ni zimekufa, zimezima, tuna dhambi za mauti moyoni na kuishi hivyo bila wasiwasi wowote. Sakramenti zipo, sala na ibada mbalimbali zipo, vyote hivyo havitushawishi wala kutuchochea tunasinzia mpaka tunakoroma pindi tummeshikilia taa zilizozima na tunamngoja bwana harusi je tunajua kweli tunachofanya au tunajisahaulisha kuwa Mungu ni mwenye haki na humpa kila mmoja kadiri ya anachostahili na iliyo haki yake?

Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao
Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao

KATIKA MAISHA: Ndugu zangu katika Kristo tusiwe wapumbavu tunajua neno upumbau jinsi lisivyolia vema masikioni mwetu halifai ni wazi lakini kwa uzito huo tunapaswa kubadilika na kuitwa wenye akili wengi hupenda kuitwa hiyo ingawa kwa wengi ni kinyume na uhalisia, maisha ya leo ni ya hatari kama nini. Ajali ngapi zinatokea? Watu wangapi wanakufa ghafla bila ya masakramenti ya Kanisa? Magonjwa mangapi yamezuka yasiyoponyeka hata kwa sayansi za kisasa? Sasa ndugu ndo wakati wa kulia:” Bwana, Bwana tufungulie!” Kanisa liko macho muda wote na linawaalika waamini wote kukesha katika kuwahudumia maskini, wagonjwa kimwili na kiroho, kuwafariji yatima kwa upendo. Tunahitaji kuzidi kuhusiana naye, kumkumbuka, kuongea naye hata katika shughuli zetu za kila siku. Kufanya mambo yote kwa ajili ya utukufu wake. Inawezekana wengine wetu wanaendelea kutangatanga mbali na Bwana kwa muda wa kutosha, tunajua urafiki wetu naye umeharibika na dhambi zetu kubwa mnoo, ni wazi tunalitambua jambo hilo, Je, tunachukua hatua gani madhubuti kujipatanisha naye tena Mungu ana upendo kwa viumbe wake na yuko tayari kutusamehe dhambi zetu tukimwendea kwa moyo wa toba, unyenyekevu na kuahidi kutotenda dhambi tena. Tumwombe Mungu atujalie Hekima ya kujua mambo ya baadaye. TUMSIFU YESU KRISTO!

Liturujia D32

10 November 2023, 09:59