Bahrain:zaidi ya washiriki 20elfu wa makabila tofauti katika misa ya mkesha wa Noeli
Na Angella Rwezaula – Vatican.
“Mbele ya pango la Bethlehemu tunawasilisha maombi yetu na sifa zetu. Tunatafuta baraka na neema. Mtoto mpya aliyezaliwa atatuongoza kwenye maisha ya kung'aa na ushiriki mpya katika maisha ya kimungu. Hivyo ndivyo Askofu Aldo Berardi, O.SS.T. Msimamizi wa Kitume wa Kaskazini mwa Arabia, alizungumza na waamini waliokusanyika katika Shule ya Moyo Mtakatifu(SHS)katika Mji wa Isa kwa ajili ya misa ya mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2023. Askofu alitaka kuakisi umuhimu wa upendo, huruma na msamaha wakati wa sikukuu ya Noeli na jinsi kuzaliwa kwa Yesu kunaonesha upendo wa Mungu kwa wanadamu.
Kanisa nchini Bahrain na Noeli 2023
Tarehe 24 Disemba 2023, Kanisa Katoliki nchini Bahrain lilisherehekea Mkesha wa Noeli kwa furaha na shukrani nyingi kwa Wakatoliki zaidi ya 20,000 waliokusanyika kushiriki katika ibada zilizoadhimishwa kwenye Kanisa Kuu la Mama Yetu wa Arabia huko Awali, katika Shule ya Moyo Mtakatifu na katika Kanisa la Moyo Mtakatifu huko Manama, ambapo sherehe ilifanyika kwa lugha ya Kimalayalam. Misa hiyo adhimu ilikuwa ni ishara ya matumaini na umoja kwa jumuiya ya Kikatoliki, inayojumuisha watu wa makabila na mataifa mbalimbali na wa lugha na taratibu mbalimbali.
Shukrani kwa Mfalme Hamad Bin Isa Al Khalifa
Kulikuwa na maneno ya furaha kutoka kwa Padre Francis Joseph(OFM), Paroko wa Kanisa la Moyo Mtakatifu huko Manama, ambaye pia alimshukuru Mfalme Hamad Bin Isa Al Khalifa, familia nzima ya kifalme ya Ufalme wa Bahrain, Waziri Mkuu na wizara zote za Serikali pia kwa msaada na ukarimu wao kwa Kanisa Katoliki na uwepo wa Wakristo nchini humo. Vile vile alipongeza moyo wa uvumilivu na kuishi pamoja unaoitambulisha nchi ya Bahrain na kuwataka waamini hao kuwa mashahidi wa amani na upendo katika jamii.