Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Maskini Duniani tarehe 19 Novemba 20223 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Wala usiugeuzie uso wako mbali na mtu maskini.” Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Maskini Duniani tarehe 19 Novemba 20223 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Wala usiugeuzie uso wako mbali na mtu maskini.”   (AFP or licensors)

Tafakari Dominika ya 33 ya Mwaka A wa Kanisa: Siku ya Saba ya Maskini Duniani 2023

Ni kipindi cha kufanya tathimini jinsi tulivyoyaishi mafumbo matakatifu mwaka huu wa kiliturujia. Swali la kujiuliza, Je, tumejichotea neema kwa kuzitumia vyema karama/talanta tulizojaliwa na Mungu au tumepoteza neema kwa kuzificha talanta zetu? Kama tumezipoteza neema zitokanazo na matumizi mabaya ya talanta tulizopewa mathalani kuzificha, tusikate tamaa, tuanze upya, tumlilie Mungu na kumwomba msamaha ili atujalie neema na baraka za kuanza upya!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 33 ya Mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tuko mwishoni mwa kipindi cha mwaka A wa kiliturujia. Dominika ijayo ya 34 tutahitimisha mwaka A wa Kiliturujia kwa sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Maskini Duniani tarehe 19 Novemba 20223 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Wala usiugeuzie uso wako mbali na mtu maskini.” Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano na tabia ya maamuzi mbele. Maadhimisho haya yanakamilishwa kwa namna ya pekee, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Ni kipindi cha kufanya tathimini jinsi tulivyoyaishi mafumbo matakatifu mwaka huu wa kiliturujia. Swali la kujiuliza, Je, tumejichotea neema kwa kuzitumia vyema karama/talanta tulizojaliwa na Mungu au tumepoteza neema kwa kuzificha talanta zetu? Kama tumezipoteza neema zitokanazo na matumizi mabaya ya talanta tulizopewa mathalani kuzificha, tusikate tamaa, tuanze upya, tumlilie Mungu na kumwomba msamaha ili atujalie neema na baraka za kuanza upya maana Nabii Yeremia anasema hivi katika wimbo wa mwanzo; “Bwana asema: Mawazo ninayowawazia ninyi ni mawazo ya amani wala si ya mabaya. Nanyi mtaniita nami nitawasikiliza, nami nitawarudisha kutoka mahali pote watu wenu waliofungwa” (Yer. 29:11, 12, 14). Ndiyo maana mama Kanisa anatuombea katika sala ya mwanzo akisema; “Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utujalie tufurahi daima katika kukutumikia, maana kama tunakutumikia daima wewe Mwumba wa mema yote, tunayo heri iliyo kamili siku zote."

Furaha katika huduma kwa watu wa Mungu
Furaha katika huduma kwa watu wa Mungu

Somo la kwanza ni la kitabu cha Mithali (Mit. 31:10-13, 19-20, 30-31). Somo hili linaeleza wasifu wa mke mwema. Sifa za huyu mke mwema hazitokani na uzuri wa sura yake, urembo wake wala mavazi yake, bali na hekima na uchaji kwa Mungu ambazo kwazo zinamuwezesha daima afanye kila awezalo ili ampendeze mume wake hata kupelekea moyo wake kumwamini na kumtendea mema siku zote. Mke huyu ana heshima, ni mwaminifu, mchapa kazi na anaepukana na makundi ya uvivu na umbea, huwakunjulia maskini na wahitaji mikono yake, hana upendeleo wala hudanganyi. Mke huyu kwa mikono yake huilisha na kuitunza familia yake na Jumuiya nzima. Ana upendo kwa mume wake, watoto, majirani na watu wote. Ni mcha Mungu, mtu wa sala, anashika Amri za Mungu, anawapenda wote, anapenda amani na usitawi. Hivyo anakuwa utukufu kwa mume wake. Katika Maandiko Matakatifu, Agano la Kale uhusiano kati ya Mungu na Taifa teule la Israeli unaelezwa kwa lugha ya uhusiano wa mume na mke. Katika Agano jipya Bwana wetu Yesu Kristo anajifananisha na Bwana Arusi kwa Kanisa lake na vivyo hivyo na kila mkristo. Kumbe kama mke mwema na mwenye hekima anavyokuwa kwa mme wake, ndivyo mkristo anavyopaswa kuwa mbele za Mungu na mbele za Kristo. Jinsi mke mwema anavyojitahidi kumpendeza bwana wake, ndivyo mkristo anavyopaswa kumpendeza Mungu, naye atamwamini na kumjaza neema na baraka zake ili imani yake isitetereke hata nyakati za majaribu na siku ya mwisho isimpate ghafla. Haya yanawezekana tukiwa na hekima ya Mungu. Basi tuitafute daima hekima hii ya Mungu ili itusaidie kukesha na kutenda mema kwa ajili ya sifa na utukufu wake kwa kuwahudumia ndugu zetu kadiri ya uwezo aliotujalia mwenyezi Mungu. Tukifanya hivi neema na baraka za Mungu zitatumiminikia ziko zote kama wimbo wa katikati unavyosisitiza kusema; “Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia yake. Heri yao wale wamchao Bwana, utakuwa mwenye heri na baraka tele. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao vyumbani mwa nyumba yako, wanao kama miche ya mizeituni, wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo yule amchaye Bwana, Bwana akubariki toka Sayuni, uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako (Zab. 128:1-5).

Mke mwema ni baraka kwa familia yake.
Mke mwema ni baraka kwa familia yake.

Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (1The. 5:1-6).  Somo hili linatukumbusha wajibu wetu wa kuwa tayari daima kila wakati kwa ujio wa Kristo maana hatujui siku wala saa atayokuja kama anavyosema mtume Paulo; “Ndugu zangu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula”. Kumbe wajibu wetu ni kuziishi ahadi zetu za ubatizo kwa kuitunza nuru tuliyoipokea tulipobatizwa kila siku ya maisha yetu kama anavyosisitiza Paulo mtume akisema; “Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi…bali tukeshe, na kuwa na kiasi”  Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 25:14-30). Sehemu hii ya Injili inahimiza umuhimu wa kukesha, kuwa tayari kukipokea kifo kama njia ya kuingia katika uzima wa milele wakati wowote, kwa kuishi vyema maisha yetu kwa kuzitumia vyema talanta tulizojali kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Yesu anamfananisha Mungu na mfalme, mtu tajiri aliyewaita watumishi wake watatu, akawapa mmoja talanta tano, mwingine mbili na mwingine moja, kisha akasafiri. Mtumwa aliyepewa talanta tano alizalisha talanta tano zaidi, na aliyepewa mbili alizalisha talanta mbili zaidi. Lakini yule aliyepewa talanta moja aliificha ile talanta asizalishe chochote. Bwana wao aliporudi aliwasifu watumwa waliozalisha talanta na kuwaongezea zaidi na yule aliyeficha ile talanta moja alihukumiwa na kupewa adhabu kali. Kila binadamu amepewa vipaji au talanta na Mungu, kila mmoja kadiri alivyopenda yeye. Vipaji hivi havifanani kwa aina wala kwa idadi ili tuweze kufaana sisi kwa sisi kila mmoja akitumia kipaji chake vyema kuwahudumia wengine. Ni kwa mpango wa Mungu hakuna aliyejaliwa karama zote wala hakuna karama iliyo bora zaidi kuliko nyingine kwani kila karama inatoka kwa Mungu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wengine na kwa kufanya hivi zitusaidie kufikia utakatifu.

Karama za Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa
Karama za Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa

Kama aliyeficha talanta moja ya Bwana wake, wapo hata nyakati zetu wanaoficha vipaji vyao kwa visingizio mbalimbali. Tunaonywa tusifiche vipaji na karama alizotujalia Mungu. Mungu anataka tutumie karama tulizonazo ili kuujenga ufalme wake kwa kuwasaidiana sisi kwa sisi. Na tukitaka kutumia vema karama zetu, hatuna budi kuondoa hofu, uvivu, wivu na ubinafsi na kujivika moyo wa kudhubutu, kujaribu, ujasiri na majitoleo. Tukumbuke kuwa mwisho wa yote hata kwa kidogo ulichojaliwa na Mungu utatakiwa kutoa hesabu yake ni jinsi gani ulivyokitumia kwako mwenyewe na kwa ajili ya wengine. Basi kila mmoja afanye jitihada za kutambua vipawa alivyopewa na Mungu na avitumie ipasavyo katika kumtumikia Mungu na jirani ili siku moja kila mmoja aweze kusikia sauti ya Mungu ikimwambia; “Vema mtumwa mwema na mwaminifu, ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi. Ingia katika furaha ya Bwana wako.” Tumwombe Mungu atujalie ujasiri tusiogope kujaribu na kuthubutu kama aliyepewa talanta moja alivyoogopa kuifanyia kazi na kwasababu hiyo aliadhibiwa. Zaidi sana atusaidie tuwe watumishi wema na waaminifu tunaokaa macho ili siku ya hukumu isitupate ghafla bali tuwe tayari kutoa hesabu za faida kwa vipawa tulivyopewa. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisali na kusema; “Ee Bwana, tunaomba sadaka tuliyotoa mbele ya macho yako wewe mtukufu, itupatie neema ya kukutumikia na kutuletea heri ya milele”. Nayo antifona ya wimbo wa komunyo inatilia mkazo kusema; “Bwana asema: Amini, nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu” (Mk. 11:23, 24). Mama Kanisa anahitimisha kwa sala baada ya komunyo kwa matumaini makubwa akisema; “Ee Bwana, tumepokea mapaji ya fumbo hili takatifu; na sasa tunakuomba kwa unyenyekevu, hayo aliyotuamuru Mwanao tuyafanye kwa ukumbusho wake, yafae kutuongezea mapendo daima na milele”. Na hili ndilo tumaini letu, kuupata uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D33
14 November 2023, 16:04