Tafakari Dominika 32 ya Mwaka A wa Kanisa: Tokeni Mkamlaki!
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia.
Maisha na Ufuasi wetu hapa duniani ni fumbo linalotudai daima kujiandaa muda wote na kuwa tayari “kutoka” ili tuweze kumlaki Bwana. Ni mwaliko wa “kutoka” katika maisha ya uovu na kuweka mafuta ya kutosha katika maisha ya imani na matendo ili tuweze kuangaza maisha yetu na ya wengine. SOMO LA KWANZA: Hek. 6:12-16: Mwandishi wa kitabu cha Hekima anatuletea somo linalohusu Hekima ya Mungu. Hekima hii ya Mungu haimfikii tu mtu “automatically” bila kujishughulisha. Yaani mtu hapaswi kubweteka tu akifikiri kuwa hii hekima itajileta yenyewe. Ni Hekima ambayo tunapaswa kuonesha utashi wa kuitafuta maana ndiyo iongozayo maisha yetu na ya kwamba inamsaidia mtu kuwa mkamilifu katika uetendaji wake. Hekima hii ya Mungu hutuwezesha kutofautisha jema na baya, kujua mahitaji msingi kwa ustawi wetu kiroho na namna ya kuenenda katika maisha. Swali la msingi ni je: Hekima ya Mungu inapatikana wapi? Hekima ya Mungu inapatikana katika kusoma na kuishi Neno la Mungu, katika vipindi vya mafungo na tafakari za kiroho, katika maisha ya Sakramenti. Kila mmoja wetu anaalikwa kuitafuta Hekima ya Mungu. Hekima ya Mungu inaangaza akili zetu kujua namna ya kuenenda tunapomsubiri Kristo bwana arusi wetu kama hekima ilivyowaangaza wanawali watano wenye busara kujiandaa vizuri kumlaki bwana arusi.
SOMO LA PILI (Thes. 4:13-18a): Wakristo wa Thesalonike, kama ilivyo kwa Wakristo wa zama zetu, walisumbuliwa sana na maswali mengi juu ya kifo: nini maana halisi ya kifo? Nini kitatokea huko mbeleni kwa waliokufa? Wakifa wanakwenda wapi? Je, watafufuliwa? Na kama watafufuliwa: je watafufuliwa lini, watafufuliwa kwa namna gani, watafufuliwa wapi? Maswali haya yaliwafanya Wathesalonike kuwa na huzuni sana na maombolezo makubwa wakati wa misiba ya wapendwa wao maana ni kama hawakuwa na majibu. Kwa hakika maswali haya yalichagizwa zaidi na uwepo wa wapagani katika jamii yao ambao hawakusadiki katika utufuko wa wafu. Maswali haya ndiyo yanayomfanya Mtume Paulo kuandika sehemu hii ya somo la pili, ambayo inadhaniwa ilikuwa ni sehemu ya maelezo ya Mtume Paulo kwa Wakristo wa Thesalonike kufuatia kifo cha mmoja wa wanajumuiya yao ya kikristo. Paulo anatoa maana ya kikristo kuhusu kifo: kifo ni kulala katika Yesu, kutakakofuatiwa na hakikisho la kuamshwa, na hivyo kifo siyo kikomo cha maisha na wala siyo kupotea kwa aliyekufa. Mtume Paulo anawapa ulinganisho: Kama Kristo alikufa, basi na waamini lazima wafe; na kama Kristo alifufuka, basi na waamini waliolala watafufuliwa. Hivyo kifo siyo hasara. Hili lilikuwa ni fundisho la matumaini na faraja kubwa sana kwa waamini wa Thesalonike. Paulo anaeleza kuwa haya yote yatatokea katika ujio wa utukufu wa Kristo Yesu. Hata sisi leo pengine tunahuzunishwa na habari za kifo na kwa kiasi fulani tunakuwa kama watu wasioamini katika ufufuko wa wafu. Neno hili ni la faraja kwetu ya kuwa “tukilala” katika Kristo tutafufuliwa na Kristo. Na hivyo kwetu kifo ni njia ya kuungana na Kristo na kushiriki utukufu wake. Hata hivyo tumaini hili linapaswa kutufanya kujiandaa vizuri katika maisha yetu ya hapa duniani na kukesha kila wakati kama tunavyoalikwa na somo la Injili. Tunapaswa kutumia busara kung’amua na kujiandaa na mambo yajayo.
SOMO LA INJILI: Mt. 25:1-13: Yesu, katika Injili yetu ya leo (Mt. 25:1-13) anaulinganisha ufalme wa mbinguni na wanawali kumi. Yesu anatoa mfano kwa kutumia mazingira ya harusi za Kiyahudi. Hebu tuone kidogo utaratibu ulivyokuwa ili tuelewe zaidi kusudi la Injili yetu ya leo. Tunaweza kueleza matukio makubwa mawili katika mfumo wa ndoa za Kiyahudi: kwanza, kuposa na pili kumchukua mke na kuanza kuishi naye nyumba moja. Katika tukio la kuposa liliandaliwa na wazazi wa pande zote mbili. Wanandoa watarajiwa (pamoja na wazazi wao na mashuhuda) walikutanishwa na kufanya makubaliano rasmi ya kuwa mke na mume mbele ya wazazi wao na mashahidi (ikiwa ni pamoja na kuamua masharti yahusuyo mahari). Kwa makubaliano haya “walifanyika rasmi mume na mke kisheria.” Baada ya tukio hili la kuposa, mwanamke aliendelea kukaa kwa wazazi wake na mume alirudi kwao kuandaa makazi rasmi kabla ya kurudi kumchukua mke wake na kuanza kuishi naye nyumba moja (neno ‘kabla hawajakaribiana’ tunalosoma katika Injili ya Matayo 1:18 juu ya Maria na Yosefu lilimaanisha ‘kabla hawajaanza kuishi pamoja katika nyumba moja’). Kipindi cha mwanaume kuandaa makazi kwao kabla ya kwenda kumchukua mke wake kilichukua miezi kadhaa (na hata mwaka mzima). Baada ya kukamilisha maandalizi yote kwao mume sasa alipanga siku rasmi ya kwenda kumchukua mkewe na kumleta kwake. Kwa kawaida tukio hili lilifanyika kuanzia nyakati za jioni. Katika makazi ya mwanaume walikuwepo watu wakisubiri kwa hamu bwana arusi afike na mkewe toka ukweni. Hii ilikuwa ni siku ya furaha sana. Hawa wanawali kumi wanaotajwa katika mfano wa Yesu ni miongoni mwa watu waliokuwa nyumbani kwa bwana arusi wakimngoja aje na mkewe ili kuanza rasmi kuishi naye nyumba moja. Hawa wanawali walikuwepo kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali katika tukio husika. Walipaswa kuwa tayari maana hawakujua muda maalumu wa kufika msafara toka ukweni kwa bwana arusi.
Hivyo mfano wa Yesu unahusu arusi. Kwa kadiri ya Yesu kulikuwa na wanawali kumi: watano wenye busara na watano wapumbavu. “Busara na upumbavu” ndivyo vinawatofautisha hawa wanawali kumi. Busara ya wanawali watano inaonekana katika mambo mawili: (i) kwa kutambua kwamba bwana arusi anaweza kuchelewa kuja kuliko muda tarajiwa na (ii) ya kwamba wawe na mafuta ya akiba ya kuwatosha usiku kucha. Hii ndiyo busara au hekima ambayo kila mmoja anaalikwa kuwa nayo katika somo la kwanza (rejea Hek. 6:12-16). Na upumbavu wa wanawali wengine watano unaonekana katika mambo matatu: (i) kushindwa kutambua kuwa bwana arusi anaweza kuchelewa kuliko matarajio yao, (ii) kutokuwa na mafuta ya akiba na (iii) kufikiri kuwa ni rahisi kupata mafuta nyakati za usiku kwa wauzao mafuta. Tunayo mambo ya kujifunza katika Injili hii ambayo inatualika kuwa tayari kumlaki Kristo, Bwana arusi wetu ambaye anatualika kushiriki “arusi ya milele nyumbani mwake mbinguni.” Jambo la kwanza la kujifunza ni kuwa (1) Tunapaswa kujiandaa kwa wingi wa matendo yetu mema, yaani wingi wa “mafuta ya akiba.” Mafuta ya akiba siyo kitu kingine bali “matendo yetu mema” yanayotusaidia kuendelea kuangaza maisha yetu na ya wengine. Matendo yetu mema ndiyo tiketi ya kuingia kwenye arusi ya mbinguni na siyo kufikiri tutaingia mbinguni kwa kuomba au kuazima matendo ya wengine kama wale wapumbavu walivyoanza kuomba mafuta ya wanawali wenye busara: “tupeni mafuta yenu kidogo.” Na hapa tupo wapumbavu wengi ambao tunafikiri tutaingia mbinguni kwa mgongo wa matendo mema ya watu wengine. Mara nyingi tunasema: mimi sisali lakini mama yangu anasali; mimi siendi Kanisani lakini nawahimiza watoto wangu kwenda Kanisani. Tufahamu kuwa hatuingii mbinguni kwa mgongo wa matendo mema ya wengine. Hayo matendo yao mema yanawatosha wao tu, hayawezi kututosha wao na sisi. Sisi tutafute ya kwetu wenyewe. Hivyo matendo mema ni suala la mtu binafsi. Taa za maisha yetu ya imani, matumaini na mapendo hazipaswi kuzima kamwe, licha ya ukweli kwamba hapa na pale “tunaweza kusinzia kiimani na kimatendo” kama wanawali wote kumi walivyosinzia.
(2) Muda wowote, hasa ule tusiofikiria, ndio bwana arusi atafika. Hivyo tunapaswa kuwa tayari muda wowote. Wanawali wapumbavu walijisahau “wakatengeneza muda wao rasmi vichwani mwao atakaofika bwana arusi,” bila kujua kuwa anaweza kuwahi au kukawia kuliko wanavyofikiri. Hata sisi kuna wakati tunatengeneza muda wetu: siwezi kufa mapema hivi, bado ni kijana; mbona wengine wanabatizwa wakiwa wazee, bado nina muda n.k. Tukumbuke kuwa hatujui “muda halisi” wa hatima ya maisha yetu hapa duniani ambao tunapaswa kuondoka ili kwenda kukutana na Kristo, hakimu wa maisha yetu. Tusisubiri wakati “usiku umeingia” ili kutafuta mafuta, yaani tusisubiri kutenda mema mwishoni mwa maisha yetu, bali tutumie vizuri muda tulionao sasa kujiandaa. Maisha yetu yote yanapaswa kuwa “kesha” yaani kuwa macho kiroho na kutenda mema siku zote. Hivyo Injili inatukumbusha umuhimu wa kutumia vyema “muda wa sasa” kwa ajili ya kujiandaa na yajayo. Tukitumia vizuri muda wa sasa tunaweza kusema kwa furaha: “Yajayo Yanafurahisha.” Hivyo lazima tuone mbali. (3) Tuwe tayari “kutoka” maana maisha yetu ya hapa duniani ni mwaliko wa “kutoka”: “tokeni mwende kumlaki.” Injili inatukumbusha kuwa maisha yetu ya hapa duniani mwaliko wa kutoka katika maisha ya giza kwenda maisha ya mwanga, ni mwaliko wa kutoka katika maisha ya dhambi na kwenda katika maisha ya wongofu ili mwisho tuweze kumlaki Bwana. Lakini kutoka huku kunatudai maandalizi thabiti ya vitendea kazi tulivyonayo: taa na mafuta, yaani imani dumifu na matendo mema. Je, umejiandaaje kutoka katika maisha ya dhambi: uvivu wa sala, utegemezi wa nguvu za giza, dhuluma, rushwa, visasi, chuki, majivuno na mengineyo. “Toka” sasa, muda ndio huu. Dominika Njema!