Tafakari Dominika ya Kwanza ya Majilio Mwaka B wa Kanisa: Matumaini
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa. Kabla ya kuzama katika tafakari ya masomo tujikumbushe baadhi ya mambo muhimu katika maadhimisho ya vipindi vya kiliturujia. Kwa jumapili ya kwanza ya majilio tunaanza mwaka mpya wa kiliturujia katika Kanisa. Huu ni tofauti na mwaka mpya wa asili unaoanza Januari Mosi. Dominika iliyopita ya 34 tulifunga mwaka 2023, mzunguko A wa kiliturujia kwa sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Kumbe huu ni mwaka B wa kiliturujia 2024. Katika Kalenda ya liturujia, Kanisa limeweka vipindi Vikuu sita ambavyo ni Majilio, Noeli, Kwaresima, Pasaka, Pentekoste na Kipindi cha Kawaida cha mwaka. Majilio ni kipindi cha maandalizi ya ujio wa Yesu Kristo. Noeli ni kipindi cha kusherehekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Kwaresma ni kipindi cha kufunga na kusali kwa bidii tukikumbuka mateso na kifo chake Yesu Kristo ili kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Pasaka ni kipindi cha kusherehekea kufufuka kwake Yesu Kristo na kukombolewa kwetu kutoka utumwa wa dhambi. Pentekoste ni kipindi cha kumpokea Roho Mtakatifu, mfariji na kiongozi wetu katika kweli na uzima. Kipindi cha kawaida cha mwaka kinatuongoza namna tunavyopaswa kuishi maisha yetu ya Kikristo tukiongozwa na Roho Mtakatifu. Kumbe, sehemu ya kwanza katika mwaka wa Kiliturujia inaitwa “Kipindi cha majilio”. Hiki ni kipindi cha kujiandaa kiroho kumpokea Bwana wetu Yesu Kristo, Emanueli; Mungu pamoja nasi katika kusherehekea kuzaliwa kwake ili kuhuisha maisha yetu ya kiroho. Ni kipindi cha kungojea kwa matumaini ujio wake Bwana kama wimbo wa mwanzo unavyoashiria ukisema; “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, ee Mungu wangu, nimekutumainia wewe, nisiaibike milele, adui zangu wasifurahie kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata milele” (Zab. 25:1-3). Kipindi hiki cha Majilio kinadumu majuma manne nacho kimegawanywa katika sehemu kuu mbili.
Sehemu ya kwanza huanza na Dominika ya kwanza ya Majilio na huishia tarehe 16 Desemba. Mama Kanisa katika Liturujia ya sehemu hii, ametuwekea sala, nyimbo na masomo yanayotuongoza kutafakari juu ya ujio wa pili wa Yesu Kristo katika utukufu wake, siku ya mwisho, atakapowahukumu watu wote na kuukamilishi wokovu. Ndiyo maana katika sala ya mwanzo mama Kanisa anatuombea akisema; “Ee Mungu Mwenyenzi, tunakuomba utujalie sisi watumishi wako neema hii, ya kwamba Kristo atakapokuja, tumlaki na matendo mema, atuweke kuume kwake, tustahili kupata ufalme wa mbinguni”. Katika utanguzi wa wakati huu mama Kanisa anasali hivi: “Sasa tunangojea kwa hamu siku ile atakapokuja mara ya pili Kristo katika utukufu wake”. Kumbe Liturujia ya sehemu hii ya kwanza inatutia nguvu ya kuendelea kuishi maisha mema bila kuchoka, huku tukingojea kwa matumaini kurudi kwake Kristo siku ya mwisho. Ujumbe mkuu ni huu; “Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Bwana yu karibu. Atakuja kuliokoa na kulihukumu taifa lake.” Sehemu ya pili ya kipindi cha majilio huanzia tarehe 17 hadi 24 Desemba. Masomo ya sehemu hii yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo katika historia, yaani kuzaliwa kwake duniani. Sala, nyimbo na masomo ya sehemu hii yanatukumbusha zile siku Wasraeli walipokuwa wakimsubiri mkombozi. Wakati huu Kanisa linajifananisha na taifa la Mungu la Agano la Kale linalotarajia kwa hamu kubwa ujio wa Mkombozi likiyaangalia na kuyaona mateso na maumivu yote ya binadamu wasiokombolewa bado, lakini huishi pia kwa kujaa matumaini yenye furaha ya kumngojea Mkombozi aliyeahidiwa na Mungu na ujio wake uliotangazwa na manabii. Huu ni wakati wa matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo. Hamu ya wanadamu wote ya kupata wokovu imo ndani ya Liturujia ya sehemu hii hasa katika nyimbo za katikati zenye vibwagizo vya maneno kama haya: “Ee hekima, ee mwana, ee kimea cha Yese, ee ufunguo wa Daudi, ee Mawio, ee Mfalme wa mataifa, ee Emmanueli, uje kutuokoa."
Jambo la pili ni hili, tukumbuke kuwa kila tukio katika historia ya wokovu wetu linapoadhimishwa kiliturujia lina hali mbili; kwanza ni kutukumbusha yaliyotokea katika historia ya ukombozi wetu na pili kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho. Kumbe kila mwaka wa kiliturujia ni mpya na wa pekee. Hakuna mwaka unaofanana na mwingine. Maana kila mwaka unapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na hivyo kutuleta karibu zaidi kwa Mungu na kutuonjesha upendo wake. Kumbe kila mara yanapoadhimishwa vyema mafumbo ya ukombozi wetu ynahuisha na kupyaisha maisha yetu ya hapa duniani, tunapoelekea katika maisha ya umilele mbinguni. Kumbe tusikianze kipindi hiki kwa mazoea kana kwamba hakuna jipya lolote bali kwa unyenyekevu na usikivu tufungue mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi kwa kusikiliza maongozi ya mama Kanisa. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 63:16-17; 64: 1, 4-8). Somo hili ni sala ya kiri kuu ya dhambi ya Taifa la Israeli waliosali kundi la kwanza la waliorudi kutoka uhamishoni Babeli wakifuata tamka la ruhusu ya kurudi Yerusalemu lililotolewa na mfalme Koreshi 538 KK. Kundi hili walipoona madhara ya dhambi na uovu wao kama vile kubomolewa kwa kuta za mji na hekalu lao walifanya kiri kuu ya dhambi yao na kutambua kuwa Mungu pekee ndiye Baba na mkombozi wao hakuna mwingine. Tunasoma hivi; “Wewe, Bwana, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako. Urudi kwa ajili ya watumishi wako, kabila za urithi wako. Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo. Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu. Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako” (Isaya 63:16-17).
Hii ni kiri kuu na nzito ya dhambi ya Israeli, ni toba ya kweli isiyo na waa lolote. Sisi nasi tunapoanza kipindi hiki cha majilio tunaitwa kuifanya toba ya kweli ndani kabisa mwa mtima wa mioyo yetu, bila kusita ili tuweze kujiandaa vyema kumpokea Masiha, Bwana wetu Yesu Kristo, atakapozaliwa ndani ya mioyo yetu na kutufanya upya watoto wa Mungu na wa Kanisa. Tujichunguze ni wapi tumekosea, ni wapi tumeanguka, ni wapi kuna mapungufu ili tupate kumuomba mwenyezi Mungu msamaha kama mzaburi anavyotuongoza katika kiitikio cha wimbo wa katikati akisema; “Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka” (Zab. 80:3). Tukifanya hivi Yeye atatupokee tena kama wanawe wapendwa na pale tulipofanya vizuri tuombe neema na baraka zake ili tuendelee kudumu katika kutenda mema. Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 1:3-9). Katika somo hili Mtume Paulo anamshukuru Mungu kwa neema zote walizopewa Wakorintho katika kupokea imani ya Kristo na anawaombea ili wabaki imara katika imani hiyo mpaka siku ya mwisho watakapoingia katika ufalme wa Mungu mbinguni wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Sisi nasi kwa ubatizo tumepewa kila aina ya neema kutoka kwa Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu tuliyempokea, na hivyo tukafanywa upya wana wa Mungu na wa Kanisa. Naye mama Kanisa ametuwekea kipindi hiki cha majilio ili tujikumbushe tena na tena wajibu wetu wa kujiweka tayari kila mara ili Kristo atakapofunuliwa kwetu pale tutakapokufa tuweze kuingia katika ushirika wake katika ufalme wa Mungu mbinguni milele yote.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk. 13:33-37). Katika sehemu hii ya Injili msisitizo ni kuwa tayari kufa mda na wakati wowote tukiwa na muunganiko na Mungu. Na kwa kuwa hatujui siku wala saa ya kifo chetu ambayo ndiyo siku na saa ya hukumu yetu kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi. Basi tuwe tayari daima mda wote kwa kuzishika na kuziishi amri za Mungu ili siku ifikapo tuweze kustahilishwa kuingia katika ufalme wa mbinguni. Kwa kuwa kuna dhambi za mazoea nazo ni ngumu kuziacha bila ya msaada wa Roho Mtakatifu. Tunapaswa kuwa watu wa sala ili tujipatie nguvu ya kushindana na tabia na mazoea ya dhambi huku tukiwa wasikivu kwa neno la Mungu ambalo ni kama kengele inayotuamsha ili kukesha, tukimsubiria ndugu yetu kifo. Huku ndiko kuwa tayari daima kumpokea Emanueli Mungu pamoja nasi siku ya Noeli. Kumbe, kwa minajili hii maisha yetu yote ni kipindi cha majilio, yaani mwendelezo wa kumsubiri Kristo hadi atakapokuja tena kutuita kwa njia ya kifo tukaishi milele yote mbinguni kama sala baada ya komunyo inavyosema: “Ee Bwana, tunakuomba mafumbo haya tuliyoadhimisha, yatufae sisi tunaotembea katika malimwengu, nawe utufundishe kupenda mambo ya mbinguni na kuzingatia ya milele.” Nawatakia mwanzo mwema wa Mwaka Mpya wa Kiliturujia, Mwaka B, na Kipindi chema cha Majilio. Tujiandae vyema kiroho ili Kristo aje azaliwe ndani ya mioyo yetu na kutuhuisha katika maisha ya kiroho kwa kutuweka karibu zaidi na Mungu Baba yetu.