Tanzania:Waseminari 85 wavaa makanzu Seminari Kuu Ntungamo
Na Patrick Tibanga, - Radio Mbiu-Bukoba & Angella Rwezaula-Vatican.
Furaha ya ukweli (Veritatis gaudium) inaeleza shauku kuu inayofanya moyo wa kila mtu kuhangaika hadi anapokutana, kukaa na kushiriki Nuru ya Mungu na kila mtu. Ukweli, kwa hakika, siyo wazo lisiloeleweka, bali ni Yesu, Neno la Mungu ambaye ndani yake mna Uzima ambao ni Nuru ya wanadamu (rej. Yh 1:4), Mwana wa Mungu ambaye wakati huo huo ni Mwana wa mtu. Ni Yeye peke yake, “anayefunua Fumbo la Baba na upendo wake, humfunua mwanadamu kwa mwanadamu na kumjulisha wito wake mkuu.” Ni katika mkutadha huo ambao Baba Mtakatifu Francisko anaanza kueleza katika Katiba ya kitume ya Veritatis gaudium akifafanua, vema kuhusu majiundo ya kikuhani. Kwa njia hiyo hata Kanisa la Tanzania, linazidi kuchanua miito ya kikuhani, kwa ajili ya utume wa Watoto wa Mungu ambao ni kama Kondoo wasio na mchungaji.
Jumamosi, tarehe 25 Novemba 2023, Kanisa katoliki la Tanzania lilikuwa na furaha kwa kuwapokea rasimi wafundwa wao katika majiundo endelevu ambapo, Askofu Method Kilaini, Msimamizi wa kitume Jimbo Katoliki la Bukoba aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika fursa ya kuvishwa vazi la uklero(makanzu) kwa mafrateli 85 kutoka majimbo mbali mbalimbali katoliki wanaosoma katika Seminari kuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua - Ntungamo Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania. Katika homilia yake, Askofu Kilaini, alisema kuwa, kupitia Vazi la Uklero wanafanywa kutambuliwa na jamii pamoja na wote wanowazunguka ambapo pia wanatakiwa kutambua majukumu yao kutokana na kuvaa vazi na kukubali uchaguzi wa Bwana aliowaitia wa kulitumikia Kanisa kwa kutambua kile ambacho Mungu amewaita na kutambua ni wapi wanaelekea ikiwemo wito wa upadre.
“Yeye ndiye aliyewaita hapa ili muweze kuvaa vazi hilo. Hii ni hatua kubwa mliyoichagua, na vazi hilo linakuonesha wewe unajitambua kuwa ni nani, lazima ujitambue wewe mwenyewe na ukikubali kulivaa inamaana umetambua kuingia katika kundi hili ni hatua kubwa sana ya kuchagua,” Alisema Askofu Kilaini. Katika mahubiri hayo Askofu alisema kuwa Upadre ni wito ambao sio chakula bali wao wanaliwa wao wanaotumikia na kuwasihi Mafrateli kutambua kuwa wito huo ni kujitoa na kuacha nafsi zao na kufa katika Upadre, wala siyo kutumikia mali. “Unapokwenda katika Upadre ukasema utajenga nyumba yako, hayo hakuna huko, kikubwa ni kufa kwa nafsi yako na kusema tazama Mimi hapa, unitume na sio kujisemea nafsi yako vile unavyotaka. Ni utii kwa wakubwa na kuachilia mbali umimi na kuwa wa Mungu na kufa kwa nafsi yako,” Alielezea Askofu Kilaini.
Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania akiendelea aliwataka Mafrateli na Mapadre kushika amri za Mungu na kukaa katika pendo kwa kupendana na kurekebishana pale wanapokosea na kusaidiana katika wema ili kufanya vizuri katika wito walioitwa na kupeleka upendo kwa waamini wanao wahudumia katika utume wa wito huo na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine na wakati huo huo, aliwageukia waseminari hao akiwashauri kumtegemea na kuomba kupitia Mama Bikira Maria katika magumu na changamoto zote watakazokutana nazo naye atawabeba katika kila changamoto. “Mkitoka hapa na kuelekea katika parokia mambo yote yatakuwa mazuri na kufanikiwa hivyo muanzie hapa na kama mkipendana na kusaidiana katika wema na kukuzana katika vipaji, maadili mazuri, kusaidia katika vitu vidogo vidogo na kufanikiwa katika masomo, maisha yenu yatakuwa mazuri na upendo mtakao kuwa nao utamiminika kwenda kwa waamini mtakao wahudumia, hivyo ninaomba niwaweke katika mikono ya mama Maria ambaye anatubeba kila wakati, na yeyote yule anaye muomba Mama Maria hapati shida hata mara moja hivyo mumkimbilie mama atawabeba na atawasaida vizuri,” Alihitimisha Askofu Kilaini mahubiri yake. Katika Misa hiyo jumla Mafrateli 85 ni kutoka majimbo mbali mbali na mashiriki ya kitawa na ya Kipapa nchini Tanzania katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba.
Ikumbukwe kwamba mnamo 2021 Kanisa Katoliki nchini lilianza mchakakato wa kufanya mabadiliko ya utoaji Elimu katika Seminari Kuu za Kanisa Katoliki za Falsafa na Taalimungu, wengi wanatambua kama (Teolojia), kwa kuziingiza kwenye mfumo wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na mfumo wa Elimu ya Ngazi za Juu duniani. Hayo yalithibitishwa na Makamu Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Flavian Kasala, wa Jimbo Katoliki la Geita, wakati wa mahojiano na kurugenzi ya mawasiliano ya Baraza la Maaskofu TEC, jijini Dar es Salaam. Sababu za mabadiliko hayo yalikuwa ni kutii maombi Baba Mtakatifu, Francisko; ambaye aliomba kubadili mfumo wa Seminari zote kuu katika ngazi zote za Falsafa na Taalimungu, ili kuingia katika mfumo wa Vyuo vya Elimu ya juu, tofauti na mfumo wa awali ambapo seminari hizo zilizokuwa ni taasisi za kidini, zikijihusisha zaidi na malezi ya Mapadre, katika hatua ya Falsafa na Taalimungu. (Rej.Costituzione Apostolica «Veritatis gaudium» yaani Katiba ya Kitume ya Papa Francisko ya Furaha ya Ukweli iliochapishwa mnamo tarehe 29 Januari 2018.
Mabadiliko ya Siminari Kuu
Kufuatia na mabadiliko hayo ni wazi kwamba Seminari kuu hasa zile ambazo zilikuwa hazijawa na mfumo huo kwa upande wa Makanisa Mahalia zingeanza mara moja kupokea Wanafunzi mbalimbali wakiwemo Walei Wakatoliki na kutoka dini na madhehebu mbalimbali, wakiwemo Wanaume na Wanawake, wenye lengo la kupata shahada ya Falsafa na Taalimungu katika Seminari Kuu hizo. Kwa upande wa Kanisa la Tanzania, kuna Seminari Kuu saba, ambazo ni Kibosho -Moshi, Ntungamo - Bukoba, Segerea -Dar es Salaam, Nazareth - Mwendakulima (Kahama), Jordani - Morogoro, Peramiho - Songea na Kipalapala - Tabora. Tangu kufanyika mabadiliko hayo, mfumo wa Seminari Kuu uliokuwa ukitumika nchini Tanzania ambao ulikuwa hautambuliwi na Mfumo wa Vyuo Vikuu vya Kipapa vilivyopo Ulaya, na mbapo sasa unawezesha tayari hata mwanafunzi anatoka katika mafunzo ya Taalimungu kutoka Tanzania kuja Vyuo Vikuu vyaUlaya kutambuliwa moja kwa moja bila kurudia masomo.
Majiundo ya Kikuhani
Katika majiundo ya Upadre, tangu kuhitimu kidato Cha VI, Mhusika anapaswa kusoma Falsafa ambayo ni miaka mitatu, halafu Taalimungu ambayo ni miaka minne na mwaka mmoja wa Kichungaji, jumla miaka nane, Utaratibu huo pia unategemea na walezi wakuu kama maaaskofu na wakuu wa Mashirika katika majiundo yao ya mashirika, na hivyo miaka inaweza kuwa zaidi kabla mseminari hajawa Padre. Hata hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Veritatis Gaudium ya Papa Francisko Vitivo vya Falsafa na Taalimungu mtahiniwa anajifunza hayafuatayo:
Mtaala wa masomo ya Kitivo cha Taalimungu ni pamoja na:
a) mzunguko wa kwanza, wa kitaasisi, ambao hudumu kwa kipindi cha miaka mitano au mihula kumi, au kwa kipindi cha miaka mitatu au mihula sita, ikiwa kipindi cha miaka miwili ya falsafa inahitajika kabla yake. Miaka miwili ya kwanza lazima ijikite zaidi katika elimu dhabiti ya falsafa ambayo ni muhimu kushughulikia ipasavyo somo la taalimungu. Shahada iliyopatikana katika Kitivo cha Falsafa ya kikanisa inachukua nafasi ya kozi za mzunguko wa kwanza wa falsafa katika vitivo vya taalimungu. Shahada katika Falsafa iliyopatikana katika kitivo kisicho cha kikanisa haijumuishi sababu ya kumfukuza kabisa mwanafunzi kutokana na kozi za mzunguko wa kwanza wa falsafa katika vitivo vya taalimungu. Taaluma za kitaalimungu lazima zifundishwe kwa namna ya kuwasilisha ufafanuzi wa kiungo cha mafundisho yote ya Kikatoliki, pamoja na utangulizi wa mbinu ya utafiti wa kisayansi. Mzunguko huo unaisha na shahada ya kitaaluma ya Shahada au nyingine inayofaa, itakayobainishwa katika Kanuni za Kitivo.
b) Mzunguko wa pili, wa utaalam, ambao hudumu kwa miaka miwili au mihula minne. Ndani yake, taaluma fulani hufundishwa, kulingana na asili tofauti ya utaalamu, na semina na mazoezi hufanyika ili kupata uwezo wa kufanya utafiti wa kisayansi. Mzunguko huo unaisha na shahada ya kitaaluma ya leseni maalum.
c) Mzunguko wa tatu ambapo mafunzo ya kisayansi yanakamilishwa kwa muda unaofaa, hasa kupitia utayarishaji wa tasnifu ya udaktari. Mzunguko huo unaisha na digrii ya kitaaluma ya Udaktari.
Kifungu cha 75. §1. Ili mtu ajiandikishe katika Kitivo cha Taalimungu, ni muhimu kuwa amekamilisha masomo ya masharti, kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Katiba hiyo. §2. Ambapo mzunguko wa kwanza wa Kitivo ni wa miaka mitatu, mwanafunzi lazima awasilishe cheti cha kipindi cha falsafa cha miaka miwili, kilichokamilishwa ipasavyo katika Kitivo au Taasisi ya falsafa ya kikanisa iliyoidhinishwa.
Kifungu cha 76. §1. Ni kazi ya pekee ya Kitivo cha Taalimungu kutunza mafunzo ya kitaalimungu ya kisayansi kwa wale wanaoelekea kwenye upadre na wale wanaojiandaa kutekeleza majukumu maalum ya kikanisa; kwa sababu hiyo ni lazima kuwe na idadi inayofaa ya walimu wa makuhani. §2. Kwa ajili hiyo pia kuna taaluma maalum zinazofaa kwa waseminari; Hakika, "Mwaka wa Kichungaji" unaweza kuanzishwa ipasavyo na Kitivo chenyewe ili kukamilisha mafunzo ya kichungaji, ambayo yanahitajika, baada ya kukamilika kwa kipindi cha kitaasisi cha miaka mitano, kwa upadre, na inaweza kuhitimishwa kwa kutoa Diploma maalum.
Kitivo cha Kifalsafa
Kifungu cha 81. §1. Kitivo cha kikanisa cha Falsafa kina lengo la kuchunguza kwa kina matatizo ya kifalsafa na, kwa kuzingatia urithi halali wa kudumu wa kifalsafa (rej. Optatam totius, 15: AAS 58 [1966], 722), ya kutafuta suluhisho lake katika nuru ya kawaida ya sababu, na zaidi ya hayo, kuonesha mshikamano wao na maono ya Kikristo ya ulimwengu, ya mwanadamu na ya Mungu, yakionesha uhusiano kati ya falsafa na taalimungu. §2. Kisha inalenga kuwaelimisha wanafunzi, ili kuwafanya kufaa kwa kufundisha na kufanya shughuli nyingine zinazofaa za kiakili, pamoja na kukuza utamaduni wa Kikristo na kuanzisha mazungumzo yenye matunda na Watu wa wakati wao.
Kifungu cha 82. Mtaala wa masomo wa Kitivo cha Falsafa ni pamoja na: a) mzunguko wa kwanza wa kitaasisi, ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu au mihula sita, kuna udhihirisho wa kiungo cha sehemu mbali mbali za falsafa, ambazo zinahusika na ulimwengu, mwanadamu na Mungu, na vile vile historia ya falsafa, kwa kuanzisha mbinu za kazi ya kisayansi; b) Mzunguko wa pili, au utaalam wa awali, ambapo, kwa miaka miwili au mihula minne, kupitia taaluma maalum na semina, tafakari ya kina ya falsafa imeanzishwa katika sekta fulani ya falsafa; c) mzunguko wa tatu ambao, kwa kipindi cha angalau miaka mitatu, mafunzo ya kisayansi yanakamilika, hasa kupitia maandalizi ya tasnifu ya udaktari.
Kifungu cha 83. Mzunguko wa kwanza unaishia na shajada ya pili na Leseni maalum, na tatu ni Shahada ya Uzamivu.
Kifungu cha 84. Kujiandikisha katika mzunguko wa kwanza wa Kitivo cha Falsafa ni muhimu kukamilisha masomo ya masharti, kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Katiba hiyo ya Kitume. Ikiwa mwanafunzi, ambaye amemaliza kwa mafanikio kozi za kawaida za falsafa katika mzunguko wa kwanza wa kitivo cha taalimungu, basi anataka kuendelea na masomo yake ya falsafa ili kupata Shahada katika kitivo cha kikanisa cha falsafa, kozi zinazohudhuriwa wakati wa njia iliyotajwa hapo juu lazima zizingatiwe kwa makini.